Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
(22). UUME NA UKIKE KWA PAMOJA

Al-Hasan bin Ali al-Abdi ameripoti kwa mamlaka ya Sa'ad bin Tarif kwa mamlaka ya al-Asbagh bin Nubata ambaye alisema:

Wakati Shurayh, alipokuwa katika kikao cha kutoa hukumu, mtu mmoja alimwijia akisema: "Abu Umayya, naomba kuongea nawe katika faragha, kwani nahitaji hivyo mno."

Aliwaamrisha wote waondoke, isipokuwa wale waliokuwa washiriki (Khassa) wake tu ndio waliobakia. Ndipo alipomwambia:"Haya sema, unahitaji nini?"

"Abu Umayya," aliyasema huyo mtu, "mimi ninacho kile walichonacho wanaume na kile walichonacho wanawake. Hivyo nataka uamuzi wako iwapo mimi ni mwanamme au mwanamke."

Shurayh alijibu: "Mimi nimewahi kuyasikia hayo kutoka kwa Amirul Muminiin Ali bin Abi Talib a.s. na ninayakumbuka vyema. Hebu uniambie ni kutokea tundu lipi ambalo mkojo wako unatikea?"

"Kutoka katika matundu yote mawili," alijibu yule mtu.

"Huishia tundu lipi?" aliuliza Shurayh.

"Katika matundu yote mawili kwa pamoja." alijibiwa.

Shuray alistaajabishwa. Yule mtu aliongezea kusema:

"Mimi ninakuambia kuhusu tabia zangu za ajabu ambazo zitakustaajabisha kabisa."

"Ehee! Ati tabia zipi hizo?" aliuliza Shurayh.

"Baba yangu alinioza kwa kunichukulia kuwa mimi ni mwanamke. Nami nilishika mimba kwa bwana wangu na nilimnunua kijakazi ili anitunze. Siku moja nilimwingilia huyo kijakazi wangu, naye akashika mimba yangu."

Loh! Shurayh alipiga makofi kwa mshangao mkubwa na alisema: "Swala hili ni lazima lichukuliwe mbele ya Imam Ali a.s. ili alitatue kwani mimi sina Ilimu ya kutoa hukumu yake."

Yeye aliinuka na yule mtu pamoja na wengineo wafuata. Walipomfikia Amirul Muminiin Ali Abi Talib a.s. alimwelezea mambo yote. Imam Ali a.s. alimwita huyo mtu na akamwuliza habari zote alizoelezwa na Shurayh, naye alikiri yote yote hayo.

"Je, mume wako ni nani?" aliuliza:

"Fulani bin fulani," alijibu, "Naye pia yupo hapa mjini."

Huyo mume wake pia aliitea, na baada ya kuelezwa yote hayo, naye pia aliyasadikisha hivyo. "Naam yote ni kweli," alijibu.

"Kwa hakika inakubidi uwe mshupavu kuliko simba unapokutana na hali kama hii." alisema Imam Ali a.s. Hapo alimwita Qambar na kumwambia: "Mchukue mtu huyo katika chumba pamoja na wanawake wanne walio waadilifu na uwaambie wamvue nguo na wazihesabu mifupa ya mbavu zake baada ya kuhakikisha kuwa sehemu zake zimefunikwa. Qambar alisema: "Ewe Amirul Muminiin! Si wanaume au wanawake watakaosalimika naye."

Kwa hiyo, Imam Ali a.s. aliamrisha kuwa afunikwe kwa majani makavu na kuachwa pekee katika chumba. Hapo ndipo alipokwenda chumbani na kuzihesabu mbavu zake. Zilikuwa saba upande wa kushoto na upande wa kulia kulikuwa na nane. Hapo alipobainisha wazi wazi kuwa "Huyu ni mwanamme."

Hapo ndipo Imam Ali a.s. alipoamrisha akatwe nywele zake na amvalishe pamoja na kofia, viatu na joho (rida). Yeye pia alimtenganisha na mume wake.