Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
Ushauri wa 'uwongo mweupe'

Katika kurasa zilizopita tumeona kuwa kuzungumza uwongo ni dhambi, na sasa ni wakati wa kusemea uwongo mweupe ambao unaonekana kama nasiha.

Kimsingi, katika Islam madhambi yanayokubaliwa na yanayo katazwa yapo katika makundi mawili :

  1. Imekaa ndani mwa mtu na mbaya kabisa ambayo moja kwa moja inachukuliwa kuwa ni mbaya na ovu, kama vile mauaji, ukandamizwaji, ukiukwaji wa haki za wengine, uwizi na kama hayo.
  2. Aina ya pili ni yanatokana na udhaifu na kuchafuliwa kusababisha madhambi mengine.

Uwongo upo katika kundi la pili la madhambi na kama ilivyokwisha semwa hapo awali, ni ufunguo wa kila dhambi. Iwapo uwongo ndio utakaotokea kila mara katika kuondoa dhambi lingine au kuondolewa dhuluma kwa mdhulumiwa, basi haiwezi kukubalika basi haitatambuliwa kuwa ni dhambi, hivyo ubaya unatokomezwa kwa kutumiwa kwake, hivyo haiharamishwi bali inafaradhishwa kutumia ili kulinda hadhi na heshima na maisha ya Mwislamu, iwapo atakuwa hatarini.

Amesema al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. :

"Iwapo Mwislamu mmoja ataulizwa kuhusu Mwislamu mwingine naye akasema ukweli ambao utamdhuru huyo Mwislamu wa pili, basi jina lake litaingizwa katika majina ya waongo.

Na iwapo Mwislamu mmoja ataulizwa kuhusu Mwislamu mwingine naye akajibu kwa kusema uwongo ambapo utamfaidisha Mwislamu wa pili, basi mtu huyo atahesabiwa na Allah swt miongoni mwa wasema ukweli."

Mshairi Sa'adi anasema katika kitabu chake Gulistan :

"Mfalme alitoa amri ya kumwua mateka moja.

Masikin.huyo mtu kwa hamaki na ghadhabu alianza kumsema vibaya na kumkaripia kama kwamba inasemekana kuwa mtu asiye na matumaini atasema kila kitu alichonacho moyoni mwake na kama ubeti unavyoendelea :

Wakati wa dharura ambapo kunakuwa hakukubakia njia yoyote, mkono hutokezea mbele kuunoa upanga.

Mfalme aliwauliza watu kile alichokuwa akikisema huyo bwana. Waziri mwema akasema : "Ewe Mfalme ! Yeye anasema kuwa wale wanaoweza kuzuia ghdhabu zao basi wanaweza kudhibiti hasira zao na hivyo wanauwezo mkubwa wa kusamehe watu "

Kwa hayo mfalme alimwonea huruma na kumsamehe.

Lakini Waziri mwingine aliyekuwa na chuki na Waziri huyu, alisema :

"Haitulazimishi sisi kuingilia na kusema uwongo katika baraza la Mfalme. Huyu mtu amekutukana na kukukashifu."

Kwa kuyasikia hayo, Mfalme alikasirishwa mno na akasema : "Mimi ninapendelea kusikia uwongo huo kuliko ukweli wako, kwani hayo yalikusudiwa kwa nia njema, ambapo nia yako ni mbaya." Kama vile wenye hekima wasemavyo : "Uwongo wa kiushauri ni afadhali ya ukweli unaoangamiza."

Mtume Muhammad s.a.w.w. anasema :

"Zipo nafasi tatu ambapo uwongo unapendeza: kudanganya katika vita, ahadi aitoayo mume kwa mke wake na kuwapatanisha watu."

Maelezo:

  • Ama kuhusiana na kudanganya vitani, wasomaji wetu mnajua kuwa Islam haupendelei vita na kile kinachomaanishwa hapa kwa vita ni baina ya haki na batili, ambavyo udanganyifu hapa utaimarisha haki na kuwadhoofisha batili, na hivyo inakubalika.
  • Ama kuhusiana na ahadi ya mume kwa mke wake, Islam inapendelea kuwaona wakiishi kwa raha na mustarehe na waishi kwa kupendana. Hivyo kumwambia mke wako uwongo wa kumtimizia jambo fulani, kama unao uwezo basi vyema kabisa, lakini kama hana uwezo, basi anaweza kumpa ahadi ya uongo ili kuepukana na ugomvi na kumuudhi mke wake.

Kwa mfano, wewe hauna uwezo wa kumtimizia ombi fulani la mke wako, kama kwa mfano anataka nyumba, lakini wewe kwa kutokuwa na uwezo huo, utamdanganya kuwa nitakujengea au kukununulia ili kumridhisha mke wako. Sote tunajua kuwa ukaidi wa mwanamke ni ukaidi mkubwa kabisa na vile vile Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema kuwa "mwanamke ni kama mfupa wa ubavu, upo umepinda, hivyo usijaribu kuunyosha, utavunjika" hivyo tutumie mbinu kama hizi kwa nia njema ili kutuliza mambo nyumbani.

  • Ama jambo la tatu, yaani kuwapatanisha na kuwaunganisha watu, Islam inataka kuwepo uhusiano wa kidugu na kirafiki miongoni mwa watu, na pale panapotokea mtafuruku baina yao au kati ya watu wawili, basi ni lazima kufanyike kwa jitihada za kuwaunganisha na kuwapatanisha. Kwa hakika kuondolewa tofauti hizi baina yao ndiyo faida na maslahi ya jamii nzima kwa ujumla. Na hivyo, kusema uwongo kwa nia ya kuwapatanisha watu walio katika ugomvi umeruhusiwa katika Islam.

Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema :

"Hakuna uwongo kwa mtu anayesuluhisha."

Amesema al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. :

"Uwongo ni mwovu na haikubaliki isipokuwa katika sura mbili :

  • Katika kuuondoa shari ya mdhalimu
  • Kuwapatanisha watu."

Kwa kusema kwa ujumla, popote pale patakapokuwa na kusudi la kuondoa shari ya mdhalimu anayewahasarisha Waislamu na kwa kuwasuluhisha watu, basi Islam inatambua kuwa uwongo katika sura hizi si dhambi tena. Hapa uwongo unaruhusiwa na ukweli unakatazwa.

Kwa kukamilisha , ni lazima ikumbukwe kuwa 'uwongo mweupe' unavyojulikana unaruhusiwa katika sura ambazo Islam imeruhusu tu, ambapo katika sura zingine itakuwa ni tendo la dhambi kutumia uwongo.

Hata hivyo uwongo unaotumiwa kwa kujipatia faida na kujipatia chochote kwa maslahi yake mwenyewe haviwezi kutambuliwa kama 'uwongo mweupe' na hivyo imeharamishwa katika Islam kwa mujibu wa Ayah za Qur'an Tukufu na Ahadith za Mtume Muhammad s.a.w.w. na Maimamu a.s. na kutenda dhambi kutampatia adhabu kali huko Aakhera.

T A M A T I - WALHAMDU LILLAAH