Ulithibiti Uimamu kwa Imam Husein (a.s.) baada ya kufariki kwa nduguye Al-Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib (a.s.) na hapo ikawa ni faradhi kwa viumbe wote kumtii Imam Husein (a.s.). Na Uimamu wake ulikuwa ni kwa mujibu wa kauli ya baba yake na babu yake (a.s.) na pia usia wa nduguye Imam Hasan (a.s). Imam Hasan na Imam Husein (a.s.) wao ni Mabwana wa vijana wa peponi kwa mujibu wa Mwenyewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye ni babu yao. Miongoni mwa ubora waliokuwa nao Imam Hasan na Imam Husein (a.s.), baada ya kuwa ni wajukuu wa Mtume (s.a.w.) na vipenzi vyake katika watu wa nyumba yake, pia ni miongoni mwa watu aliotokanao kwenda kuapizana na wakristo wa Najran pale iliposhuka aya ya 61 Sura ya Tatu: "Basi watakaokuhoji kuhusu Nabii Issa, baada ya kukufikia ujuzi (wa-jambo hili) basi waambie njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu na wanawake wetu na wanawake wenu na sisi wenyewe na ninyi, kisha tuapizane tuombe laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo". Aya hii inaitwa aya ya Mubahala, na sababu ya kushuka kwake, ni pale viongozi wa Kikristo kutoka Najran walipokuja Madina katika mwaka wa tisa Hijiriya kumjadili Bwana Mtume (s.a.w.) kuhusu Nabii Isa (a.s.) Mtume akawajibu kwamba; "Hakika mfano wa Isa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam". Wakristo hao waliendelea kumjadili Mtume (s.a.w) hata baada ya jibu hili, ndipo Mwenyezi Mungu aliposhusha aya hii ya 61 Sura ya Tatu, Mtume akaambiwa kama wataendelea kumhoji, basi awaambie waje waapizane kama ilivyoashiria aya hiyo. Kutokana na uzito wa suala la kuapizana baina ya Mtume (s.a.w.) na Wakristo hao, ilibidi Bwana Mtume (s.a.w) kwa upande wa Waislamu atoke na watu ambao pia watakuwa na uzito wa kukabili maapizano hayo. Ndipo alipowachukua Hasan na Husein kama wawakilishi wa watoto wa Kiislamu, na Bi Fatma (a.s.) kama muwakilishi upande wa wanawake wa Kiislamu na yeye Mtume (s.a.w.) na Imam Ali (a.s.) wakawa ndiyo nafsi za Waislamu. Kwa mujibu wa uwakilishi wa Imam Hasan na Imam Husein (a.s.) katika tukio hili unadhihiri ubora na utukufu wa vijana hawa wawili ndani ya Uislamu, na inamuwajibikia kila Muislamu kuitambua heshima yao na daraja waliyopewa na Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa Wakristo hao kutoka Najran alivyokiri ubora na utukufu uliomo ndani ya nyumba ya Mtume (s.a.w.) siku hiyo ya mapinzano akasema: Hakika mimi naziona nyuso za watu ambao lau watamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima mahala ulipo atauondoa, hivyo basi musiapizane nao mtaangmia na hatabakia Mkristo yeyote ulimwenguni baada ya leo". Pia miongoni mwa hoja zilizowazi kuhusiana na utukufu walio kuwa nao Imam Hasan na Imam Husein ni kuteremka aya zinazothibitisha kuwa wao ni katika watu watakaoingia Peponi hali ya kuwa bado wakiwa ni vijana wadogo, na jambo hili linapatikana katika Surat Ad-Dahr kuanzia aya ya saba mpaka aya ya kumi na mbili. Kabla ya kuzitaja aya hizo ni bora kukisimulia kisa cha kushuka aya hizo japo kwa mukhtasar. Imepokewa kwa Ibn Abbas kwamba, Hasan na Husein (a.s.) waliugua. Basi Mtume na baadhi ya watu wakenda kuwaona, watu hao wakamwambia Imam Ali (a.s.) "Lau utaweka nadhiri itakuwa bora". Imam Ali, Bi Fatma (a.s.) na Mjakazi wao aliyekuwa akiitwa Fiza, wakaweka nadhiri ya kufunga siku tatu ikiwa Hasan na Husein watapona. Vijana hawa wawili walipona na ikawa kipindi cha kutekeleza ile nadhiri kimefika, lakini ndani ya Nyumba hamkuwa na kitu. Hivyo Imam Ali (a.s.) alikwenda kwa Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa Sham-uun na akakopa vibaba vitatu vya shayiri. Bi Fatma (a.s.) akaisaga shayiri hiyo na akaoka mikate mitano kwa ajili ya kufuturu kulingana na idadi yao katika nyumba yao. Chakula hicho kilipowekwa ili waanze kula, alibisha hodi mgeni na akawatolea salam akasema: "Asalaam Alaikum enyi watu wa Nyumba ya Mtume, mimi ni Masikini wa Kiislamu naomba munipe chakula, nanyi Mwenyezi Mungu atakulisheni chakula cha Peponi". Basi wakamuonea huruma wakampa chakula chote, nao wakanywa maji kisha wakalala. Asubuhi wakaamka na saumu na jioni mwana Fatma aliandaa tena mikate na ilipowekwa tayari kufuturu alibisha hodi yatima na kuomba chakula, wakampa na wao wakanywa maji kisha wakalala. Asubuhi waliamka na saumu, kisha jioni Bi Fatma alioka tena mikate mitano kwa ajili ya kufuturu. Walipoketi kufuturu alibisha hodi mtu aliyekuwa mateka akaomba chakula wakampa mikate yote kisha wakanywa maji wakalala. Kwa ajili ya wao kujinyima kwa muda huo wa siku tatu mfulululizo ndipo ziliposhuka aya zifuatazo katika Sura Ad-Dahr "Wanaotekeleza nadhiri (zao) wanaiogopa siku ambayo shari yake itaenea na wanawalisha chakula masikini na yatima na mateka hali wao pia wanakitaka chakula hicho. (nao husema watoapo chakula hicho) tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani. Hakika tunaogopa kwa Mola wetu siku hiyo yenye taabu na shida. Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha. Na atawalipa kwa kuwapa Bustani (Pepo) na (Mavazi) ya hariri kutokana na kusubiri kwao. Taz. Tafsiri Al- Kashaaf. Zaidi ya hayo ni kwamba Bwana Mtume (s.a.w.) alidhihirisha wazi Uimamu wao kwa Ummah wake pale aliposema: "Wanangu hawa (Hasan na Husein) ni Maimamu wawe wima au wawe wamekaa". Mlolongo wa uimamu wa Maimamu wetu umekuja kwa kila mmoja kumbainisha atakayechukua nafasi ya Imam anayeondoka. Na jambo hili Ia kubainisha Imamu anayefuata IiIianzia kwa mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.) kumbainisha Imam Ali (a.s.) katika bonde Ia Khum pale alipokuwa akitoka katika Hija ya mwisho. (Mwenye kutaka ziada kuhusu jambo la Uimamu wa Ali bin Abi Talib (a.s.) atizame vitabu vya hadithi za Mtume na vitabu vya Historia vinavyotegemewa usahihi wake atalikuta liko wazi). Naye Imam Ali (a.s) alimbainisha Imam Hasan kuwa ndiye atakaye chukua nafasi yake, naye Imam Hasan alimbainisha nduguye Husein (a.s.) kuwa ndiyo Imam wa haki baada yake. Lakini kwa bahati mbaya sana siyo Imam Ali wala Imam Hasan na Husein (a.s.) aliyepata fursa ya kuongoza Ummah kama ilivyotarajiwa. Na hii ilitokana na hali iliyowasibu watukufu hawa baada ya Mtume kuondoka. Tukimuangalia Imam Husein unakuta matatizo yaliyomkuta ni kama yale yaliyomkuta baba yake hata akasema lmamu Ali kama ifuatavyo: "Nikawa nafikiri baina ya kuwa niupate (Ukhalifa) kwa kuuvuta kwa nguvu au nivumilie uvumilivu wa vipofu wasiojua kitu" Mpaka alifikia kusema, "Basi nikaamua kuvumilia hali ya kuwa jichoni mwangu mna mchanga, na katika koo langu mna dukuduku, nauona urithi wangu umechukuliwa kwa nguvu". Kwa mwendo kama huu, ndivyo alivyofanya Imam Hasan (a.s.) katika siku za uhasama wa Bani Umayya, pindi Mu'awiya bin Abi Sufiyan alipotwaa madaraka ya Ukhalifa kwa nguvu. Lakini ifahamike wazi sera ya Maimamu wetu kuwa ni sera ya Mtume (s.a.w.) kwani taabu ilimpata Mtume mwanzo wa kubashiria Uislamu, hakupata utulivu kila alipokuwa akiwaita watu kwenye Uislamu. Kwa hiyo hali ya Mawasii wake baada yake ni kama ilivyokuwa kwake Mtume (s.a.w.) hasa itakapokumbukwa kwamba, Maquraishi walipata kumtenga Bwana Mtume (s.a.w.) na baadaye akalazimika kujificha pangoni wakati akihama Makkah kwenda Madina. Hali ya matatizo na usumbufu, kama ilivyowapata Manabii ndivyo ilivyokuwa kwa Maimamu. Muawiyyah bin Abi Sufiyani alipofariki na hali ya vita ikawa imemalizika, hali ambayo ilikuwa ikimzuia Imam Husein (a.s.) kujitangaza Uimamu wake wazi wazi, kipindi hiki walitokea watu wa kumsaidia Imam Husein (a.s.) katika kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu, Imam Husein (a.s.) alisimama na kujiandaa kufikisha na kusimamia Dini ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Ili kuanza utekelezaji wa kazi hii, ilimbidi Imam Husein asafiri kutoka Madina kwenda Makkah na hatimaye aelekee Iraq kutokana na wito wa watu wa Al-Kufa waliomtaka aende huko ili akawasaidie na kuwaokoa dhidi ya watawala dhalimu. Kabla yeye Imam Husein (a.s.) kuelekea huko, alimtanguliza Ibn ammi yake Bwana Muslim Bin Aqiil ili akaanze kuwalingania Dini ya Mwenyezi Mungu na kuchukua kwao baia (kiapo cha utii) kwa niaba ya Imamu Husein (a.s.) kwamba watakuwa naye katika Jihadi ya kutetea neno Ia Mwenyezi Mungu, na kuiokoa Dini na Waislamu kutokana na wanafiki waliokuwa wamewakalia Waislainu kwa mabavu. Muslim Bin Aqiil alipofika huko, watu hao walimpokea na kumuahidi kumsaidia. Lakini haukupita muda mrefu watu hao wakatangua kiapo chao kwa Muslim Bin Aqiil na wakamuacha akauawa mbele yao kifo cha dhulma akiwa ugenini, lakini pia alikufa akiwa ni shahidi. Na wao hao hao waliomuita Imam Husein wakatoka hapo Al-Kufa kumfuata Imam Husein kwenda kumpiga vita, na wakamtendea mambo ambayo hawakuyatenda Khawarij (Kundi lililomuasi Imamu Ali (a. s.). Wahinsonga Imam Husein (a.s.), wakamzuia asirudi Makkah wala Madina, wakaweka vizuizi baina yake na maji ya mto Furat mpaka wakamuua hali akiwa na kiu, na wakamdhulumu hali akiwa katika Jihadi, mwenye subira akitaraji radhi za Mola wake. Hakika ilitenguliwa baia yake na heshima yake ilivunjwa na wala ahadi alizoahidiwa hazikutekelezwa na wakapora mali zake, wakawashika mateka familia yake, wakakidhulumu kizazi cha Mtume (s.a.w.) hali ya kuwa kimekosa ni mahali gani kitakwenda, njia zote zimefungua. Kizazi cha Mtume (s.a.w.) kikawa na huzuni isiyokifani.
|