Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
(4). MTUMWA NA TUHUMA

Imeelezwa na kulaini na Sheikh Sadduq vile vile katika sahihi Bukhari, kwa mamlaka ya Imam Jaafar as-Sadiq a.s. kuwa kijakazi aliletwa mbele ya Bwana Umar kwa mashtaka ya kwenda kinyume na bwana wake.

Kisa chenyewe kilikuwa hivi:-

Mtu mmoja alimtunza binti mmoja yatima. Kwa kuwa alikuwa akienda safari za kikazi kila mara, hivyo alimkabidhi mke wake ili amlee.

Hali hii iliendelea kwa miaka kadhaa na binti yule alikua na kupendeza. Yule mwanamke, akitafuta mbinu za kumzuia mume wake asimwoe kijakazi huyo, alimlewesha, kwa mbinu zake na kwa msaada wa wanawake wenzake na vile vile alithubutu hata kuuharibu ubikira wake.

Bwana yule aliporudi kutoka safari, alimkuta yule kijakazi hayupo na hivyo alimwuliza mke wake kuhusu huyo.

Mwanamke huyo alijibu: "Huyu ametoroka pamoja na kijana wa majirani."

Bwana huyo kwa hasira, alitoka kumtafuta huyo kijakazi, na alipompata, alimburuta hadi mbele ya Umar, allipokuwa Khalifa.

Bwana Umar alipoisikiliza kesi hiyo, aliiona ngumu kuihukumu na hivyo aliielekeza kwa Imam Ali a.s. kwani alikwisha shughulikia kesi kama hizo.

Imam Ali a.s. aliwaagiza Bwana, Bibi, kijakazi na mashahidi wote kuhudhuria mbele yake katika kesi hiyo. Bwana na Bibi walisimulia kisa vile vile walivyofanya mbele ya bwana Umar, na waliwaleta wanawake wanne kwa upande wao wa ushahidi kama vile alivyotaja yule mke wake, dhidi ya mshitakiwa.

Imam Ali a.s. allimwita mwanamke wa kwanza wa upande wa mashtaka na aliuweka upanga baina yake na ya yule, na akasema: "Je wajua, kuwa mimi ni Ali ibn Abi Talib? Na hivyo nakutaka uniambie ukweli na ukweli mtupu na kwamba si chochote kile ila ukweli mtupu."

Kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa mjanja, hivyo alielezea uongo vile vile kama alivyokuwa ameelezea mbele ya Umar, na alisisitizia pia.

Imam Ali a.s. alipoyaona hayo, alisema kuwa huyo atengwe na mashahidi wengine. Baada ya hapo, Ali a.s. alimwita shahidi mwingine, kumwambia: "Je unauona upanga huu? Iwapo hautaniambia ukweli basi nitakukata kichwa chako kwa upanga huu huu . Vile vile kumbuka kuwa huyo mwanamke aliyekutangulia katika kutoa ushahidi, amenielezea yote kwa ukweli na wazi wazi, kwa sababu hiyo, nimemsamehe. "Kwa kusikia hayo na kwa kuhofia maisha yake, alielezea yote kwa ukweli, bila ubishi au uzushi wowote.

Baada ya kusikiliza hayo yaliyo ya ukweli, Imam Ali a.s. alisema: "Baada ya Mtume Daniel, mimi ni mtu wa kwanza katika kulazimisha mshahidi wa tofauti katika mashahidi wawili."

Alitoa hukumu ya adhabu kwa mke wa yule. Na alimwamrisha yule mtu kumpa talaqa mkewe na kumwoa yule kijakazi. Baada ya kutekelezwa kwa hukumu zake, alilipa mahari kutoka mfukoni mwake. Vile vile aliwatoza adhabu ya Dirham mia moja kila mmoja wa mashahidi katika kesi hiyo, na alimpa yule kijakazi Dirham zote hizo.

Baada ya kumalizika kwa maamuzi yaliyo sahihi, Bwana Umar alimshukuru mno Imam Ali a.s. kwa yote hayo na vile vile alimwomba amsimulie masimulizi ya Mtume Daniel a.s.

Imam Ali a.s. kwa ombi hilo, alianza:

"Mtume Daniel alikuwa ni yatima, ambaye alifiwa na wazazi wake wote wawili. Wakati huo kulikuwa na mtawala kutoka Bani Israili, ambaye alikuwa na Qadhi wawili katika Baraza lake. Qadhi wote wawili, walikuwa wakimtembelea mtawala huyo wakiwa pamoja na mcha Mungu mno mmoja katika siku zao.

Siku moja mtawala ikamtokea kazi ya dharura na muhimu kabisa nje ya dola yake, hivyo aliwaomba wale Qadhi wamtafutie mtu mwaminifu mno katika raia wake.

Qadhi wale walimshauri amtume yule yule mcha Mungu ambaye huwa wanakwenda wote kila leo.

Mtawala alimkabidhi kazi hiyo yule mcha mcha Mungu pamoja na maelekezo yote.

Yule mcha Mungu alikuwa na mke mrembo mno na mwenye kupendeza pia, vile vile alikuwa mcha Mungu kama bwana wake. Sasa yule bwana alipokuwa akienda safari hiyo aliyotumwa, aliwaomba Qadhi wale wawili wamtunze mke wake kwa uwema na vyema na kumsaidia iwapo angalihitaji msaada wao. Ndipo alipoondoka.

Siku moja Qadhi hao walifikia nyumbani mwa huyo mcha Mungu, na waliweza kumwona mke wake na vile alivyo. Kwa kumwona huyo mwanamke, wote wawili walighadhalibiwa na shaitani na hivyo walimwashiki.

Wao walimwelezea mwanamke huyo tamaa yao na mwanamke yule mwema, alikataa kata kata. Kwa hayo wao walimtishia kwa kumstaki kwa Mfalme kwa kuzini hivyo angaliuawa kwa kupigwa na mawe.

Katika majibu yake, aliwaambia: ,"semeni chochote kile mukitakacho, lakini mimi kamwe sitakubali uovu huo."

Baada ya hapo, wale Qadhi walimwambia mfalme kuwa mke wa yule mcha Mungu amezini. Kwa hayo, Mfalme alishangaa mno kwa taarifa hiyo kwani alijua luwa mwanamke yule alikuwa mcha Mungu. Alikiinamisha kichwa chake chini, na alipokiinua, aliwaambia:

"Mimi naamini ushahidi wenu lakini nawaombeni munipatie siku tatu kabla sijatoa amri yoyote katika swala hili."

Hapo Mfalme alishauriana na Waziri wake, akimwambia "Mimi sidhani kuwa yeye amezini, je wasemaje?"

Kwa kuyasikia hayo, Waziri pia alistajaabishwa na alimwambia Mfalme: "Mimi pia nimestaajabishwa kwa hayo!"

Siku ya tatu, Waziri huyo alipita mahala ambapo walikuwa wakicheza watoto wadogo, na Mtume Daniel a.s. alikuwa mmoja wa watoto hao.

Kwa kumwona Waziri huyo akipita, Mtume Daniel a.s. alimwambia mmoja wa watoto wenzake: "Njooni sisi tucheze mchezo wa kuigiza - Mchezo wa Qadhi wawili na mke wa mcha Mungu. Wewe utakuwa mke wa mcha Mungu na nyie mutakuwa Qadhi.

Wakati huo Mfalme alikuwa ameshapiga mbiu ya mgambo, kwa kuwaita watu wote kuja kushuhudia kutolewa hukumu ya mwanamke wa Mcha Mungu kunyongwa kwa kuzini kwa mujibu na desturi zao kwani Qadhi wawili waliripoti hivyo.

Mtume Daniel alimwita kijana mmoja ambaye alikuwa akiigiza kama Qadhi, na kumwuliza:- "Je wewe unasemaje kuhusu swala hili?" Yeye pia aliuelekeza upanga wa ubao ulioviringwa katika nguo, "iwapo utasema uongo basi nitakukata kichwa chako kwa upanga huu."

Kijana huyo, kama Qadhi, alimjibu: "Ewe Mfalme! mke wa mcha Mungu huyo amezini, na mimi ninatoa ushahidi wangu kwa hayo."

Hapo Mtume Daniel a.s. alimwuliza: "Wapi na lini na siku gani na wakati gani?"

Kijana huyo aliyejibu maswali yote aliyokuwa ameulizwa na Mtume Daniel a.s. Baadaye, Mtume Daniel a.s. alimwita kijana wa pili, kama Qadhi wa pili, na alimwuliza maswali hayo hayo, lakini majibu yake yalikuwa ni tofauti kabisa.

Baada ya kuyasikia yote hayo, Mtume Daniel a.s. alisema: "Allah Akbar! Nyie mmetoa ushahidi wa uongo na kumsingizia mwanamke mcha Mungu katika kesi hii."

Baada ya hapo alimwachilia yule mwanamke kwa heshima zote na kuwahukumu kifo wale vijana waliocheza kama Qadhi wawili.

Yule Waziri aliutazama kwa makini mno ule mchezo wa watoto wale na uamuzi ulivyotolewa na Mtume Daniel a.s. katika mchezo huo, na aliripoti vyote kwa Mfalme ambaye pia alifuata vile vile ile kesi na akatoa hukumu yake vivyo hivyo."