Subject Index 
Search
Announcements
Feedback
ORODHA YA MAJINA YA WAKEZE MTUME [s]

Baada ya kifo cha mke wake wakwanza Bibi Khadija [a] Mtume [s] alioa wanawake wafuatayo:

(1) Saudah, (2) Ayisha, (3) Umus-Salamah bint Khuzaimah, (4) Zainabu Binti Jahash, (5) Ummu-Habibah (Ramla), (6) Mayimunah, (7) Zainab bint Umais, (8) Juwairiyah, (9) Safiyyah na (10) Khaulah binti Hakim.

Hebu tuyechunguze matukio na hali zisizosababisha ndoa hizi kufungwa. Ukweli ni kuwa, tunaweza kusema kuwa ndoa hizi zilifungwa kwa moja au zaidi ya sababu hizi zifuatazo:

  1. Kwa sababu ya kuwatunza watoto yatima na mama zao waliokuwa wajene. Wajane hawa walikuwa ni Waislamu ambao hapo awali walikuwa wakipata heshima kubwa katika jamii ya Kiarabu. Lakini baada ya vifo vya waume wao, hadhi zao na hata imani zao zilikuwa hatarini, kwa sababu watemi (machifu) wa makabila yao wangewachukua na kuwalazimisha kuikana dini ya Uislamu na hivyo wangelirudi ukafirini tena.

Kwa mfano Bibi Saudah (r.a.) alihamia Uhabeshi na huko mume wake alifariki, hivyo alikuwa hana msaidizi ye ypte. Wakati huo ambapo Mtume [s] naye alikuwa keshafiwa na mkewe wa kwanza Bibi Khadija [a], hivyo alimuoa Bibi Saudah (r.a.).

Vivyo hivyo, Bibi Zainabu binti Khuzaim (r.a.) naye alikuwa mjane mwenye umri mkubwa ambaye baada ya kufiwa na mume wake alibaki katika hali ye umaskini, ingawa alikuwa mwenye tabia njema na aliyejulikana sana kwa jina la "Ummul-Masaakin (Mama wa maskini)". Mtume [s] alimuoa Bibi Zainab (r.a.) ili kuendeleza hadhi yake na baadaye Bibi huyu alifariki kwa uzee, miaka miwili tu tangu kuolewa na Mtume [s].

  1. Kwa madhumuni ya kuzithibitisha umri mpya (Mwenyezi Mungu) na kuondoa uonevu uliokuwa unaendelezwa na makabila yasiyostarabika. Kwa mfano Bibi Zainab bint Jahash (r.a.) alikuwa ni binti wa shangazi yake Mtume [s]. Bibi huyu aliolewa na Bwana Zaid bin Haritha kwa mapendekezo ya Mtume [s]. Bwana Zaidi bin Haritha (r.a.) alikuwa huria wa Mtume [s] na akamfanya mwanawe wa kulea. Ndoa hii ilifungwa kwa ajili ya kuondoa ubaguzi kati ya watumwa maskini na kusisitiza usawa na udugu wa Waislamu, kwa kuwa Bibi Zainab (r.a.) alitoka katika ukoo wa Bwana Abdul-Muttalib [a] babu yake Mtakatifu Mtume [s] na mtemi wa Waquraishi, ambapo Bwana Zaid (r. a.) alikuwa mtumwa huria wa Mtume [s].

Kwa bahati mbaya, kwa sababu ya majivuno ya Bibi Zainab (r.a.) kuhusu ubora wa familia yake, Bwana Zaid hakuweza kuishi na mke huyo, ingawaje Mtume [s] aliwasihi ndoa yao iendelee. Tofauti hizo zilizaa talaka. Wakati huo, mtindo wa watoto wa kulea ulikuwa umekatazwa na Mwenyezi Mungu (Qur'ani 33:45). Kwa hiyo, Bwana Zaid (r.a.) alipomtaliki Bibi Zainab (r.a.), Mtume wa Islamu [s] kwa amri ya Mwenyezi Mungu, (Qur'ani 33:37) alimuoa Bibi Zainab (r.a.), na hivyo basi aliiulia mbali imani iliyokuwepo isemeyo kuwa watoto wa kulea walikuwa sawa na watoto wa kuzaa na kuwa wake au wajane wa watoto wa kulea walikuwa sawa na wakawana wa watoto wa kuzaa.

  1. Kwa madhumuni ya kuwapa uhuru wafungwa na watumwa. Kwa mfano Bibi Juwairiyah (r.a.) alikuwa wa ukoo wa kabila maarufu wana wa Bani Mustalaq. Kabila hili lilipopigana dhidi ya Kiislamu na kushindwa na Bibi Juwairiyah ambaye ni binti wa mtemi wa kablia hilo, alichukuliwa mateka. Mtume [s] alimuoa Bibi Juwairiyah (r.a.) ili kutoa mfano mwema kuhusu jinsi ya kuwalinda na kuwafanyia mema mateka wa vita. Waislamu walipoona kuwa mateka wa vita wamekuwa na uhusiano wakindoa na Mtakatifu [s] waliwaachia mateka waliokuwa wakiwamiliki. Bwana ibni Hisham amesema katika kitabu chake cha Historia (kiitwacho "Sirat Rasulullahi") kuwa zaidi ya familia mia moja za Banul-Mustalaq ziliachiliwa huru baada ya ndoa hiyo.

  2. Kwa madhumuni ya kuyaanganisha makabila maarufu kadha, ya Kiarabu ambayo mara nyingi yalikuwa katika hali ya uadui na pia kuilinda hali ya kisiasa miongoni mwa Waislamu.

Mtume [s] alimuoa Bibi Ayesha bint Abu-Bakar (Abdul Kaabah au Abdallah bin Abi Quhaafah) kutoka katika kabila la Bani Taim, Bibi Hafsa (r.a.) binti Umar bin Khattab kutoka kabila la Adi, Bibi Ummu Habibah (r.a.) binti Abu Sufyani toka katika kabila la Umayya, Bibi Safiyyah (r.a.) binti Huaiy bin Akhtab wa kabila la Kiyahudi la Bani Nazir, na Bibi Mayimuunah (r.a.) kutoka kabila la Bani Makhzuum.

Bibi Ummu-Habibah (r.a.) (Ramla) alikuwa mtoto wa Abu Sufyan wa kabila la Banu Umayya ambaye alikuwa adui mkubwa wa Mtume [s] na alipigana naye mara nyingi. Bibi Ummu Habibah (r.a.) baada ya kusilimu alikuwa katika hali mbaya sana kwani alikuwa ameachwa na mume wake wa kwanza (aliyeingia dini ya Kikristo huko Uhabashi) na wakati huo huo baba yake alikuwa adui mkubwa wa Uislamu.

Mtume [s] alipomuona Bibi huyu katika hali ile, akiwa hana msaada wo wote toka kwa wazazi wake na mume wake kamtaliki, alimuoa kwa kumuonea huruma. Ndoa hii pia ilitowa mfano kwa watu wa Bani Umayya kuilegeza mioyo yao kwa dini ya Kiislamu.

Bibi Safiyyah (r.a.) alikuwa mjane na binti wa Bwana Huaiy bin Akhtab, mmoja wa watemi wa kabila la Kiyahudi la Bani Nazir. Mateka wa kabila hili walipoachiliwa na Waislamu, Mtume [s] alimuoa Bibi Safiyyah (r.a.) kwa madhumuni ya kulinda hadhi ya bibi huyu na pia kwa kufanya hivyo Mtume [s] akajihusisha na moja ya makabila makubwa ya Kiyahudi ya wakati huo na kuyasogeza karibu na Islamu.

Bibi Mayimuunah (r.a.) ambaye Mtume [s] alimuoa katika mwaka wa 7 baada ya Hijja, akiwa na umri wa miaka 51 na alitoka katika kabila maarufu sana la Bani-Makhzuum.

Historia iliyoelezwa hapo juu, ya ndoa za Mtume [s] inaonyesha wazi umuhimu wa madhumuni hayo ya kuoa wanawake kadhaa. Si ngumu hata kidogo kuona kuwa hakuna hata ndoa moja ambayo madhumuni yake yalikuwa kuridhisha tamaa za kimwini za kibinafsi kama wasemavyo waandishi wa Kikristo wanaomlaumu Mtume [s] . Pia ni muhimu kukumbuka kuwa ndoa hizi zote, ila ile ya Bibi Ayesha (r.a.), zilifungwa na wanawake waliokuwa wajane, si mara moja tu bali mara mbili au tatu.