Sharia Zinazo Wahusu Watoto Wa Kike: Utangulizi

Ni jambo la wajibu juu ya (kila) mtu kujifunza mas’ala ambayo yanamtokea mara kwa mara. (Hii ni kauli ya Wanavyuoni Ndani ya Vitabu vinavyohusu Matendo ya Kisharia.)
Hakika kipindi cha ujana kinahesabika kuwa ndiyo fursa yenye thamani katika kujipatia maarifa na kuyavuta kutoka kwenye vyanzo vya elimu ambavyo mtu atafaidika navyo muda wote wa uhai wake.

Kila umri wa mwanadamu unavyosonga mbele, ndivyo majukumu yake yanavyozidi na maisha yake kuwa na msongamano. Kwa hali hiyo basi hukosa fursa ya faragha itakayomruhusu kujifunza yale yanayomlazimu miongoni mwa kanuni za sharia, na maoni ya wanachuoni wa sharia, ambazo nyingi miongoni mwa hizo huenda atazihitajia katika maisha yake hapo baadaye.

Bila shaka mwanadamu anahitaji kuwa na wigo katika kufanya mabadiliko ya kibinadamu ndani ya safari yake ya maisha. Na wigo huu ni mambo matatu yafuatayo:-

Kwanza: Utashi. Pili: Maarifa, na tatu: Ni Uwezo wa kusubiri na kuyavumilia matatizo mpaka afikie kwenye lengo. Kwa hali hiyo basi, mtu mwenye (tabia ya kuwa na) matarajio (bila kujituma) hawezi kuyafikia baadhi ya matarajio yake au yote, isipokuwa tu kama atakuwa amebeba ndani ya moyo wake utashi na mapenzi ya dhati katika kuiendea njia hiyo. Inampasa (mtu huyu) ajiandae kwa silaha ya maarifa na ujuzi utakaomnufaisha katika hilo, na awe na uwezo wa kusimama kidete kukabiliana na vikwazo na matatizo.

Na zaidi ya hayo yote ni kuwa; mwenye kupita njia ya haki na mwenye kutafuta wema wa dunia na akhera, anahitaji huruma na msaada wa Mwenyezi Mungu. Kadhalika (anahitaji kupata) uangalizi na usaidizi kutoka kwa Imamu wa zama hizi (Imamul-Mahdi a.s.) ili aweze kuendelea, na kuimarika juu ya njia ya uongofu wa Mwenyezi Mungu mpaka mwisho wa njia.

Tumeandika mafunzo haya ambayo yanahusu kanuni za wanawake, ili nasi tupate kutoa mchango (wetu) miongoni mwa wale wenye mapenzi ya kuchukua maarifa (ya dini) kutoka kwenye chem chem asilia ya mafunzo ya sharia kutoka kwa kizazi cha watu wa nyumba ya Mtume s.a.w. Kisha juu ya hayo yameongezwa mas’ala na uchambuzi mwingine, ambapo yamefikia hapo yalipo sasa.

Wakati tunapo kiwasilisha kitabu hiki mbele ya dada zetu waumini (wa kawaida) na wale wahubiri wa kike wenye kufuata nyayo za Bibi Fatmah Zahraa (a.s) na bibi Zainab, tunataraji mtatupa maoni na rai zitakazo tun- ufaisha ili tuweze kuzitumia kwenye chapa zitakazofuatia.

Kipindi hiki tulicho nacho, ni kipindi cha kumbukumbu ya miaka kumi na minane tangu kuondoka kwa mmoja miongoni mwa waalimu wakubwa wa sharia ya ki-Islamu na muasisi wa jamuhuri ya ki-Isilamu ya Iran iliyobarikiwa, naye ni Imam Khomein (Mwenyeezi Mungu amrehemu).

Tunamwomba Mwenyeezi Mungu Mtukufu Atuongoze katika yale Ayapendayo. Na (tunamuomba) ayakubali na kuyaridhia matendo yetu (mema). Na (tunamuomba pia) aturuzuku maombezi ya Mtume Muhammad (s.a.w.), na kizazi chake kilichotakasika. Na mwisho wa maombi yetu tunasema: “Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu Mola Mlezi wa Viumbe.”

Mustafa Ranjbar Shirazi.
E- mail: Ranjbar85@yahoo.com