3.Aliyoyafanya Yazid Alipotawala

Kwa ufupi, anavyotueleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29 - 41 wa kitabu chake hicho, alifanya yafuatayo:

1. Alimpelekea habari Liwali wake wa Madina wa wakati huo, naye ni Khalid bin Hakam, awaapishe mabwana hawa: Hussein bin Ali bin Abi Talib, Abdalla bin Umar bin Al Khattab, Abdalla bin Al Abbas na Abdalla bin Zubeir. (Abdur Rahman bin Abi Bakr hakuwamo; alikuwa ashakufa). Alimwamrisha “awaapishe yamini kali kabisa kuwa wamekwisha mkubali Yazidi kuwa ndiye Khalifa wa Waislamu wote. Na kuwa wakienda kinyume naye, mali yao yawe halali yake, wake zao waachike na watumwa wao wawe mahuru.”

2. Liwali huyo alipowaita Imam Hussein a.s. na Abdalla bin Zubeir, waliomba waachwe mpaka siku ya pili. “Kufika majumbani mwao tu”, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 30),“waliwaaga watu wao wakatoka kwa siri kwenda Makka kukaa huko kwani mwenye kuweko huko huwa katika amani…” Yazidi, kupata habari hiyo tu, alihamaki “akamtoa ( Liwali huyo) katika Uliwali wake.”

3. Alipotawala Yazid, kimabavu kama tulivyokwisha kuona, watu wa Al Kufa (Iraq) walimpelekea Imam Hussein a.s. “mabarua ya kumhimiza aende huko Iraq, azatiti vita huko kumuondoa huyo asiyestahiki kuwa Khalifa wa Waislamu”. Hata hivyo, Imam Hussein a.s. hakwenda papo hapo, bali alimtuma binami yake (Muslim bin Aqyl) aende huko ili amjulishe ukweli wa mambo ulivyo. Alipopata habari hiyo, Sheikh Abdalla anatueleza (uk. 34-35), Yazid “alimchagua Liwali qatili, dhalimu, jabbar, shujaa, anayemchukia Sayyidna Ali na kizazi chake, aliyekuwa akiitwa Ubeydillah bin Ziyad ambaye baba yake alithibitishwa na Muawiya, kwa siyasa tu, kuwa ndugu yake.

Akatiwa katika kabila yake ya Bani Umayya hali ya kuwa hakhusiani naye hata chembe, wala hakhusu Uqureshi hata kidogo, bali wala Uwarabu. Ni mtu mwanaharamu tu aliyekuwa hodari sana hata akampinga Muawiya kweli kweli. Akaona amthibitishe kuwa ndugu yake na amwachie amri ya Iraqi yote". Hivyo akawa mwana haramu wa kwanza, katika historia ya Uislamu, kufanywa mwana halali!

4. Baada ya kumchagua Liwali huyo, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 35), Yazid alimpa amri hii: "Muuwe huyu Muslim bin Aqyl, na kila waliokuja pamoja naye, na kila waliompokea, na kila walio pamoja naye; na mfunge umuadhibu jamaa na jirani wa kila mmoja katika hawa, usiwe na huruma na yeyote." Na hivyo khaswa ndivyo ilivyokuwa. "Alifanya kama alivyoamrishwa na Yazid, akawamaliza hao wote alioamrishwa awaue, na akawafunga hao alioamrishwa awafunge…"

Katika kitabu chake, Sheikh Abdalla S. Farsy hakueleza jinsi alivyouliwa Muslim bin Aqyl. Lakini vitabu vyengine vya historia vinaeleza kwamba alichukuliwa mpaka juu ya kasri moja, akakatwa kichwa ambacho kilitupwa chini kikifuatishwa na pingiti lake. Baadaye kichwa hicho kikapelekwa kwa Yazid!

5. Kama tulivyokwisha kuona humu uk. 1 - 3, baada ya Imam Hussein a.s. na aliokuwa nao kuuwawa kikatili na kukatwa vichwa vyao, Yazid (alipopelekewa vichwa hivyo) alikamata kifimbo, Sheikh Abdalla S. Farsy anatueleza (uk 40), "akawa anayagonga meno ya Husssein na kuimba kusema, ‘Nimemlipa leo Muhammad! Kama alivyoniuliya wazee wangu siku ya Vita vya Badr, leo nimemuulia wajukuu wake. Na huu ndio mwendo wetu utakaokuwa. Kila anayetupinga tutamwua japokuwa anatukhusu…"

Ewe ndugu Mwislamu! Hebu jiulize: Mtu anayejasiri kusema kuwa anamlipa kisasi Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa kuwauwa makafiri (waliokuwa babu zake yeye Yazid) hufaa au huweza kuitwa Amiirul-mu'minin? Acha hilo! Huweza hata kuitwa Mwislamu? Hivi hao mawahabi wetu hawakulijua hilo? Au watatuambia kuwa Sheikh Abdalla Saleh Farsy alikuwa Shia?

Kuna yaliyobaki, na si madogo!

6. Baada ya kumuuwa Imam Husein a.s. na aliokuwa nao katika mwaka wa 61 BH, Yazid aliiingilia Madina. Sheikh Abdalla Saleh Farsy anatuambia (uk. 41): "Wakauawa Masahaba wengi hapo Madina na wasiokuwa Masahaba. Na wakafanya fisadi kubwa sana hapo Madina muda wa siku tatu mfululizo. Ikawa hakuna kisichoharibiwa; si roho wala mali wala hishima. Aliwaamrisha Yazid wafanye hivyo. Na masahaba wasiokufa aliwaamrisha wapigwe chapa za mgongo za kuonyesha kuwa wao ni watumwa wa Yazid." Subhaanallah! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi wetu!

Katika dondoo hilo hapo juu, hata hivyo, Sheikh Abdalla "amefinika kombe"; hakulifunua. Lakini wanazuoni wenziwe wamelifunua. Kati ya hao ni Ibn Kathir ambaye, kwa mawahabi wa ulimwengu, ni kama Sheikh Abdalla Saleh Farsy kwa mawahabi wa Afrika ya Mashariki; wanamuenzi sana. Yeye, katika uk. 220 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, amesema kuwa idadi ya hao "masahaba wengi" waliouwawa ilikuwa " mia sabaa: vigogo vya muhaajiriin na answaar"; na "wasiokuwa masahaba" walikuwa " elfu kumi". Kuhusu "fisadi kubwa sana", alizosema Sheikh Abdalla S. Farsy, Ibn Kathir anasema (uk. 222) kuwa "hazisemeki hazielezeki; hakuna anayezijua ila Mwenyezi Mungu" japokuwa, kabla ya hapo katika uk. 220, alikuwa ameshatasua kuwa
"wanawake walihashiriwa mpaka ikasemwa kuwa 1000 (elfu moja) walishika mimba na kuzaa bila kuwa na waume"!

Baada ya Ibn Kathir kuyaeleza hayo, na kama kwamba anataka kuzindua tumfahamu Yazid ni nani, anatutajia (uk. 223) Hadith tatu za Bwana Mtume s.a.w.w. Ya kwanza, iliyopokewa na Bukhari, inasema: "Hakuna yoyote atakayewafanyia vitimbi watu wa Madina ila atayayuka kama inavyoyayuka chumvi katika maji." Ya pili, iliyopokewa na Muslim, inasema: " Haikusudii Madina yoyote kwa uovu ila Mwenyezi Mungu atamyayusha katika moto myayusho wa risasi, au myayusho wa chumvi katika maji." Ya tatu, iliyopokewa na Imam Ahmad bin Hambal, inasema: "Anayewatakia khofu watu wa Madina kwa dhulma, Mwenyezi Mungu naye atamtia khofu na ashukiwe na laana ya Mwenyezi Mungu na malaika na watu wote. Wala Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, hatamkubalia toba wala fidia."

Haya! Kama hayo yaliyofanywa Madina yalifanywa kwa amri ya Yazid, kama asemavyo Ibn Kathir (uk. 220 ) na Sheikh Abdalla S. Farsy (uk. 41), mtu huyo kwa Hadith zilizotajwa hapo juu , bado yu salama? Ni Amiirul-mu'minin gani huyo anayeshukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu, malaika Wake na watu wote?

7. Mwaka mmoja baada ya kuiingilia Madina, aliiingilia Makka (katika mwaka wa 64 BH)! Huko, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk.41): "Majeshi ya Yazid yaliuwa watu wengi na kuivunja Al Ka’aba."

Hapo pia Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; lakini wenziwe wamelifunua. Kwa mfano, huyo huyo Ibn Kathir ameandika (uk. 225) kuwa majeshi hayo "yaliipiga mawe Al Ka’aba kwa teo (manjaniiq) na kuishambulia hata kwa moto mpaka ukuta wake ukaungua"! Na katika uk. 72 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab, Ibnul Imaad al Hambalii anasema: "mpaka likaanguka jengo lake"!

Haya! Hiyo ni "Nyumba ya Mwenyezi Mungu" ambayo Qur'ani Tukufu inatuambia (Sura 3:97) kwamba aliyeko nje akakimbilia huko, huwa katika amani; leo Yazid anaiondolea amani hivyo! Na huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi ambaye wanataka Waislamu wamtambue hivyo! Subhaanallah!

Hayo basi, kwa mukhtasari, ndiyo yaliyofanywa na Yazid. Jee, acha ya Amiirul-mu'minin, Mwislamu wa kawaida tu anaweza kuyafanya kama hayo? Bila shaka hawezi. Ikiwa ni hivyo basi, vipi Yazid aliweza?

Kuijibu suali hiyo, itabidi tujue Yazid alikuwa ni mtu wa aina gani. Hilo inshallah tutalitizama katika sura ijayo kwa kunukuu maneno yaliyomo katika vitabu vilivyotungwa na wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kisunni (si wa Kishia).