Imamu Husayn [a] alizaliwa mnamo siku ya Alhamisi tarehe tatu ya mwezi wa Shaaban mnamo mwaka wa nne wa Hijiriya. Alipozaliwa Mtume [s] alikuja, akamchukua mikononi mwake na akatia ulimi wake kinywani mwa mtoto huyu mchanga ambaye aliunyonya. Mnamo siku ya saba ilifanyika sherehe ya Aqiqa (kunyolewa kwa nywele alizozaliwa nazo mtoto). Kuzaliwa kwa mtoto huyu kulikuwa chanzo cha furaha kwa familia yote lakini Mtukufu Mtume [s] alijua yatakayomtokea mtoto huyu baadaye na hivyo alilia sana. Tokea wakati huo jamii nzima ya Mtume [s] ilianza kuyazungumzia masaibu ya maishani mwake yatakayomsibu na ambayo yatahusiana kabisa na maisha yake.
|