Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
Ya Husaini Bin Ali

  1. Kwajina lako Jalali nasema yenye ukweli

  2. Ya Husaini Bin Ali niwe nikihadithia

  3. Mama yake ni Fatima, na babu yake Hashima

  4. Na Madina mji mwema, ndiko aliko zaliwa

  5. Na Sayidi na Husain, kaka yake ni Hasan

  6. Akiwapenda amini, kisha akiwa sifia

  7. Mtume amebaini, ya kama huyu Husaini

  8. Na mwingine ni Hasani, Peponi wataingia

  9. Yaani wao ni mabwana, wa peponi vijana

  10. Subhana maulana, wote amewaridhia

  11. Ni mwezi wa Shabani, alozaliwa Husain

  12. Na siku yake yakini, ni jumanne sikia

  13. Mwaka wa nne Hijira, Ndio kazawa mbora

  14. Na siku ya saba mara, kamwakikiya Nabia

  15. Mtume kamwadhinia, sikioni Ia kulia

  16. Kinywa kamsugulia, kwa mate alafunua

  17. AIikuwa ni mzuri, wa umbo la kunawili

  18. Sura kama ya Bashiri, kwani kamshabihia

  19. Akipigania dini, kwa udhati moyoni

  20. Hajali nini na nini, ila dini ya jalia

  21. Husaini akiwa Maka, aliupata waraka

  22. Kuwa aende haraka, Iraqi kum-baiya

  23. Watu wangu simameni, Twende Iraqi mjini

  24. Aliwambia Husseini, Nao wakafuatia

  25. Husseini aliambiwa, Huko acha kuendea

  26. Twakusihi kusikia, Huko hapatakufaa

  27. Abdallah wa Abasi, Kasema kinga nafusi

  28. Zao japo wafuasi, Japo na watoto pia

  29. Wende wewe peke yako, Sio na ahali zako

  30. Bwana kwa hisani yako, Shika ninayo kwambia

  31. Bwana Husseini kasema, Kwenda huko ni lazima

  32. Litalonipata nijema, Mimi nimesafi nia

  33. Nikenda wakiniuwa, Peponi nitaingia

  34. Kwani nimesafi nia, Dini kuisimamia

  35. Liwalo lote na liwe, Iraqi ni paendewe

  36. Sio mimi niofie Niache kupaendea

  37. Hapo Seyyidi Husseini, Katoka Makka mjini

  38. Na watu wake sabini, Wote wakamfatia

  39. Wenye farasi yakini, Walikuwa thalathini

  40. Wengine arubaini, Kwa miguu ilikuwa

  41. Alipokuwa njiani, Wakazidi yakini

  42. Mia moja khamsini, Ndio waliozidiya

  43. Hao miya khamsini, Walirudia njiani

  44. Hawakumfata Husain, Hadi Iraqi sikiya

  45. Husseini na watu wake, Ni Iraqi Wapafike

  46. Na taabu iwafike, Kwa humo Karbala

  47. Mto ulio karibu, Nae Husseini Muhubi

  48. Alizuiwa ajabu, Na maadui kutumia

  49. Maji wakazuiliwa, Wasiwe wayatumia

  50. Kambi akajipigia, Bwana Husseini sikia

  51. Akawa maji anyimwa, Huku kiu Chawauma

  52. Watoto wanalalama, Kwa vile wanaumia

  53. Husseini na watu wake, Ati wao wateseka

  54. Na maji yasitumike, Kunywewa na watu hawa

  55. Hapo Husseini hakika, Vikali aliteseka

  56. Watoto walalamika, Baba! Baba! twaumia

  57. Jeshi hilo lilikuwa, Kabisa lamzuia

  58. Husseini kukaribia, Maji yale kutumia

  59. Watoto waliumia, Kwa kiu kuwazidia

  60. Kati yao alikuwa, Mtoto mdogo pia

  61. Mtoto huyu ni Ali, Alizidiwa kikweli

  62. Zeinabu binti Ali, Sanasana alilia

  63. Machozi yalimtoka, Mengi yakatiririka

  64. Akayafonza hakika, Mtoto kujimezeya

  65. Zeinabu binti Ali, Ni shangazi lake Ali

  66. Kwa ala kulihali, Machozi maji yakawa

  67. Hata ile siku ya ashura, Kwa mwezi kumi dhahira

  68. Muharamu ndio mara, Wakaanza kuuwawa

  69. Kwanza wafuasi wake, Kisha wa nyumbani kwake

  70. Alibaki ye na chake, Kijitoto kikilia

  71. Umri miezi sita, Hivyo hanavyo matata

  72. Hivyo maji angepata, Yangali msaidia

  73. Mtoto mchanga yule, Wakampiga mishale

  74. Na mtoto pale pale, Aliiaga dunia

  75. Kisha wakamzunguka, Husseini mwenye baraka

  76. Wakamuuwa hakika, Nae kaaga dunia

  77. Baada ya kumuuwa, Hema moto walitia

  78. Hata wakawachukua, Banati zake Nabiya

  79. Wakawafanya mateka, Kisha wakawapeleka

  80. Huko Kufa kupafika, Bila kuwahurumia

  81. Ni kwa Ibni Ziyadi, Ndiko iliko wabidi

  82. Gavana wake Yazidi, Yeye ndie alikiuwa

  83. Hivyo watu wa Iraqi, Walikataa haki

  84. Kumuuwa mwenye haki, Kipenzi chake Nabia

  85. Kuuwawa kwa Husseini, Ni jambo lenye huzuni

  86. Katu haiwezekani, Machozi kuyazuia

  87. Machozi shuti kutoka, Na watu kuhuzunika

  88. Kwa kipenzi msifika, Kinyume alofanyiwa

  89. Ewe Seyyidi Husseini, Ulotoka duniani

  90. Kwa kupigania dini, Peponi wenda ingia

  91. Umekufa ni shahidi, Hivyo ni kama zawadi

  92. Allahu Mola wadudi, Shahidi kakwandikia

  93. Waswalatu wa Salamu, Zimfikie Hashimu

  94. Na Husseini Muadhamu, Na walio bakiya

    Na: Saidi Musa
    ZANZIBAR

     

    ALLAMAH SAYYID SAEED AKHTAR RIZVI ASEMA:

    Imam Hassan na Imam
    Husain (a.s.) wameuhurisha
    Uislamu kutokana na utumwa wa
    Wafalme na hivyo basi, wameuhifadhi
    kutokana na uharibifu daima. Wafalme
    watakuja, na Wafalme watakwenda,
    lakini Uislamu utadumu milele. Kwa
    Uislamu, majina matakatifu ya Hassan
    na Husain yataangaza milele.