read

Aya 14 – 30: Kila Siku Yumo Katika Mambo

Maana

Amemuumba mtu kwa udongo mkavu kama uliookwa.

Makusudio ya mtu ni Adam baba wa watu.

Katika Juz. 14 (15: 26 – 31) Tumechanganya Aya nne; ambazo ni:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنْ صَلْصَالٍ مِنْ حَمَإٍ مَسْنُونٍ {26}

“Na hakika tulimuumba mtu kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.” Juz. 14 (15:26).

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ مِنَ الْمَاءِ بَشَرًا فَجَعَلَهُ{54}

Yeye ndiye aliyemuumba mtu kutokana na maji” Juz. 19 (25:54).

هِ كَمَثَلِ آدَمَ ۖ خَلَقَهُ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ {59}

“Ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.” Juz.3 (3:59) .

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ طِينٍ {2}

Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo.” Juz. 7 (6:2)

Huko tulithibitisha kuwa hakuna njia ya kujua asili ya mtu isipokuwa kwa wahyi utokao kwa aliyemuumba mtu. Na katika Juz. 8 (7:11) tumedokeza majibu ya nadharia ya Darwin.

Na akawaumba majini kwa ulimi wa moto.

Mara nyingi tumesema kuwa tunaamini kuweko majini kwa vile wahyi umeyathibitisha na akili haikani. Katika kufasiri kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na majini tumewaumba kwa moto wenye joto kali.”

Juz. 14 (15:27), tulisema kuwa wataalamu wamegundua aina ya vidudu ambavyo haviishi isipokuwa katika hewa ya sumu na aina nyingine haiwezi kupata uhai isipokuwa kwenye visima vya mafuta na vitu vinavyowaka.

Maana ni kuwa katika viumbe hai kuna vinavyotokana na maji na vinavyotokana na moto. Vile vile kuna vilivyo katika ulimwengu wa kuonekana na vilivyo kwenye ulimwengu wa ghaibu.

Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Ni kwa kuumbwa mtu kutokana na udongo au kuumbwa jini kutokana na ulimi wa moto?

Maana ya ulimi wa moto ni moto bila ya moshi. Nahofia wale wanaolazimisha wahyi uafikiane na sayansi wasiseme kuwa ulimi wa moto ni ishara ya kugunduliwa petroli na sipiriti!

Kukaririka kauli yake Mwenyezi Mungu: “Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili,” ni kwa kukaririka sababu ambazo ni neema zenye kuulizwa; sawa na unavyoweza kumwambia uliyemsaidia mambo tofauti: Nimekuokoa na adui yako aliyekuweza na nikakupa pesa, sasa ni lipi kati ya haya mawili unalolikataa? Tena nikakusomeshea watoto wako na nikakujengea nyumba, ni lipi kati ya haya mawili unalolikataa?

Kwa hiyo basi hakuna kukaririka wala msisitizo wa kitu kimoja; isipokuwa ni vitu mabalimbali.

Mola wa mashariki mbili na wa magharibi mbili.

Makusudio ya mashariki mbili na magharibi mbili ni mashariki ya jua na mwezi na magahribi ya jua na mwezi. Maana haya ndiyo yanayokuja haraka akilini na si mengineyo.

Hakuna mwenye shaka kwamba uhai mwingi unahitajia kuangaziwa na kuchwewa na jua na mwezi; bali wamesema kuwa maisha hayayezi kuwa ardhini bila ya hivyo.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Je, neema ya kuangaziwa au ya kuchwewa.

Anaziendesha bahari mbili zikutane; baina yao kipo kizuizi, haziingiliani.

Neno Bahari tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu bahr lenye maana ya maji mengi, yawe tamu au chumvi. Makusudio ya bahari mbili hapa ni maji ya bahari na ya mito.
Makusudio ya kizuizi hapa ni uweza wa Mwenyezi Mungu unaofanya zisichanganyike zikageuzana. Tazama tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَهُوَ الَّذِي مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ هَٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ وَهَٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ وَجَعَلَ بَيْنَهُمَا بَرْزَخًا وَحِجْرًا مَحْجُورًا {53}

“Naye ndiye aliyezichanganya bahari mbili, hii ni tamu mno na hii ni chumvi sana, na akaweka kinga kati yake na kizuizi kizuiacho.” Juz. 19 (25:53).

Bahari zina manufaa mengi na faida kwa viumbe wa Mwenyezi Mungu na waja wake.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Ni neema ya bahari au mito au nyingineyo?

Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani.

Wafasiri wengi wametatizika kufasiri Aya hii. Hilo ni kwa kuwa wao walikata kauli kuwa lulu haipatikanai isipokuwa kwenye maji chumvi tu, na Mwenyezi Mungu anasema kuwa inatoka kwenye maji chumvi na maji tamu. Wakatafuta visingizio vya kuleta taawili.

Lakini Razi amesema: “Inawezekana vipi kuamua kuwa lulu inatoka baharini tu, ikiwa waliotembea wameshindwa hata kuyajua yaliyoko nchi kavu wataweza kujua yaliyoko majini?

Ile kuwa wazamiaji hawakutoa lulu isipokuwa baharini, hakulazimishi kuwa haiwezi kupatikana kwingine. Dhahiri ya maneno ya Mwenyezi Mungu ndiyo inayofaa kuzingatiwa kuliko maneno ya watu.”

Sisi tunaunga mkono mantiki hii ya sawa, na inaungwa mkono na Sheikh Maraghi katika tafsiri yake aliposema: “Imethibitika katika ugunduzi wa sasa kwamba, kama inavyotolea lulu kutoka katika maji chumvi, vilevile inaweza kutolewa katika maji tamu. Pia marijani; ingawaje sana sana huwa zinatoka kwenye maji chumvi.”

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Je ni neema hii ndio manyoikadhibisha?

Shia Imamiya wameambiwa kuwa wao wanaitakidi kuwa makusudio ya bahari mbili ni Ali na Fatima, kizuizi ni Muhammad (s.a.w.) na lulu na marijani ni Hasan na Husein.

Mimi kwa wasifu wangu kuwa ni mshia ninakana kabisa madai haya wanayobandikizwa shia na kwamba wao wanaharamisha tafsiri ya undani. Ikiwa atapatikana mwenye rai hiyo basi itakuwa ni rai yake binafsi.

Hii pia inapatikana kwa sunni; kama ilivyoelezwa katika tafsiri zao; ikiwemo Adduril manthur ya Suyut wa madhehebu ya Shafiy, anasema: “Ametoa Ibn Mardawayh kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba bahari mbili ni Ali na Fatima, kizuizi ni Nabii na lulu na marijani ni Hasan na Husein. Vile vile ameyatoa haya kutoka kwa Anas bin Malik.”

Ya kushangaza zaidi kuliko haya ni yale aliyoyanukuu Ismail Haqqi, kati- ka tafsiri yake Ruhul-bayan, kutoka kwa baadhi ya ulama kuwa nusu ya wanane aliowaashiria Mwenyezi Mungu katika kauli yake:

 وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ {17}

“Na wanane juu ya hawa watachukua Arshi ya Mola wako,” (69:17),

Kuwa ni Abu Hanifa, Shafiy, Malik na Hambali!
Na ni vyake Yeye hivi viendavyo baharini vilivyoundwa kama vilima.

Maana ni kuwa vyombo vya majini vinatembea kwa manufaa ya watu.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa ikiwemo Juz. 21 (31:31).

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Je, ni kule kuumbwa kwenu na kuumbwa mali ghafi ya vyombo vya majini au ni kwa kutembea majini n.k.?

Kila kilicho juu yake kitatoweka. Na itabakia dhati ya Mola wako Mwenye utukufu na ukarimu.

Yeye ambaye imetukuka heshima yake, yuko hai kwa dhati yake; kama ambavyo amepatikana kwa dhati yake, na kila mwenye kupatikana kwa dhati hawezi kutoweka wala kubadilika. Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndio chimbuko la uhai na anayeutoa.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Je, ni utukufu wake au ukarimu wake na yasiyokuwa hayo?

Mwenyezi Mungu Na Mtu Na Ibn Al-Arabiy

Muhyiddin Ibn Al-arabiy, katika Futuhatul-Makkiyya kuhusiana na kauli yake Mwenyezi Mungu: Mwenye utukufu na ukarimu,’ ana maneno haya yafutayo:

“Hakika Mwenyezi Mungu ameunganisha ukarimu baada ya utukufu, kwa sababu mtu akisikia wasifa wa Mwenyezi wa utukufu bila ya ukarimu, basi atakata tamaa ya kufika kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa vile hajioni kuwa ana nafasi yoyote mbele ya Mtukufu.

“Ndio akaondoa Mwenyezi Mungu dhana hii, kwa mtu, kwa kuuunganisha ukarimu kwenye utukufu, kwa sababu maana ya sifa mbili hizi ni kuwa Mwenyezi Mungu hata kama ni mtukufu, lakini Yeye anamkirimu mtu na kumwangalia kwa jicho la huruma kwa kumfadhili na kumkirimu.

“Mtu akijua nafasi yake hii kwa Mwenyezi Mungu, basi anahisi ukarimu wake na kutambua kuwa lau asingelikuwa ni mkarimu asingejishughulisha na usaidizi huu. Hapo anazidi kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa sababu naye anajikuta ni mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu.”

Tunaunganisha kauli ya Ibn Al-arabi, kwamba mwenye kukana kuweko Mwenyezi Mungu atakuwa ameiangusha nafsi na mazingatio yote na kuikana dhati yake na utukufu wake bila ya kutaka. Kwa sababu atakuwa amemkosea yule aliyemfanya aweko na kumtukuza, na atastahiki adhabu:

 وَمَنْ جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَى الَّذِينَ عَمِلُوا السَّيِّئَاتِ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {84}

“Na Mwenye kutenda uovu hawalipwi wanaotendao uovu ila yale waliyokuwa wakiyatenda.” Juz. 20 (28:84).

Vinamwomba Yeye vilivyo katika mbingu na ardhi.

Makusudio ya kuomba hapa ni mahitajio. Maana ni kuwa viumbe vyote vinamuhitajia Mwenyezi Mungu katika kubakia kwake na katika hali zote; kama vinavyomuhitajia katika asili ya kuweko kwake, na kwamaba Yeye anavisaidia kuweko, lau anaviacha kwa muda wa kupepesa jicho tu, kusingelikuwa na kitu.

Kila siku Yeye yumo katika mambo.
Makusudio ya siku hapa ni wakati bila ya kuwa na mpaka. Maana ni kuwa hakuna chochote kinachokuwa ila kinagura kutoka hali moja hadi nyingine wakati wote. Ndio maana ikasemwa: “Ni muhali kudumu hali.” Na vyenye kuweko vinamuhitajia Mwenyezi Mungu katika hali zote. Mwenye nguvu anamhitajia Yeye katika kubakia nguvu zake, na mdhaifu pia anamhitajia kuondoa udhaifu wake.

Hiyo haimaanishi kuwa mtu aache kuhangakia na kufanya kazi kwa kumwachia Mwenyezi Mungu, hapana! Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha na akahimiza kuhangaika; ndiye aliyesema:

وَأَنْ لَيْسَ لِلْإِنْسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ {39}

“Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyahangaikia.” (53:39).

Maana yake hasa ni kuwa mtu afanye matendo kwa kuamini kuwa nyuma yake kuna nguvu iliyojificha ikimsaidia kufanya kazi na kumwandalia njia ya kufaulu.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Je, ni huko kuwasaidia kila wakati au ni neema nyinginezo?

سَنَفْرُغُ لَكُمْ أَيُّهَ الثَّقَلَانِ {31}

Tutawakusudia enyi wazito wawili.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {32}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَنْ تَنْفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانْفُذُوا ۚ لَا تَنْفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ {33}

Enyi makundi ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni! Hamtapenya ila kwa madaraka.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {34}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

يُرْسَلُ عَلَيْكُمَا شُوَاظٌ مِنْ نَارٍ وَنُحَاسٌ فَلَا تَنْتَصِرَانِ {35}

Mtapelekewa muwako wa moto na ufukizo; wala hamtanusurika.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {36}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

فَإِذَا انْشَقَّتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ وَرْدَةً كَالدِّهَانِ {37}

Itakapopasuka mbingu ikawa nyekundu kama mafuta.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {38}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

فَيَوْمَئِذٍ لَا يُسْأَلُ عَنْ ذَنْبِهِ إِنْسٌ وَلَا جَانٌّ {39}

Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {40}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

يُعْرَفُ الْمُجْرِمُونَ بِسِيمَاهُمْ فَيُؤْخَذُ بِالنَّوَاصِي وَالْأَقْدَامِ {41}

Watajulikana wakosefu kwa alama zao, basi watakamatwa kwa nywele zao za utosi na kwa miguu.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {42}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

هَٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي يُكَذِّبُ بِهَا الْمُجْرِمُونَ {43}

Hii ndiyo Jahannamu ambayo wakosefu wakiikadhibisha.

يَطُوفُونَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ حَمِيمٍ آنٍ {44}

Watakuwa wakizunguka baina ya hiyo na maji ya moto yanayochemka.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ {45}

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?