read

Aya 1 – 18: Alimwona Kwenye Mkunazi Wa Mwisho Maana

Naapa kwa nyota inapoanguka.

Mwenye tafsir Al-Bahrul-muhit ametaja kauli kumi kuhusiana na Aya hii. Iliyo karibu zaidi ni ile isemayo kuwa Makusudio ya nyota ni nyota yoyote, kwa sababu Alif na laam iliyoko katika neno hilo ni za jinsia. Na kwamba maana ya kuanguka nyota ni kuwa zitaanguka na kutawanyika katika anga siku ya kiyama, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na nyota zitakapotawanyika.” (82:1). Kwa sababu Qur’an inajitafsiri yenyewe. Katika kiapo hiki kuna ishara kuwa mwenye kumkana Muhammad (s.a.w.) atapata malipo yake Siku ya Kiyama.

Mwenzenu hakupotea, wala hakukosea, wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni wahyi uliotolewa.

Mwenzenu, ndiye anayeapiwa, ambaye ni Muhammad (s.a.w.) anatamka na kutenda kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, si kwa shaka wala kwa kutojua, au kupotea wala kwa msukumuo wa matamanio yake. Vipi asitamke na kutenda kulingana na wahyi na hali yeye amekuja kutengeneza na kumaliza ufisadi na tamaa?

Umbali Wa Pande Mbili

Aya hizi kuanzia 5 – 18, zinaashiria tukio maalum lisiloweza kujulikana isipokuwa kwa njia ya wahyi. Kwa sababu maudhui yake ni kujitokeza Jibril kwa Mtume mara mbili kwa sura yake halisi aliyomuumba nayo Mwenyezi Mungu na sio sura aliyozoea kuiona Mtume pale anapomletea wahyi.

Maneno yamekuwa mengi sana kuhusiana na Aya hizi; mpaka wengine wakathubutu kutaja wasifu wa Jibril na mbawa zake bila ya hoja wala dalili. Sisi tutafupiliza yale yanayofahamiushwa na dhahiri ya Aya na yanoingia akilini, bila ya kujilazimisha na kauli ya mfasiri au mpokezi; na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuombwa msaada:

1. Amemfundisha mwenye nguvu sana.

Kumfundisha Maana yake ni kumfikishia; yaani Jibril alimfikishia Muhammad (s.a.w.). Makusudio ya nguvu hapa ni sifa zinazomwandaa Jibril (a.s.) kuufikisha wahyi; kama vile kuhifadhi, uaminifu na uhakika; kama kwamba Nabii anausikia moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Dalili ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na hakika hiyo ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote. Ameiteremsha Roho mwaminifu.” Juz. 19 (26:192-193). Vile vile neno ‘amemfundisha,’ linaashiria hivyo.

Kwa hiyo Maana ni kuwa Jibril mwenye nguvu na mwaminifu, alimfkishia Muhammad (s.a.w.) wahyi kwa uhakika wake kama ulivyo katika ilimu ya Mwenyezi Mungu.

2. Mwenye umbo la sura, akatulia.

Hiyo ni sifa ya Jibril; yaani alimtokea Mtume (s.a.w.) sawasawa kama alivyoumbwa.

3. Naye yuko upeo wa juu kabisa.

Ni huyo huyo Jibril. Yaani alimpomtokezea Mtume kwa sura yake alikuwa amenyooka juu ya anga. Wafasiri wanasema: Upeo wa juu ni mawiyo ya jua; yaani mashariki na upeo wa chini ni magharibi. Kwa hali yoyote iwayo ni kuwa Makusudio yake ni kueleza kuwa Jibril sura yake ilitanda angani; wala si muhimu kuwa anga hiyo ilikuwa mashariki au magharibi.

4. Kisha akakaribia na akateremka. Akawa umbali wa pinde mbili, au karibu zaidi.

Hapa kuna maneno ya kutangulizwa; yaani aliteremka akakaribia. Maana ni kuwa Jibri baada ya kumdhirikia Mtume kama alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu na umbo lake kupanda hadi juu, alirudi kwenye sura aliyokuwa akikutana nayo Mtume wakati akimpa wahyi na akamkurubia mpaka akawa kiasi cha umbali wa pinde mbili au chini yake. Ni maarufu kuwa Jibril alikuwa akimjia Mtume kwa sura ya Dahiya Al-Kalbiy

5. Akampa wahyi mja wake alichompa wahyi.

Aliyetoa wahyi ni Mwenyezi Mungu na mja ni Muhammad (s.a.w.). Maana ni kuwa Jibril baada ya kurudia sura yake aliyokuwa akikutana na Mtume na kumkurubia, Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Muhammad (s.a.w.) mambo muhimu kupitia kwa Jibril.

6. Moyo haukusema uwongo uliyoyaona.

Yaani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimuona Jibril kwa macho yake, kama alivyomuumba; jicho halikukosea lilichokiona wala moyo hakutuia shaka kilichoonwa na jicho; bali alikuwa na yakini na akasadiki.

Je, mnabishana naye juu ya aliyoyaona?

Wanaambiwa washirikina kuwa je, mnamkadhibisha Muhammad na kubishana naye kwa aliyoyaona kwa macho yake na kuyaamini kwa moyo wake na akili yake; na hali nyinyi mumeujua ukweli wake, uaminifu wake, akili yake na usawa wake?

7. Na alimuona mara nyingine, penye Mkunazi wa mwisho. Karibu yake pana Bustani ya makazi.

Mtume alimuona Jibril mara nyingine. Makusudio ya Mkunazi wa mwisho ni mahali pa mwisho na ukomo wanapopafikia viumbe; hata Malaika. Kundi la wafasiri wamesema kuwa katika mbingu ya saba kuna mti ulio kuume mwa Arshi unaoitwa, Mkunazi wa mwisho!

Kauli hii inahitajia dalili. Vyovyote iwavyo sisi hatuna majukumu ya kuu- jua hasa maadamu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameunyamazia kuufafanua. Tunavyofahamu kutokana na Aya pamoja na maelezo yaliyokuja kwenye Juz.15 (17:1), ni kuwa Jibril alimchukua Mtume (s.a.w.) usiku wa Miraji na kuzunguka naye mbinguni mpaka akafikia umbali aliouita Mwenyezi Mungu Mkunazi wa mwisho. Hapo akasimama na hakuendelea.

Ama kuhusu Bustani ya makazi, kauli zimegongana katika tafsiri yake. Lakini dhahiri ni kuwa ni Pepo ya milele aliyoijaalia Mwenyezi Mungu kuwa ni malipo ya wale wanaomcha, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na ama yule mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake, na akaikataza nafsi na matamanio, basi hakika Pepo ndio makazi.” (79:40-41). Kwani Qur’an inajifasiri yenyewe.

Maana yanayopatikana ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimuona Jibril mara mbili kwa umbo lake, kama alivyo. Mara ya kwanza ni ile iliyoashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Naye yuko upeo wa juu kabisa;” na mara ya pili ni katika usiku wa Miraji pale alipozunguka naye mpaka akafika mahali pasipovukwa.

Haya ndiyo yote yaliyojulishwa na dhahiri ya Aya, au tuliyoyafahamu sisi kutokana na dhahiri ya Aya. Zaidi ya hapo – kwa maoni yetu – ni katika mambo ya ghaibu, yaliyofichwa.

Kilipoufunika huo Mkunazi kilichoufunuika.

Neno kufunika tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu yaghsha ambalo pia lina maana ya kuja. Inafaa kufasiri Aya kwa maana zote mbili, kwa sababu makusudio yake ni kuwa kwenye Mkunazi wa mwisho kunapatikana maajabu ya athari ya uweza Mwenyezi Mungu na ukuu wake yasiyokuwa na kipimo wala kudhibitiwa na akili, ndio maana Mwenyezi Mungu akayafumba na kuacha kuyafafanua.

Jicho halikuhangaika wala halikupetuka mpaka.

Kabisa! Jicho la Mtume halikuepuka hali halisi. Kila aliloliona kwa Jibril na mbinguni usiku wa Miraji ni haki na kweli.

Hakika aliona katika Ishara kubwa kabisa za Mola wake.

Kuona ishara alizozishuhudia Mtume katika miraji ziko zaidi ya mahisabu yote na wakati na mahali pote, ni muhali kuziona binadamu isipokuwa kwa uweza wa Mwenyezi Mungu na matakwa yake. Tumezungumzia Israi na Miraji katika Juz. 15 (17:1) kifungu cha: “Israi kwa roho na mwili.’

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ {19}

Je, mmemuona Lata na Uzza?

وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ {20}

Na Manata, mwingine wa tatu?

أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنْثَىٰ {21}

Je, nyinyi mnao watoto wa kiume na Yeye ndio awe na watoto wa kike?

تِلْكَ إِذًا قِسْمَةٌ ضِيزَىٰ {22}

Huo ni mgawanyo wa dhulma!

إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمْ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ بِهَا مِنْ سُلْطَانٍ ۚ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَمَا تَهْوَى الْأَنْفُسُ ۖ وَلَقَدْ جَاءَهُمْ مِنْ رَبِّهِمُ الْهُدَىٰ {23}

Hayo hayakuwa ila ni majina mliyowapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha dalili yoyote juu ya hayo. Hawafuati ila dhana tu na kipendacho nafsi. Na kwa hakika uwongofu ulikwishawafikia kutoka kwa Mola wao.

أَمْ لِلْإِنْسَانِ مَا تَمَنَّىٰ {24}

Je, mtu anakipata kila anachokitamani?

فَلِلَّهِ الْآخِرَةُ وَالْأُولَىٰ {25}

Ni wa Mwenyezi Mungu mwisho na mwanzo.

وَكَمْ مِنْ مَلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِنْ بَعْدِ أَنْ يَأْذَنَ اللَّهُ لِمَنْ يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ {26}

Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.