Hambali faqihi, Ibrahim bin Ali bin Muhammad bin Danwiri anaandika kisa kimoja kirefu sana katika kitabu chake Nihayaat-ul-Talib kwa kumnakili Taus bin Abbas, kuwa: Mtume Muhammad [s] alimwambia Bwana Abbas (r.a.) (i.e. ndugu wa baba yake) kuwa: "Mwenyezi Mungu amenibashiria Utume, Unabii pamoja na risala Tukufu na ameniamrisha nitangaze wazi wazi mahubiri na Da'awa, Naomba kujua rai yako?" Bwana Abbas (r.a.) akasema: "Ewe kipenzi cha ndugu yangu! Wewe unaelewa waziwazi kuwa Maquraish wanahusuda mno na ukoo wako. Kwa hakika kila usemacho kwa hakika kama itatokea kuwa hivyo hivyo basi kunaweza kutokea machafuko makubwa kabisa ya kuangamizana. Wao watatulenga sote kwa pamoja katika kutuangamiza na watatung'oa kutoka mizizi yetu na kututupilia mbali. Wewe tuache katika hali hii tulivyo na hivyo uache harakati zako hizo. Hata hivyo ni ushauri wangu kuwa umwendee baba yako mkubwa, Bwana Abu Talib [a] kwa sababu yeye ndiye kaka yetu mkubwa kuliko sisi sote. Usikie na ushauri wake unasemaje. Yeye atakusudia na vile vile hatakuacha peke yako wala hatakusalimisha kwa maadui zako. Baada ya hapo Mtume Muhammad [s] pamoja na baba yake mdogo Bwana Abbas (r.a.) walikwenda kwa Bwana Abu Talib [a] na Bwana Abu Talib [a] alipowaona hao wawili wakija, akawaambia "Kwa hakika leo kunajambo muhimu sana, je ni swala gani lililowaleteni kwangu mimi wakati huu?" Bwana Abbas (r.a) akamwambia Bwana Abu Talib [a] mazungumzo yote yaliyotokea baina yake na Mtume Muhammad [s] na kwa kuyasikia hayo Bwana Abu Talib [a] alimtazama Mtume Muhammad [s] na akasema: "Ewe mtoto wa ndugu yangu! Inuka na tangaza kile ulichoamrishwa na Mwenyezi Mungu bila ya woga au kusita kwa sababu wewe ni mtu mwema na hodari na wewe unatokana na nyumba moja tukufu na madhubuti kabisa na ya viongozi. Nakula kiapo cha Mwenyezi Mungu, hakuna hata ulimi mmoja ambao utakaokuletea shida wewe ila utakabiliwa kwa ulimi mkali na wenye kuzikata hizo zote na mapanga makali yatavurumishwa. Kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu! Makabila ya Waarabu watakuwa watiifu kwako kama vile wanyama watoto wanapokuwa watiifu na wanyenyekevu kwa wale wawanyweshao maziwa. Uhakika huu ni kwamba mtukufu baba yangu Bwana Abdul Muttalib alikuwa daima akikisoma kitabu na kuniambia: "Bila shaka atatokezea Mtume katika kizazi changu. Ni matumaini yangu kuwa niwe hai katika zama za Mtume huyo na niletee imani dini yake huo ni usia wangu kwa watoto wangu wote wale watakaokuwa hai katika zama hizo za mtume huyo waikubalie dini yake.[10] Allamah Amini anasema: Ndugu wasomaji ninyi mmejionea kwa roho tulivu vile Bwana Abu Talib [a] anamnakili baba yake Abdul Muttalib. Yeye anampa nguvu na hima na moyo Mtume Muhammad [s] autangaze utume wake na kufanya Da'awa na alitukuze jina Ia Mwenyezi Mungu na kulifikisha kwa watu wote. Yeye vile vile anakubali na kuamini uhakika huu uliodhahiri kuwa Mtume Muhammad [s] ndiye mtume aliyebashiriwa katika vitabu vya mitume iliyotangulia na kwamba Waarabu watajisalimisha mbele ya utume wake na kuleta imani juu ya dini yake. Ndugu msomaji, jee kweli unaweza kuamini na hata kuthubutu kusema kuwa Bwana Abu Talib [a] akiwa anayajua yote hayo kuhusu mtume na utume wake na vile ilivyokuwa imebashiriwa katika vitabu vitukufu vya mitume iliyomtangulia bado akawa mushrik na kafiri? Yeye awaambie watu wote waje kumsikia Mtume Muhammad [s] juu ya Da'awa ya dini ya Kiislamu wakati huo huo yeye akajiepusha na maneno ya Mtume Muhammad [s] akabakia kafiri? Kwa hakika kufuatana na mambo yalivyo bayana mtu yeyote atakayethubutu kusema kuwa Bwana Abu Talib [a] alikuwa ni mushriki au kafiri basi mtu kama huyo ni mnafiki na muongo na tumwelewe waziwazi kuwa mtu huyo anazo tuhuma na mawazo ya kishetani ambayo hayatamfikisha popote ila katika shimo la upotofu na maangamizo. Hizo ndiyo njama za Mawahabi kutaka kumdhalilisha Bwana Abu Talib [a] kwa sababu ni baba yake Imam Ali [a]. [10] Sayyid bin Tausi: taraif, uk. 85; Abul Hasan Shariff: Dhiya al-Aalamiin
|