Watu wa Ukoo wa Bani Abbas walikataa tangazo la Mfalme kumteua Imamu Ali Ridha [a] kuwa mrithi wake wa kiti cha Ufalme. Lakini walirithishwa kidogo na kuuawa kwa Imamu [a] kwa sumu. Hivyo basi walimlazimisha Mamun atangaze kuteuliwa kwa ndugu yake Mu'tamin kuwa mrithi wa kiti cha enzi. Zaidi ya hapo yale majoho meusi waliyokuwa wakiyavaa watu wa ukoo wa Bani Abbas yaliyokomeshwa na badala yake kutumiwa majoho ya kijani kama alivyoshauri Imamu Ridha [a] yalianza kutumika tena. Mambo haya yote yaliwahakikishia watu kimawazo, lakini sasa uamuzi wake wa kumuoza binti wake kwa Imamu Muhammad Taqi [a], uliwakasirisha tena hivyo walingojea kuonyesha kutoridhika kwao na uamuzi wa Mamun kwamba mtoto mdogo apendelewe badala ya wanavyuoni wakuu wa zama hizo, na katika azima ya kutaka kumuoza binti wake kwa mtoto huyo (Imamu Taqi [a] ambapo ndoa kati ya dada yake na baba wa Imamu huyo haikutoa matokeo mazuri. Mamun aliwajibu kuwa, ingawa yu mdogo kwa umri, Imamu Muhammad Taqi [a] alikuwa mrithi wa kweli wa baba yake na hakika alikuwa na elimu zaidi kuliko wanavyuoni wote na kama wana wasiwasi na jambo hili wanaruhusiwa kumleta mtu yeyote na kujadiliana naye na wataamini kuwa ni kweli. Walikwenda kumshawishi mmoja wa wanavyuoni mashuhuri wa Baghdad aitwaye Yahya bin Aksam kuja kujadiliana na Imamu [a]. Mamun alitayarisha mkutano mkubwa kwa ajili ya majadiliano hayo na watu wengi walialikwa. Kila mtu alikuwa na hamu ya kuona pambano hilo kati ya mtoto mdogo wa umri wa miaka tisa na mwanachuoni mwenye ujuzi wa siku nyingi na pia aliyekuwa kadhi mkuu wa nchi. Wanahistoria wameandika kuwa, achilia mbali wakuu wa baraza la Mfalme Mamun, viti mia tisa viliwekwa kwa ajili ya wanavyuoni. Mamun aliweka kiti karibu naye kwa ajili ya lmamu [a] na kiti kingine mbele yake kwa ajili ya Yahya. Palikuwa kimya kabisa na mara Yahya alianza kusema kwa kuomba ruhusa ya Mfalme amuulize swali Imamu [a]. Mamun alimwambia Yahya aombe ruhusa kwa Imamu mwenyewe. Hapo alimgeukia Imamu na kumwomba ruhusa ya kumuuliza swali. Imamu [a] alimruhusu. Yahya aliuliza "Kama mtu akiwinda hali ya kuwa yu katika Hijah, Kafara yake ni nini? Swali hili lilionyesha kwamba Yahya alikuwa hajui kiasi cha elimu ya Imamu [a]. Katika kumjibu Yahya, Imamu [a] alilifafanua swali hilo katika kila uwezekano wake kwa utaratibu na uangalifu wa kitaalam mpaka wasikilizaji pamoja na Yahya mwenyewe waliweza kuielewa elimu ya Imamu kabla swali hilo halijajibiwa. Imamu [a] akasema, "Swali lako halieleweki. Ungelisema kama kitendo hicho kilitendwa ndani ya mipaka mitakatifu ya Kaabah au nje yake; kama mtu yule alifanya kitendo hicho akiwa anazijua sheria za jambo hilo au Ia; kama alimwua mnyama huyo makusudi au kwa bahati mbaya tu; kama mtu yule alikuwa mungwana au mtumwa, mtu mzima au mtoto; kama ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo au vipi; kama aliua ndege au kwa kufanya hivyo au la; kama alifanya kitendo hicho usiku; au kwa siri au mchana na kama alikuwa anakwenda "Hajj" au "Umrah". Haiwezekani kutoa jibu kamili kwa swali hili mpaka mambo hayo yamefafanuliwa vizuri kwa sababu kafara ya kila kosa kati ya hayo itakuwa tofauti". Yahya hakuwa na la kusema, hakujitayarisha ujibu maswali ya kiuchunguzi namna hiyo. Alama za kufadhaika zilionekana usoni mwake. Mamun alipoona hivyo, aliona kuwa ingelikuwa vema kumuomba Imamu [a], "Ni vizuri uyaeleze wewe mwenyewe yote haya. Na hapo Imamu [a] alieleza kwa kirefu na kwa makini mambo yote aliyoyasema. Mamun sasa alitaka kufanya vichekesho kutokana na ujinga wa Yahya. Hivyo alimgeukia Imamu na kumwambia, "Sasa mwuulize Yahya swali lolote lile". Imamu alimgeukia Yahya na kuuliza. "Naomba nikuulize swali". Yahya sasa alikwishaelewa wazi kuhusu tofauti baina ya ujuzi wake na wa Imamu [a], hivyo hakuwa na wasiwasi wa kujidanganya. Hivyo alijibu, "Ndiyo Bwana, kama nikiweza kulijibu swali lako nitalijibu la sivyo nitakuomba kulielezea". Ndipo Imamu [a] alipomuuliza Yahya swali na mara moja Yahya alikiri kutoweza kwake kulijibu. Na Imamu akalielezea. Kisha Mamun akaanza kuwatangazia wale watu waliokuwepo akasema, "Sasa mmeona kuwa sikukosea niliposema kuwa ukoo huu unaelimishwa na Mwenyezi Mungu na hakuna mtu awezaye kuzungumza hata na watoto wao." Waliokuwepo wote walikubali ukweli wa jambo hilo. Mamun alimuoza binti wake kwa Imamu [a] pale pale. Imamu [a] alitoa hotuba ambayo husomwa katika 'Nikah' (kusoma kanuni zilizowekwa na zilizothibitishwa kuonyesha maafikiano ya ndoa kati ya mume na mke) ya Waislamu. Mamun alionyesha ukarimu mkubwa siku hiyo na aligawa kiasi kikubwa cha pesa kwa raia wake.
|