read

Aya 25 – 29: Chuma Kina Nguvu Nyingi

Maana

Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu.

Kila ambalo unajulikana uhakika kwalo basi hilo ni mizani, ni sawa uwe ni wahyi, akili au hisia; kama vile majaribio na ushuhuda. kwa hiyo basi kuunganisha mizani kwenye Kitabu ni kuunganisha mahsusi kwenye ujumla; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na alichopewa Musa na Isa na manabii kutoka kwa Mola wao.”

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwatuma mitume kwa hoja zinazojulisha juu ya utume wao na risala yao na kwa lile litakalowaongoza watu kwenye haki na uadilifu, ili wawe katika njia iliyonyooka.

Na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu.

Wafasiri wa kale walisema katika kufasiri Aya hii kuwa chuma ni nguvu katika vita, watu wanatengeneza panga na diraya. Pia wanatengeneza visu shoka na sindano. Mifano hii ilikuja kuakisi zama zao na maisha yao. Sisi tungelikuwa wakati wao, nasi tungelisema kama walivyosema. Na wao wangelikuwa zama zetu wangelisema: Chuma ni uti wa mgongo wa maisha katika nyanja zote.

Nyenzo za mawasiliano ya nchi kavu angani na baharini zinatokana nacho. Pia vyombo kadha anavyovihitaji mtu tajiri au fukara, madaraja, majengo, kuta na maghala, vyote vinahitajia chuma. Lau si chuma mtu asingelijua umeme na petrol. Chuma ni msingi wa ilimu nyinyi za kisasa, bali ndio kila kitu cha maendeleo ya karne ya ishirini.

Na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu.

Yaani atakayenusuru mafunzo ya mitume wa Mwenyezi Mungu hata kama hakuwaona.

Kila kitu katika maisha haya kina pande mbili: chanya na hasi; manufaa na madhara. Ikiwa chuma kina manufaa hayo, ya kumhudumia mtu, tuliyoyataja, basi vie vile kina madhara ya kumwangamiza mtu. Kabla ya kugunduliwa chuma mauji yalikuwa ni kwa makumi, lakini baada ya kugunduliwa mauji yamekuwa kwa mamilioni.

Hofu na utisho wanaoishi nao wa magharibi na wa mashariki, damu inayomwagika kama mito huko Cambodia, Laos, Vietnam, Guatemala na mashariki ya kati1, maangamizi yote haya na mengineyo ni natija ya nguvu ya silaha ya shari ya chuma dhidi ya wananchi na harakati za ukombozi.

Hapa ndio tunatambua siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu. Na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu.”

Yaani ameumba chuma ili awatie mtihani waja wake kwa yaliyomo ndani ya nyoyo zao ya heri na shari, na kudhihirisha wazi kwenye ulimwengu, ili apambanuke muovu ambaye anaifanya nguvu ni nyenzo ya kutekeleza matamanio yake na malengo yake, na apambanuke mwema ambaye anaona nguvu ni neema ya Mwenyezi Mungu na kuitumia kwa manufaa ya watu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema yake.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.

Atawaadhibu mataghuti madhalimu kwa mikono ya wenye haki ambao hawataki katika maisha haya isipokuwa uhuru, uadilifu na kuishi wote kwa utulivu na amani.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mapinduzi dhidi ya dhulma yanayotokea leo kila pembe ya ardhi. Hakuna mwenye shaka kwamba mapinduzi haya yana nguvu za Mwenyezi Mungu, hayatazuilika maadamu yanatafuta haki na uadilifu. Ama malipo ya mataghuti huko Akhera ni Jahannam, makao mabaya kabisa.

Na hakika tulimtuma Nuh na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao Unabii na Kitabu.

Mwenyezi Mungu alimtuma Nuh na Ibrahim kulingania kwenye haki, kila mmoja akafikisha risala ya Mola wake akapigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu; kama ilivyo habari ya Nuh katika Juz. 12 (11:25-49) na kuhusu Ibrahim katika Juz. 17 (21:51-74).

Basi wapo miongoni mwao walioongoka, na wengi katika wao ni wapotovu.

Yaani katika kizazi chao kuna baadhi ni wema, lakini wengi wao walikuwa bila dini wala dhamiri; kama walivyo watoto wa ulama wa dini.

Kisha tukafuatisha nyuma yao Mitume wetu, wengine wengi.

Baada ya Nuh na Ibrahim, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alituma mitume wengi; kama vile Hud, Swaleh, Musa n.k.

Na tukamfuatisha Isa bin Maryam, na tukampa Injili.

Waliendelea kufuatana mitume hadi Isa (a.s.) akiwa na Injil. Wakati huo ilikuwa ni mwongozo na nuru.

Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema.

Hao ni wale waliomfuta Bwana Masih na wakayatumia mafunzo yake kwa nukuu na kwa kiroho bila ya kugeuza yale yanayotamaniwa na nafsi zao. Hilo linaashiriwa na neno wakamfuata. Tazama mwanzo wa Juzuu ya saba.

Na utawa wameuzua wao. Hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata.

‘Ila’ hapa ni kwa maana ya lakini. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaelezea utawa, isipokuwa viongozi wa kinaswara ndio waliouanzisha kwa madai kuwa unawakurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa vile unawaweka mbali na dunia na starehe zake.

Pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaamuru utawa, bali amewahalalishia riziki njema; hata hivyo bado wao hawakujilazimisha na zuhudi ya utawa, bali waliufanya ni nyenzo ya matamanio na kutawala. Aya hii inafahamisha kuwa hakuna utawa katika Uislamu wala katika dini aliyokuja nayo Bwana Masih.

Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao.

Hao ni wale waliokuwa wafuasi wa Isa halisi na ukweli, waliokuwa wakiamini kwa kauli na vitendo kwamba umasihi ni upendo na huruma, ni usafi na ubinadamu, sio ubaguzi na chuki, dhulma na unyanyasaji, vita na mapinduzi, kuanzisha vita na vurugu wala sio silaha za maangamizi. Pia wakaamini kuwa Umasihi sio nembo za uongo kuzuia uhuru, kueneza hofu na wasiwasi katika nyoyo za waja wa Mwenyezi Mungu.

Na wengi wao ni mafasiki wakiongozwa na kambi ya ukoloni mambo leo na maadui nambari moja wa ubinadamu ambao wana sifa zote zinazowatoa kwenye umasihi wa kihaki na ukweli.

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu.

Yaani enyi ambao mmemkubali Mwenyezi Mungu, fanyeni kwa mujibu wa kuuamini kwenu. wala matendo yenu yasiende kinyume na kauli zenu.

Na muaminini Mtume wake. Mtiini Muhammad (s.a.w.) na mfuate sera yake na mwongozo wake.

Atawapa sehemu mbili katika rehema yake

Makusudio ya rehema hapa ni thawabu. Maana ni kuwa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akatenda kwa mujibu wa imani yake atakuwa na aina mbili ya tahawabu: thawabu za imani na thawabu za matendo.

Na atawajalia muwe na nuru ya kwenda nayo siku ya Kiyama.

Ambaye Mwenyezi Mungu hatamjalia nuru siku hii atahangaika kwenye giza na atatokeza kwenye machungu.

Na atawaghufiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Atawasamehe maasi yaliyopita, kwa vile Yeye ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu. Ibn Al-arabi anasema katika Futuhat: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakutanishi maghufira na toba wala na matendo mema, kwa hiyo hapana budi rehema na maghufira imwendee kwenye kuifanyia israf nafsi yake.” Na rehema yake imekienea kila kitu.

Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya kuwa hawana uweza ni kuwa wao hawatapata chcochote katika fadhila za Mwenyezi Mungu siku ya kiyama.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kesho atawaghufiria waliomwamini Muhammad (s.a.w.). Na mwenye kufanya mema atampa ujira wake mara mbili, kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu ni mkarimu. Vile vile wajue mayahudi kuwa na manaswara waliokataa kumwamini Muhammad (s.a.w.) kwamba wao hawana fungu la maghufira na rehema yake, kwa vile wamejizuia kumsadiki Muhammad (s.a.w.).

Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.

Anayowafadhili wale ambao wamemwamini Muhammad (s.a.w.), wala hakuna wa kuzuia alilolitaka, kwa sababu kila kitu kiko mikononi mwake naye ni muweza wa kila kitu.

  • 1. Mwandishi hapa alikuwa katika mwaka wa 1970