read

Aya 27 – 32: Dhana Haisaidi Kitu Mbele Ya Haifai

Maana

Hakika wasioamini Akhera wanawaita Malaika kwa majina ya kike.

Waliikadhibisha haki kwa ujinga na inadi. Kila moja kati ya mawili hayo linatosha kuwa ni tafsiri na sababu ya uzushi wao kwa Mwenyezi Mungu kwamba ana washirika, mke na watoto wa kike. Hawakutosheka kusema ana watoto mpaka wakawapa majina maalum.

Nao hawana ujuzi wowote wa hayo isipokuwa wanafuata dhana tu, ndio wakathibitisha vitu visivyokuwako wala kuwa na dalili yoyote isipokuwa njozi tu zinazopita vichwani mwao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwarudi kwa kuwaambia kuwa hajui yeye kama ana mabinti aliposema:

 قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ {18}

“Sema je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi? Ametakasika na ametukuka na hao wanaomshirikisha naye.” Juz. 11 (10:18).

Na hakika dhana haifai kitu mbele ya haki.

Lau watu wangelifuata dhana, mambo yasingelikwenda sawa katika maisha haya. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 11 (10:36).

Basi mwachilie mbali anayeupa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.

Maneno yaaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) lakini yanakusudiwa kila mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Maana ni kuwa usiwajadili wale ambao wamezama kwenye uasi na upotevu, wasioamini kitu wala kuona kima chochote isipokuwa nafsi zao na chumo lao:

وَإِنْ يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَا يُؤْمِنُوا بِهَا ۚ {25}

“Na wakiona kila ishara hawaiamini.” Juz. 7 (6:25).

Basi kuna haja gani ya kubishana nao. Tazama kifungu: ‘Haki na manufaa’ katika Juz. 3 (3:52-54) na kifungu: ‘Mjadala wa kijinga na upotevu.’ Juz.17 (22: 1-7).

Huo ndio mwisho wao wa ujuzi na haki. Hawana ujuzi, dini dhamiri, haki na msimamo isipokuwa anasa na kutukuza mali. Tazama Juz. 18 (25:7-16). Kifungu: ‘Mantiki ya watu wa pesa ni benki na ardhi.’

Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi mwenye kuipotea njia yake, na Yeye ndiye anayemjua zaidi mwenye kuongoka.

Ewe Muhammad! Mola wako anajua kuwa wale walioukadhibisha unabii wako hawakataziki na upotevu. Vile vile anajua kuwa wewe uko kwenye uongofu na wale wanaokufuata katika waumini. Kwa sababu Yeye amekizunguka kila kitu na ni muweza wa kumlipa mwenye kuamini na kuongoka na adhabu ya mwenye kupotea.

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo katika ardhi, ili awalipe waliotenda ubaya kwa waliyoyatenda, na waliotenda mema awalipe mema.

Aya hii ni kemeo na kiaga kwa yule aliyemwashiria Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: “Anayeupa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.”

Njia ya ukemeo ni kuwa dunia na Akhera ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye peke yake ndiye mmiliki wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Kwa hiyo atakayeiacha Akhera na akaitafuta dunia na akaihangaikia, tutampa hiyo dunia na katika Akhera hana isipokuwa adhabu; ambapo kila mtu atapata malipo ya matendo yake, ikiwa ni heri basi ni heri na ikiwa ni shari basi ni shari.

Ambao wanajiepusha na madhambi makubwa na vitendo vichafu, isipokuwa makosa madogo. Hakika Mola wako ni Mkunjufu wa maghufira.

Madhambi makubwa ni kama kufru, shirk na dhulma. Na kila linalopituka mpaka kwenye uovu ni katika vitendo vichafu na ni dhambi kubwa pia; kama vile zina na ulawiti. Ama madhambi madogo ni yale ambayo mara nyingi yanampitia mtu; isipokuwa wale maasumu; kama kuangalia na kukaa kwenye meza ya pombe. Tumezungumza kwa ufafanuzi katika Juz.5 (4:31).
Maana ya Aya ni kuwa mwenye kujing’oa kwenye madhambi makubwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) huumpa msamaha na hisani yake hata kama aki- fanya madhambi madogo. Lakini hii haimaanishi kwamba mtu anaruhusiwa kufanya madhambi madogo; hapana! Vinginevyo itakuwa ni halali; isipokuwa ni kwamba mwenye kujiepusha na madhambi makubwa awe na matumaini ya kusamehewa madogo kutoka kwa Mola wake. Vinginevyo ingelikuwa Pepo ni ya maasumu tu.

Imeelezwa katika Nahju-Bbalagha: “Dhambi kubwa ni ile aliyoidharau mtendaji… Na kuyakuza mtu maasi ya mwingine na kuadharau yake na kujiona ana twaa nyingi kuliko mwingine.”

Naye anawajua sana tangu alipowaumba kutoka kwenye ardhi, na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijitakase nafsi zenu, Yeye anamjua sana mwenye takua.

Ndio! Mwenyezi Mungu anamjua zaidi mtu kuliko anavyojijua yeye mwenyewe vyovyote atakavyokua na ilimu. Haiwezekani mtu kujijua kuliko anavyojuliwa na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyemfanya aweko na kumpa uhai, akamficha na atamfufua. Yuko naye akimjua tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake mpaka pumzi yake ya mwisho.

Zaidi ya hayo ni kuwa viungo vya mtu hata moyo wake ni shahidi wake mbele ya muumba wake. Shahidi mkali zaidi atakayetamka kumtakasa mtu na kufanya awe katika wenye ikhlasi ni matendo yake mema. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:49) na Juz. 18 (24:21).

أَفَرَأَيْتَ الَّذِي تَوَلَّىٰ {33}

Je, Umemwona yule aliyegeuka?

وَأَعْطَىٰ قَلِيلًا وَأَكْدَىٰ {34}

Na akatoa kidogo, kisha akajizuia?

أَعِنْدَهُ عِلْمُ الْغَيْبِ فَهُوَ يَرَىٰ {35}

Je, anayo ilimu ya ghaibu, basi ndio anaona?

أَمْ لَمْ يُنَبَّأْ بِمَا فِي صُحُفِ مُوسَىٰ {36}

Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa?

وَإِبْرَاهِيمَ الَّذِي وَفَّىٰ {37}

Na vya Ibrahim aliyetimiza ahadi?

أَلَّا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ {38}

Kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwingine?

وَأَنْ لَيْسَ لِلْإِنْسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ {39}

Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyahangaikia.

وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ {40}

Na kwamba mahangaiko yake yataonekana.

ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ {41}

Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu.