Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
Machozi yamiminika

Kwa Jina Ia Rahmani

Na Muhammad Amini

Na Anza nudhumuhini

Kwa Machungu na Kuliya

   

Siku hizi za Ashura

Twazitaja kila mara

Kwa kubwa mno hasara

Maadui walotiya

   

Kiswache cha tuumiza

Na roho kutuunguza

Hatuwezi kunyamaza

Mashingo kuvumiliya

   

Twadhihirisha Majonzi

Kwa Imamu na kipenzi

Na nyoyo zina simanzi

Kwa haya yalotokea

   

Twakumbuka siku hini

Ya vilio na huzuni

Ya kuuwawa Huseini

Mjukuu wa Nabiya

   

Wallahi Tunakatika

Machozi ya miminika

Mitilizi inashuka

Hatuna budi kuliya

   

Huseini kudhulumiwa

Kwa machungu kuuliwa

Kanyimwa maji kupewa

Yeye na wake dhuriya

   

Hata watoto wachanga

Wasibali kuwanyonga

Kwa mishale kuwadunga

Na maji kuwazuwiya

   

Wakamchinja Huseini

Bila kite na imani

Mjukuu wa Amini

Pasina kuzingatiya

   

Na kicha kukitundika

Kwa shangwe wakizunguka

Kwa mizozo na dhihaka

Kwa kipenzi cha Nabiya

   

Tuliye kiliyo gani

Tudhihirishe Imani

Kwa kiongozi wa dini

Huyu walo tuuliya

   

Walomuuwa Imamu

Wakashika yake damu

Hao ndio madhalimu

Tarikhi inatwambiya

   

Bila shaka yupeponi

Yeye na tumwa Amini

Owe nao makhaini

Huseini kutuuliya

   

Kula alo muumini

Atajawa na huzuni

Kwa kifo chake Huseini

Kipenzi cha Hashimiya

   

Na mengi tukiyaeleza

Maovu ya kuchukiza

Ya akili kushangaza

Na moyo kutosheya

   

Tumefika kikomoni

Tushukuru Manani

Atupe nyingi Imani

Ya dini kusimamiya

   

Muliyoko Hadhirani

Amina kikieni

Rabi atiye auni

Dini kuipiganiya

 

Umetungwa na:

Sheikh Ahmed Sheikh Nabhany
P.O. Box 86876
Mombasa, Kenya