read

Aya 1 – 13: Amemuumba Mtu Akamfundisha Ubainifu

Maana

Mwingi wa Rehema

Katika sura hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja neema kadhaa kwa waja wake. Ameanza kwa kwa neno Mwingi wa rehma, kwa vile linaashiria neema na fadhila.

Amefundisha Qur’an.

Yaani ameiteremsha. Qur’an inafana na ulimwengu katika njia kadhaa; miongoni mwazo ni haizi zifutazo:

• Qur’an ni katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na ulimwengu umepatakina kwa neno ‘Kuwa.’

• Kila moja kati ya Qur’an na ulimwengu unafahamisha kwa hisia uwezo na ukuu wa Mwenyezi Mungu. Ulimwengu unaonekana kwa macho na Qur’an inasikiwa kwa masikio. Ndio mmoja wa waumini akasema kuwa Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: kimoja kinasomwa na kusikiwa nacho ni Qur’an na kingine kinaonekana na kuguswa nacho ni ulimwengu.

• Ulimwengu na Qur’an ni katika uweza wa Mwenyezi Mungu pekee yake hakuna anayeweza kuleta mafano wake.

• Qur’an na ulimwengu ni katika neema kubwa aliyoileta Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mtu. Ananeemeka na heri za ardhi na mbingu na anaongoka kwa Qur’an kueleka kwenye raha na wema wa nyumba mbili.

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemneemesha mtu kwa jua, mwezi, ardhi, mvua, upepo, mimea, miti, wanyama na mengineyo yasiyokuwa na mwisho.

Amemuumba mtu. Akamfundisha ubainifu.

Makusudio ya ubainifu ni kila linalofahamisha makusudio ya kutamka, hati kuchora au ishara. Hata hivyo kusema, ndio kiungo muhimu zaidi cha ubainifu na chombo chake ni ulimi ambao ndio kiungo kitiifu zaidi kwa mtu, chenye harakati nyingi zaidi na chepesi. Hakijui kuchoka wala kutaabika. Sifa hizi hazipatikani katika viungo vingine.

Ubainifu, hasa maneno, ni katika neema kuu zaidi. Kwayo mtu anaeleza makusudio yake, kufahamu makusudio ya wengine, kujibizana nao kwa upendo, kutekeleza haja zake na za wengine.

Ubainifu unabainisha kufuru na imani, inajikita ilimu, fasihi na fani mbalimbali na kujulikana dini. Baadhi ya ulama wanasema: Kila matumizi ya ilimu yanaelezea ubainifu. Hakuna kitu chochote ila kinatumia ilimu.

Jua na mwezi ni kwa hisabu.

Yaani vinakwenda kwa nidhamu kamili na kanuni thabiti. Kwa nidhamu hii ndio yanahifadhika maisha katika ardhi, ikatofautiana misimu na zikajulikana nyakati.

Na mimea yenye kutambaa, na miti, inanyenyekea.

Neno ‘mimea yenye kutambaa’ tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu annajm kama walivyosema hivyo wafasiri wengi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelitaja pamoja na mti kwa mkabala wa jua na mwezi.

Maana ya kusujudi ni kuwa yote hiyo inafahamisha kuweko Mwenyezi Mungu na ukuu wake kutokana na usanii wa hali ya juu kabisa. Tazama kifungu cha maneno:

وَإِنْ مِنْ شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ {44}

Na pana kila kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake.’ katika Juz. 15 (17:44) .

Na mbingu ameziinua, na ameweka mizani.

Makusudio ya mbingu hapa ni kila kilichomo ndani yake miongoni mwa sayari. Na mizani ni kila hakika ya vitu na vipimo vyake vinavyojulikana; viwe vya kimaada kama vile makopo, mita na mizani au vya kimaana kama vile wahyi na misingi ya kiakili na maumbile.

Vile vile makusudio ni kuwa ulimwengu huu wa maajabu umepangika vizuri. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameziweka sayari kwenye sehemu zake zinapotakikana; kiasi ambacho lau kama sayari itasogea kidogo tu zaidi ya sehemu yake ilipopangiwa, basi nidhamu ya uliwengu ingelivurugika na kubadilika kila kitu.

Pia hakuna jamii inayoweza kuwa sawa isipokuwa kwa kufuata mizani ya maadili.

Ili msidhulumu katika mizani. Na wekeni mizani kwa haki, wala msipunje katika mizani.

Dhulma ni kupora na kunyang’anya, kupunja ni kutotekeleza haki kwa anayestahiki na kuweka mizani kwa haki ni kutojipunja wala kuwapunja wengine. Ni muhali kupatikana utulivu katika jamii itakayopuuza haki na uadilifu.

Kwa muhtasari ni kuwa Aya hii, pamoja na ufupi wake, ni kuwa imeashiria yale yanayotimiza na yanayoweka nidhamu ya ulimwengu na jamii. La kwanza ni nidhamu ya ulimwengu aliyoitimiza Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa ukamilifu. Ya pili ni nidhamu ya sharia aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa waja wake, waichunge na waitekeleze kwa mujibu wake.

Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe kuwa ni tandiko na kutafutia maisha. Humo yamo matunda mengi na vyakula vinginevyo na vinywaji na mitende yenye mafumba yanayopasuka na kutoa matunda yanapofikia kuiva.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kutaja mti wa mtende kutokana na umuhimu wake kwa waarabu wakati huo.1

Na nafaka zenye makapi.

Nafaka ni kwa ajili ya chakula cha binadamu na makapi ni kwa ajili ya wanyama.

Na mrehani kwa ajili ya manukato na kujipamba.

Mrehani ni ule mti maarufu unaoitwa hivyo, lakini imesemekena kuwa makusudio yake hapa ni kila mmea wenye harufu nzuri.

Chakula, matunda na maua yote hayo ni katika heri za ardhi na baraka zake alizowaneemesha Mwenyezi Mungu waja wake, lakini wao wanaishi kwa kuziharibu na ufisadi.

Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Wawili hapa anaambiwa jinni na mtu kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kwa ajili ya viumbe,’ inayochanganya aina mbili hizi za viumbe, na pia kauli itakayokuja badae. “Tutawakusudia enyi wazito wawili.”

Maana ni kuwa, je anaweza kukana yeyote, katika majini na watu, neema alizozitaja Mwenyezi Mungu (s.w.t.)? Vipi anaweza kuzikataa na yeye yumo ndani yake?

خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ صَلْصَالٍ كَالْفَخَّارِ {14}

Amemuumba mtu kwa udongo mkavu kama uliookwa.

وَخَلَقَ الْجَانَّ مِنْ مَارِجٍ مِنْ نَارٍ {15}

Na akawaumba majini kwa ulimi wa moto.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {16}

Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

رَبُّ الْمَشْرِقَيْنِ وَرَبُّ الْمَغْرِبَيْنِ {17}

Mola wa mashariki mbili na wa magharibi mbili.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {18}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ يَلْتَقِيَانِ {19}

Anaziendesha bahari mbili zikutane;

بَيْنَهُمَا بَرْزَخٌ لَا يَبْغِيَانِ {20}

Baina yao kipo kizuizi, haziingiliani.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {21}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

يَخْرُجُ مِنْهُمَا اللُّؤْلُؤُ وَالْمَرْجَانُ {22}

Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {23}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

وَلَهُ الْجَوَارِ الْمُنْشَآتُ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ {24}

Na ni vyake Yeye hivi viendavyo baharini vilivyoundwa kama vilima.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {25}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ {26}

Kila kilicho juu yake kitatoweka.

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ {27}

Na itabakia dhati ya Mola wako Mwenye utukufu na ukarimu.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {28}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

يَسْأَلُهُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ كُلَّ يَوْمٍ هُوَ فِي شَأْنٍ {29}

Vinamwomba Yeye vilivyo katika mbingu na ardhi. Kila siku Yeye yumo katika mambo.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {30}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
  • 1. Hata hivyo kuna maoni kuwa bado una umuhimu hadi sasa na baadae kutokana na ubora wa lishe yake yenye faida nyingi za kiafya -Mtarjumu.