read

Aya 1 – 16: Naapa Kwa Mlima

Lugha

Anasema Fayruzi Abad katika Kamusi yake Al-Muhit: Neno Tur linatumika kwa maana ya uga wa nyumba, kila mlima na mlima ulio karibu na Ayla unaoitwa mlima Sinai. Pia hutumika kwa milima miwili, mmoja uko Qudus na mwingine ulioko Raasul-ayn. Vile vile mlima ulioko Tiberias.

Maana

Naapa kwa Mlima, na kitabu kilichoandikwa katika waraka wa ngozi iliyo kunjuliwa, na kwa Nyumba iliyojengwa, na kwa sakafu iliyonyanyuliwa, na kwa bahari iliyojazwa.

Mlima hapa ni ule mlima Sinai aliozungumza Mwenyezi Mungu na Musa. Pia Mwenyezi Mungu ameapa na mlima huu katika (95:2).

Makusudio ya kitabu chenye kuandikwa ni kila kitabu cha mbinguni. Kwa sababu neno kitabu hapa limekuja kwa kuenea kwenye jinsia yake (nakra). Kulihusisha neno hilo na kitabu maalum kutahitajia maunganishao. Kule kutajwa mlima sinai tu, hakutoshi kuwa makusuidio yawe ni Tawrat.

Makusudio ya kusema kilichoandikwa katika waraka, ni kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha kitabu ila alikifanya kitumike mikononi mwa watu na kila mtu aweze kukifikia na kukijua kwa ukamilifu. Imam Aliy (a.s.) anasema:
“Nashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na ni Mtume wake aliyemtuma kwa dini liliyo mashuhuri na kitabu kilichoandikwa.”

Nyumba iliyojengwa ni Al-Kaa’ba. Mwenyezi Mungu anasema:

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ {127}

“Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile nyumba.” Juz. 1 (2:127).

Sakafu iliyonyanyuliwa ni mbingu:

وَجَعَلْنَا السَّمَاءَ سَقْفًا {32}

“Na tukaifanya mbingu kuwa sakafu.” Juz. 17 (21:32).

Yani iko kama sakafu katika jicho la mwenye kutazama. Bahari iliyojazwa ni kujaa maji:

وَإِذَا الْبِحَارُ سُجِّرَتْ {6}

“Na bahari zitakapojazwa.” (81:6).

Mwenyezi Mungu ameapa na vitu hivi vitano kuashiria uweza wake. Tazama Juz. 23 (37:1) kifungu cha: ‘Mwenyezi Mungu na kuapa na viumbe vyake.’

Hakika adhabu ya Mola wako hapana shaka itatokea kwa wakosefu. Jumla hii ni jawabu la kiapo. Hapana wa kuizuia; kama yalivyo mauti hakuna wa kuyarudisha ila yule mwenye kuleta uhai na mauti.

Siku zitakapotikisika mbingu kwa mtikiso.

Yaani kani mvutano itaondoka, uzani baina ya sayari utaharibika na kutokea mparaganyo utakaoenea.

Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. Itakapotikisika mbigu ardhi itatetemeka na milima itaondoka sehemu zake.

Aya mbili hizi zinaashiria kusimama kiyama na kuharibika ulimwengu, ambapo viumbe watakusnywa kwa ajili ya hisabu.

Basi ole wao siku hiyo wanaokadhibisha. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.

Waliichezea dunia nayo ikawachezea, lakini hawakuiweza, kwa hiyo ikawapiga mweleka na ikawapeleka haraka kwenye Jahannam ambayo ni makazi mabaya.

Siku wataposukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu.

Watasukumwa kwa nguvu na Malaika wa adhabu watawaambia: Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukadhibisha! “Ionjeni adhabu iunguzayo. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyokwishatangulizwa na mikono yenu. Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.” Juz. 10 (8:50-51).

Je, huu ni uchawi, au hamuoni.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliwahofisha na Moto wa Jahannam wakamwambia wewe ni mchawi. Siku ya malipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawafanya ni kuni za Jahannam na awaambie, je mmeona sasa? Je, Muhammad ni mchawi? Je, adhabu ya kuungua ni uchawi? Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu, adhabu ni hiyo hiyo haipungui wala haiishi. Hakika mnalipwa kwa mliyokuwa mkiyatenda ya dhulma na ufisadi.

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَعِيمٍ {17}

Hakika wenye takua watakua katika Mabustani na neema,

فَاكِهِينَ بِمَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ وَوَقَاهُمْ رَبُّهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ {18}

Wakifurahi kwa yale aliyowapa Mola wao. Na Mola wao atawalinda na adhabu ya Motoni.

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {19}

Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyatenda.

مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ سُرُرٍ مَصْفُوفَةٍ ۖ وَزَوَّجْنَاهُمْ بِحُورٍ عِينٍ {20}

Wakiegema viti vya fahari vilivyopangwa safu. Na tutawaoza mahurulaini.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُمْ بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُمْ مِنْ عَمَلِهِمْ مِنْ شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ {21}

Na walioamini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja kitu katika vitendo vyao kila mtu ni rehani wa alichokichuma.

وَأَمْدَدْنَاهُمْ بِفَاكِهَةٍ وَلَحْمٍ مِمَّا يَشْتَهُونَ {22}

Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyopenda.

يَتَنَازَعُونَ فِيهَا كَأْسًا لَا لَغْوٌ فِيهَا وَلَا تَأْثِيمٌ {23}

Watapeana humo bilauri zisio na (vinywaji) vya upuuzi wala dhambi.

وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ غِلْمَانٌ لَهُمْ كَأَنَّهُمْ لُؤْلُؤٌ مَكْنُونٌ {24}

Na watawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizofichwa.

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ {25}

Wataelekeana wakiulizana.

قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ {26}

Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa.

فَمَنَّ اللَّهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ {27}

Basi MwenyeziMungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.

إِنَّا كُنَّا مِنْ قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ {28}

Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.