(Mtunzi wa kitabu cha Al-Ghadiir) Allamah Sheikh Abdul Hussain (Amini) -- mtoto wa Sheikh Ahmad na mjukuu wa Sheikh Najaf Ali Mulaqqab Amin Shar'a. Jina Ia Amini limetokana na mababu zake. Allamah Amini alizaliwa katika nyumba ya wazee waliobobea katika ilimu na Dini mjini Tabriz (Iran) mnamo mwaka 1320 A.H. Kwa kuwa baba yake alikuwa ni mtu ambaye amesoma sana hivyo maisha yake yakawa katika fani hii ya kujipatia ilimu na maarifa ya Dini na nyanja zinginezo za fani hii. Ilithibitika kuwa Al-Amini alikuwa ni mwenye akili na maarifa ya aina yake - alikuwa na upeo mkubwa wa kuhifadhi ilimu na mwenye nguvu. Alijipata ilimu ya mwanzo kutoka kwa wazazi wake na baadaye alijiunga katika chuo ambacho hadi leo ni mashuhuri huko mjini Tabriz. Katika chuo hicho alijifunza misingi ya awali ya Fiqh na Usuul kutoka kwa ma-Ulamaa wafuatao: Ayatullah Sayyid Muhammad ibn Abdul Karim Musawi, Araf Maulana Ayatullah Sayyid Murtadha ibn Muhammad Husseini Khusrushahi, Ayatullah Sheikh Hussein ibn Abd Ali Tutunchi na Allamah Sheikh Mirza Ali Asghar Maliki.
|