read

Hii ni Makala ya Mahari ya Damu.

Mahari ya Damu

*****

Wakati vita vya Siffin vilipokaribia kumalizika na majeshi ya Sham (Syria) kushindwa, Amr Aas alitumia njama moja ambayo iliwasaidia Washamu wasishindwe na mapigano yakasimama.

Amr Aas alipoona kwamba majeshi ya Sham yatashindwa tu, akaamrisha Misahafu itundikwe kwenye mikuki ikiwa ni ishara kwamba "tuko tayari Kitabu cha Mwenyezi Mungu kiwe ni hakimu baina yetu na nyinyi."

Masahaba wote wa Ali bin Abu Talib (AS) waliokuwa na busara waling'amua mapema kwamba hiyo ilikuwa ni hila ya kutaka kusimamisha mapigano ili wasishindwe, kwani kabla ya hapo Ali alipendekeza jambo hilohilo lakini Washamu hawakukubali.

Lakini kikundi kimoja cha watu wenye akili fupi na ambao huangalia yaliyo dhahiri tu, walisimamisha mapigano bila ya kujali nidhamu ya kijeshi na amri ya amiri jeshi. Isitoshe, wakamwendea Ali na wakamshikilia atoe amri haraka mapigano yasimamishwe kabisa kwenye medani ya vita. Walikuwa wakiitakidi kwamba kama mtu angepigana katika bali hiyo basi ingekuwa anapigana na Qur'ani!!! Ali aliwaambia: "Msidanganyike na jambo hilo ambalo ni ujanja tu. Qur'ani inatuamrisha tuendelee na mapigano. Wao hawakuwa wala hawako tayari kufuata Qur'ani. Tofauti baina yetu na wao inatokana na suala la kufuata Qur'ani. Sasa wakati tunapokaribia kupata ushindi na kuwamaliza ndipo wanatumia mbinu hii."

Waasi wakasema: "Baada ya wao kusema rasmi kwamba Qur'ani iamue baina yao na yetu, kupigana dhidi yao hakuruhusiwi. Tangu sasa kupigana dhidi yao ni kupigana dhidi ya Qur'ani. Ikiwa hutoamrisha jeshi kurudi nyuma haraka sisi tutakukata wewe vipandevipande hapahapa."

Kupigana hakukuleta faida tena. Mgawanyiko mkubwa ukaanza kutokea katika jeshi la Ali. Lau Ali angeshikilia msimamo wake, kadhia ingemalizikia katika hali mbaya sana kwa faida ya adui na kushindwa kwake. Akaamrisha mapigano yasimamishwe kwa muda na wapiganaji waondoke kwenye medani ya vita.

Amr Aas na Muawiyah walipoona kwamba njama yao imefaulu walifurahi bila kiasi. Furaha yao iliongezeka zaidi walipoona kwamba kumetokea hitilafu na mfarakano miongoni mwa wafuasi wa Ali. Lakini hakuna hata mtu mmoja - Muawiyah au Amr Aas au mwanasiasa yeyote mwingine - ambaye aliweza kutambua kwamba kadhia ndogo kama hiyo ingekuwa ni chanzo cha kubuniwa aina moja ya itikadi katika masiala ya dini ya Kiislamu ambayo kwayo ingeundwa madhehebu moja ya hatari ambayo baadaye ingeleta matatizo makubwa kwake yeye Muawiyah na makhalifa wengine kama yeye.

Kwa hivyo, wakatokeza watu wenye fikra kama hizo ambao walikuwa ni waasi (wabaghi) wa jeshi la Ali, na walijulikana kwa jina la Khawarij, yaani waliotoka nje. Katika siku hiyo ya historia, Makhawariji hao walitumia udikteta mkubwa katika kusimamisha vita na kulazimisha kutolewe uamuzi. Waliagana kwamba kila upande wamteue mtu wao mmoja ambaye atawawakilisha katika kutoa maamuzi kwa mujibu wa misingi ya Qur'ani. Kwa upande wa Muawiyah aliteuliwa Amr Aas. Kwa upande wa pili, Ali alitaka kumteua Abdullah bin Abbas ambaye angeweza kumkabili Amr Aas. Lakini hapo tena Makhawariji wakamwingilia Ali katika uteuzi wake kwa kisingizio kwamba kwa kuwa mwamuzi lazima awe mtu asiyependelea upande wowote na kwa kuwa Abdullah bin Abbas alikuwa ni sahaba na jamaa wa Ali, hivyo wakampinga na wao wenyewe wakamteua mtu mwingine asiyefaa.

Maamuzi yakamalizika bila kupatikana natija wala mawafikiano yoyote kutokana na ujanja alioutumia Amr Aas.

Kisa cha maamuzi kilipita kipumbavu kabisa na hakijaleta faida hata kidogo kwa jamii na hata kwa Muawiyah na Amr Aas. Faida walipata Muawiyah na Amr Aas kutokana na tukio hilo ni kusimamisha vita, kusahabisha mfarakano kati ya wafuasi wa Ali, na kuwapatia fursa ya kutosha ya kudhatiti majeshi yake na harakati zake.

Kwa upande wa Makhawariji, ilipowadhihirikia kwamba mbinu iliyotumiwa ya kuchomeka Misahafu katika mikuki na kupendekeza kufanywe maamuzi ilikuwa ni hila na ujanja wa Muawiyah na Amr Aas, wakafahamu kosa walilolifanya, lakini kosa hilo walilitafsiri hivi kwamba kwa kuwa binadamu kimsingi hana haki ya kuhukumu (kutawala) na kuamua, hivyo hukumu ni haki ya Mwenyezi Mungu tu na mwamuzi ni Qur'ani.

Makhawariji walitaka kusahihisha kosa lao, lakini njia waliyoitumia iliwafanya wafanye makosa mengi mengine na ya hatari zaidi.

Kosa lao la kwanza lilikuwa ni la kijeshi na kisiasa. Na kosa Ia kijeshi hata liwe la ukubwa gani linahusu wakati na mahali maalum na linaweza kusahihishwa. Lakini kosa lao la pili lilikuwa ni la kifikra lililozua falsafa isiyo sahihi katika masiala ya jamii ya Kiislamu, falsafa au itikadi ambayo ilihatarisha msingi wa Uislamu na isiyoweza kusahihishwa.

Kutokana na msingi wa fikra hiyo, Makhawariji wakatunga mwito mmoja usemao: "Laa-hukm iIlallaah", yaani isipokuwa Mwenyezi Mungu hakuna mtu mwenye haki ya kuwahukumu na kuwatawala watu.

Ali (AS) aliwaambia: "Maneno hayo ni sawa lakini mnayatumia kwa lengo lisilo sawa. Hukm (hukumu) maana yake ni kanuni (sheria). Utungaji wa sheria ni haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya yule aliyeruhusiwa na Mwenyezi Mungu. Lakini makusudio ya Makhawariji katika mwito huu ni kuwa hukumu (utawala) ni haki ya Mwenyezi Mungu tu ambapo ukweli ni kuwa jamii ya wanadamu kwa vyovyote vile wanahitajia kuwa na mtawala na kiongozi atakayetekeleza sheria."

Ilibidi baadaye Makhawariji wasawazishe kwa kadiri maalum itikadi yao.

Kutokana na fikra hiyo kwamba ni dhambi kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuhukumu, Makhawariji walitubia kwa sababu ya kuhusika na dbambi hiyo. Na wakamtaka Ali atubie pia kwa sababu yeye alikubali kufanywe maamuzi na kutolewe hukumu mwisho wake. Ali aliwajibu kwamba: "Kusimamisha vita na kutaka kufanywe maamuzi kulikuwa ni makosa yenu. Nyinyi ndio wenye kubeba makosa hayo wala si mimi. Lakini mimi sikubaliani nanyi kusema kwamba asili ya kuhukumu kwenyewe ni kosa au hakuruhusiwi."

Makhawariji walishikilia itikadi na fikra zao na wakamtakafiri Ali kwa kuruhusu kwake hukumu. Hatua kwa hatua, fikra na itikadi hizo zikaimarika na kugeuka kuwa ni madhehebu moja ya Kiislamu ambayo ilihitalifiana katika mambo mengi na Waislamu wengine. Madhehebu hiyo ikawa na sifa ya ukatili na kuchukulia mambo dhahiri yake. Katika kuamrisha mema na kukataza maovu hakuna sharti lolote bali ni lazima kutekeleza bila ya kujali na kuwa na hofu.

Ali (AS) hakuwasumbua Makhawariji katika muda wote ambao walitosheka na kutangaza itikadi yao tu, na hakuwajali ingawa walimwita kafiri (walimtakafiri). Hakuwafungia haki zao za kusaidiwa kutoka mfuko wa taifa (Baitul Maal); isitoshe aliwavumilia pia na kuwapa uhuru wa kutangaza itikadi yao na kujadiliana. Lakini walipoanzisha rasmi uasi wao kwa kisingizio cha kuamrisha mema na kukataza maovu, aliwatia adabu na kuwakomesha.

Katika Nahrawan, vilipiganwa vita kati ya Ali na Makhawariji, na Ali akawashinda kwa ushindi mkubwa.

Kupigana na Makhawariji kulikuwa ni kazi ngumu sana kwa sababu walikuwa ni watu wenye imani, na maadui na marafiki wanakiri kwamba walikuwa ni watu wasiosema uwongo. Walikuwa wakisema kinagaubaga, wakiabudu sana, wakisoma sana Qur'ani, wakikesha usiku kwa kufanya ibada na kusali na wengi wao walikuwa na alama za sijida kwenye mapaji ya nyuso zao, lakini kwa wakati huohuo walikuwa majahili na wenye mawazo finyu. Uislamu walioujua wao haukuwa wenye mvuto, hamasa au roho.

Ni watu wachache tu walioweza kujitolea kupigana na watu wa aina hiyo na kumwaga damu zao. Lau si kuwepo mtu mtukufu na mpiganaji shujaa kama Ali (AS) basi askari wake wasingepigana na Makhawariji. Ali alichukulia vita dhidi ya Makhawariji kuwa ni fahari kubwa aliyoipata yeye. Alisema: "Mimi ndiye niliyeweza kuzima moto wa fitina na hakuna mtu yeyote aliyethubutu kuchukua hatua kama hivo." Hakika hali ndiyo hivyo ilivyokuwa, kwani Ali peke yake ndiye ambaye hakuutilia maanani udhahiri wa ibada na unyofu wao na alikuwa akijua kwamba ucha Mungu na utakatifu wa kujigamba ulikuwa ni adui wa hatari sana kwa dini. Ali (AS) alitambua kwamba kama falsafa -ambazo kwa kawaida huwa na wafuasi wengi miongoni mwa watu wa kawaida - zingeota mizizi katika ulimwengu wa Kiislamu, basi Waislamu wangepatwa na msiba wa kuwa na akili fupi na ujahili, na mti wa Kiislamu ungekauka toka mizizini. Kupigana na Makhawariji kwa mawazo ya Ali hakukuwa ni kupigana na jeshi la elfu kadhaa ya watu bali kulikuwa ni kupigana na ukaidi wa kifikra, mawazo ya kijahili na falsafa potofu kuhusu masiala ya jamii ya Kiislamu. Ni nani ghairi ya Ali aliyeweza kuingia kwenye medani ya aina hiyo?

Vita vya Nahrawan vilikuwa ni pigo kubwa kwa Makhawariji kwa kadiri kwamba walishindwa kupata mwanya katika dunia ya Kiislamu kama walivyokuwa wakitegemea. Mapigano ya Ali dhidi yao yalikuwa ni ushahidi bora kabisa kwa makhalifa waliomfuatia katika kuhalalisha na kuwajibisha vita vyao dhidi ya Makhawariji. Lakini wale Makhawariji waliobaki wazima hawakukomesha harakati zao.

Makhawariji watatu walikutana mjini Makka kuzingatia hali ya dunia ya Kiislamu na wakafikia uamuzi kwamba balaa zote na migogoro yote inayoikumba dunia ya Kiislamu chanzo chake ni watu watatu - Ali, Muawiyah na Amr Aas.

Ali (AS) ndiye aliyekuwa kiongozi wao wa kijeshi wa awali. Na Muawiyah na Amr Aas ndio ambao kutokana na njama yao ya kisiasa na mbinu ya kijeshi walisababisha kuundwa kwa madhehebu hiyo ya hatari.

Watu watatu hao walikuwa, Abdulrahman bin Muljim, Burak bin Abdullab na Amr bin Bakr Tamimi. Makhawariji hao wakakubaliana na kula kiapo kwenye Kaaba kwamba watawaua Ali, Muawiyah na Amr Aas usiku wa kuamkia tarehe 19 (au 17) mwezi wa Ramadhani. Wakakubaliana kwamba Abdulrahman bin Muljim amwue Ali, Burak bin Abdullah amwue Muawiyah na Amr bin Bakr amwue Amr Aas. Baada ya makubaliano hayo na uamuzi huo wakaachana, na kila mmoja akashika njia yake kuelekea alipopewa kazi ya kuua. Abdulrahman alielekea Kufa (Iraq) makao makuu ya ukhalifa wa Ali (AS). Burak alifunga safari kwenda Sham (Syria) mji mkuu wa utawala wa Muawiyah. Na Amr bin Bakr alikwenda Misri ambako Amr Aas alikuwa liwali (gavana).

Wawili kati yao, yaani Burak bin Abdullah na Amr bin Bakr hawakutekeleza kazi muhimu, kwa sababu Burak ambaye alipewa kazi ya kumwua Muawiyah aliweza usiku huo wa miadi kupiga pigo moja tu la upanga kwenye tako Ia Muawiyah ambaye akatibiwa na kupata nafuu. Amr bin Bakr ambaye alitumwa kumwua Amr Aas hakuwa akimjua. Kwa bahati, usiku huo wa miadi Amr Aas alikuwa mgonjwa na hakuweza kwenda msikitini na badala yake akamtuma Kharija bin Abi Habiba al-Amiri kusalisha kwa niaba yake. Amr bin Bakr kwa kudhania kwamba bwana huyo alikuwa Amr Aas alimpiga upanga na kumwua. Baadaye akafahamu kuwa amemwua mtu mwingine. Aliyeweza kutekeleza njama hiyo kati ya watatu hao alikuwa ni Abdulrahman bin Muljim tu.

Abdulrahman aliingia mjini Kufa. Hakumwelezea mtu yeyote dhamiri na nia yake. Mara kwa mara alitaka kughairi kutekeleza njama hiyo na akawa akiogopa sana, kwa sababu hadhi ya Ali ilikuwa kubwa sana kwa kadiri kwamba ilimtisha hata katili kujaribu kumwua. Sadfa zilizotukia Sham na Misri ziliwasaidia kuwaokoa Muawiyah na Amr Aas. Lakini sadfa ilivotukia Iraq ikawa ndiyo sababu ya Abdulrahman kuazimia kutekeleza njama yake. Lau si hiyo sadfa ya kumuashiki (kumpenda) mwanamke mmoja, basi Abdulrahman angeghairi kutekeleza njama yake ya hatari.

Siku moja Abdulrahman alikwenda kuonana na Khawariji mmoja. Huko alijuana na mwanamke mmoja aitwaye Qutaam ambaye baba yake aliyekuwa Khawariji aliuawa katika vita vya Nahrawan. Qutaam alikuwa mwanamke mrembo sana na mchangamfu. Abdulrahman alipomwona Qutaam kwa mara ya kwanza, moyo wake ulipiga na akasahau mapatano ya Makka. Akaamua atumie umri wake wote uliobakia kustarehe naye na asahau fikra zote alizokuwa nazo.

Abdulrahman akamtaka Qutaam akubali aolewe naye. Qutaam alikubali pendekezo lake. Lakini alipomtajia vitu alivyotaka avitoe kama mahari yake, Abdulrahman alipigwa na bumbuazi. Qutaam alisema: 'Mahari yangu ni dirham elfu tatu, mtumwa mmoja, kijakazi mmoja na damu ya Ali bin Abu Talib!!!"

Abdulrahman akajibu: "Nipo tayari kutoa pesa, mtumwa, mjakazi na kitu kingine ukipendacho, lakini kumwua Ali si kazi rahisi. Kwani hatutaki kuishi pamoja? Vipi nitaweza kumkabili Ali na kumwua kisha nivuke salama?" Qutaam akasema: "Mahari yangu ndiyo hiyohiyo nillyotaja. Ndiyo, huwezi kumwua Ali katika medani ya vita lakini unaweza kumwua akiwa katika hali ya kuabudu. Ikiwa utavuka salama basi maisha yetu yote tutaishi pamoja kwa starehe, na ikiwa utauawa basi malipo utakayopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni makubwa na bora zaidi. Isitoshe, mimi ninaweza kukupa watu wengine ambao watakusaidia ili usiwe peke yako."

Abdulrahman ambaye alikufa juu ya Qutaam akaazimia tena kumwua Ali (AS) kwa sababu ya ashiki hiyo. Hivyo, kwa mara ya kwanza akadhihirisha yaliyo moyoni mwake na akasema: "Ukweli ni kuwa mimi nilikimbia kutoka mji huu tangu zamani na sasa nimerejea ili nimwue Ali bin Abu Talib." Qutaam alifurahishwa sana na maneno hayo. Alimpata mtu mwingine aitwaye Wardan na akamwamuru amsaidie Abdulrahman. Siku moja Abdulrahman alionana na rafiki yake mmoja aliyekuwa akimwamini na mwenye fikra kama yeye aitwaye Shabib bin Bajura, akamwambia:

"Je uko tayari kushiriki katika kazi ambayo itakupa heshima ya duniani na Akhera pia?"

"Kazi gani?"

"Kumwua Ali bin Abu Talib."

"Mungu akulaani! Unasema nini!? Kumwua Ali? Mtu ambaye ana jina zuri katika Uislamu?"

"Ndiyo! Lakini yeye amekuwa kafiri kwa sababu ya kukubali kwake maamuzi. Jina lake zuri na huduma zake hata ziwe nyingi kiasi gani katika Uislamu hazifai. Isitoshe, katika Nahrawan aliwaua ndugu zetu waliokuwa wasalihina na wacha Mungu. Hivyo sisi tunaweza kisheria kumwua yeye kwa kulipiza kisasi."

"Vipi utaweza kumkabili Ali?"

"Rahisi. Tutamvizia msikitini. Atakapokuja kusali sala ya asubuhi tutamshambulia kwa panga tutakazoficha ndani ya kanzu zetu na tutammaliza."

Abdulrahman akamshawishi sana mpaka Shabib akakubali kushirikiana naye. Kisha akamchukua Shabib katika msikiti wa Kufa kumjulisha kwa Qutaam. Wakati huo Qutaam alikuwa akitawa msikitini. Qutaam alisema:

"Vizuri sana. Wardan atakuwa pamoja nanyi. Usiku wowote mtakaoamua, kwanza fikeni kwangu." Abdulrahman alisubiri mpaka usiku wa Ijumaa kuamkia tarehe 19 Ramadhani kama alivyoagana na wenzake waliokutana Makka. Usiku huo ulipoingia alikwenda pamoja na Shabib kwa Qutaam. Qutaam alichukua vitambaa vya hariri na akawavisha kwenye vifua vyao. Wardan alikuwa tayari pia, na wote watatu wakakaa karibu na mlango wa msikiti ambao Ali (AS) huingilia humo siku zote. Usiku huo ulikuwa ni usiku wa kukesha na kufanya ibada; na watu watatu hao wakajishughulisha kuabudu na kusali kama watu wengine.

Chuki ilikuwa ikisokota nyoyo za watu watatu hao kwa kadiri kwamba walikuwa wakirukuu na kusujudu bila ya kuonyesha uchovu wowote ili waabudio wengine wasishangae na kugundua hali isiyo ya kawaida.

Ali (AS) kwa upande wake alipanga ratiba mahsusi ya mwezi wa Ramadhani kwa ajili yake.

KiIa siku alikuwa akifuturu katika nyumba moja ya wanawe. Alikuwa hali zaidi ya matonge matatu. Na alipokuwa akaiambiwa na wanawe ale zaidi, alijibu: "Napenda wakati wa kuonana na Mola wangu tumbo langu liwe linaniuma njaa." Mara kwa mara alikuwa akisema "Kufuatana na ishara nilizoashiriwa na Mtume Mtukufu (SAW), karibu ndevu zangu za nyeupe zitabadilishwa rangi yake na damu ya kichwa changu."

Usiku huo Ali (AS) alikuwa mgeni wa bintiye Umm Kulthum. Athari za msisimko na tumaini zilidhihirika usoni mwake. Baada ya kuwalaza akakaa katika msala wake na kushughulika na ibada.

Karibu na alfajiri, Hasan alikwenda kwa baba yake. Ali akamwambia mwanawe kipenzi: "Mwanangu! Leo usiku sijalala kabisa na nimewaamsha watu wa nyumbani, kwani leo ni usiku wa (kuamkia) Ijumaa ukisadifu usiku wa Qadr. Lakini nikiwa katika hali ya kuka, ghafla usingizi ulinichukua kidogo na nikamwota Mtume Mtukufu, na nikamwambia: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Watu wako wamenitaabisha sana.' Mtume Mtukufu akajibu: 'Waapize.' Mimi niliwaapiza na kuomba: 'Ewe Mola wangu! Niondoe kwa haraka zaidi ili unifufue pamoja na walio bora kuliko wao. Watumie mtu atakayewafaa wao ambaye ataonekana mbele yao kuwa mbaya kuliko mimi.'"

Wakati huohuo akaja mwadhini wa msikiti na kumkumbusha Ali kwamba wakati wa sala ulikuwa unakaribia. Ali akaelekea msikitini. Nyumbani mwa Ali walikuwepo mabata wachache ambao walianza kupiga makelelewakati huo. Mmojawapo kati ya watu wa nyumbani alitaka kuwanyamazisha, Ali akamkataza na akamwambia: "Waache! Makelele yao ni maombolezo."

Huko nyuma, Abdulrahman na wenzake walikuwa wakimngojea Ali. Hakuna mtu aliyejua siri ya mpango wao isipokuwa Qutaam na Ash'ath bin Qays - mtu duni ambaye alipinga uadilifu wa Ali na aliingiliana na Muawiyah. Tukio moja dogo lililotukia nusra mpango huo ufichulike, lakini ukafichika tena kwa kutukia tukio jingine. Ash'ath alimsogelea Abdulrahman na akamwambia: "Muda mfupi umebaki mpaka mapambazuko. Pakipambazuka mtafedheheka. Tekelezeni haraka kazi yenu." Hujr bin Adi - aliyekuwa miongoni mwa masahaba waaminifu wa Ali - alisikia maneno hayo ya mafumbo aliyosema Ash'ath kumwambia Abdulrahman, na akatia shaka kwamba kuna njama wanayotaka kufanya. Hujr alikuwa ndiyo kwanza amerejea safarini. Farasi wake alimweka mbele ya msikiti. Huenda alikuwa amerejea baada ya kutumwa kwa kazi muhimu na alikuwa anataka kumpa ripoti Amirul Au'miniyn Ali (AS).

Hujr aliposikia maneno ya Ash'ath akamlaani na akatoka msikitini kumfuatia Ali ili kumkinga kutokana na hatari, lakini wakati huohuo alipokuwa Hujr anaelekea nyumbani kwa Ali, Ali alikuwa akipita njia nyingine kuelekea msikitini, hivyo wakakoseana njia.

Juu ya kuwa wana wa Ali mara kwa mara walimwomba baba yao wawaruhusu wamwekee walinzi wa kumlinda, lakini Imam Ali hakuruhusu na alikuwa akitoka na kurudi nyumbani peke yake. Hata usiku huo pia aliombwa tena awekewe wajinzi wa kumhifadhi lakini akakataa tena.

Ali (AS) akaingia msikitini na akaita: "Enyi watu! Sala! Sala!" Katika kiza hicho makelele ya "Hukumu ni ya Mwenyezi Mungu tu, ewe Ali, si yako!" yakavuma msikitini na dharuba mbili za panga zilizokuwa ziking'ara zilifuatana kwa muda mdogo. Dharuba ya kwanza iliyopigwa na Shabib ilikosea na kupiga ukuta, lakini dharuba ya pili ambayo ilipigwa na Abdulrahman bin Muljim ilimpata Ali kwenye kichwa. Wakati huohuo Hujr akarejea msikitini, lakini alipofika alisikia sauti ya watu wakilia: "Amirul Mu'miniyn ameuawa shahidi! Amirul Mu'miniyn ameuawa shahidi!"

Maneno aliyosema Ali (AS) mara tu baada ya kupata dharuba ya upanga yalikuwa: "Naapa kwa Rabi wa Kaaba! Nimefuzu!" na "Msimwache mtu huyo akimbie!"

Abdulrahman, Shabib na Wardan wote wakakimbia. Wardan hakutambulikana kwa sababu hakusogea karibu. Shabib alipokuwa akikimbia alikamatwa na sahaba mmoja wa Ali. Akamnyang'anya upanga wake na akamkalia juu ya kifua chake amwue. Lakini kwa kuwa watu wengine walikuwa wakikusanyika, aliogopa kwamba wasije wakakosea kumtambua yeye na wakamwua yeye badala ya Shabib. Hivyo akaondoka kwenye kifua chake na Shabib akakimbia nyumbani kwake. Binamu yake alipofika nyumbani kwake na kufahamu kwamba Shabib alishiriki katika mauaji ya Ali (AS), haraka akatoka kwenda kuchukua upanga wake na akamwendea Shabib na kumwua.

Abdulrahman alikamatwa, akafungwa mikono yake na akapelekwa msikitini. Watu walipandwa na hamaki sana kwa kadiri kwamba walitaka kumkata vipandevipande.

Ali (AS) alisema: "Nileteeni mimi Abdulrahman!" Na alipoletwa mbele yake akamwuliza "Je, mimi sijakufanyia wema?!"

"Kwa nini?"

"Basi kwa nini umefanya jambo hili?"

"Kwa vyovyote vile, upanga huu niliuweka kwenye maji ya sumu kwa muda wa siku arobaini na nikamwomba Mwenyezi Mungu kwa upanga huu auliwe kiumbe mbaya kabisa."

"Dua yako imekubaliwa kwa sababu karibu wewe mwenyewe utauawa kwa upanga huuhuu."

Kisha Ali (AS) akawaambia jamaa zake:

"Enyi wana wa Abdul Muttalib! Jihadharini msije mkawashika watu na kuuawa kwangu kukawa ni kisingizio. Msimtuhumu mtu kwa kosa la kushiriki katika jinai hiyo au kosa jingine. Msimwage damu!"

Tena akamwambia mwanawe Hasan:

"Mwanangu! Mimi kama nitabaki mzima, ninajua nitakalomfanyia mtu huyu. Na nikifa, usimpige zaidi ya pigo moja tu la upanga kwani yeye amenipiga pigo moja tu. Msije mkamkata vipandevipande. Msimkate sikio, pua an ulimi, kwa sababu Mtume (SAW) amesema: 'Jihadharini msimkate mtu vipandevipande hata akiwa mbwa atafunaye.' Mtendeeni vyema mfungwa wenu [Ibn Muljim]. Mpeni chakula na nguo!"

Kwa amri ya Imam Hasan, Athir bin Amr, tabibu na mtaalamu mashuhuri aliitwa. Akamwangalia Ali (AS) na akasema: "Upanga ulikuwa na sumu ambayo imeingia katika ubongo wake. Hivyo, matibabu yoyote hayatomfaa."

Ali (AS) hakuishi zaidi ya saa arobaini na nane tangu alipopigwa upanga na Ibn Muljim. Hakupoteza wakati wake bure bali kila dakika alikuwa akitoa nasaha na miongozo. Alitoa wasia huu wenye vifungu ishirini ambao uliandikwa:

Huu ni wasia wa Ali, mwana wa Abu Talib. Ali anashuhudia kuwa hakuna Mungu ila Mmoja tu. Na anashuhudia kuwa Muhammad (SAW) ni mja na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amemtuma kwa mwongozo na dini ya haki ili ishinde dini zote. Hakika sala yangu, na ibada yangu, na uhai wangu, na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allah, Rabi wa ulimwengu, Asiye na mshirika. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha.

Mwanangu Hassan! Nakuusia wewe, wanangu wote, ahali ya nyumbani na kila mwenye kupokea risala hii mambo yafuatayo:

1. Mcheni Mwenyezi Mungu na jitahidini mbakie katika dini ya Mwenyezi Mungu mpaka mtakapokufa.

2. Yapangeni vizuri mambo yenu na jirekebisheni wenyewe kwa wenyewe, kwani nimemsikia babu yenu (Mtume Mtukufu SAW) akisema: "Kujirekebisha wenyewe kwa wenyewe ni bora zaidi kuliko kusali na kufunga. Yanayoharibu dini ni ufisadi na hitilafu."

3. Msisahau kuwaangalia wazee, ndugu na jamaa zenu, kwani kuunga ujamaa hurahisisha hesabu ya mtu mbele ya Mwenyezi Mungu.

4. Allah, Allah na mayatima! Wasikae na njaa na bila ya mlezi.

5. Allah, Allah na majirani zenu! Mtume Mtukafu (SAW) ametuusia sana majirani zetu hata tukadhani kwamba anataka wawe na sehemu katika urithi wetu.

6. Allah, Allah na Qur'ani! Msije mkapitwa na wengine katika kuifuata.

7. Allah, Allah na sala! Kwani ni miongoni mwa misingi ya dini yenu.

8. Allah, Allah na Nyumba ya Mungu (Kaaba)! Msiache kuhiji madhali mko hai au mtakosa fursa hiyo.

9. Allah, Allah na Jihadi! Piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu, nafsi zenu na ndimi zenu.

10. Allah, Allah na zaka! Zaka huzima moto mkali wa Mwenyezi Mungu.

11. Allah, Allah na dhuria (wazawa) wa Mtume Mtukufu! Wasije wakaonewa.

12. Allah, Allah na masahaba wa Mtume! Mtume Mtukufu ameagizia sana juu yao.

13. Allah, Allah na maskini na mafakiri! Washirikisheni katika maisha yenu.

14. Allah, Allah na watumwa! Agizo la mwisho la Mtume Mtukufu lilikuwa juu yao.

15. Jitahidini kufanya kazi yenye ridhaa ya Mwenyezi Mungu wala msijali maneno ya watu.

16. Watendeeni watu wema na ihsani kama Qur'ani inavyoamrisha.

17 .Msiache kuamrisha mema na kukataza maovu, kwani mkiacha mtakabiliwa na maovu; hapo tena kila mtakapoomba hamtajibiwa.

18. Nakuusieni mzidishe uhusiano na marafiki zenu na mtendeane mema. Msitengane wala msivunje uhusiano wenu.

19. Saidianeni katika kazi za kheri mmoja mmoja na kwa pamoja. Na jiepusheni katika kushirikiana katika madhambi na katika mambo yanayosababisha uadui.

20. Mcheni Mwenyezi Munga, kwani adhabu yake ni kali.

Mwenyezi Mungu akulindeni nyote katika hifadbi Yake, na aupe mwafaka umma wa Mtume Mtukufu (SAW), ili uweke heshima yenu na heshima ya Mtume Mtukufu. Nakuwekeni katika amana ya Mwenyezi Mungu, na salamu ziwe juu yenu.

Baada ya wasia huo, Imam Ali bin Abi Talib hakusema kitu isipokuwa Laa ilaaha illallaah (Hakuna mungu ila Allah) mpaka aliporejea kwa Mola wake.