Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
MAADILI YAKE

Maisha yake yalikuwa ni yale ya wenzake wa Ukoo wa Mtukufu Mtume (s.a.w.). Alikuwa wa pekee katika upole ustahimilivu, ukarimu, uvumilivu, huruma na Kumuabudu Mungu kwake kulifanyika kiasi ambacho, hata wakati alipokuwa kafungwa katika kizuizi kikali sana kila Mu'tamad alipoulizia habari zake, aliambiwa kuwa Imamu alikuwa aki funga mchana na usiku kucha akisali na alikuwa hasemi neno ila maneno ya ibada tu.

Ingawaje Imamu (a.s.) alikuwa na uhuru mdogo sana hata hivyo ilipowezekana watu walikwenda kumwona na kutoa hamu yao ya kujifunza na walirudi wakiwa wametosheka kabisa.

Maadili yake na tabia zake viliwavutia watu wote. Bwana Ahmad bin Khazan aliyekuwa mwangalizi mkuu wa zaka, khums, sadaka, n.k., katika Mji wa Qum (nchini Iran), kila walipotajwa mbele yake Masayyid wa Alawi (wa ukoo wa Ali a.s.), alisema kuwa alikuwa hajapata kuona mtu mwingine mwenye tabia nzuri kama za Imamu Hasan Askari (a.s.) au Mchamungu na mwenye kumwabudu Mungu, mpole, anayeheshimiwa,mwenye kustahili heshima au anayefikiriwa kuwa yu astahili kuheshimiwa sana.

Alipofariki Imamu Ali Naqi na watu wote walipokuwa wakishughulika na mipango ya maziko yake, baadhi ya watumishi wa nyumbani waliiba vitu kadhaa. Walikuwa hawakufikiria kuwa labda Imamu angejua yote hayo.Shughuli za maziko zilipomalizika aliwaita wote wale waliohusika na kuwaambia kuwa kama wakimwambia ukweli atawasamehe kwa yale yote waliyoyatenda, la sivyo watavirudisha vile vitu walivyoviiba na atawaadhibu. Kisha akavitaja vile vitu vyote kila mmoja wao alivyoiba na walipokubali aliwasamehe.