 |
KULELEWA KWAKE
Mtukufu Mtume [s] alikuwa akiwalea wajukuu zake Hasan [a] na Husayn [a] na vile vile alikuwa akiulea Uislamu; na Hadhrat Ali [a] na Bibi Fatimah [a] walikuwa nao vile vile wakiwalea watoto hawa ambao Mtukufu Mtume [s] aliwaita wanawe. Alikuwa akiwachukua popote pale aendapo. Mara nyingi Imamu Hasan [a] alikaa katika bega lake Ia kuume na Imamu Husayn [a] alikaa katika bega lake Ia kushoto. Kila mara Mtume [s] aliwataka Waislamu wawapende hao watoto wake Mtume [s], na mapenzi yake kwa Imamu Husayn [a] yalikuwa na kiwango kikubwa. Mtume [s] alipokuwa akisali, Imamu Husayn [a] alikuwa akija na kukaa mgongoni pake. Mtume [s] alikuwa akiendeleza Sajdah yake mpaka Imamu Husayn atelemke kwa hiari yake. Wakati fulani Imamu Husayn [a] alikuja kwenye Msikiti wa Mtume [s], msikiti wa mjini Madina, wakati Mtume [s] alipokuwa akihutubia. Imamu Husayn [a] alijikwaa na kuanguka chini. Mtume [s] mara moja aliacha kuhutubia, akateremka chini na kumnyanyua mwanawe kwanza. Kisha aliwahutubia watu waliokuwepo hapo akisema, "Huyu ni Husayn; mfahamuni vizuri". Vile vile Mtume [s] alisema, "HUSAYN ANATOKANA NA MIMI, NA MIMI NINATOKANA NA HUSAYN", akiwa na maana ya kuwa lmamu Husayn [a] alikuwa ndio maisha ya Mtukufu Mtume [s] na jina Ia Mtume [s] litadumu kupitia kwake.
|