read

Aya 19 – 26: Lata Na Uzza

Maana

Je, mmemuona Lata na Uzza? Na Manata, mwingine wa tatu?

Wanaambiwa washirikina wa kikuraishi waliokuwa wakiabudu masanamu haya na kuyaita ni mabinti wa Mungu, kwa hiyo ndio wakayapa majina yenye ishara ya kike ya herufi ta na alif.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alizikejeli akili zao kwa kusema:

Je, nyinyi mnao watoto wa kiume na Yeye ndio awe na watoto wa kike? Huo ni mgawanyo wa dhulma!

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu yale wanayoyachukia.” Juz. 14 (16:62).

Hayo hayakuwa ila ni majina mliyowapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha dalili yoyote juu ya hayo, kwa sababu hayo ni mawe tu hayadhuru wala hayanufaishi.

Yametangulia mazungumzo kuhusu masanamu na ibada yake katika makumi ya Aya. Inatosha kuwa ni kuwarudi wanaoyaabudu na kuyatukuza, kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu hawatoumba nzi wajapojumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika atakaye na anayetakiwa.” Juz. 17 (22:73).

Mwanafasihi mmoja anasema: “Akikunyang’anya nzi maisha yako kwa kukuletea maradhi, ni nani anayeweza kukurudishia uhai huo? Na ikikutoka chembe moja tu ya chakula chako inayogeuka sukari katika matumbo yako, je wakemia wakikusanyika wote wataweza kukurudishia chembe yako?

Hawafuati ila dhana tu na kipendacho nafsi.

Makusudio ya dhana hapa ni ujinga. Mtu anayadhibiti matamanio yake kwa akili yake na ilimu yake. Akiwa ni mjinga au dhaifu wa akili, matamanio yake yatamhukumu na kumwongoza kwenye maangamizi.

Na kwa hakika uwongofu ulikwishawafikia kutoka kwa Mola wao, wakasema nyoyo zetu zimefunikwa na katika masikio yetu mna uziwi. Basi neno la adhabu likawathibitikia.

Je, mtu anakipata kila anachokitamani?

Washirikina walitamani shafaa ya masanamu, ndio Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kuwauliza, je, mtu anaweza kupata kila anachotamani? Kwa maneno mengine ni kuwa waabudu masanamu walichanganya ujinga na matamanio yanayopofusha na kutia uziwi, basi ujinga ukapanda juu ya ujinga mwingine.

Ni wa Mwenyezi Mungu mwisho na mwanzo. Ufalme na amri ni yake peke yake duniani na akhera.

Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.

Walisema kuwa sisi tunaabudu masanamu ili yatuombee kwa Mungu! Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawaambia kuwa Malaika wa mbinguni pamoja na ukubwa na utukufu wao nao hawataombea isipokuwa kwa idhini yake, vipi mawe yenye uziwi yaweze kuwaombea?

Tumezungumzia kuhusu shafaa katika Juz.1 (2:48) kifungu cha: ‘Shafaa.’

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ لَيُسَمُّونَ الْمَلَائِكَةَ تَسْمِيَةَ الْأُنْثَىٰ {27}

Hakika wasioamini Akhera wanawaita Malaika kwa majina ya kike.

وَمَا لَهُمْ بِهِ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ ۖ وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا{28}

Nao hawana ujuzi wowote wa hayo isipokuwa wanafuata dhana tu, na hakika dhana haifai kitu mbele ya haki.

فَأَعْرِضْ عَنْ مَنْ تَوَلَّىٰ عَنْ ذِكْرِنَا وَلَمْ يُرِدْ إِلَّا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا {29}

Basi mwachilie mbali anayeupa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.

ذَٰلِكَ مَبْلَغُهُمْ مِنَ الْعِلْمِ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنْ ضَلَّ عَنْ سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اهْتَدَىٰ {30}

Huo ndio mwisho wao wa ujuzi. Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi mwenye kuipotea njia yake, na Yeye ndiye anayemjua zaidi mwenye kuongoka.

وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى {31}

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo katika ardhi, ili awalipe waliotenda ubaya kwa waliyoyatenda, na waliotenda mema awalipe mema.

الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ وَاسِعُ الْمَغْفِرَةِ ۚ هُوَ أَعْلَمُ بِكُمْ إِذْ أَنْشَأَكُمْ مِنَ الْأَرْضِ وَإِذْ أَنْتُمْ أَجِنَّةٌ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ ۖ فَلَا تُزَكُّوا أَنْفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ {32}

Ambao wanajiepusha na madhambi makubwa na vitendo vichafu, isipokuwa makosa madogo. Hakika Mola wako ni Mkunjufu Naye anawajua sana tangu alipowaumba kutoka kwenye ardhi, na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijitakase nafsi zenu, Yeye anamjua sana mwenye takua.