Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu Surah An-Nahl 16, Ayah ya 105: 'Wanaozua uwongo hawana imani' Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema : "Mtu mwovu kabisa ni yule ambaye ni msema uwongo." Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema : "Allah swt humlaani mwongo hata kama atasema ukweli" Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema : "Ugonjwa wa kusema uwongo ndio ugonjwa mbaya kabisa." Amesema al-Imam Musa ibn Ja'afar a.s. : "Mtu mwenye busara kamwe hawezi kusema uwongo hata kwa matamanio yake mwenyewe." Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema : "Itakuwa vyema kwa Waislamu iwapo hawatafanya urafiki na udugu pamoja na Mwongo." Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Al-Kafi, j.2: "Uwongo unateketeza misingi ya Imani." Mwanadamu ameumbwa kwa maumbile ya ukweli na uaminifu. Iwapo yeye ataweza kudumisha maumbile hayo bila ya kushawishiwa na vitu vya nje na mambo yanayomvutia, basi daima atasonga mbele katika uwema na utakatifu, na kuepukana na maovu na machafu. Mwanadamu kimaumbile ni mkweli, mwaminifu, mtukuzwa na mwadilifu. Lakini kuna mambo kama elimu, mazingira n.k. zinaweza kuathiri sifa hizi na kuzibadilisha kwa maovu. Mojawapo ya muhimu wa umisionari wa Mitume a.s. ilikuwa ni kusaidia maumbile ya mwanadamu dhidi ya misukumo ya nje ili kwa kutokana na mafunzo yao wao waweze kuimarisha na kuifanya madhubuti uwezo wao walionao ili waimarishe sifa njema walizonazo za kitukufu. Uwongo ni kinyume na maumbile ya kibinadamu na hivyo humvuta mbali na uaminifu na kuna uwezekano kuwa mwongo na mwovu, na inaweza kuwa ni kama ugonjwa ulioambukizwa na kuenea kutoka kwa baba hadi vizazi yake, kutoka mwalimu kwa wanafunzi wake, kutoka mnunuzi kwa muuzaji na kuendelea, na hivyo kuigeuza maumbile kutoka vile ilivyokuwa imeumbwa. Wengi wanachukulia uwongo kama hafifu na isiyo na umuhimu, ambapo hasara inayopatikana kutokana na uwongo haiwezi kamwe kulinganishwa na dhambi lolote lile na ni hatari kwa jumuiya ya watu kwa maovu yanayotokana na uwongo ambayo ni mengi kupita kiasi, kiasi kisichoweza kuhesabiwa. Mara nyingi imetokea kuwa mwongo na mzushi, kwa ajili ya kutaka kujichomeka, wamedai utume na kwa uwongo tu wamekuwa wakiwapotosha maelfu ya watu kutoka haki na kuwaingiza katika upotofu na maangamizo. Au mzushi mwingine amedai Ubabi na wngineo kama hao, na hivyo kuwapotosha watu kwa wingi. Je madhambi haya yanaweza kulinganishwa na madhambi mengine au hasara zinazopatikana kulinganishwa na hasara na maafa mengine ? Ndiyo maana Dini ya Islam inawakana sana watu waongo na Qur'an Tukufu inasema waziwazi katika Surah An-Nahl 16, Ayah 105 : ''Wanaozua uwongo hawana imani" Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema , Amali cha As-Sadduq, uk. 193 : "Hakuna kilicho ovu na kibaya kabisa kuliko uwongo." Kwa kuona kuwa uwongo unadhalilisha Dini, amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Al-Kafi, j.2 : "Uwongo unaharibu misingi ya Dini." Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. anaamini kuwa kuuelewa ukweli wa imani ni kule kutokomezwa kwa uwongo wa kila aina, na anasema, katika Muhasin ya Barqi : "Mtu hawezi kujipatia ukweli wa Imani hadi hapo aachilie mbali uwongo, ama uwe wa kweli au mzaha." Ipo riwaya moja katika Wasa'il al-Shiah , j.3 izungumziayo kuwa Aaliulizwa Mtume Muhammad s.a.w.w. "Je inawezekana kwa mtu mwenye imani akawa mwoga ?" Naye alijibu : "Naam !" Nao walimwuliza tena : "Je inawezakana akawa na husuda ?" Naye akajibu, "Naam !" Nao wakamwuliza, "Je inawezekana akawa mwongo ? Naye akajibu "Haiwezekani kamwe !" Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema katika Bihar al- Anwar, j.72, uk.259 "Neno lililo baya na chafu kabisa ni uwongo" Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Khasail cha Sadduq : "Tabia ya kusema uwongo kunaleta ufukara na majuto." Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema Al-Makasib : "Ninawaonyeni nyinyi dhidi ya dhambi kubwa kuliko madhambi mengine, yaani, ukafiri, kutotendea wema na kuwa bughudhi wazazi na kusema uwongo." Mwanasaikolojia maarufu anasema, Samuel Smiles, Ethics, uk. 281 : "Katika maovu yote ambayo inahitaji kushutumiwa vikali ni uwongo ambayo ndiyo ovu na mbaya kabisa. Tabia hii mbaya inatokana na kuoza kwa maadili na maovu au kwa udhaifu na uwoga. Ni jambo la kustaajabisha kabisa kuwa watu wanaliangalia swala hili kwa dharau na tofauti kiasi kwamba wao hata huwafunza wafanyakazi wao mafunzo ya usemaji uwongo na ulaghai. Hivyo wao kamwe wasishangae wala kuhamaki iwapo wafanyakazi hao hao watawadanganya na kuwalaghai wao wenyewe." Al - Imam Muhammad al-Baqir a.s. anasadiki kuwa uwongo ndio ufunguo wa kila ain ya uchafu, na anasema , katika Al-Mustadrak, j.2 : "Madhambi yote na kila aina ya uchafu vimekusanyikana katika nyumba moja, na ufunguo wake ni uwongo." Hivyo inamaanisha kuwa kusema uwongo na kuchafuliwa nayo ndiko njia kwa ajili uchafuzi wa kila aina ya ubaya. Katika Islam, usemaji wa uwongo tu haujaharamishwa bali hata kufunga urafiki na ushirikiano pamoja na waongo pia umeharamishwa. Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. akimpa nasiha mwana wake al-Imam Hassan ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. alimwambia, katika Nahjul Balagha,Faizul Islam, j.6 : "Ewe Mwanangu !Jiepushe na urafiki wa mpumbavu; kwani ingawaje yeye anaweza kukufaidisha lakini yeye hawezi kutofautisha baina ya faida na hasara, na hivyo atakuingiza katika hasara. Vile vile jiepushe na urafiki wa mlaghai, kwa kutokana na ulaghai wake, yeye daima atakunyima kile unachokihitaji sana. Vile vile jiepushe na urafiki wa msingiziaji au mchongezi, kwani yeye ataweza kukuzuli amambo yake kwa urahisi. Na vile vile jiepushe na urafiki wa mtu ambaye anayotabia mbovu yaani kusema uwongo, kwani yeye ni kama mazuazua [1] anakudanganyia wewe kwa kudhani kuwa kitu cha mbali kuwa karibu nawe, na kile kilicho karibu nawe kuwa mbali. Kimatokeo, yeye anakuweka mbali ili usiweze kufikia malengo yako. Katika maneno mengine, yeye pamoja na uwongo wake, anakuonyesha kile kilicho rahisi kuwa kigumu, na kile kilichokuwa kigumu kuwa rahisi, na hivyo kukuhadaa na kukuzuia wewe usifikie malengo yako." Kama vile ilivyokuwa uwongo unavyomchafua mtu kwa madhambi mbalimbali, vivyo hivyo kuacha kwa kusema uwongo na kufanya Tawba basi itarudisha na kudumisha usalama wa mtu dhidi ya madhambi mengi sana. Imepokelewa riwaya kutoka Mustadrak - al-Wasail kuwa mtu mmoja alimwendea Mtume Muhammad s.a.w.w. na kusema : "Mimi huwa ninasali, lakini nimechafuliwa kwa uwongo na zinaa, na hivyo ninataka kutakasika kwa dhambi mojawapo kati ya mawili. Hivyo ni dhambi gani nilifanyie Tawba ?" Kwa kuyasikia hayo, Mtume Muhammad s.a.w.w. alimjibu: "Fanya Tawba ya kuacha kusema uwongo !" Mtu huyo aliikubalia amri ya Mtume Muhammad s.a.w.w. ya kufanya Tawba na kamwe hatasema uwongo. Na yeye kwa kweli aliacha dhambi moja kati ya mawili la kusema uwongo, lakini tawba hii ilimfanya awe mwangalifu wa kutenda madhambi mengine kwani alipotaka kutenda dhambi la kuzini, aliwaza: "Iwapo Mtume Muhammad s.a.w.w. ataniuliza iwapo mimi nimezini baada ya kula kiapo cha kutosema uwongo, bila shaka nitamjibu 'la sikuzini' wakati nimezini, hivyo nitakuwa nimesema uwongo ambavyo ni kinyume na ahadi niliyokula kiapo. Na iwapo nitamjibu 'Naam nimezini' basi nitakuwa nimekiri kuzini na nitakuwa nimejitolea kuwa mustahiki wa kuadhibiwa Shariah za Dini." Fikara kama hizi zilikuwa zikimjia kila mara alipotaka kutenda dhambi na hivyo kwa hakika kufanya kwake Tawba kwa kutosema uwongo ulimzuia na kumsaidia asitende madhambi kuanzia siku hiyo, hivyo alijiokoa kutoka Moto wa Jahannam. Hapa ninaomba tuzingatie swala moja kuwa kama vile ilivyokwisha semwa, uwongo unao kasoro za kiakili, na ili kuwaponyesha waongo, ni lazima kujua sababu za ugonjwa huu, na ndipo tuweze kuutibu, kwani bila ya uchunguzi, ugonjwa hautaweza kutambuliwa na hivyo hautatibiwa. Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, Mustadrak al-Wasail, j. 2: "Msema uwongo haingii katika uwongo isipokuwa kwa udhilifu na kujiona duni ambavyo anahisi undani mwake." Kwa sababu hizo, utafiti mdogo wa mwongo unapambanua ukweli kuwa udhaifu wa akili, kutofaa, kuwa chini na masuala kama hayo ya kiakili ndizo sababu zake. Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, Ihtisas, uk.232 : "Mwongo ni mtu aliyekosa adabu." Mtu ambaye anahima ya kutojichafua kamwe kwa kusema uwongo. Kwa hakika mtu ambaye anasema uwongo ni dhaifu na asiyefaa kwake mwenyewe. Kwa hakika, tunaweza kusema kuwa uwongo ni kambi ya mpumbavu na mtu asiyefaa. Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Ghura al-Hukam : "Iwapo vitu vitagawanywa katika makundi kwa mujibu wa asili yao, ukweli unasimama kidete kwa uwezo na uwongo kwa uoga." Mwanasaikolojia anasema : "Kusema uwongo ni silaha kubwa ya udhaifu, na ni njia moja ya haraka ya kuondoa hatari kwa muda mfupi. Kwa sababu hii, udanganyifu umekuwa ni jambo la kawaida miongoni mwa tabaka la watu wenye rangi ambao daima wamekumbwa na ubaguzi wa rangi wa weupe na shinikizo na ambao wanahisi nguvu na uwezo wa kundi hili. Katika baadhi ya hali, usemaji uwongo si kitu kingine isipokuwa ni udhaifu. Wakati sisi tunapomwambia mtoto : 'Je ni wewe umechukua hizi pipi ?' au 'Je ni wewe uliyeivunja hii chupa ?' iwapo yeye atahisi kuwa kwa kukiri ataadhibiwa na kushutumiwa vikali, basi ile hisia ya kujikinga na kujinusuru itamfanya yeye akane kuwa hakufanya hivyo. Wajibu wa kwanza wa waalimu na wazazi kwa watoto ,kwa ujumla, ni kutokuwadanganya na wala kutokuwapa ahadi za uwongo zisizotimizwa. Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Al-Kafi, j. 2 : "Allah swt amrehemu yule baba ambaye anamsaidia watoto wake wawe watoto-wazuri kwake yeye Mwulizaji aliuliza : "Je anawezaje kuwasaidia watoto wake ?". Mtume s.a.w.w. alimjibu nasiha nne: "Kwanza ,inambidi atilie maanani uwezo wa watoto wake na wakubali kazi alizozifanya kwa mujibu wa uwezo wao. Pili, Asiwashurutishie jambo ambalo lipo nje ya uwezo wao. Tatu, kamwe asimlazimishe kuingia katika upinzani au kutenda kosa. Nne, yeye kamwe asimwambie uwongo wala kutenda mambo ya kipumbavu mbele yake." Mojawapo ya sababu ya watoto kushurutishwa kusema uwongo ni kutokana na kubebeshwa mzigo mzito juu yao na kutegemea mambo na kubwa kutoka kwao hata kama itakuwa ni nje ya uwezo wao. Ukali wa wazazi juu ya watoto wao na mategemeo makubwa ambayo yapo nje ya uwezo wa watoto, ndivyo vinavyowalazimisha wao kusema uwongo, na hivyo kunamaanisha kuwa wazazi ndio wazinduzi na waanzilishi wa uovu huu katika watoto. Betrand Rusell anasema: "Uwezekano wa kusema uwongo unakuwa hauingii katika akili ya mtoto. Lakini uwezo huu unaingizwa akilini mwake vile wakati unavyokwenda. Yeye anayashuhudia hayo kwa wakubwa na hofu ndiyo inayomfanya kuyachukua hayo. Mtoto anavumbua kuwa wakubwa wanamdanganya na kusema uwongo waziwazi, naye anaona iwapo watawaambia ukweli, basi kutamletea hatari yeye. Hivyo kimatokeo, yeye anakuwa tayari kusema uwongo. Hivyo iwapo wewe utajiepusha na vichangio na viambatanisho kama hivyo, basi mtoto kamwe hatasema uwongo." (juu ya Elimu, uk. 146) Raymond Peach anasema : "Mimi ninamjua binti mmoja ambaye ni mwongo asiyetibika. Wakati yeye alipokuwa na umri wa miaka saba yeye alikuwa akihudhuria darasa lenye wanafunzi ishirini na watano. Nesi alikuwa akimchukua huko kila siku na kumrudisha nyumbani baada ya masomo ya shuleni. Kazi yake ilikuwa ni kuangalia na kuhakikisha kuwa binti huyo alikuwa akifanya mazoezi alizokuwa amepewa shuleni na kwamba alikuwa akijifunza masomo yake. Hivyo kwa kifupi yeye alikuwa akiwajibika na elimu ya binti huyo. Katika siku hizo, utaratibu wa elimu ulikuwa mbaya ambavyo siku hizi hautumiki wala kufuatwa. Wanafunzi walikuwa wakibaguliwa kila siku kwa mujibu wa kuandika majaribio,kwa kuwachagua wanafunzi wa ngazi za juu. Kila siku alipokuwa akitoka shuleni kwenda nyumbani, yule nesi alikuwa akimwuliza swali moja tu la kila siku na shauku yake ya kutaka kujua daraja alilolipata hapo shuleni siku hiyo. Na kama alimjibu kuwa yeye amekuwa mwanafunzi bora hapo shuleni kwa siku hiyo, basi mambo yalikwenda mazuri ama sivyo misengenyo na maneno chungu nzima zilikuwa zikimiminwa kwake. Lakini itakea mara moja kwa siku tatu mfululizo yeye akawa wa tatu katika darasa, ambavyo ilikuwa ni vema kwa nafasi hiyo kati ya wanafunzi ishirini na watano. Lakini huyo nesi, hakufurahishwa kwa ukweli huo. Kwa muda wa siku mbili, yeye alivumilia, na kwa siku ya tatu hakuweza kuvumilia hata kidogo na kusikia kwa siku ya tatu ya binti huyo kuwa wa tatu kwa shida na tabu zote alizozikumbana nazo binti huyo, nesi huyo alipiga kelele 'kwa hivyo kutokea kwako kuwa wa tatu hakuna mwisho ! Wewe lazima uwe wa kwanza kesho, je umenisikia vyema ? Lazima wa kwanza !" Siku nzima binti huyo alikuwa mashughuli kwa kazi hii ngumu na wazo hilo la kuwa wa kwanza darasani. Na siku ya pili alipata shida kubwa darasani. Yeye aliutumia uangalifu wake wote katika masomo na kazi za darasani. Viongezeo na vitowavyo vyake vyote vilikuwa sahihi. Alijibu vyema na kwa usahihi maswali ya masomo yote, na katika imla wakati wa adhuhuri ya siku hiyo, alifanya makosa manne, ambavyo imemrudisha katika nafasi yake ya tatu darasani siku hiyo. Wakati kengele ilipolia kwa mwisho wa siku ya masomo, nesi yule alikuwa akimsubiri kwa hamu mlangoni mwa darasa, na punde alipomwona tu binti huyo, alipiga kelele : "Je una habari gani ?" Binti huyo aliyekuwa amejawa kwa khofu hakusema ukweli bali alimdanganya kwa kusema "Mimi nimekuwa wa kwanza !" na kuanzia hapo ameanza tabia ya kusema uwongo. Je ni wazazi wangapi kama hawa wanawatendea watoto wao hivi na hivyo lazima washutumiwe kwa tabia ya makosa ya watoto wao kusema uwongo." Bertrand Rusell anasema : "Iwapo mtoto anapojitumbukiza katika usemaji uwongo, basi ni wajibu wa wazazi kujilaumu wao wenyewe, na wala si kumlaumu mtoto na hivyo inawabidi watafute ufumbuzi wa tatizo hilo la mtoto wao. Hivyo inamaanisha kuwa wazazi itawabidi watafute mbinu za kutokomeza sababu na kwa upole na kwa mantiki wawaeleze watoto kuwa si vyema kusema uwongo. Ama kama tiba, haitakiwi mzazi achukue hatamu la kuwapiga na kuwaadhibu watoto wao, kwani kwa kufanya hivyo kunamfanya mtoto kuingiwa na hofu na hivyo kumfanya awe mwongo kwa kupita kiasi. Bila shaka, iwapo wewe utapenda watoto wako wasijifunze uwongo wa aina yoyote, wakubwa itawabidi wawe waangalifu katika kusema ukweli wanapokuwa mbele ya watoto wao. Wazazi wanaowaambia watoto wao ukweli kuwa kusema uwongo ni dhambi, wakati watoto wanajionea kuwa wazazi wao ndio mabingwa wa kwanza kusema uwongo, basi bila shaka watoto hawa hawatayajali yale wanayoambiwa na wazazi wao na hivyo watakuwa daima wakiwapuuza wazazi wao na hivyo maneno na matendo ya wazazi wao hayatawaathiri watoto hao na hivyo watakuwa wakifuata vile watakavyo wao wenyewe. Jambo lingine la uwongo ni lile ambalo ni baya kwa watoto ni kule kuwatishia kuwa wataadhibiwa adhabu fulani kwa nia ya kutoitekeleza (yaani nitakupiga iwapo hivi na hivi ..., lakini mtoto haadhibiwi). Dr. Bollard anaielezea swala hili kwa mapana katika kijitabu chake kivutiacho 'Changing school .' Yeye anasema katika ukurasa 112: "Usiwatishie, lakini iwapo utafanya hivyo, basi angalia kuwa hakuna kizuizi chochote kwako wewe kuitekeleza tishio lako ." Kuwa makini na waangalifu kwa wazazi na waalimu kunaweza kuwazuia watoto wasiambukizwe uovu huu wa kusema uwongo. Iwapo mtoto hatadhalilishwa na utu wake kukandamizwa, na iwapo wakubwa hawatawafundisha kusema uwongo, iwapo mambo yanayomtelekeza katika au kushurutisha kusema uwongo yataondolewa kama hofu, vitisho n.k., na iwapo wazazi hawatamwonyesha ukali na kuwa kama madhalimu, na kwa kifupi, iwapo wao watawawia kwa wema na upole, kwa busara na kwa uangalifu, basi mtoto huyo kamwe hatakumbwa na ugonjwa mbaya huu unaoangamiza wa kusema uwongo. Wazazi huwa wanaghadhibishwa mno pale watoto wao wanaposema uongo wa kiajabu na mwongo anapokuwa mgeni katika uwongo. Je kwa nini mtoto aseme uwongo ? Mara nyingi watoto wanalazimika kusema uwongo kwa sababu hawatakiwi kusema ukweli. Iwapo mtoto atamwambia mamake kuwa yeye hampendi ndugu yake, basi inawezekana akachapwa kibao usoni mwake kwa ukweli huo. Lakini mtoto kwa kupika vyema uwongo wake akamwambia mamake kuwa sasa yeye anampenda ndugu yake, basi mamake atakimbia na kumbusu, na hata kuthubutu kumpa kazawadi. Je katika sura hizi mbili mtoto huyu atajifunza na kujipatia nini katika majaribio na utafiti wake ? Bila shaka mtoto huyu atajifunza kuwa kusema uwongo ndiko kunakompatia mapenzi na furaha wakati ambapo kusema ukweli kunamdhalilisha na kumpatia adhabu. Mama akiwa katika fahamu zake zote anamzawadia mwongo mdogo. Kwa hivyo, iwapo sisi tunataka kuwafundisha watoto wetu ukweli na uaminifu, sisi hatuna budi kuyasikia na kuyazingatia kila ukweli unaozungumzwa na watoto wetu na kuyakubali yote yale yaliyo machungu. Tuwape fursa ya kuyasema kwa uwazi ili wasitafute mbinu za kusema uwongo. Iwapo mtoto ataadhibiwa kwa kusema ukweli na kuwa mkweli, basi yeye hatakuwa na chaguo lingine isipokuwa kuchukulia uwongo katika kujikinga na kujihami na hasa kwa kujipenda ili asipoteze heshima na hadhi yake. Vile vile wazazi kamwe wasiwe wakiwauliza maswali ambayo yanawalazimisha watoto kuwajibu kwa kuchanganya uwongo ili kujilinda. Watoto kikanuni hawapendelei wazazi wao wawe wanawahoji kila mara wakati ambapo wao wanatambua waziwazi majibu yatakayokuwa. Madhumuni yetu lazima yawe ya kumfanya mtoto wetu atambue kuwa yeye asiwe na wasiwasi wala woga wa aina yoyote ile katika kusema ukweli. Inatubidi vile vile tuwatambulishe watoto wetu umuhimu wa mafunzo na utekelezaji wa maamrisho ya Allah swt kuwa uwongo ni dhambi mbele ya Allah swt na kwamba Allah swt huwa na uadui pamoja na msema uwongo. Iwapo mafunzo ya watoto yatakuwa katika misingi ya Dini ya Kiislamu, na maadili katika mafunzo ya Allah swt, basi hakuna upotofu utakaotokea, kwani hakuna ufuatiliaji wa Sharia unaofanywa na chombo chochote kile isipokuwa Dini tu ndiyo inayoweza kutekeleza. Hii ni kanuni ambayo inazuia kuzagaa kwa watu wa dini wenye uwongo na kila madhambi, na kuwapa hifadhi ya kiroho na kiakili. Kuelezea madhara yatokanayo na uwongo pamoja na mifano ya kihistoria, angalia athari za ugonjwa huu ulivyowaathiri watu. Marehemu Kiongozi wa Kidini, Al-Naraqi, anasema : "Ili kutaka kutengeneza ugonjwa huu uwe sawa, ni lazima tuzingatie na kufuata maamrisho ya Qur'an Tukufu na Ahadiith za Mtume Muhammad s.a.w.w. na Maimamu a.s. hususan zinazokana na kupiga vita uwongo, ili mtu aweze kutambua na kujua kuwa malipo yake mbele ya Allah swt yatakuwa makali na ya kutisha, yote yenye kudumu. Zaidi ya hayo ya maangamizo ya milele, mtu huyo atakoseshwa heshima ya kijamii na umaarufu, na bila wasiwasi atadhalilika wakati uwongo wake utakapokuja kujulikana na watu." (Jamea-Sa'adat, j.2, uk.256) Dr. Alexis Karl anasema : "Katika tabia zote, hakuna inayoidhuru akili kuliko uwongo, uchochezi, shawishi, kuwasingizia watu kwa uwongo, kuwadhuru wao, uwizi, na kujitakia kila kitu kwa ajili yake mwenyewe. Akili ya mtu kamwe haielekei kujisalimisha katikati ya maovu na uwongo. Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Bihar al-Anwar, j.72,uk.260 : "Semeni ukweli kwani Allah swt yupo pamoja na wasema ukweli, Jiepusheni na uwongo, kwani inaondia Imani. Msema ukweli yupo ataongoka wakati mwongo yuko anadhalilika na kuangamia." Mshairi anasema : "Ni lazima mtu awe msema ukweli hata kama atakumbwa na tufani. Sema ukweli na wala usiogope, kwani ukweli haukuondolei rizikii, wala haukusabababishii kifo." Uchunguzi wa akili za waongo unabainisha kuwa kunakuwapo na kasoro mbalimbali zinazotokana na uwongo. Kutoka mtizamo wa kijamii, uwongo unalemaza bila kupatiwa ufumbuzi. Heshima ya mwongo ipo hatarini katika jamii, na yeye daima yupo ukingoni mwa kukashifiwa. Je kuna hasara yoyote zaidi ya kutangazwa na kuwa mwongo bayana na ustahi wake wa kijamii ? Mwerevu daima atajaribu kushinda heshima na hadhi katika jamiii na kwa hayo yupo tayari hata kutumia mali na utajiri wake, kwani heshima katika jamii ni rasilimali kubwa katika jamii. Lakini mwongo anaiharibu mwenyewe rasilimali hiyo adhimu aliyonayo kwa mikono yake mwenyewe kwa matendo yake maovu. Kisa kifuatacho kimetolewa kutoka Uwongo, uk. 204: Kiongozi wa madhehebu ya Shaikhia alikuwa akihubiri huko Tabriz, na katikati ya hotuba yake alitaja majina ya wafalme majini ambao nani alikuwa wa kwanza na nani alifuatia. Yeye anasema kuwa Tahtah Shah alikuwa ndiye mfalme wa kijini wa kwanza, alifuatiwa na Ghahghah Shah, na baadaye Jahjah Shah na kendelea. Wakati alipofikia wa kumi ambaye jina lake lilikuwa likifanana na la waliotangulia, mmoja wa watu aliyekuwa amekaa karibu naye, alimwambia, "Ewe bwana ! Naomba urudie mfalme wa tano. " Mhubiri huyo alisita na akashikwa na bumbuwazi kwani hakukumbuka ni mfalme yupo aliyokuwa amemzua yeye. Kwa hayo msomaji utakuwa umeona vile atakavyokuwa ameaibika huyu mhubiri mwongo na mzushi. George Herbert anasema : "Haijali hata kama vazi gani litavishwa uwongo, hatimaye itadhihirika ." Pamoja na ukweli kuwa uwongo unapoteza sura yake katika jamii na vile vile hupoteza imani ya watu juu yake jambo ambalo ndilo msingi wa jamii kwake yeye. Hakuna atakayemwamini yeye, na hata kama atasema ukweli siku moja, basi hakuna atakayemwamini. Aristotle anasema: "Wale wasemao uwongo wanaadhibiwa kwa njia ambayo wao wanaposema ukweli basi hakuna anayewasadiki." Sa'adi, mshairi mashuhuri wa Kiirani anasema : "Yeyote mwenye tabia ya kusema ukweli daima, anapokosea, basi husamehewa. Lakini yule anayekuwa mwongo wa kupindukia, hasadikiwi hata kama atasema ukweli." Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema : "Jiepusheni na uwongo, kwani uwongo unadhalilisha na kuaibisha." Aibisho hili liko mbele ya Allah swt na kuendelea kubakia katika njia potofu; na aibu pamoja na watu kwa kupoteza heshima na staha ya watu. Kwa kuangalia mtazamo wa kiuchumi, vile vile, uwongo unaleta hasara kubwa mno, katika kufanya biashara pamoja na watu, tunatambua waziwazi kuwa biashara na mapatano mengi yanafanywa kwa mikopo ambayo inakuwa katika misingi ya uaminifu na ukweli miongoni mwao. Uwongo unaleta uaibisho, na hivyo hata biashara na mapatano yake pia yataathirika na hivyo kuporomoka kwa biashara yake na mwisho ndio udhalillisho utakuwa mavuno ya tabia zake. Hasara nyingine inayofanywa na uwongo ni kwamba inaleta matakwa ya kiakili na kimatendo ya mwongo, na hatimaye hao waongo wanakumbwa na matatizo makubwa ya kiakili. Mwandishi mashuhuri anaandika katika kitabu chake :"Kwa kutokana na uwongo mmoja, mimi nimejuta kwa miaka thelethini. Kisa chenyewe ni kama ifuatavyo : 'Usiku mmoja katika mkusanyiko wa marafiki na wenzangu, kulizuka gumzo kuhusu usafiri. Kila mmoja wetu aliyekuwapo alizungumzia kuhusu safari yake ya huko Ulaya, Amerika, Mashariki ya karibu na mbali. Kwa kutotaka mimi nibaki nyuma, nami nilijibwaga katika gumzo hilo, ingawaje mimi kamwe nilikuwa sijawahi kusafiri kwenda Ufaransa, lakini nilizungumzia safari yangu ya kwenda Ufaransa. Lakini mara wazo likanijia akilini kuwa mimi sijawahi kwenda huko, na iwapo kuna mmoja wetu ambaye amekwenda huko na akaniuliza maswali kuhusiana na safari yangu hiyo, bila shaka nitashindwa kumjibu na hivyo nitadhalilika na kupoteza heshima yangu, Sikujisikia vizuri na wala sikuwa na raha lakini niliamua kubakia katika hafla hiyo hadi mwisho. Lakini kuanzia usiku huo mimi nimekuwa nikisumbuliwa na jinamizi la kuaibika lilikuwa mbele ya macho yangu kama kweli angalijitokeza mtu kuniuliza swali kuhusu safari yangu hiyo ya Ufaransa, ningalimjibu nini. Hali hii ilinisumbua sana kiasi kwamba ilinibidi nisafiri kwenda Ufaransa, lakini safari haikufanyika. Na baada ya miaka thelethini ndipo nilipofanikiwa kusafiri na sasa ndipo ninajisikia vyema. Kwa hivyo, kwa uwongo mmoja tu, nimetaabika kwa miaka thelathini, na hivyo nilikula kiapo kuwa kuanzia usiku huo kamwe sitasema uwongo hadi mwisho wa maisha yangu, na nitajiepusha na uovu mkubwa wa aina hii." Wanahistoria wanaandika : "Kulikuwapo na uhusiano mzuri baina ya Sultan Boyghora, Mfalme wa Khurasaan na Zabulistan, na Sultan Ya'aqub, Mfalme wa Iraq na Azarbaijan na walikuwa wakiwasiliana daima miongoni mwao. Mfalme wa Iran aliamua kumtumia zawadi ya vito vya thamani kwa Sultan Ya'aqub. Wakati zawadi zilipokuwa tayari, yeye aliamrisha kuongezewa miandiko ya Jami' ambayo yalikuwa mashuhuri siku hizo katika zawadi. Mwanamaktaba, Mulla Abdul Karim, alifanya kosa wakati wa kufunga kifurushi cha kitabu cha Jami' na badala yake alikituma kitabu kilicho zungumzia Ushindi wa makkah ambacho kilikuwa sawa kwa jalada na saizi. Mheshimiwa katika Baraza la Mfalme, Amir Husain Abivardi, ndiye aliyepewa jukumu la kufikisha zawadi hizo hadi kwa Sultan Ya'aqub. Abivardi, naye pia bila ya kukagua zawadi zilizokuwa, aliondoka katika kufikisha zawadi hizo. Wakati Amir Husain aliwasili Tabriz na alipopokelewa, Sultan Ya'aqub alimpokea kwa wema na kumkirimu na kusema : "Lazima utakuwa umechoka kwa safari iliyokuwa ndefu." Kama vile Amir Husain alivyokuwa akijua kuwa Sultan aliipenda sana Jami' , alisema : "Mimi nilikuwa ninaye rafiki mwema safarini hivyo sijisikii uchovu wa safari." Sultan alimwuliza kuhusu rafiki huyo, naye alimjibu : "Jami' kazi za ushairi." Sultan alifurahishwa mno kwa kusikia hivyo na alimtuma akilete kitabu hicho haraka iwezekanavyo, na wakati walipokifungua kifurushi waliona kwa masikitiko makubwa kuwa si kitabu chenyewe bali kilikuwa ni kitabu juu ya ukombozi wa Makkah. Amir Husain alishikwa na aibu kubwa kwa kusema uwongo, lakini alikuwa amekwisha chelewa kwa ajili ya kufanya marekebisho. Mwanabalozi huyo mkongwe alikuwa ameadhirika na kudhalilika katika nchi zote mbili na kupoteza heshima zake." Matukio kama haya yapo mengi katika historia na kuonyesha kuwa hasara kubwa kubwa zimepatikana. Ufuatilaji wa shakhsiya zilizokuwa maarufu pia zinathibitisha swala hili. Kwa misingi hiyo hiyo ndiyo Islam inapigana vita vikali dhidi ya uwongo na haya ndiyo mambo ya watu wasio na imani wala Dini na hivyo mwongo anastahili kila aina ya laana na shutuma. Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Jami' as-Sa'ada : "Yeyote yule anayeigeukia kusema na kutumia uwongo basi Malaika wanamlaani. " Amesema al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Khasail, cha Sadduq : "Upimaji wa imani ya mtu ni kwa ukweli na kuweka amana." Vile vile yeye amenakiliwa katika Ghurarul Hukam kuwa ameongezea kusema "Uwajaribu watu kwa mambo mawili: "Ukweli katika maneno yake na pili, mwaminifu katika kuweka amana ya watu."
|