read

Tahreef: Jee Quran imepunguzwa au kuongezwa?

Jee Shia huamini tahreef?

Kwa kujibu suala kuhusu 'yaliyotajwa kwenye kitabu cha Al-Kafi kwamba Quran iko na Tahreef, inasemekana kuwa Imam Ali (a.s) ndiye pekee aliyehifadhi Quran yenyewe, na Uthman alipokuwa Khalifa aliichukua Quran hii kwa sababu ilikuwa na majina ya Ahlul Bayt ndipo Quran tuliyo nayo ikapatikana. Kwa hali hiyo basi yasemekana Ma-Shia wanayo Quran yao ya kisiri. Tunajibu suala hili kama ifuatavyo:

Kwanza tunaanza kwa kueleza maana ya neno hili 'Tahreef'. Tahreef ni kuongezwa au kupunguzwa kwa aya kutoka kitabu kitakatifu cha Quran.

1. Tahreef ya Quran imepingwa sana na wengi wa wanavyuoni wa Ki-Shia kwa sababu zifuatazo:

(a) Quran yenyewe yathibitisha ya kwamba 'Allah pekee ndiye Mwenye kuilinda na kuihifadhi Quran; Tazama Sura Hijr (15) Aya 9.

(b) Imam Ali (a.s) katika hotuba zake zilizotolewa wakati wa ukhalifa wake zinawaita watu kutafuta uongofu kutoka kwa Quran hii ambayo tuko nayo hivi sasa. Tazama hotuba 176, 198.

(c) Hadith ya Thaqalain (vizito viwili) imetajwa na wapokezi wa Kisunni na Shia kwa pamoja kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema, "Naacha nyuma vitu vizito viwili vyenye thamani, mkivifuata vyote viwili kamwe hamtapotea …" Na kama Quran imebadilishwa, basi vipi itaweza kuongoza watu?

(d) Riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Maimamu watukufu wa Mashia zaonyesha wazi kuwa Quran ndio njia ya kuhukumu ukweli kutoka kwa upotofu, hivyo basi riwaya inakanusha kinachosemwa na Quran ni potofu / batili na kikataliwe, sisi (maimamu) hatujakisema.

(e) Wanavyuoni wengi wa Ki-Shia wamethibitisha utakatifu wa kitabu (Quran) ambacho ni kitukufu kutoka kitambo kwa mfano Sheikh Sadooq, Sayyid Murtadha, Sheikh Toosi, Sheikh Bahaai, Sayyid Ibn Tawoos, Qadhi Shushtari, Sheikh Hurr Amili, Sheikh Kashif al-Ghitaa, Sayyid Al-Khui, Imam Khomeini na wengine.

(f) Mwisho kuna wachache miongoni mwa wanavyuoni wa Ki-Shia wenye kuamini kuwepo na Tahreef katika Quran lakini wao wanategemea riwaya ambazo ni:

- Dhaifu katika usahihi wake.
• Baadhi ya wasimulizi hawajulikani kabisa.

• Hata tukichukulia kuwa baadhi ni sahihi mbele ya ushahidi mwingi wa kuzipinga riwaya kama hizi zitafasiriwa kumaanisha kuwa Quran nyengine ilikuwa na maelezo zaidi kutoka kwake Imam Ali (a.s) sio chochote cha kuongezea maneno ya mwanzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

2. Kwa kusema kweli wachache miongoni mwa wanavyuoni wa Ki-Sunni pia huamini Tahreef kama inavyoonekana katika mifano iliyotajwa hapo chini:

(a) Qurtubi katika Tafsiri yake (Juzu 14, ukurasa 113) amesema kutoka kwa Ubayy bin Ka'b (kwamba) sura Ahzaab (yenye aya 73 sasa) ilikuwa ndefu kama sura Baqarah (yenye aya 286) wakati wa Mtume (s.a.w.w.) na ilikuwa pamoja na aya juu ya Rajm (kupigwa mawe).

(b) Vile vile anasema (Juzu 14 ukurasa 113) kutoka kwa Bi-Aisha kwamba wakati wa Mtume (s.a.w.w.) sura Ahzaab ilikuwa na aya 200 lakini iliponakiliwa hawakuweza kupata zaidi ya aya zilizopo sasa.

(c) Suyooti katika Al-Itqaan yake (Juzu 1, Ukurasa 67) anaandika kwamba Quran iliyokusanywa na Ubayy ilikuwa na sura 116 (sio 114 za hii leo).

(d) Ibn Salaam katika Al-Nasikh wal Malik kwamba, wakati wa Mtume (s.a.w.w.) tulikuwa tukisoma sura ndefu sawa na Baqarah (sura) lakini ninakumbuka tu aya moja toka kwake (hiyo sura), 'Kama mwana wa Adam angekuwa na mabwawa mawili (2) ya dhahabu angetaka la tatu, angekuwa na matatu (3) angetamani la nne, hakuna chochote kitakachomshibisha tumbo la binadamu ila changarawe, Mungu humsamehe atubiaye.

(e) Suyooti katika Tafsir yake, Al-Durr-al-Manthoor (Juzu 5, Ukurasa 180) anasimulia kutoka kwa Umar bin Khattab kwamba sura Ahzaab ilikuwa ndefu kama vile (sura) Baqarah na ilikuwa pamoja na aya juu ya Rajm.

Taarifa fupi ya mwisho

Ni wachache tu miongoni mwa Masunni na Mashia wanaoamini Tahreef. Wengi wamepinga vikali uwezekano wa kupatikana mabadiliko katika neno lake Mungu.

Mwenyezi Mungu amfungulie njia na uongofu kwa mwenye kutafuta ukweli.

Kwa maelezo zaidi soma kitabu 'Shia na Quran' au tuma maswali yako kwa:

Bilal Muslim Mission of Kenya
P.O. Box 82508
Mombasa
Kenya