read

Aya 20 – 24: Maisha Ya Dunia Ni Mchezo Na Upuzi

Maana.

Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na upuzi, na pambo, na kujifaharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an yenye hikima, ataona kuwa thawabu za Mwenyezi Mungu zimewekewa wanaoamini, wakatenda mema duniani na wakatekeleza haki na wajibu; na kwamba hakuna nyenzo ya kufikia wema wa Akhera isipokuwa kazi ya manufaa katika maisha ya dunia.

Ni kama mfano wa mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yana rangi ya njano kisha yakawa makapi.

Sifa hii inalingana na dunia kwa sababu haiudumu kwenye hali moja. Inakuwa kijani kisha manjano, inakuwa ngumu kisha laini na inatoa na kuzuia. Lau itampa mtu kila analolipenda, basi muda mchache tu inamnyang’anya kila kitu mpaka maisha yake yeye mwenyewe na ya watu wake.

Vile vile mfano unaendana na sifa za mtu duniani. Anakuwa kijana mwenye nguvu ya mifupa, kushupaa nyama yake na kuwa nyororo ngozi; kisha anazeeka na kuwa mnyonge, nyama zinasinyaa, mifupa inakuwa dhaifu na ngozi kuwa manjano. Kila siku zinavyoendelea ndivyo anavyozidi kuwa katika hali mbaya mpaka anakuwa kama makapi na kumalizika.

Ikiwa dunia iko hivi na mtu naye anakuwa hivyo, basi lililo bora kwake ni kuyafanyia kazi maisha ya daima isiyokwisha neema yake wala kuzeeka mkazi wake.

Na akhera kuna adhabu kali na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kuwa dunia haidumu raha yake wala tabu yake, sasa anataja kuwa Akhera ni thabiti kwenye hali moja tu. Neema yake ni ya kudumu na adhabu yake pia ni ya kudumu. Kwa vile inayosababisha neema ni radhi ya Mwenyezi Mungu na sababu ya moto ni ghadhabu zake na zote hizo ziko.

Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

Razi anamnukuu sahaba mtukufu Said bin Jubayr, kwamba amesema katika kufasiri Aya hii: “Dunia ni starehe ya udanganyifu kama ikikufanya upuuze kuitafuta Akhera, lakini kama itakupa mwito wa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kuitafuta Akhera, basi itakuwa ni starehe nzuri na nyenzo bora.”

Sahaba huyu mtukufu ni katika wanafunzi wa Mtume (s.a.w.) waliokuwa karibu naye.

Kimbilieni maghufira ya Mola wenu, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake.

Makusudio ya maghufira hapa ni sababu zake; kama vile toba na matendo mema. Baadhi ya wafasiri wamesema, ikiwa upana ni hivyo je, urefu? Wengine wakasema: imegunduliwa kuwa umbali wa ulimwengu hauna mwisho. Kwa hiyo basi upana utakuwa ni wa uhakika sio majazi.

Sisi hatufahamu upana isipokuwa ni ibara ya utukufu wa Pepo na upana wake usiokuwa na kiwango. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:133).

Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu kwa watu, lakini watu wengi hawashukuru.

Hakuna mwenye shaka kwamba utiifu ni sababu ya kuzidishiwa fadhila, bali ndio sababu ya fadhila ya Mwenyezi Mungu na radhi yake siku ya hukumu.

Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujaziumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

Maana ya dhahiri ya Aya hii yanaonyesha kuwa masaibu yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu; ni sawa yawe ni katika aina ya majanga ya maumbile; kama matetemeko na mafuriko, au yawe ya kijamii; kama vile vita ufukara na uadui.

Lakini haya siyo makusudio yake moja kwa moja kwa hukumu ya wahyi na akili. Ufafunuzi ni kama ufuatavyo:-

Masaibu Na Mwenye Idhlal

Mwenye Idhlal katika kufasiri Aya hii anasema: “Tamko kwa kuliachia kilugha halihusiani na heri au shari. Kila msiba unaotokea kwenye ardhi yote au kwenye nafsi ya mtu au wanaoambiwa, utakua uko katika kitabu tangu azali kabla ya kudhihiri ardhi na kudhihiri nafsi.”

Tunamuuliza mwenye Idhlal: ukiwa kweli unategemea dhahiri ya tamko na kuliachia kilugha, mbona hukufanya hivyo ulipokuwa unafasiri Aya hii: “Na misiba iliyowasibu ni kwa sababu ya ilivyotenda mikono yenu.” Juz. 25 (42:30). Je, umesahau katika tafsiri yako kuwa ulisema ninanunukuu: “Kila msiba uliomsibu mtu una sababu zake kutokana na ilivyofanya mikono yake.” Jalada la 7, uk.38, Juzuu ya 25.

Je, utakuwa unategemea dhahiri ya tamko na kuliachia kilugha hata kama hilo litafanya Aya mbili zigongane?

Je, pia utategemea dhahiri ya tamko likiwa litagongana na hukumu ya akili na uhalisia, na kufahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ana mkono, uso, usikizi na macho?

Je, uzayuni na ukoloni ambao ni chimbuko la masaibu na mabalaa yanayopatikana hivi sasa yanatokana na wao au yanotokana na Mwenyezi Mungu?

Ni jambo lisilowezekana kutokea mgongano baina ya Aya mbili kiuhakika ni kiuhalisi. Pia ni jambo lisilowezekana kugongana Aya na hukumu ya akili. Itakuwaje hivyo na hali imetokea kwa mwenye hikima mwenye ujuzi?

Ikitokea dhahiri ya Aya kugongana na Aya nyingine au kugongana na hukumu ya kiakili, tutajua dhahiri hii siyo aliyoikusudia Mwenyezi Mungu Mtukufu; isipokuwa ameliachia tamko kutegemea desturi yake ya kuleta ibara; kama kuleta ibara ya watu wa Kitabu kwa maana ya mayahudi na wanaswara. Au kuleta ibara kutokana na ilivyozoeleka kiakili; kama uweza wa Mwenyezi Mungu kuuletea ibara ya mkono. Au kuleta ibara kutegema Aya nyingine; kama Aya hizi zifuatazo:-

وَمَا أَصَابَكُمْ مِنْ مُصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ {30}

“Na misiba iliyowasibu ni kwa sababu ya ilivyotenda mikono yenu.” Juz. 25 (42:30).

 وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّهُ وَلَٰكِنْ أَنْفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ {117}

“Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wanajidhulumu wenyewe.” Juz. 4 (3:117).

ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي {41}

“Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa sababu ya iliyoyafanya mikono ya watu.”
Juz.21 (30:41).

Aya zote hizi na maana yake ni dalili mkataa kwamba makusudio ya Aya tuliyonayo siyo ya kidhahiri ya lugha na kwamba Mwenyezi Mungu ameiacha hivyo kwa kutegema aliyoyasema katika Aya hizo nyingine.

Kwa hiyo basi makusudio ya misiba ya ardhi, katika Aya tuliyonayo, ni majanga ya kimaumbile; kama vile matetemeko n.k. Na makusudio ya masaibu ya nafsi ni baadhi ya magonjwa yasiyokuwa na kinga wala hadhari n.k.

Ama makusudio ya misiba katika Aya zile tatu ni masaibu yanayotokana na binadamu mwenyewe; kama vile dhulma vita njaa n.k.

Ili msihuzunike kwa kilichowapotea, wala msifurahi kwa alichowapa.

Imam Aliy (a.s.) anasema: “Zuhudi yote iko katika matamshi mawili katika Qur’an; kisha akasoma Aya hii na akaendelea kusema: “Asiyekata tamaa kwa yaliyopita wala asifurahi kwa yanayokuja atakuwa ameichukua zuhudi kwa pande zake mbili.”

Hakuna asiyehuzunika na kufurahi; hata mitume pia. Isipokuwa makusu- dio ni furaha isimwingize mtu kwenye batili na huzuni isimtoe kwenye haki. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwamba yeye alisema wakati wa mauti ya mwanawe Ibrahim: “Jicho linalia na moyo unahuzunika wala hatusemi isipokuwa yanayomridhisha Mola wetu. Nasi tunakuhuzunikia ewe Ibrahim.”

Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna, anayejifaharisha.

Hakuna kitu kinachofahamisha ujinga kuliko kiburi na kujiona. Imam Aliy (a.s.) anasema: “Ana nini binadamu na kujifaharisha? Mwanzo wake ni tone la manii na mwisho wake ni mzoga. Hawezi kujipa riziki wala kujikinga na mauti.”

Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili.

Anayefanya ubakhili na akawaamuru wengine wafanye ubakhili, ndiye aliyekusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

مَنَّاعٍ لِلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ {12}

عُتُلٍّ بَعْدَ ذَٰلِكَ زَنِيمٍ {13}

“Mwenye kuzuia heri arukaye mipaka mwenye dhambi, mgumu, juu ya hayo ni mshenzi.”
(68:12-13).

Razi anasema hizi ni sifa za mayahudi. Ikumbukwe kuwa Razi alifariki mwaka 606 AH.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:37).

Na anayegeuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

Bakhili hajidhuru ila yeye mwenyewe, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi wala haumnufaishi utiifu wa mwenye kutii. Umetangulia mfano wake katika Juz. 26 (47:37).

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنْزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ ۖ وَأَنْزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّهُ مَنْ يَنْصُرُهُ وَرُسُلَهُ بِالْغَيْبِ ۚ إِنَّ اللَّهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ {25}

Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili wazi-wazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا وَإِبْرَاهِيمَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِمَا النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ ۖ فَمِنْهُمْ مُهْتَدٍ ۖ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ {26}

Na hakika tulimtuma Nuh na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao Unabii na Kitabu. Basi wapo miongoni mwao walioongoka, na wengi katika wao ni mafasiki.

ثُمَّ قَفَّيْنَا عَلَىٰ آثَارِهِمْ بِرُسُلِنَا وَقَفَّيْنَا بِعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ وَآتَيْنَاهُ الْإِنْجِيلَ وَجَعَلْنَا فِي قُلُوبِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ رَأْفَةً وَرَحْمَةً وَرَهْبَانِيَّةً ابْتَدَعُوهَا مَا كَتَبْنَاهَا عَلَيْهِمْ إِلَّا ابْتِغَاءَ رِضْوَانِ اللَّهِ فَمَا رَعَوْهَا حَقَّ رِعَايَتِهَا ۖ فَآتَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا مِنْهُمْ أَجْرَهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ {27}

Kisha tukafuatisha nyuma yao Mitume wetu, na tukamfuatisha Isa bin Maryam, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema. Na utawa wameuzua wao. Hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata. Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni mafasiki.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَآمِنُوا بِرَسُولِهِ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِنْ رَحْمَتِهِ وَيَجْعَلْ لَكُمْ نُورًا تَمْشُونَ بِهِ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {28}

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atawapa sehemu mbili katika rehema yake, na atawajaalia muwe na nuru ya kwenda nayo, na atawaghufiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

لِئَلَّا يَعْلَمَ أَهْلُ الْكِتَابِ أَلَّا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِنْ فَضْلِ اللَّهِ ۙ وَأَنَّ الْفَضْلَ بِيَدِ اللَّهِ يُؤْتِيهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ {29}

Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.