Al-Kulaini na Sheikh Muhiyud-Din ibn 'Arabi wameelezea kwa mamlaka ya Aasim bin Hamza Al-Saluli,ambaye anasema kuwa yeye alimwona kijana mmoja akilia katika mtaa mmoja mjini Madina:"Ewe Allah swt! Amua kesi baina yangu na mama yangu." Umar al-Khattab,ambaye alikuwa akipita hapo,alimkanya kijana huyo:"Usilitaje jina la mama yako!" Kijana huyo alisema:"Ewe Amiral-muminiin! Mama yangu alinizaa na kuninyonyesha maziwa kwa miaka miwili,lakini sasa nilipokua,ananikataa kata kata kuwa mimi si mtoto wake.Yeye pia anakana kuolewa na baba yangu,ambaye alishafariki,na anataka kujichukulia milki yote huku akidai kuwa alikuwa ni ndugu yake tu,na hivyo kuninyima sehemu yangu ya urithi." Kwa kuyasikia hayo, Umar alimwita yule mwanamke ambaye alikuja na mashahidi arobaini wa upande wake. Hao wote walitoa ushahidi kumpendelea yeye. Kwa hayo, Umar alitoa hukumu ya kijana yule kufungwa kwa kosa la 'iftara (kusingizia). Wakati yule kijana alipokuwa akichukuliwa kifungoni, alikutana njiani na Imam Ali a.s. Kijana yule alimlilia Imam Ali a.s. kumsaidia na akamwelezea kisa chote. Hapo Imam Ali a.s. aliwaamrisha wasindikizaji wake kumpeleka tena kwa Umar. Walipofika Umar aliwauliza sababu ya kumrudisha, nao walijibu kuwa Imam Ali a.s. ndiye aliyewaambia hivyo kuwa wamrudishe. Na wakati huo Imam Ali a.s. alifika hapo na kumwambia Umar kutaka kwake kutoa uamuzi. Kwa hiyo, Umar alisema: "Vyovyote iwe vile, je ni kipi kitakachokuwa afadhali kuliko haya? Mimi nimemsikia Mtume s.a.w.w. akisema kuwa ilimu yako ni bora kuliko sisi sote." Imam Ali a.s. alimwita yule mwanamke pamoja na mashahidi wake wote. Wao wote mmoja baada ya mwingine walisema vile vile walivyokuwa wamesema mbele ya Umar. Baada ya kuyasikiliza hayo, Imam Ali a.s. aliwaambia jamaa zake mwanamke iwapo wataridhika kuolewa kwa mwanamke huyo, nao wote walikubali. Hapo ndipo Imam Ali a.s. alipomwambia mtumwa wake Qambar alete Dirham 400, na alimwambia yule mwanamke: "Mimi nakuoza wewe kwa huyu kijana kwa mahari ya Dirham 400." Wakati Dirham zilipoletwa alimkabidhi kijana huyo na alimwambia aende na mwanamke huyo na ampatie mahari yake. Wakati yule kijana alipotaka kuondoka, Imam Ali a.s. alisema: "Njoo kwangu tena, kwa sharti la kupitisha usiku mmoja kama bibi na bwana!" Kwa kuyasikia hayo, yule mwanamke akapiga kelele: "Loh! Ewe nduguye Mtume s.a.w.w. wewe unanioza mtoto wangu?" Mwanamke akaomba msamaha na kwa kushika mkono wa mtoto wake, wote waliondoka kwa furaha. Baada ya hao wote kuondoka Bwana Umar alisema: "Lau asingalikuwapo Ali, Umar angalikuwa ameangamia. Tukio hilo pia limeelezwa na Sahab Fazail ibn Shaazan kutokea Waqadi, kutokea Jabir na kutokea Salman kwa wakati, pamoja na tofauti kidogo.
|