read

Aya 29 – 44: Hana Udhuru Mwenye Kuukana Utume Wa Muhamad

Maana

Aya hizi zinaashiria hali ya Mtume (s.a.w.) pamoja na washirikina pale alipowapa mwito wa Tawhid na kutupilia mbali ushirikina.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alianza kumwambia Mtume wake mtukufu kwa namna zifuatazo:-

1. Basi kumbusha! na wewe, kwa neema ya Mola wako, si kuhani wala mwendawazimu.

Endela na kazi yako ya kulingania kwa Mwenyezi Mungu na kuhadharisha adhabu yake; wala usijali na wayasemayo baadhi ya wapinzani kuwa wewe ni kuhani unayedai kujua ghaibu na wengine wakisema kuwa wewe ni mwendawazimu. Wewe kwa fadhila za Mwenyezi Mungu uko mbali kabisa na madai yao na urongo wao. Utakuwaje kuhani au mwendawazimu na hali Mwenyezi Mungu amekujaalia kuwa ni mwaminifu kwa wahyi wake na akakuchagua kwa risala yake?

2. Au wanasema: mshairi, tunamtazamia kupatilizwa na dahari kwa mauti.

Wengine wakisema ni mshairi anayezungumza kutokana na mawazo. Sema: tazamieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika wanaotazamia. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume wake kuwaambia kuwa ngojeni na mimi ninangoja, mtajua nani atakayefikwa na adhabu ifedheheshayo na kuwa katika wanaojuta.

3. Au akili zao ndio zinawaamrisha haya ya uzushi na uwongo?

Makusudio ya ya akili zao, neno liliofasiriwa kutoka ‘Ahlam’ yenye maana ya noto, ni matamanio yao ya hadaa.

4. Au wao ni watu waasi?

Wao wanajua fika kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu wa haki na ukweli, lakini wanaikana haki kwa uasi, inadi na kupupia vyeo vyao na chumo lao.

5. Au wanasema: Ameitunga hiyo Qur’an! Bali hawaamini tu haki wala hawajizuii na batili!

Basi na walete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli kuwa Qur’an ni ushairi au ukuhani. Wanao washairi wengi na makuhani.

6. Au wao wameumbwa pasipo kutokana na chochote kwa sadfa tu, hakuna muumbaji wala mpangiliaji, hakuna lengo wala majukumu? Je hakuna chochote kabisa sawa na wanavyopatikana wadudu kwenye uvundo na uchafu?

7. Au wao ndio waumbaji waliojiumba wenyewe kwa uweza wao?

8. Au wameziumba mbingu na ardhi?

Unaweza kuuliza: washirikina hawadai kwamba wao wamejiumba wala kuumba wengine; bali Qur’an imenukuu kukiri kwao kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba na akaumba mbingu na ardhi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ مَنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ {87}

“Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu!”
Juz. 25 (43:87).

Pia amesema:

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ مَنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ ۖ {61}

“Na ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu.” Juz. 21 (29:61).

Sasa je, kuna utetezi gani wa kauli yake Mwenyezi Mungu: “Au wao ndio waumbaji au wameziumba mbingu na ardhi?”

Jibu: wao kwa upande wa nadharia wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu, lakini kwa upande wa kimatendo wanafanya kama anavyofanya asiyemwamini Mungu wala kukubali kuwa yuko. Bali matendo yao yanajulisha kuwa wao wanadai ni waumbaji na miungu. Haya ameyadokeza Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

Bali hawana yakini. Wasifu huu unawahusu wengi hivi sasa wanaodai kumwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.

9. Au wanazo hazina za Mola wako.

Ikiwa wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, je, basi wanadai kuwa Mungu amewaachia idara ya milki yake, kuchagua manabii wake, kugawanya riziki na umri kwa waja? Umetangulia mfano wake katika Juz. 25 (44:32).

10. Au wao ndio wenye madaraka kwa viumbe wote, atake Mwenyezi Mungu au asitake?

11. Au wanayo ngazi ya kusikilizia?

Ikiwa wao hawadai kitu katika hayo je, basi wanadai kuwa wamepanda kwa Mwenyezi Mungu na wakamsikia akisema kuwa Muhammad ni mwongo?

Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi!

Haya ndio mantiki ya haki na uadilifu na ukomo wa kumfanyia haki hasimu. Kila mtu anaweza kudai anavyotaka, hata ilimu ya ghaibu, lakini kwa sharti ya kuleta ushahidi wazi wa madai yake; vinginevyo atakuwa ni mzushi mrongo.

12. Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi mna wavu- lana?

Hakuna tofauti kabisa baina ya kusema kwao Muhammad ni mshairi, kuhani, mwendawazimu na kusema kwao kuwa Mwenyzi Mungu ana wasichana na wao wana wavulana. Uzushi kwa Mtume hauishilii tu kwa kusema kuwa yeye ni mwendawazimu wala kwa kumnasibishia Mwenyzi Mungu washirika au watoto; bali kila mwenye kuhalalisha haramu au aka- haramisha halali atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume.

13. Au wewe unawaomba ujira, kwa hiyo wanalemewa na gharama?

Kwanini wamemkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu? Je amewalazimisha gharama inayowashinda kuitekeleza?

14. Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wanaandika?
Je, wao ni waandishi wa wahyi mbele ya Mwenyezi Mungu wakisajili riziki na umri na yule watakayemchagua katika manabii, kwa hiyo Mwenyezi Mungu hakuwapa jina la Muhammad kulisajili?

15. Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini walio kufuru ndio watakaotegeka.

Hii ndio hakika yao. Wao hawataki chochote isipokuwa vitimbi na uovu kwa Muhammad (s.a.w.), lakini vitimbi vitawarudia wao wenyewe, kwa sababu: “vitimbi viovu havimpati ilia mwenyewe” Juz. 22 (35:43)

16. Au wanaye mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanaowashirikisha naye.

Ni nani huyo na yuko wapi huyo mungu ambaye atawaepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu itakapowashukia. Mwenyezi Mungu ametakata kabisa kuwa na mfano na mapinzani.

Na hata wangeona pande linatoka mbinguni linaanguka wangesema: Ni mawingu yaliyobebana.

Hata wangeiona adhabu, ana kwa ana, wangelifanya kiburi na kusema haya ni mawingu na sarabi tu. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلَوْ فَتَحْنَا عَلَيْهِمْ بَابًا مِنَ السَّمَاءِ فَظَلُّوا فِيهِ يَعْرُجُونَ {14}

لَقَالُوا إِنَّمَا سُكِّرَتْ أَبْصَارُنَا بَلْ نَحْنُ قَوْمٌ مَسْحُورُونَ {15}

“Na lau tungeliwafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda. Basi wangelisema: Macho yetu yamelevywa; bali sisi ni watu waliorogwa.” Juz. 14 (15:14-15).

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakumwachia udhuru wowote yule mwenye kukadhibisha au kuukadhibisha utume wa Muhammad (s.a.w.), ila akane kuweko Mwenyezi Mungu kabisa.

فَذَرْهُمْ حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي فِيهِ يُصْعَقُونَ {45}

Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakaangamizwa.

يَوْمَ لَا يُغْنِي عَنْهُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنْصَرُونَ {46}

Siku ambayo hila zao hazitawafaa kitu, wala wao hawatanusuriwa.

وَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا عَذَابًا دُونَ ذَٰلِكَ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {47}

Na hakika waliodhulumu watapata adhabu nyengine isiyokuwa hiyo, lakini wengi wao hawajui.

وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ {48}

Na ingojee hukumu ya Mola wako. Kwani wewe hakika uko machoni mwetu. Na mtakase kwa kumsifu Mola wako unaposimama.

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَإِدْبَارَ النُّجُومِ {49}

Na usiku pia msabihi, na zinapokuchwa nyota.