Sehemu Ya Kwanza: Wajibu Wa Wanawake

Madhumuni ya ndoa

Ndoa ni haja ya kawaida kwa kila mwanadamu. Inayo manufaa mengi na mazuri, baadhi ya hayo manufaa mengi na mazuri yaliyo muhimu ni haya: Ujengaji wa familia ambayo kwayo mtu anaweza kupata usalama na utulivu wa akili. Mtu ambaye hakuoa au kuolewa hufanana na ndege asiye na kiota. Ndoa hutoa huduma ya hifadhi kwa kila mtu anayehisi amepotea kwenye maisha yasiyo na mpango; mtu anaweza kupata mwenzi wa maisha ambaye anaweza kushirikiana naye katika furaha na huzuni.

Matamanio ya kawaida ya kijinsia yana nguvu na yenye maana. Kila mtu anatakiwa kuwa na mwenzi kwa lengo la kujitosheleza kijinsia kwenye mazingira yaliyo salama na tulivu. Kila mtu anapaswa kufaidi raha mustarehe ya kijinsia katika namna iliyo sahihi na inayostahiki. Wale wanao jiepusha na ndoa mara kwa mara husumbuliwa na maradhi ya kimwili na kisaikolojia.

Maradhi hayo na matatizo fulani ya jamii ni matokeo ya moja kwa moja ya vijana kujiepusha na ndoa.

Uzazi: Kupitia kwenye ndoa, binadamu wanaendelea kuzaana. Watoto ni matokeo ya ndoa na ni vipengele muhimu katika kuimarisha misingi ya familia na halikadhalika kama chanzo cha furaha kwa wazazi wao. Msisimko mkubwa sana umebainishwa kwenye Qur’ani Tukufu na Hadith kuhusu ndoa na kupata watoto. Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anasema kwenye Qur’ani Tukufu:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ {21}

“Na katika Ishara zake ni kuwa Amekuumbieni wenza kutokana na nafsi zenu...” (Quran 30:21).

Mtume (s.aw) alisema: “Hapana muundo ulio bora zaidi ulio asisiwa katika Uislamu kuliko ndoa.”

Imam Ali (a.s) alisema: “Shiriki katika ndoa; kwa sababu hii ni Suna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Yeyote anayefuata Suna yangu lazima aowe na kuzaa watoto ambao ni matokeo ya ndoa na kuongeza umma wa Waislamu ili kwamba katika Siku ya Ufufuo nitakabiliana na umma wa mataifa mengine nikiwa na idadi kubwa ya umma wangu.”

Imam Ridha (a.s) alisema: “Mafanikio makubwa sana ya mtu ni kuoa mke mwaminifu, ambaye kila amuonapo anafurahi na hulinda mali yake na heshima yake mwenyewe wakati akiwa hayupo.”

Kilichozungumziwa katika sura hii kwa upande wa ndoa ni mambo yahusuyo dunia na maumbile tu ambayo pia wanyama wanayo; manufaa ya urafiki na kuzaana.

Kama ilivyo madhumuni ya kweli ya ndoa kwa jamii ya binadamu ni ya aina tofauti. Binadamu hakukusudiwa kuingia katika dunia hii kwa sababu ya kula, kunywa, kulala, kutafuta starehe au kuendekeza ashiki na halafu kufa na kuharibika. Hadhi ya mwanadamu ni ya juu zaidi kuliko matendo kama hayo. Wanadamu wanakusudiwa kujifunza wenyewe na roho zao katika kupata ujuzi, kufanya matendo mema na kuwa na tabia njema. Binadamu amekusudiwa kuchukua hatua kwenye njia iliyonyooka ili apate ukaribu wa Mwenyezi Mungu Mweza wa yote.

Mwanadamu ni kiumbe ambacho kinaweza kusafisha roho yake kwa kuepuka matendo maovu na kujizoeza kuwa na tabia njema hufikia kiwango cha hadhi ya juu sana ambayo kwamba hata malaika hawezi kuipata.

Binadamu ni kiumbe ambacho ni cha milele. Amekuja hapa duniani ili kwa mwongozo wa manabii na utekelezaji wa utaratibu uliowekwa na dini ya Uislamu, aweze kupata furaha yake hapa duniani na Peponi, ili kwamba aweze kuishi maisha ya amani katika dunia ijayo daima milele.

Kwa hiyo, madhumuni ya ndoa lazima yatafutwe katika muktadha huu wa kiroho. Lengo la ndoa kwa mtu wa dini lazima iwe ni njia ya kuepusha matendo maovu na kutakasa roho kutokana na madhambi. Lazima iwe ni njia ya kupata ukaribu kwa Mwenyezi Mungu Mweza wa yote. Ni katika muktadha huu kwamba mwenza anayefaa na mwema huchukua jukumu muhimu.

Waumini wawili wanapounda familia kupitia katika ndoa, uhusiano wao wa kijinsia utawanufaisha katika kuimarisha mapenzi na wema wao, kwa wanandoa wa aina hiyo hapangekuwepo na hatari ya kutishia potovu wa kijinsia, mazoea mbaya au matendo ya haramu. Mtume (s.a.w) wa Uislamu na Maimamu wote (a.s) wamesisitiza sana kuhusu taasisi hii ya ndoa.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Yeyote anayeoa amelinda nusu ya dini yake.”

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Rakaa mbili za Swala ya mtu aliyeoa ni zaidi ya rakaa sabini za Swala ya mtu ambaye hakuoa.”

Mumini mchamungu na mwenzi mpatanifu hutekeleza jukumu la maana sana katika kupata na maisha ya kuheshimika na kuaminika.

Kwa kweli kuwa na mwenzi wa aina hii ni kipengele muhimu kwa mtu anapotaka kuepuka matendo maovu na kuwezesha msimamo wa mtu katika kutekeleza matendo ya wajibu ya ibada.

Wanandoa wachamungu, si tu kwamba hawatakutana na vikwazo vyovyote katika kufanikisha malengo ya kidini, bali watakuwa chanzo cha kutiana moyo wenyewe kwa wenyewe.

Je, inawezekana kwa mtu muumini wa Mwenyezi Mungu kupigana kwa utukufu katika njia Yake bila ya uthibitisho wa mke wake? Je, inawezekana mtu yeyote mchamungu kupata riziki yake kihalali, kwa kuzingatia vipengele vyote vya kidini, kulipa sadaka iliyoamriwa kisheria ili kuepuka ubadhirifu, na kutumia katika kutoa msaada bila ya idhini ya mkewe?

Mchamungu kila mara angemlingania mwenzi wake kwenye wema, kama vile ambavyo mtu mpotovu angemshawishi mwenzi wake kuwa mpotovu.

Halafu ni jambo la maana kwamba kwenye Uislamu wanamume na wanawake ambao wanataka kuoa au kuolewa wanashauriwa kuangalia usafi na tabia njema za wale wanaotaka kuwa wenzi wao katika maisha ya ndoa, kama masharti ya muhimu.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Kama ingetokea mimi nimpe mtu Mwislamu mazuri ya dunia na akhera, ningemjalia moyo wa unyenyekevu, ulimi ambao ungetamka sifa Zake mfululizo, mwili wenye kuvumilia maafa yote, na ningempa mwenza katika ndoa mchamungu ambaye akimuona tu anafurahi, na analinda mali yake na heshima yake mwenyewe asipokuwepo.”

Mtu mmoja alikwenda kwa Mtume na akasema: “Ninaye mke ambaye hunikaribisha nyumbani kila ninaporudi na hunisindikiza hadi mlangoni ninapoondoka.

Anaponiona mimi nimehuzunika na sina furaha, kwa kuniliwaza na husema: ‘Kama unafikiria kuhusu riziki, basi usikate tamaa, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa riziki na kama unafikiria maisha yajayo, basi Mwenyezi Mungu na akuongeze akili yako na jitihada zako.’ Halafu Mtume (s.a.w.w) akasema; “Hakika Mwenyezi Mungu anao watendaji na wawakilishi hapa duniani na mke ni mmojawapo. Mwanamke wa namna hii atazawadiwa thawabu nusu ya mtu aliyejitolea mhanga.”

Imam Ali (a.s) alikuwa anafikiria haya haya aliposema kuhusu Hadhrat Zahra (a.s). Alisema kwamba mkewe alikuwa msaada mkubwa katika kumcha Mwenyezi Mungu Mweza wa yote.

Historia inatuambia kwamba, siku moja kipindi kifupi baada ya harusi ya imam Ali (a.s) na Hadhrat Zahra (a.s), Mtume (s.a.w.w) alikwenda kuwapongeza nyumbani kwao na kujua hali yao. Alimuuliza Imam Ali (a.s): “Unamuonaje mkeo?” Imam akajibu; “Nilimuona Zahra kama msaada mzuri sana katika kumuabudu Mwenyezi Mungu Mweza wa yote.

Halafu Mtume aliuliza swali hilo hilo kwa Zahra (a.s) naye alijibu: “Mwenzangu ni mume mzuri sana.”

Katika sentensi moja, Imam Ali (a.s) alimtambulisha mwanamke bora katika Uislamu na akaelezea madhumuni makuu ya ndoa.

Kuishi Na Mume

Kazi ya mke ni kumtunza na kumlea mume. Si kazi rahisi. Wanawake hao ambao hawatambui sifa hii ya wajibu wao, wataona vigumu katika kutimiza kazi hii.

Ni kazi ya mwanamke ambaye anatambua kwamba kazi hii inahitaji kiwango fulani cha busara, mtindo na ustadi. Kwa mwanamke kuwa mke aliyefuzu, lazima auteke moyo wa mume wake na kuwa chanzo cha furaha kwake.

Lazima amtie moyo katika kutenda matendo mema na kumshawishi asifanye matendo maovu. Lazima pia mke achukue hatua za kutosha kutunza afya yake na ustawi wake. Matokeo ya bidii yake yanaelekezwa katika kumfanya mume awe mwema na anaye heshimika ambaye atastahili kuwa mlezi wa familia yake, na baba mzuri ambapo watoto watapata mwongozo na heshima. Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa yote amemjaalia mwanamke uwezo usio wa kawaida. Mafanikio na furaha, na pia mateso ya familia yapo mikononi mwake.

Mwanamke anaweza kuifanya nyumba kuwa pepo ya hali ya juu au jahanamu inayowaka moto. Anaweza akamfikisha mume wake kwenye kilele cha mafanikio au balaa isiyofaa. Mwanamke mwenye sifa alizopewa na Mwenyezi Mungu, ambaye anatambua wajibu wake kama mke, anaweza kumnyanyua mume wake kuwa mtu wa kuheshimika hata kama alikuwa mtu wa chini sana kuliko wote.

Mwanachuoni mmoja aliandika: Wanawake wanao uwezo wa ajabu ambao kutokana nao wanaweza kupata chochote wanachotaka.”

Katika Uislamu, mke kumtunza mume kuna daraja la maana sana. Imelinganishwa na jukumu la Jihadi (vita takatifu katika njia ya Mwenyezi Mungu). Imam Ali (a.s) alisema: “Jihadi ya mwanamke ni kumtunza mume wake vizuri.”

Fikiria kwamba Jihadi ni mapambano na vita vitakatifu katika njia ya Mwenyezi Mungu, pamoja na mapambano ya kuendeleza heshima ya Uislamu, kulinda nchi za kiislamu na kutekeleza haki katika jamii, ni mojawapo ya matendo ya kiwango cha juu sana ya ibada.

Faida ya kutekeleza majukumu ya mke mzuri, vile vile huakisiwa wakati wa kufikiriwa kwa Jihadi.

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema: “Mwanamke yeyote anayekufa ambapo mume wake yuko radhi naye, huingia Peponi.”

Mtume pia alisema “Kama mwanamke hatatimiza wajibu wake kama mke, hajafanya wajibu wake kwa Mwenyezi Mungu.”

Wema

Kila mtu ana hamu ya urafiki na wema. Wote wanataka kupendwa na wengine. Moyo wa mwanadamu hunemeeka kwa hilo.

Mtu ambaye hapendwi na mtu yeyote anajifikiria yeye mwenyewe kama yupo peke yake na ametelekezwa. Bibi mpendwa! Mumeo hajawa tofauti. Yeye pia anahitaji mapenzi na huba. Kabla ya kuoa mapenzi na huba ya wazazi wake yalitimiza haja hii, lakini sasa, anayo matumaini kwamba wewe ndiye utakae timiza haja hii.

Mwanaume anategemea kwa mkewe kupata urafiki na mapenzi, ambyo ni haja ya wanadamu wote. Hujitahidi sana ili apate riziki na kukufurahisha wewe.

Hushirikiana na wewe matatizo yote ya maisha, na kama mwenza wako wa kweli, anajali kukufurahisha wewe kuliko hata wazazi wako wafanyavyo. Kwa hiyo, onesha shukurani zako kwake na umpende yeye, atakupenda wewe. Mapenzi ni uhusiano wa huku na huku ambao huunganisha nyoyo.

“Mvulana wa miaka ishirini ambaye alikuja Tehran kusoma kwenye chuo Kikuu, alimpenda mjane mwenye umri wa miaka thelathini na tisa ambaye alikuwa mama mwenye nyumba wake.” Hii ni kwa sababu mwanamke huyu aliijaza nafasi tupu iliyoachwa wazi na mama yake moyoni mwake kupitia wema wake.

Kama mapenzi yanatoka sehemu zote mbili, msingi wa ndoa unakuwa na nguvu na hatari za kutengana zinaepukwa. Usifikiri kwa majivuno kwamba mumeo alikupenda wewe alipokuona mara ya kwanza, kwa sababu mapenzi ya aina hiyo hayadumu. Mapenzi yanayodumu ni yale yanayopitia kwenye wema na huba ya kudumu katika namna ya urafiki wa karibu sana.

Kama unampenda mumeo na unao urafiki mzuri naye, atafurahi na atakuwa radhi kujitahidi na kujitolea kwa ajili ya ustawi wako.

Mwanaume anayefurahia mapenzi ya mkewe, husumbuliwa na maradhi mara chache au matatizo ya mshtuko. Kama mwamaume hapewi uhusiano mwema na wa kirafiki na mkewe anaweza kukata tamaa na kuanza kuikwepa nyumba yake. Anaweza kujikuta anatumia muda wake mwingi sana katika kutafuta marafiki na watu wa kumjali. Anaweza akajisemea mwenyewe: “Kwa nini nifanye kazi na kuwasaidia watu ambao hawanitaki. Inawezekana labda nikajifurahisha mwenyewe na kujaribu kupata marafiki wa kweli.”

Mwanamke anaweza akampenda mumewe kwa uaminifu, lakini mara nyingi haoneshi au kuyadhihirishi mapenzi yake.

Haitoshi kuanzisha uhusiano wa kirafiki na kuchukulia kwamba hali hiyo ni sawa. Matamshi ya mara kwa mara kama vile, ‘ninakupenda,’ ‘umepotea machoni kwangu sana,’ Ninafurahi kukuona,’ husaidia sana kuendeleza uhusiano mzuri. Mume anapokuwa safarini, mwanamke lazima amwandikie barua kuonesha kwamba haoni raha bila kumuona.

Kama ipo simu ofisini kwa mwanamume, mke anatakiwa kumpigia simu mara kwa mara, lakini isizidi kiasi. Mke amsifu mumewe kwa marafiki na ndugu zake wakati hayupo, na kumtetea endapo mtu anamsema kwa ubaya.

Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anazungumzia kuhusu mapatano haya ya mapenzi na huba ya mume na mke ndani ya Qur’an:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ {21}

“Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wenza kwa ajili yenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. hakika katika haya bila shaka; zipo Ishara kwa watu wanao fikiri ”.(Quran 30:21)

Imam Ridha (a.s) alisema: “Wanawake wengine ni baraka kwa waume zao ambao huonesha mapenzi na huba yao.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Watu walio bora sana miongoni mwa wanawake ni wale wenye mapenzi na huba.” Imam Sadiq (a.s) alisema: “Ukimpenda mtu mwoneshe kwamba unampenda.”

Heshima Ya Mume

Hamu ya kuheshimiwa ni jambo la asili, lakini si kila mtu yupo tayari kuitoa. Mumeo hukutana na watu wengi katika shughuli zake wakati hayupo nyumbani. Baadhi ya watu hao wanaweza kuwa hawana staha na kumfedhehesha hali ambayo hatimaye humtibua mtu.

Wewe kama mke wake, anakutarajia wewe kuonesha heshima na ari akiwa nyumbani na kwa hali hiyo unaipandisha hadhi ya nafsi yake iliyokanyagwa.

Kumstahi na kumheshimu mume wako hakukudhalilishi wewe, lakini huongeza nguvu na mwelekeo kwenye harakati za kuyafanya maisha kuwa bora. Kila mara unatakiwa umsalimie na kwa hayo maamkizi yako mfanye ahisi unamjali. Usiingilie kati mazungumzo yake. Uwe na adabu na mpole unapozungumza naye na usimpigie makelele. Inapotokea wote wawili mnakwenda kwenye mkutano ngoja mumeo aingie kwanza. Msifie mbele ya watu wengine. Waambie watoto wenu kumheshimu baba yao na uwakaripie kama hawaoneshi adabu kwake. Mheshimu mbele ya wageni na uwe makini kwa mahitaji yake, na yale ya wageni.

Anapogonga mlango jaribu kufungua mlango huku ukitabasamu na kuonesha uso wenye furaha. Tendo hili dogo la kuonesha furaha, athari yake ni kwamba huburudisha moyo na kumwondolea uchovu mumeo. Baadhi ya wanawake wanaweza kudhani kwamba tabia ya aina hiyo si ya kawaida. Fikiria unapomwamkia mumeo kama mgeni. Hii si tabia nzuri kwa sababu mumeo amekuwa kwenye harakati siku nzima kwa ajili ya ustawi wa familia yake na anastahiki kufikiriwa na kuheshimiwa anaporudi nyumbani. Maamkuzi hayo ya kwanza huleta picha nzuri sana, na lililo zuri kwa mgeni ni zuri pia kwa jamaa wa familia.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wajibu wa mwanamke ni kujibu hodi ya mlangoni na kumkaribisha mume wake.”

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke anayemheshimu mume wake na hamsumbui, atapata bahati na mafanikio.”

Mtukufu Mtume (s.a.w) alisema: “Mke anawajibika kutayarisha beseni na taulo ili mumewe anawe mikono.”

Uwe mwangalifu usije ukamfedhehesha mumeo, usizungumze naye kwa ukali, usimtukane, uwe msikivu kwake na usimuite kwa majina machafu. Ukimkosea na yeye atakufedhehesha wewe. Hatimaye, moyo wa mapenzi na kuaminiana utamomonyoka. Kwa hiyo, mtagombana mara kwa mara na kubishana, hali ambayo itasababisha mtalikiane.

Hata kama mtaendelea kuishi pamoja, maisha yenu kwa hakika yatajaa fujo. Hisia za uadui na usumbufu wa kisaikolojia unaweza kuanza kujengeka hadi kufikia kiwango cha kuhatarisha maisha ya wanandoa na hali hiyo inaweza kusababisha uhalifu. visa vifuatavyo vinaonesha baadhi ya mambo haya:

“Mtu mmoja mwenye umri wa miaka ishirini alimchoma kisu mkewe mwenye umri wa miaka kumi na tisa hadi akafa kwa sababu mke alimtukana mume. Mahakamani mume alisema; ‘nilimuoa mwanamke huyu mwaka moja uliopita. Mwanzoni mke wangu alinipenda sana. Lakini baada ya kipindi kifupi mke wangu alibadilika na kuanza kunidhalilisha.

Alianza kutumia lugha ya matusi kwangu kila ilipowezekana na kwa sababu ndogo sana, alianza kunikebehi. Kwa sababu jicho langu la kushoto ni kengeza, akawa na desturi ya kuniita mimi ‘punda kipofu.’ Siku moja, akaniita ‘punda kipofu’ nilikasirika sana hivyo kwamba nilimchoma kisu mara kumi na tano.’ ”

“Mtu mwenye umri wa miaka sabini na moja (71) ambaye alimuua mkewe, alitoa maelezo yafuatayo: ‘Ghafla tabia ilibadilika kwangu na akaanza kutonijali mimi. Wakati mmoja akaniita ‘mtu nisiyevumilika.’ nikagundua kwamba alikuwa hanipendi tena, nikamshuku na nilimuua kwa kumkata shoka mara mbili.”

Malalamiko Na Manung’uniko

Hakuna mtu yeyote asiyekuwa na matatizo na manung’uniko kuhusiana na maisha ya kila siku. Kila mtu hupenda kuwa na mtu wa kumhurumia ambaye anaweza kuwa mwandani wake na kumsikiliza matatizo yake. Lakini jambo la kukumbuka ni kwamba “upo wakati na mahali kwa kila jambo.” Mtu lazima aelewe wakati muafaka na mahali pa kulalamikia. Baadhi ya wanawake wajinga na wabinafsi hawatambui kwamba waume zao wanachoka sana na fadhaa baada ya kazi ya siku nzima. Badala ya kungoja kwa muda wa saa moja au mbili ili apumzike na kupata nguvu, huanza kumshambulia kwa mfululizo wa malalamiko. Mathalani mke anaweza kusema:

“uliniacha mimi na watoto hawa maluuni na ukaenda zako. Ahmad amevunja kioo cha mlango wa chumba cha mbele. Watoto wetu wa kike walipigana. Makelele ya watoto wa majirani zetu yananiudhi kweli. Hasan hajifunzi hata kidogo na amepata maksi za chini sana. Nimefanya kazi sana leo najisikia nimechoka. Hakuna hata mtu wa kusikiliza kilio changu!

“Watoto hawa hawanisaidii hata kidogo kwa kazi za hapa ndani. Afadhali nisingezaa watoto kabisa! Unayo habari dada yako alikuwa hapa leo? Sijui tatizo lake nini; alikuwa anafanya mambo kama vile nimemeza urithi wa baba yake.

“Mungu na aninusuru kutoka na mama yako! Amekuwa ananisengenya. Nimechoshwa na wote hao. Pia nimejikata kidole leo kwa kisu na kuumia sana.

“Ingekuwa vema kama nisingekwenda kwenye harusi ya Muhamedi jana. Ungemuona mke wa Rashid! Alivyopendeza, ungeshangaa! Mwenyezi Mungu angenipa na mimi bahati kama hiyo! Wanaume wengine wanawapenda wake zao na huwanunulia vitu vizuri. Hao ndio waoaji wa kweli.

“Rashid alipoingia kila mtu alimpa heshima. Ni kweli kwamba watu hupendelea kuona tu vazi ulilovaa. Anacho nini ambacho mimi sina? Kwa nini ajioneshe mbele yangu? Ndio, anayo bahati kuolewa na mume ambaye anampenda, yeye si kama wewe!

“Siwezi kuvumilia kuendelea kuishi kwenye nyumba iliyolaaniwa, kukutunza wewe na watoto. Kwa hiyo fanya utakalo!”

Msimamo wa namna hi si sahihi. Wanawake wa aina hii hudhani kwamba waume zao huondoka kwenda kwenye pikiniki au burudani kila asubuhi. Wanaume hukutana na mamia ya matatizo kila siku. Bibi mpenzi! Hujui mumeo amepita kwenye mambo gani anapokuwa katika kazi yake. Hujui ni watu fidhuli na wenye karaha kiwango gani mumeo ameshughulika nao siku nzima. Kwa hiyo, anapokuja nyumbani usiwasilishe malalamiko yako yote kwa wakati moja. Usimfanye ajihisi kuwa imekuwa hatia kuwa mwanamume.

Uwe na wastani na umfikirie. Endapo kwa kunung’unika kwako na kumsumbua, kutamuongezea wasi wasi na machungu, basi, ama anaweza akaanza ugomvi au akaondoka hapo nyumbani na kwenda kwenye mgahawa au filamu au hata kutembea tu mitaani.

Kwa hiyo, ewe Bibi mpenzi! Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, acha mazoea haya ya kulalamika hata wakati usio muafaka. Tafuta muda unaofaa na halafu mpe matatizo yako ambayo ni ya kweli, si kwa kulalamika, lakini fanya hivyo, kwa namna ya kushauriana. Kwa njia hii, hutasababisha yeye kuanza kujenga hisia za uadui na mapatano ya familia yanabaki kuwa salama.

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema:

“Sala za mwanamke anayemchokoza mume wake kwa ulimi wake, hazikubaliwi na Mwenyezi Mungu hata kama akifunga saumu kila siku, anaamka kila siku usiku kufanya ibada, anawaachia huru watumwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mwanamke mwenye ulimi mbaya ambaye humuumiza mumewe kwa njia hii, ni mtu wa kwanza kuingia Jahanamu!”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Wanawake wa Peponi huwaambia wanawake wanaowatukana waume zao kwa njia hii: ‘Mwenyezi Mungu na akuuweni. Msiwe watovu wa adabu kwa waume zenu. Mtu huyu (mume) si kiumbe wako, na wewe hustahiki kuwa naye. Muda mfupi ujao atakuacha na atakuja kwetu.’ ”

Sijui wanawake wa aina hii wanataka kujipatia nini kwa hayo manung’uniko yao. Kama wanataka kusikilizwa na waume zao au kujionesha, basi, hakika wanajipatia kitu kinyume chake kabisa na kumkasirisha. Kama wanakusudia mateso kwa mume, kumsababishia madhara ya kisaikolojia na kumuingiza kwenye mazoea bandia ya kuangamiza, basi wapo kwenye njia potofu.

Bibi mpendwa! Kama unamjali mumeo na familia yako, basi ni lazima uache msimamo huu usio na mantiki. Je, umewahi hata kufikiria kwamba mwenendo wako mbaya unaweza ukasababisha kuvunjika kwa maisha ya familia yako?

“Daktari mmoja alitoa ushahidi mahakamani: ‘Sijapata kumuona mke wangu akifanya mambo kama mke sahihi wa nyumbani wakati wote wa ndoa yetu. Nyumba yetu mara nyingi imekuwa katika machafuko.Wakati wote mke wangu anapiga makelele na kutukana. Nimechoshwa naye.’ Baada ya kumlipa mke wake fedha nyingi tu, akapata talaka. Akasema kwa furaha: ‘Kama angetaka na angeomba utajiri wangu wote na hata shahada yangu ya taaluma ya tiba, ningempa ili niachane naye haraka sana.’ ”

Tabia Za Kupendeza

Mtu yeyote mwenye tabia njema na inayopendeza pia angepata dhiki na matatizo ya maisha kwa njia ile ile. Hawa ni aina ya watu ambao watu huvutiwa nao na wanawatafuta wakati wote. Tabia inayopendeza na msimamo wa mtu utakuwa na kinga dhidi ya maradhi ya kisaikolojia kwa kuwa kuonekana kwao katika maisha ni kushinda matatizo yao kwa njia nzuri iwezekanayo.

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Hakuna maisha yanayo kubalika zaidi kuliko yale ambayo yanatokana na tabia njema.”

Lakini mtu mwenye tabia mbaya naye pia angeyaona maisha hayafurahishi kwani uhusiano wa watu hao kuendeleza wasiwasi na fadhaa.

Mtu kama huyu hupenda kulalamika na kupigia kelele maisha. Msimamo wa namna hii huepukwa na watu wengi ambapo mtu huyo hapati marafiki wengi. Hii ndio hali ambayo huathirika kwa urahisi na matatizo mbali mbali ya kisaikolojia na maradhi mengineyo kwa sababu ya wasi wasi na utupu ambao mtu mwenye msimamo mbaya anavyoyaona maisha.

Mtukufu Mtume (s.a.s) alisema: “Mtu mwenye tabia na msimamo mbaya atakuwa kwenye masumbuko na mateso wakati wote.”

Msimamo mzuri na unaopendeza ni muhimu kwa watu wote kwa ujumla na hususan baina ya wanandoa kwani wanandoa lazima wawe pamoja.

Mpendwa Bibi! Kama unataka kufurahia maisha ya furaha na mumeo na watoto wako, ufanye msimamo wako na tabia ya kupendeza vikubalike. Uwe na tabia njema na si mgomvi. Unao uwezo wa kuifanya nyumba yako kuwa Pepo ya hali ya juu au Jahanamu iwakayo moto. Unaweza kuwa malaika wa huruma ambapo mumeo na watoto wanaweza kupata amani kupitia kwako.

Unajua utaacha mvuto wa kupendeza kiasi kwenye roho zao kwa huo msimamo wako wa kutabasamu na lugha nzuri.

Mvuto wa kupendeza ni mbichi katika akili zao wanapoondoka kwenda shuleni au kwenye shughuli za kazi na unawasaidia wao kuwa na mwanzo mzuri wa siku.

Kwa hiyo, kama unajali kuhusu sifa nzuri ya maisha yako na uhusiano ulio nao na mumeo, usiwe kinyume na tabia njema. Uwe dhahiri katika msimamo wako na tabia inayopendeza kwani nguzo bora zaidi ya kutegemea kwa usalama wa ndoa ni maadili mazuri ambayo yanaelekeza kwenye tabia inayopendeza.

Namna nyingi za talaka ni kwa sababu ya tabia zisizolingana za mume na mke. Takwimu juu ya talaka kwa uthibitisho zinaonesha kwamba msimamo wa kupatana, maadili mema na tabia ya kupendeza, hazikuwepo kwa wanandoa husika. Chanzo kikubwa cha ugomvi na kutokuelewana kwa wanandoa ni kwa sababu yakutolingana kwa tabia na kanuni za maadili za wanandoa. Takwimu zifuatazo zinavutia:

“Mwaka 1968 kesi za malalamiko ya ndoa zilizowasilishwa mahakamani zilikuwa 16,039, kesi 12,760 miongoni mwa hizo, misingi ya malalamiko yao ilikuwa kutokulingana kwa kanuni za maadili. Mwaka 1969 kesi za malalamiko ya aina hiyo hiyo 16,058 liziwasilishwa mahakamani, kesi 11,246 miongoni mwa kesi hizo, misingi ya malalamiko ilifanana na ile ya kesi za mwaka wa nyuma. Kwa hiyo, inathibitika kwamba zaidi ya asilimia sabini ya ugomvi wa kifamilia ulisababishwa na kipengele hiki.”

Mwanamke alilalamika kwenye Baraza kwamba mume wake kila siku alikuwa na desturi ya kula chakula chake cha mchana na jioni nje.

Halafu mwanaume akaeleza kwamba sababu iliyomfanya ale nje ni kwamba mke wake hakuwa mbunifu hata kidogo na alikuwa mwenye tabia isiyopendeza kuliko wanawake wote wenye tabia kama hiyo hapa duniani. Haraka sana mwanamke alinyanyuka na kuanza kumpiga mume wake mbele ya majaji.”

Mwanamke huyu mpumbavu alidhani kwamba angebadilisha tabia ya mume wake ya kula chakula chake nje badala ya nyumbani kwa kulalamika, kutukana na kumpiga.

Lakini mwanamke huyu hakutumia mbinu rahisi na ya kiakili ambapo alitakiwa kuwa na busara zaidi na kuzingatia mwenendo unaostahili.

Mwanamke mwingine alipeleka taarifa mahakamani kwamba mume wake aliacha kusema naye kwa muda wa miezi 15 na kwamba alikuwa anatoa matumizi yake kupitia kwa mama yake (mume). Mume alijibu kwamba alikwisha kinai na msimamo usiopendeza wa mke wake ambao ulimfanya yeye asizungumze naye kwa miezi.”15

Migongano mingi ya kifamilia inaweza kusuluhishwa kwa wema, huruma na tabia inayopendeza. Kama mume wako si mwema, kama anatoka kwenda kula chakula cha jioni peke yake, kama anapenda kutumia lugha ya matusi, anatumia utajiri wake wote vibaya, hupenda kusema suala la kutalikiana na kutengana au sababu kadhaa katika ugomvi wa kifamilia, ipo njia moja tu ya kusuluhisha. Njia hii ni kuwa mwema na tabia njema. Matokeo ya mazoea ya tabia kama hii ni ya kimiujiza.

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwenyezi Mungu Mweza wa yote atampa mtu mwenye tabia ya kupendeza thawabu zinazolingana na zile za Jihadi. Atamneemesha kwa wingi mtu huyo usiku na mchana.”

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke yeyote anaye msumbua na kumtesa mumewe yu mbali na neema za Mwenyezi Mungu na mwanamke yeyote anayemheshimu, anaye mtii na hamhuzunishi mumewe, ameneemeka na kufanikiwa.”

Ipo hadith inayosema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alipewa taarifa ya mwanamke mwema ambaye alifunga saumu kila siku na alikuwa anafanya ibada kila siku usiku akimuabudu Mwenyezi Mungu, lakini alikuwa na tabia isiyo pendeza ya kuwaudhi majirani zake kwa maneno yake makali. Mtukufu Mtume alisema: “Hapana jema kwake huyo na yeye ni mkazi wa Jahanamu.”

Matarajio Mabaya

Mpendwa Bibi! Wewe ni mwanamke mkuu wa familia yako. Uwe na hekima na uweledi. Panga vizuri matumizi yako. Panga bajeti ya matumizi yako kwa njia ambayo haitasababisha hasara kwa utajiri na hekima yako.

Usishindane na wengine na uwaonee wivu. Kama unaona nguo nzuri imevaliwa na mwanamke, au kama unavutiwa na fanicha na vyombo ambavyo umeviona kwenye nyumba ya rafiki, usimlazimishe mumeo kununua vitu kama hivyo ambavyo vinazidi uwezo wake wa kifedha na pengine atalazimika kukopa. Je, si vema zaidi kungoja hadi hapo ambapo hali ya kipato itaruhusu au itakapopatikana akiba ya ziada ya kuwezesha kununua vitu visivyo vya muhimu?

Mara nyingi ni wale wanawake wajinga na wanaojipendelea ambao hushindwa, na kuwa wabadhirifu na kutaka kushindana. Wanawake wa aina hii huwalazimisha waume zao kuingia kwenye madeni na huchoshwa na kukasirishwa na kujaribu kuridhisha matakwa yao yasiyo weza kutoshelezwa. Wakati mwingine, ufumbuzi wa aina moja tu uliopo kwa wanaume wa kutatua matatizo haya ni uamuzi wa kumtaliki mke au kujiua.

Wanawake ambao hawatambui madhumuni ya kweli na maana ya ndoa na badala yake wanaifikiria kama utumwa ambapo mwanamume anapatikana kwa lengo la kutimiza matamanio yao ya kitoto na mahitaji ya kiulimwengu.

Wanawake wa namna hii wanataka mume ambaye atawahudumia kama mtumwa na hawatapinga njia zao za matumizi. Wanawake wa aina hii mara nyingine huenda mbali zaidi. Wanawafanya waume zao watumie zaidi ya uwezo wao hali ambayo inaweza kuwafilisi, wanaweza kufanya mauaji au matokeo yoyote ya msiba.

Wanawake wa aina hii ni aibu kwa wanawake wenzao. Endapo matarajio yake makubwa yanasababishwa kutalikiana, mwanamke atanyang’anywa mapenzi ya watoto wake na ataishi maisha ya upweke.

Kwa wanawake wa aina hii si rahisi kuolewa tena kwa urahisi. Hata kama inatokea, hakuna uhakika wa ndoa ya pili kama itadumu, kwani binadamu wengi hawapendi kuwekwa katika utumwa. Na mume mpya inawezekana naye asiwe na uwezo wa kutimiza mahitaji yao kabisa kuliko hata wa mwanzo.

Mpendwa Bibi! Badala ya kuwa mwenye tamaa sana, jaribu kuwa mwenye busara. Tumia muda mwingi na juhudi kwa ajili ya ustawi wa familia yako na mumeo badala ya kujaribu kuiga mambo ya kila mtu. Kama mumeo anaumia kupita kiasi, mzuie na udhibiti matumizi yake yasiyo ya muhimu. Badala ya kununua bidhaa zisizo za muhimu, ni vema kuweka kiasi fulani cha akiba kwa ajili ya matatizo ya siku za usoni.

Katika hadith Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke yeyote ambaye halingani na mume wake na humshawishi afanye mambo zaidi ya uwezo wake, basi matendo yake hayatakubaliwa na Mwenyezi Mungu, ataonja ghadhabu ya Mwenyezi Mungu mnamo Siku ya Ufufuo.”

Katika hadith nyingine, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke yeyote asiyelingana na mumewe, haridhiki na kile ambacho Mwenyezi Mungu amewajaalia na humtendea mume wake ubaya kwa kudai ampe zaidi ya uwezo wake, basi matendo yake (au ibada ya mke) hayakubaliki kwa Mwenyezi Mungu na Atamkasirikia mwanamke huyo.”

Katika hadith nyingine, Mtume (s.a.w.w) alisema: “Baada ya kumwamini Mwenyezi Mungu, hapana neema iliyo kubwa zaidi ya kuwa na mume au mke mnayeelewana naye.”

Uwe Faraja Kwa Mumeo

Uzito wa mzigo wa maisha huchukuliwa na wanaume kwa sababu wao wanao wajibu wa kutunza na kusaidia familia zao. Katika kutimiza wajibu huu, mwamaume wa familia lazima akabiliane na matatizo mengi na vikwazo vingi nje ya familia yake. Baadhi ya matatizo haya yanaweza kuwa ukubwa wa kazi, mizozo kwenye msongamano wa magari na usumbufu wa kungoja na kupanda mabasi kutoka nyumbani kwenda ofisini na kurudi nyumbani, wasiwasi kuhusiana na masuala ya marafiki nawafanyakazi wenzake na wasiwasi wa kiuchumi na kisiasa ya siku hiyo, wasi wasi wa marafiki na wafanya kazi wenzake, na wasiwasi wa kujaribu kuboresha hali ya maisha ya familia yake. Kiasi cha mishughuliko na wasiwasi wa mtu mwenye kuwajibika ni mikubwa na yenye sehemu nyingi. Si jambo la kushangaza kwamba wastani wa umri wa mwanaume ni mdogo zaidi ya ule wa mwanamke.

Ili mwanadamu aweze kwenda sambamba na mizigo ya maisha ni muhimu kuwa na mtu ambaye atakusikiliza na kukuhurumia. Mumeo ni mmoja wapo wa watu hao. Anaweza akahisi yu mpweke na akahitaji kupata kimbilio na faraja akiwa katikati ya misukumo hii. Ni kawaida kwamba mwanaume hutarajia kupata faraja na utulivu kutoka kwa mke wake na familia yake. Kwa hiyo, tazamia matarajio na mahitaji yake.

Uwe mkunjufu na mchangamfu wakati ambapo kwanza ndio anarudi nyumbani kutoka katika kazi zake, na apate viburudisho au umfanye ahisi kwamba wewe upo tayari kusikiliza mahitaji yake. Jaribu kutokumwingiza kwenye shari kwa kuanza kumlaumu mara tu umuonapo.

Ngoja apumzike na apate nguvu upya kabla ya kumweleza madai binafsi ya watu wa familia.

Mumeo anapokuja nyumbani, jaribu kutabasamu na kumsalimia kwa uchangamfu. Mtimizie mahitaji yake ya kimwili ya uchovu, njaa na kiu. Halafu muulize kuhusu matatizo yake. Kama hayupo tayari kusema uwe msikilizaji mzuri na umhurumie. Jaribu kuonesha kuhusika kwako kwa dhati na halafu umsaidie kutambua kwamba matatizo si kwamba hayawezekani, na makubwa kama anavyodhani. Mpe moyo wa kumuunga mkono na kumsaidia aweze kukabiliana na masuala ipasavyo. Unaweza kusema kitu kama: “Matatizo haya yanawapata watu wengi. Kwa utashi na uvumilivu, inawezekana kuyatatua matatizo almuradi mtu asiruhusu yamshinde. Matatizo haya, kwa kweli ni mitihani na pia hujenga tabia ya kweli ya mtu. Usikate tamaa. Unaweza kuyatatua kwa kuazimia na ustahamilivu.

Kama unayo mawazo fulani kuhusu jinsi ya kuyashughulikia, mwaambie mumeo. Kama huna, labda unaweza kumshauri amuone rafiki mzuri ambaye anao ujuzi na sifa zaidi.

Mpendwa Bibi! Wakati wa matatizo, mumeo anahitaji sana umjali na mapenzi yako. Unatakiwa umsaidie na umtunze kama mtaalamu wa maradhi ya akili na mke mwenye huruma. Kiwango gani cha matunzo mtaalamu wa maradhi ya akili angempa ambacho na wewe ungempa? Usikadirie pungufu uwezo wako wa kumtuliza na kumpa nguvu. Hakuna mtu muaminifu na mwenye kuhusika zaidi kuhusu ustawi wa mumeo isipokuwa wewe. Ataweza kupata nguvu kutokana na mapenzi yako kwake na aweze kukabiliana na matatizo yake kwa hali ambayo itapunguza mhemuko wake na wasiwasi wa akili. Hatimaye, mapatano ya kuheshimiana na upendo utakuwa mkubwa zaidi.

Katika hadith, Imam Sadiq (a.s) alisema: “Hakuna kitu bora zaidi duniani kuliko kuwa na mke mwema. Na mke mwema ndiye huyo ambaye mume wake hufurahi pindi amuonapo.”

Kwenye hadith, Imam Rida (a,s) alisema: “Lipo kundi la wanawake ambalo huzaa watoto wengi. Ni wanawake wema na wana huruma. Huwasaidia waume zao wakati wa matatizo na katika mambo ya dunia hii na ile ijayo. Wanawake hawa hawafanyi matendo yoyote ambayo yangewapa hasara waume zao kuongeza matatizo yao.”

Uwe Mtu Wa Kuonesha Shukrani

Kama mtu ni mwema na mpaji wa utajiri wake ambao ameupata kutokana na kazi ngumu, shukrani na kuoenasha kufurahia kwako kwa matendo kama hayo ni hali ambayo itachangamsha hisia zake za ndani na kumfanya ahisi amefanikiwa.

Matendo ya ukarimu yanaweza kuwa kawaida ya mtu ambapo hujenga mazoea kutumia na kugawana utajiri wake na wale wanao hitaji. Hata hivyo, kama matendo ya ukarimu yanapuuzwa na hayafurahikiwi, mhusika anaweza akapoteza utashi na msukumo wa kufanya wema. Itakuwa ni kawaida kwa mtu kuhitimisha kwamba ilikuwa ni kutumia vibaya kutoa fedha yake aliyoipata kwa jasho ambapo hakuna shukrani inayotolewa.

Shukrani na kufurahishwa ni tabia za kuvutia akiwa nazo mtu na ni siri ambayo kwayo mtu anaweza kuvuta matendo ya msaada.

Hata Mwenyezi Mungu ametaja kwamba shukrani kwa neema Zake ni sharti ambalo husababisha neema Zake kuendelea kutolewa kwa wanadamu:

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِنْ شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِنْ كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ {7}

“Na alipotangaza Mola wenu : Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.” (Qur’ani 14:7).

Mpendwa Bibi! Mumeo naye pia ni binadamu. Kama mtu mwingine yeyote yule. Yupo tayari kusaidia familia yake na anaiona kama wajibu wa uadilifu na kisheria. Anapopewa shukrani na kufurahikiwa kwa kutekeleza kazi yake, kazi hizo haziwi tena mzigo kwake.

Wakati wowote anaponunua vitu vya nyumbani au kitu kama nguo na viatu kwa ajili yako na watoto, furahi na umshukuru yeye. Onesha shukrani zako kwa vitu vidogo anavyofanya kama kununua bidhaa za vyakula, kusafiri na familia na kukupa wewe fedha. Unapoonesha shukrani, unamfanya mumeo ajihisi kuwa mwema na kuzawadiwa kwa usumbufu uliompata. Uwe mwangalifu kwamba usizipuuze kazi zake na kuwa mtu asiyejali mchango wake kuhusu ustawi wa familia.

Anaweza akaanza kutumia fedha yake kwingineko au kwake yeye mwenyewe.

Ikiwa tu rafiki au ndugu amekupa zawadi ya jozi ya soksi au shada la maua, unatakiwa kumshukuru mara nyingi, hivyo, ni kawaida tu na ni haki kumfurahia mumeo kwa kukupendelea na kukufikiria. Usidhani kwamba utakuwa unajidhalilisha kwa kuonesha shukrani zako. Kinyume chake, utapendwa na kujaliwa kwa vitu vingi zaidi kwa sababu unafurahia juhudi ya mumeo ambapo dharau na ubinafsi ni tabia ambazo zinaweza kuipeleka familia kwenye mabalaa.

Zifuatazo ni Hadith zinazozungumzia tabia za shukrani: Imam Sadiq (a.s) alisema: “Wanawake bora zaidi miongoni mwa wanawake wenu ni hao ambao huonesha furaha wakati waume zao huleta kitu nyumbani na hawaoneshi kutokuridhika kama hakuna kilicho letwa nyumbani.”

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke yeyote ambaye husema kwa mumewe kwamba hajaona vitu vyovyote vizuri kutoka kwake basi anakuwa amekosa uaminifu na anavuruga ibada yake.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Yeyote asiye washukuru watu wanaomsaidia, kwa kweli, haoneshi shukrani zake kwa Mwenyezi Mungu kwa neema Zake.”

Usitafute Dosari Za Mwenzio

Hakuna mtu aliyekamilika. Watu wengine ni warefu sana au wafupi sana au wanene sana au wembamba sana, wanapua kubwa au pua ndogo, wanasema sana au wakimya sana, wana hasira zana au wanaelewana na watu haraka sana weusi sana rangi ya wastani au wanakula sana au wanakula kidogo na orodha inaweza kuendelea. Wanaume na wanawake wengi sana wanazo dosari hizi. Ni matumaini ya kila mwanaume na kila mwanamke kutafuta mwenzi aliyekamilika, lakini matumaini ya aina hiyo si sahihi. Hakuna uwezekano wa kumpata mwanamke anaye muona mumewe kama mtu aliye kamilika.

Wanawake hao ambao hutafuta makosa ya waume zao bila shaka watayapata.

Wanaweza wakaona dosari ndogo na kuzikuza kwa kushughulikia jambo hilo hadi kiwango cha kuwa kipingamizi kisichovumilika. Dosari hii huchukua nafasi ya sifa zingine zote za mume. Kila mara huwalinganisha waume zao na wanaume wengine. Wameanzisha kitu kinachoitwa mwanaume anayefaa katika dhana yao kiwango ambacho hakiafikiani na waume zao. Kwa hiyo, kila mara wanalalamika kuhusu dosari ndani ya ndoa zao. Wanawake hao hujifikiria kuwa na bahati mbaya na kushindwa na maisha na pole pole huwageuza kuwa wanawake |wenye chuki.

Tabia ya aina hiyo ya mwanamke humfanya nini mumewe? Anaweza kuwa ni mtu mvumilivu sana ambaye anaweza kustahamili ujeuri lakini upo uwezekano mkubwa atafedheheshwa na atakuwa na kinyongo kwa mkewe.

Hali hii inawezekana ikawatumbukiza wanandoa husika kwenye mabishano na kuelezana dosari za kila mwanandoa. Wote wawili watadharauliana na maisha yao yatageuka kuwa na mlolongo wa ugomvi na mabishano. Hivyo, ama wataishi katika mateso wakiwa pamoja au wataamua kutalikiana. Katika hoja zote mbili, wote watahasarika, hususan ambapo hakuna uhakikisho kwamba ndoa nyingine inaweza kuthibitisha vinginevyo.

Inasikitisha kwamba wapo wanawake wasiojua na wanakaidi katika huo ujinga wao. Inawezekana kwamba wanaweza kuharibu maisha ya familia zao kwa jambo dogo. Ifuatayo ni mifano ya wanawake wa aina hiyo: “Mwanamke alimwacha mume wake na akaenda nyumbani kwa baba yake kwa sababu mume wake alikuwa ananuka mdomo. Mwanamke huyo hakuwa tayari kurudi kwa mumewe hadi atatue tatizo lake. Kufuatana na malalamiko ya mume, mahakama iliwasuluhisha wana ndoa hao na mke akarudi kwa mumewe. Walipokwenda nyumbani, mke aligundua kwamba pumzi ya mumewe ilikua bado inanuka, kwa hiyo alihamia chumba kingine.”

“Daktari wa meno mwanamke alimtaliki mume wake kwa sababu hakuwa katika kiwango kinacholingana na cha kwake; mwanaume alifuzu na kupata taaluma hiyo miaka mitatu baada ya mke wake.”

“Mwanamke aliomba kumtaliki mume wake kwa sababu alikuwa na desturi ya kuketi chini na kula kwa kutumia vodole vyake, alikuwa hanyoi kila siku na hakujua jinsi ya kuishi na watu.”

Kama mambo yalivyo, si kwamba wanawake wote wapo hivi. Wapo wanawake wenye akili, wa kweli, na wanao utambuzi wa kutosha kwamba hawa hatarishi ndoa na furaha kwa kukuza dosari za waume zao. Mpendwa Bibi! Mumeo ni binadamu kama wewe. Hakukamilika, lakini anaweza kuwa na sifa nyingi. Kama unapendezwa na ndoa yenu na familia yenu basi usitafute udhaifu wake.

Usifikirie dosari zake ndogo kuwa muhimu. Usimlinganishe na mwanaume huyo ambaye umembuni akilini mwako. Inawezekana mumeo awe na udhaifu fulani ambao haupo kwa wengine. Lakini kumbuka kwamba wanaume wengine wanaweza kuwa na kasoro ambazo hazipo kwa mumeo. Ridhika na sifa zake. Hatimaye, utaona kwamba sifa zake zinazidi dosari zake. Zaidi ya hayo kwa nini utarajie kumpata mume mkamilifu ambapo wewe mwenyewe si mkamilifu. Kama wewe unajivuna kiasi cha kutosha kujiona wewe ni mkamilifu, basi waulize watu wengine:

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Hakuna kitu kibaya zaidi kwa binadamu kuliko kutafuta dosari za watu wengine, ambapo hawajali mapungufu yao.”

Kwa nini ukuze dosari ndogo? Kwa nini uharibu maisha yako kwa kitu kisichokuwa maanani?

Uwe na busara, acha upuuzi! Puuza dosari za mumeo na usizitaje mbele yake au nyuma yake. Jaribu kutengeneza hali ya hewa ya uchangamshi katika familia yako na ufurahie neema za Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo, inawezekana pawepo dosari katika tabia ya mumeo ambazo unaweza kuzirekebisha. Kama ni hivyo, unaweza kufaulu kufanya hivyo hapo tu ambapo utakuwa na busara na uvumilivu. Hutakiwi umlaumu au kuanza kumgombeza, lakini mwendee kwa njia ya kirafiki.

Usimwangalie Mtu Yeyote Isipokuwa Mumeo

Mpendwa Bibi! Kabla hujaolewa inaewezekana ulikwisha chumbiwa na watu wengine. Posa za uchumba huu inawezekana zilitoka kwa watu matajiri, wasomi, wenye sura nzuri na kadhalika ambao ungependa wakuoe.

Matarajio ya aina hiyo yalikuwa ni jambo la kawaida kabla ya kuolewa. Lakini sasa umechagua mwenzi wako na kuwekeana mkataba wa dhati naye kuwa wapenzi katika maisha yenu yote, hivyo, sahau yaliyopita kabisa. Lazima uyaweke pembeni matamanio yako ya zamani na usahau ofa hizo za zamani. Usimfikirie mwamanume mwingine yeyote isipokuwa mumeo na utafute amani naye. Kama ukifanya vinginevyo, utajiweka katika hali ya mashaka.

Sasa basi, umekubali kuishi na mumeo, kwa nini wakati wote uendelee kuwatilia maanani wanaume wengine? Kwa nini umlinganishe mumeo na wanaume wengine? Unapata manufaa gani unapowatazama na kuwatilia maanani wanaume wengine isipokuwa kujiweka katika hali ya mateso yasiyo na mwisho na kusababisha upate maumivu makali ya akili?

Imam Ali (a.s) alisema: “Yeyote anayeyaacha macho yake huru, kila mara atapata maumivu ya neva na atanasa kwenye mtego wa wivu wakati wote.”

Kwa kuwatazama waume wengine na kuwatilia maanani na kuwalinganisha na mumeo, utamuona mwanaume ambaye hana dosari za mumeo. Unaweza kudhani kwamba labda mwamaume huyo amekamilika kwa sababu huzijui dosari za mwanaume huyo. Utafikiria kuwa ndoa yako ina mushkeli, na fikira hii inaweza ikawafikisheni mahali penye mwisho wenye hatari.

Mke wa mtu, umri wake miaka 18 ambaye alitoroka nyumbani kwake alikamatwa na polisi usiku wa jana. Akiwa kituo cha polisi mwanamke huyu alisema kwamba baada ya miaka mitatu ya ndoa, pole pole alihisi kwamba hampendi mume wake. Alisema: “Nilikuwa na tabia ya kulinganisha uso wa mume wangu na nyuso za wanaume wengine na nikajuta kwa nini niliolewa naye.”

Mpendwa Bibi! kama unataka ndoa ya kudumu daima milele, kama hutaki mateso ya kiakili, na kama unataka muendeshe maisha ya kawaida, basi acha kuwa mbinafsi na sahau hayo matarajio yako yasiyofaa. Usiwapongeze wanaume wengine. Usimfikirie mwanaume yeyote isipokuwa mumeo. Usiendekeze fikira hizi:

‘Afadhali ningeolewa na fulani’

‘Ningependa mume wangu aonekane kama . . . . . .’

‘Natamaani mume wangu angefanya kazi ya. . .. . . . . .’

‘Natamaani….. Natamaani……. Natamaani….’

Kwa nini ujifunge jela kwa kuendekeza mawazo hayo? Kwa nini utibue misingi ya ndoa yako? Kama lolote kati ya matakwa hayo yangefanikiwa kwa kweli, ungejuaje kwamba ungefanikiwa kuridhika zaidi? Unao uhakika kwamba wake za waume wajulikanao kama ‘hawana dosari; wanaridhishwa nao?

Mpendwa Bibi! Kama mumeo anashuku kwamba unaonesha kuvutiwa na wanamume wengine, atakata tamaa na kuacha kuvutiwa na wewe. Usitaniane na wanamume wengine au kufuatana nao. Wanamume ni wepesi kuhisi hivyo kwamba hawawezi hata kuvumilia wake zao kuonesha kuvutiwa na picha ya mwanamume mwingine.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke yeyote aliyeolewa ambaye huwatazama wanamume wengine atakabiliwa na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu.”

Vazi La Hijabu La Kiislamu

Wanaume na wanawake, licha ya kwamba wanavyo vipengele vingi vinavyofanana, pia wanazo tabia za pekee. Mojawapo ya tabia hizi ni kwamba wanawake ni viumbe wa kuvutia, wazuri, na wanaopendwa. Ni wachangamfu, wanavutia na wanapendwa; ambapo wanaume huchangamshwa, huvutiwa na huwapenda wanawake kwa sifa zao.

Mwanaume anapomuoa mwanamke, hutamani uzuri wote na mapenzi yote ya mke wake visitiriwe kwa ajili yake tu.

Hutumaini kuwa ni yeye peke yake ndiye anayefaidi uchangamfu, mapenzi, kujishaua, uzuri, ukunjufu na kadhalika na kuwaepuka wanaume wengine kabisa. Mwanaume kimaumbile yu moto moto sana na hamvumilii mwanaume mwingine kumtazama mke wake au kuanzisha aina fulani ya uhusiano naye. Mwanaume ataona uhusiano wa karibu na mke wake na wanaume wengine kuwa ni kukiukwa kwa haki yake ya kisheria. Mume anatarajia mkewe kufuata kanuni ya vazi la kiislamu la Hijab na kwa kuwa mwepesi wa kubadilika kufuatana na tabia na maadili ya Kiislamu atashiriki katika kutunza haki yake ya kisheria.

Mwanaume yeyote aliye mwaminifu na hamasa lazima atakuwa na hamu hiyo. Tabia ya kijamii ya mwanamke ambayo imeegemezwa kwenye maadili ya Kiislamu, itaweka akili ya mume katika hali ya utulivu; kwa hiyo atafanya kazi kwa shauku kubwa ili aweze kutunza familia yake, na mapenzi kwa mke wake yataongezeka. Mwanaume wa namna hii hatavutiwa na wanawake wengine. Kinyume chake mwanaume ambaye mkewe havai Hijab ambayo ni vazi linalovaliwa na mwanamke Mwislamu na badala yake huonesha uzuri wake kwa wanaume wengine au anachanganyika nao, atatibuliwa sana. Atamuona mke wake kuwa anahusika na kukandamiza haki zake. Mume wa aina hiyo kila mara atapitia kwenye mateso na taabu na mapenzi kwa mkewe yatapungua pole pole.

Kwa hiyo, ni kwa manufaa ya jamii, na wanawake kwamba wanatakiwa kuvaa inavyostahiki na kuwa na tabia ya unyenyekevu, wanatakiwa kuonekana hadharani bila urembo na kuacha kuonesha uzuri wao kwa wengine.

Kuvaa Hijab ni wajibu wa Kiislamu. Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anasema kwenye Qur’ani Tukufu:

وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِنْ زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {31}

“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho Yao, Na wazilinde tupu zao, na wala wasioneshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasioneshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanamume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yanayohusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikana mapambo waoliyoyafisha. Na tubuni vyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa. (Quran 24:31)

Kuchunga vazi la Kiislamu la Hijab na kuizingatiwa matumizi yake katika jamii kuna manufaa kwa wanawake katika vipengele vingi: Kwa kutumia vazi la Hijab, wanawake wanaweza kulinda uzuri wao wa kijamii na maadili ya ndani kwa ubora zaidi, na kujilinda dhidi ya kuwa tu kitu kilichopo kwenye maonesho.

Wanaweza kuthibitisha imani na mapenzi yao kwa waume zao, kwa ukamilifu zaidi na kwa hiyo kusaidia kutengeneza na kutunza familia yenye uchangamfu na kuzuia hisia mbaya na ugomvi wa kifamilia. Kwa ufupi, wanaweza kuvutia nyoyo za waume zao na kujiimarisha kwenye familia zao.

Kwa kuzingatia matumizi ya Hijab ya Kiislamu mitazamo isiyo ya kisheria yenye dokezo ya kutamani kutoka kwa watu wenye udhaifu huo, itakoma na kusaidia kupunguza idadi ya ugomvi, kuimarisha mizizi ya familia, na matokeo yake kutengeneza mazingira ya utulivu ndani ya familia.

Hijab ya Kiislamu ya wanawake pia itasaidia vijana wa kiume ambao hawajaoa, kutokana na kujiingiza kwenye vitendo viovu. Hivyo, kuwaepusha vijana dhidi ya mazingira yanayoamsha hisia za kutamaani mwanamke aliyevaa nguo isiyo sitiri umbo lake hali ambayo pia itawanufaisha wanawake katika jamii.

Kama wanawake wote wangefuata utaratibu wa Hijab ya Kiislamu basi, wanawake wote wangekuwa na uhakika kwamba waume zao wanapokuwa nje ya familia zao, hawangekutana na mwanamke asherati ambaye angewavutia na kumtoa nje ya familia yake.

Uislamu unatambua lengo mahususi ambalo limesababisha kuumbwa kwa mwanamke na humuona yeye kama msingi muhimu wa jamii na kupewa wajibu kwa jamii. Jamii humtaka mwanamke ajitolee katika kutekeleza wajibu wake wa kuvaa Hijab ya Kiislamu, ambayo ingeepusha uovu na upotofu wa jamii na kutengeneza uimara, usalama na kutukuza taifa lake. Lakini kwa wazi wazi thawabu kubwa zaidi ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mweza wa yote kwa kutekeleza wajibu wake kwa dini.

Mpendwa Bibi! Kama unapenda uimara na amani kuwepo kwenye familia yako, na mumeo aendelee kukuamini wewe siku zote, kama unajihusisha na haki za wanawake katika jamii; kama unavutiwa na afya ya vijana kiakili na unao wasi wasi kwamba wanaweza wakaacha maadili mema, kama unataka kuchukua hatua za uhakika za wanaume waovu kuacha kuwatongoza wanawake; na kama unatafuta radhi ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa Muislamu muaminifu na mwenye kujitolea, basi tumia vazi la Hijabu ya Kiislamu.

Usioneshe uzuri wako na urembo wako kwa wageni, ama uwe ndani nyumbani kwako ukiwa na ndugu zako wa karibu, au kwenye mikusanyiko mingine ya kijamii nje ya nyumbani kwako. Lazima uvae ushungi mbele ya shemeji zako na watoto wao, waume wa wifi zako, waume wa shangazi zako, na binamu zako.

Usipovaa Hijabu ya Kiislamu mbele ya watu waliotajwa ni dhambi na pia unaweza kusababisha mateso makubwa kwa mumeo, hata kama hatasema.

Mwanamke halazimiki kuvaa Hijabu kwa kiwango kile kile mbele ya baba mkwe, kaka yake, na watoto wa kiume wa kaka au dada yake, ingawa ni vema kwa kiwango fulani kuvaa Hijabu mbele ya watu hawa pia. Kwa usemi mwingine, wanawake wasionekane mbele ya watu hawa- ndugu zake- kama ambavyo anaweza kuvaa kwa kumvutia mumewe. Hii ni kwa sababu wanaume wengi sana hawapendi wake zao waonekane katika hali ya kuvutia kwa kuvaa nguo au urembo mbele ya wanaume wengine, na kama mambo yalivyo isisahaulike kwamba utulivu wa akili na imani ya mume kwa mke wake ni muhimu sana kwa kudumu na usalama wa familia yote.

Samehe Makosa Ya Mumeo

Kila mtu isipokuwa wale ambao Mwenyezi Mungu amewatangaza kuwa


‘Maasum’


hufanya makosa. Watu wawili wanaopendana na wanashirikiana pamoja, hufanya makosa, lazima wawe wasemehevu. Kama hawatasameheana, basi ndoa yao itavunjika.

Wafanya biashara wawili ambao ni wabia, na jirani wawili, marafiki wawili na hususan mume na mke wanahitaji kusameheana.

Kama watu wa familia hawasameheani na kufuatilia makosa ya kila mmoja wao, basi ama familia itafarakana au wataishi maisha yasiyovumilika.

Mpendwa Bibi! Pengine mumeo hufanya makosa. Anaweza akakutukana, akakufedhehesha, akasema uwongo, anaweza hata kukupiga. Matendo kama hayo yanaweza kufanywa na mwanamume yeyote.

Baada ya kufanya kosa, kama mumeo hujuta kwa kosa hilo au wewe unahisi anajuta kwa kosa lake hilo, basi msamehe na usilifuatilie jambo hilo. Kama anajuta lakini hayupo tayari kuomba msamaha, basi usijaribu kuthibitisha kosa lake. Vinginevyo, anaweza kuhisi anadhalilishwa na anaweza kulipiza kisasi kwa kukumbuka makosa yako na kwa hiyo, ikawa chanzo cha ugomvi mkubwa kwa hali hiyo, ni bora wewe unyamaze kimya hadi hapo atakapo jilaani mwenyewe kutoka kwenye dhamira yake na akaanza kuhisi majuto kuhusu kosa hilo. Hapo atakuona wewe kuwa ni mtu mwenye busara na mke wa kujitoa kwa mambo mema ambaye anavutiwa na mume wake, na familia yake.

Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: Mwanamke mbaya hatoi msamaha kwa makosa ya mumewe na hakubali hata kuomba msamaha.”

Je, si ni jambo la kusikitisha kwamba mkataba wa ndoa takatifu unavunjwa kwa sababu mwanamke hayupo tayari kusamehe makosa fulani ya muewe?

Kuweza Kuishi Na Ndugu Wa Mumeo

Mojawapo ya matatizo ya kifamilia husababishwa na ndugu wa mume na mke wake.

Baadhi ya wanawake hawana uhusiano mzuri na mama wa mumewe, dada au kaka zake mumewe.

Kwa upande moja mke anaweza kujaribu kumtawala mume wake ili asiweze kumsikiliza hata mama yake au ndugu yake yeyote na anaweza kujaribu kuwafitinisha ili wasielewane wao kwa wao. Kwa upande mwingine, mama wa mume anajiona kuwa yeye ni mmiliki wa mwanae na mke wa mwanae.

Mama hujaribu sana kuwa karibu sana na mwanae na kutahadhari kwamba mke wa mwanae asiweze kummiliki mumewe kwa ukamilifu. Anaweza kusingizia uwongo kuhusu mke wa mwanae au kumuona anayo makosa.

Msimamo wa aina hii unaweza kufuatwa na mabishano mengi na hata chuki ya mara kwa mara. Hali inakuwa mbaya zaidi endapo watu hawa huishi kwenye nyumba moja. Hata kama ugomvi unaweza kutokea baina ya wanawake wawili, uchungu wa kiakili na dhiki hasa zaidi humpata mume aliyoko kati yao.

Mume ananaswa katikati ya mabishano ambapo hawezi kuegemea upande wowote. Kwa upande moja yupo mke wake ambaye angependa kuendesha maisha ya kujitegemea bila kuingiliwa na mtu yeyote. Kwa kawaida mume huhisi lazima amsaidie mke wake na amfurahishe. Lakini kwa upande mwingine, anafikiria wazazi wake ambao wamemsaidia kuingia katika maisha, wamemsomesha na wametumia muda mwingi wa maisha yao kumlea.

Anahisi kwamba wazazi wake wanatarajia awasaidie wakati wanahitaji msaada na kwamba haitakuwa busara kuwasahau. Zaidi ya hayo, kama yeye mwenyewe anayo haja ya kupata kitu fulani, hatakwenda kwingineko isipokuwa kwa wazazi wake, ambao watamsaidia yeye na familia yake. Matokeo yake ni kwamba anatambua kwamba marafiki zake wakuaminika ni wazazi wake na ndugu zake. Kwa hiyo, mtanziko kwa mtu mwenye busara ni ama kuwa upande wa mke na kuwaacha wazazi au kinyume chake, lakini hapana lolote kati ya haya mambo mawili yanawezekana.

Matokeo yake, atalazimika kwenda na pande zote mbili na kuziweza pande hizi katika hali ya kuridhika ambayo ni kazi ngumu. Njia moja tu inayoweza kurahisisha hali ni kwamba mwanamke lazima awe mwaminifu na mwenye hekima. Katika hali kama hii, mume anatarajia mkewe amsaidie katika kutatua tatizo.

Kama mke anamheshimu mama mkwe wake, humtaka ampe ushauri wake, na anakuwa mtiifu na kufanya urafiki naye basi, mama mkwe wake atakuwa msaidizi wake mkubwa sana.

Je, si jambo la kusikitisha kuona mtu ambaye anaweza kuwavutia watu wengi kwa sababu ya wema wake na tabia zake, halafu awafukuze kwa ajili ya ukaidi na ubinafsi wake? Hutambui kwamba katika mazuri na mabaya ya maisha, mtu anaweza akahitaji msada wa wengine, na hususan ule wa ndugu ambao wanaweza kukusaidia ambapo kila mtu akiwa amekukimbia? Je, si ni jambo zuri zaidi kufurahia uhusiano mzuri na ndugu wa mtu kwa kutumia busara na tabia njema? Je, hivi kweli ni busara na haki kufanya urafiki na watu wengine ambapo unavunja uhusiano na ndugu zako?

Uzoefu unaonesha kwamba mtu anapotaka msaada kutoka kwa wengine, marafiki humkimbia lakini ndugu aliwo watupa huja kumsaidia. Hii ni kwa sababu mshikamano wa kifamilia unao asili na hauwezi kuvunjika kwa urahisi. Kuna methali isemayo: “Hata kama nyama ya mtu ingeliwa na ndugu zake, wasingeitupa mifupa yake”

Imam Ali (a.s) alisema: “Mtu hawezi kamwe kuishi bila kuwa na ndugu zake, hata kama ni tayari na anao watoto.”

Mtu atataka heshima na wema wa ndugu zake. Ni wao ndio watakao msaidia kimwili na kiakili. Ni ndugu ndio wanasaidia mara nyingi. Wakati wa shida ndugu huweza kusaidia haraka zaidi kuliko wengine. Yeyote anaye watupa ndugu zake hupoteza mikono mingi, ya kumsaidia.

Mpendwa Bibi! Kwa ajili ya mume wako na faraja yako mwenyewe na pia kutafuta marafiki wengi na wanao kuunga mkono, vumilia kuwa nao ndugu wa mumeo. Usiwe mbinafsi na mjinga; uwe na busara na usisababishe usumbufu wowote kwa mumeo. Uwe mke mzuri na mwenye kujitolea ili uweze kukubalika kwa Mwenyezi Mungu na watu.

Kuvumilia Kazi Ya Mume Wako

Kila mtu anayo kazi na kazi hutofautiana; mathalan, dereva ambaye muda mwingi zaidi yupo barabarani na anashindwa kurudi nyumbani kila siku usiku; polisi ambaye anatakiwa kuwa kwenye zamu baadhi ya muda wa usiku; daktari wa tiba ambaye ana muda mfupi wa kuwa na familia yake, mkufunzi au mwanasayansi ambaye husoma sana muda wa usiku; makanika ambaye nguo zake ni chafu na hunuka mafuta, mfanyakazi kiwandani ambaye hufanya kazi usiku. Kwa hiyo ni mara chache sana mtu kuwa na kazi ambazo hazisumbui kwa namna moja au nyingine na kusababisha kero kwa familia.

Hakuna njia nyingine yeyote ya kupata riziki kihalali isipokuwa kufanya kazi. Ni muhimu kwa wanaume kuvumulia matatizo ya kazi zao. Hata hivyo, kuna tatizo lingine ambalo ni malalamiko ya familia.

Kwa kawaida wanawake hupenda waume zao kuwa karibu nao na hupendelea wawepo nyumbani giza liingiapo. Wanawake hutaka waume zao kuwa na kazi nzuri yenye mshahara mnono. Wanapenda kuwa na muda wa kutosha wa kwenda matembezi ya jioni. Lakini bahati mbaya kazi za waume walio wengi, hazikidhi matamanio ya wake zao, na hii kwa baadhi ya familia ni chanzo cha ugomvi na mabishano.

Dereva ambaye amekuwa kazini kwa mausiku kadhaa, ambaye hajalala usingizi wa kutosha na amekuwa hapati chakula kwa wakati unaostahili, anaingia nyumbani kwake apumzike na apate amani na faraja akiwa na familia yake. Halafu mke wake, bila kumpa nafasi ya kupumzika hata kidogo, anaanza kupiga kite na kugumia: “maisha gani haya? Kwa nini unaniacha mimi na watoto hawa na ulikuwa wapi? Ninafanya kazi zote kwa sababu wewe haupo ambapo ungenisaidia. Nimechoshwa na hawa watoto watundu! Na kwa kweli udereva si kazi nzuri. Ama lazima ubadili kazi au tulizana na mimi hapa nyumbani. Siwezi kuishi namna hii zaidi ya hapa!”

Masikini dereva huyu ambaye anaye mke wa aina hii hawezi kutegemewa kufanya vizuri kazi yake na anaweza kuhatarisha maisha yake; na maisha ya hao anao wasafirisha.

Daktari ambaye tangu asubuhi hadi usiku, huwatembelea wagonjwa makumi kadhaa hawezi kuvumilia malalamiko ya mke wake. Daktari huyu ataweza kuendelea na kazi yake? Mfanya kazi ambaye hufanya kazi ya zamu ya usiku hawezi kufuatilia kazi yake kwa hamasa endapo mke wake ni mwanamke mjanja.

Mwanasayansi ataweza kufuzu katika eneo la taaluma yake ya utafiti endapo mke wake anamsumbua kila wakati?

Hii ni mitihani inayo wabainisha wanawake wenye busara na wale walio wajinga.

Mpendwa Bibi! Hatuwezi kuitengeneza dunia iwe vile tunavyotaka sisi, na mazingira yaliyopo. Mume wako anahitaji kazi ili aweze kupata riziki halali kwa ajili ya familia yake. Kazi yake inayo masharti ambayo yatakufanya ubadilike ili uendane nayo. Lazima upange utaratibu wa maisha ya familia yako kufuatana na kazi yake. Kwa nini ulalamike na umuone anayo makosa kwa sababu ya kazi yake? Mkaribishe nyumbani kwa uso wenye furaha na uwe mwema kwake. Uwe na hekima na uivumilie kazi yake.

Kama mume wako ni dereva ambaye muda mwingi yupo barabarani, basi, tambua kwamba anajaribu kuleta fedha nyumbani kwa ajili yako na watoto. Kazi yake si tatizo. Yeye ni sehemu ya jamii na anaihudumia kwa namna nzuri kadiri awezavyo. Ingekuwa bora kama angekuwa mvivu au kama angekuwa anafanya kazi isiyoendana na masharti ya dini? Kwa hiyo, yeye hana ubaya wowote. Kasoro ipo kwako, unatarajia awepo nyumbani kila siku usiku na wewe unashindwa au hutaki kubadilika kufuatana na hali iliyipo sasa.

Hivi si busara kuzoea hali ya wakati uliopo na kuishi kwa raha zaidi? Si ingekuwa bora zaidi kumkaribisha mumeo kwa uso wenye tabasamu na kumshawishi aendelee na kazi yake kwa kumpa ‘kwa heri’ ya kuchangamsha anapoondoka nyumbani kwenda kwenye kazi yake? Kama ukimfanyia wema, atazidi kuvutiwa na familia yake na anaweza kuzidisha bidii kwenye kazi yake.

Hata farakana na wewe; atarudi nyumbani mapema kadiri iwezekanavyo; atajitahidi asifanye ajali na atakuwa imara kushikilia maadili mema.

Kama mume wako anafanya kazi ya zamu ya usiku, anakosa usingizi mzuri wa usiku ili aweze kumudu matumizi ya familia yake. Jaribu kuzoea hali hii na usioneshe kutokuridhika kwako. Kama unachoshwa na upweke, unaweza kufanya baadhi ya kazi za nyumbani, kushona na kusoma wakati wa usiku. Asubuhi tayarisha kifungua kinywa, mume wako anaporudi kutoka kwenye kazi, halafu tandika kitanda mahali penye kimya. Wanyamazishe watoto wawe kimya na uwafundishe wasimsumbue baba yao wakati anapumzika. Unaweza hata kulala nusu usingizi ili uweze kupumzika na mume wako wakati wa mchana. Lakini usisahau kwamba amekuwa macho usiku kucha na usingizi wake wa mchana ni sawa na usingizi wako wa usiku. Wanawake waliopo kwenye hali kama hii wanatakiwa kuwa na mipango ya aina mbili, moja wa kwao na mwingine wa waume zao.

Kama mume wako ni dereva, dakitari, mfanya kazi au bingwa wa sayansi na kadhalika, basi lazima ujivune na sababu ya kuwa naye. Mume wako si mvivu, mzururaji au hafanyi kazi isiyo afikiana na mafundisho ya dini. Kwa hiyo, umthamini na kumshukuru.

Usimtarajie yeye au kumuambia aache kazi yake, lakini jaribu kuafikiana na kazi aliyonayo. Kama anasoma au anatafiti katika eneo fulani, basi usimsumbue. Wewe unaweza kufanya kazi ya nyumbani soma kitabu au kwa ruhusa yake, nenda uwatembelee marafiki au ndugu.

Lakini, wakati anapumzika, jaribu kuwepo nyumbani. Tayarisha chakula chake na mahitaji mengine. Mpokee mume wako kwa tabasamu na tabia njema. Kwa kuonesha wema wako na kwa kumfurahisha, unaweza kumfanya asahau uchovu wake. Kama wewe ni mke mzuri, basi si tu kwamba utaharakisha kupandishwa kwake cheo, lakini unatoa mchango kwa huduma zake kwa jamii.

Si wanawake wote wanastahiki wanamume wenye bidii kama hao. Kwa hiyo, kwa kuwa na tabia njema na mwenye kujitolea, thibitisha kwamba na wewe unastahiki kuwa naye.

Kama kazi ya mume wako inamtaka avae nguo rasmi ambazo huchafuka, basi zifue nguo hizo mara kwa mara.

Usilalamike na usimwambie mambo yasiyofaa kwa sababu ya kazi yake. Usimwambie abadili kazi. Kuna ubaya gani kuwa makenika? Kwa vyovyote vile, hili si jambo la umuhimu na familia zisivunjike kwa sababu hii.

“Mwanamke alimwambia jaji mahakamani kwamba kazi ya mume wake, ilikuwa kuuza mafuta ya taa na kwa hiyo kila mara alikuwa ananuka vibaya na kwa hiyo alichoshwa na hali hiyo.”

Endapo Mnatakiwa Kuishi Nje Ya Mji Wa Nyumbani

Mtu anaweza kutakiwa kuishi nje ya mji wa nyumbani kwake. Mume wako anaweza kuwa anafanya kazi kwenye sekta binafsi au ya umma, na akahamishwa na kupelekwa kwenye mji mwingine. Watu wengine huishi hivi ama kwa muda au moja kwa moja. Wanaume wanalazimika kuvumilia hali hii lakini wanawake wengine hupenda kuwa karibu na wazazi wao na ndugu zao.

Wanawake hawa wamezoea mitaa, kuta ndefu na mazingira ya mahali walipozaliwa. Baada ya kuhama huanza kuwalaumu waume zao na kulalamika:

“Kwa nini niishi mbali na nyumbani? Hadi lini nitakuwa mbali na nyumbani, na wazazi wangu? Sina mtu mahali hapa. Umenileta wapi hapa? Siwezi kuishi hapa; Kwa hiyo fikiria namna ya kutatua tatizo hili!”

Wanawake hawa hawatakiwi kuwatibua waume zao namna hii. Wanawake hawa ni dhaifu sana kiakili hivyo kwamba wanadhani mahali waliko zaliwa ndizo sehemu nzuri zaidi kuishi. Wanafikiri kwamba hawawezi kufurahia maisha mahali pengine.

Binadamu haridhishwi hata na sayari yake, kwa hiyo, ameanza kwenda kwenye sayari nyingine. Lakini mtu anamuona mwanamke ambaye hafikirii, wakati ujao hata kidogo hivyo kwamba hayupo tayari kuishi umbali wa maili chache kutoka mji wa nyumbani kwake. Yeye anafikiri; “Kwa nini niwaache marafiki zangu na ndugu zangu wote niende ugenini?” Inakuwa kama vile mwanamke huyu hajiamini vya kutosha kuweza kupata marafiki wapya mahali pengine mbali na alikozaliwa.

Mpendwa mama! Uwe na busara na mwenye kujitolea. Usiwe mbinafsi. Sasa kazi ya mume wako imekuondosha kutoka kwenye mji wa nyumbani kwako, usimsababishie usumbufu. Kama yeye ni mfanyi kazi serikalini, ameamuriwa kuondoka kwenda kwenye kazi na kama anayo biashara binafsi, basi kwa hakika ni kwa manufaa yake mwenyewe kuishi mahali pengine.

Endapo mume wako anakutaarifu kwamba anakwenda kuishi sehemu nyingine, unatakiwa kukubali mara moja. Unatakiwa kumsaidia kufunga mizigo na kwenda mahali pa ugenini ambako lazima ujaribu kuhisi upo nyumbani. Panga maisha yako hapo ambapo ndio nyumbani kwako na ujirekebishe ili upazoee. Kwa kuwa wewe ni mgeni katika sehemu hii na labda huna mazoea na tabia za wakazi wa hapo, uwe na tahadhari nao. Baada ya muda, kwa msaada wa usimamizi wa mume wako, jaribu kupata marafiki kutoka kwa wanawake safi na wakuaminika.

Kila sehemu inayo sifa zake. Unaweza kujipumzisha kwa kuona sehemu za kuvutia na kutembelea majengo ya zamani.

Lazima muweke familia pamoja na umtie moyo mume wako katika kazi yake. Baada ya muda utazoea nyumba yako mpya na inawezekana hata ukapapenda zaidi kuliko ulikotoka. Unaweza ukaona kwamba marafiki zako wapya ni bora zaidi kuliko wa zamani.

Endapo hiyo sehemu mpya itakosa starehe za mji wa zamani, basi zoea maisha mapya na tafuta sifa zake. Endapo hakuna huduma kama vile umeme, basi mazingira yenu yanaweza kuwa na hali ya hewa nzuri zaidi na mnaweza kupata vyakula vibichi na vyenye ubora wa kiwango cha juu. Kama hakuna barabara nzuri basi hamtavuta hewa yenye sumu kutoka kwenye moshi wa magari na hamtasumbuliwa na kelele za watu na magari.

Wafikirie wanaume na wanawake wanaoishi vijijini kwa furaha kwenye nyumba za matofali ya udongo na hawatajali kwa vyovyote vile starehe za jiji na nyumba zao nzuri zifananazo na kasri. Fikiria mahitaji yao na yale wanayoyakosa. Kama unaweza kuwasaidia, basi usisite na mtie moyo mume wako kuwa na msaada kwao. Kama wewe unayo busara na unafanya kazi yako, basi utaishi kwa raha kwenye sehemu hiyo ya ugenini. Unaweza kuwa na msaada kwa maendeleo ua mume wako. Kwa njia hii utajulikana kama mke unayeheshimiwa na kujitoa katika mambo mema. Utapendwa na mume wako na utakuwa maarufu miongoni mwa watu. Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu ataridhika na wewe.

Kama Mume Anafanya Kazi Nyumbani

Wanawake wale ambao waume zao wanafanya kazi nje wana uhuru nyumbani. Lakini baadhi ya wanaume wanafanya kazi nyumbani, kama vile watunzi wa mashairi, waandishi, mafundi rangi, au wanasayansi ambao huhitaji kusoma sana. Wake wa wanaume wa aina hii wana uhuru mdogo nyumbani na kwa hiyo maisha yao ni tofauti.

Kazi zilizotajwa hapo juu zinahitaji umakini zaidi, kipaji na akili. Kwa hiyo, panahitajika faragha na ukimya. Saa moja ya kazi iliyofanywa mahali pa ukimya ni sawa na kazi iliyofanywa kwa saa kadhaa mahali penye shughuli na kelele nyingi. Tatizo liko wazi kwa upande moja, mwanaume anahitaji mahali palipo tulia afanye kazi yake na kwa upande mwingine, mke anataka apite hapa na pale ndani ya nyumba kwa uhuru.

Kama mwanamke anapanga mambo ya nyumba kama hiyo kwa namna ambayo kwamba mume wake anaweza kuendelea na kazi yake, kwa kweli atakuwa amefanikisha kazi ya manufaa. Mafanikio ya aina hiyo kwa hakika hayapatikani kwa urahisi, hususan pale ambapo wapo watoto. Lakini, hata hivyo, tatizo lazima litatuliwe, kwa sababu maendeleo ya mume katika kazi yake yatategemea kutokuwepo kwa tatizo hili.

Kama mwanamke anashirikiana na mume wake, anaweza kumfanya awe mtu wa kuheshimiwa ambaye atakuwa na sifa kwake na jamii.

Mwanamke ambaye mume wake hufanya shughuli zake nyumbani, asije akamtarajia kumlea mtoto, kufungua mlango kwa ajili ya wageni, kwenda jikoni, kusaidia kazi za nyumbani, kukemea watoto…Lakini anatakiwa afikirie kana kwamba hayupo ndani ya nyumba ambapo anaendelea na kazi.

Mpendwa Bibi! Mume wako anapotaka kwenda chumba cha kusomea tayarisha kalamu, karatasi, sigara, kisahani cha majivu, kiberiti, vitabu na vitu vingine atakavyo vihitaji.

Ukishatayarisha chumba na vitu anavyo vihitaji, mwache peke yake. Usizungumze kwa sauti kubwa na usiwaruhusu watoto wapige kelele. Wafundishe watoto wako wasicheze kwa fujo na kelele wakati baba yao anaendelea na kazi. Usiseme naye kuhusu mambo ya kila siku. Jibu hodi ya mlangoni na simu. Kama mtu anataka kumuona au kuzungumza naye mwambie anashughuli. Wakirimu wageni wakati anapopumzika.

Waambie marafiki na ndugu zako kumtembelea mume wako wakati hana shughuli. Marafiki zako wa kweli hawataudhika kwa taarifa yako hiyo. Wakati unafanya kazi zako za nyumbani, mtekelezee mahitaji yake, usimwingilie kati.

Labda baadhi ya wanawake wanafikiri haiwezekani kuishi kwa njia hii. Wanaweza wakasema: “Hivi inawezekana mwanamke kufanya kazi ngumu ya nyumbani na wakati huo huo amtunze mume wake pasipo kuruhusu kitu chochote kuingilia kazi zake?”

Ni kweli kwamba maisha ya aina hii si ya kawaida na huonekana magumu, lakini kama wanawake wahusika wanatafakari kuhusu umuhimu wa kazi za waume zao, wanaweza kuamua kutatua tatizo kwa kufanya mpango, bidii na hekima. Upekee wa baadhi ya wanawake hudhihirika katika hali kama hii. Vinginevyo, kuendesha maisha ya familia ya kawaida ni kazi ya kawaida.

Mpendwa Bibi! Kuandika kitabu, makala nzuri ya kisayansi au tungo nzuri, kuandika shairi zuri sana, kutengeneza mchoro mzuri au kutatua matatizo ya kisayansi si kazi rahisi. Lakini, moyo kwa upendo na ushirikiano, hilo linawezekana.

Je, huko tayari kuyatoa mhanga matamanio yako pamoja na mabadiliko kidogo tu katika maisha yako? Kwa kufanya hivyo utakuwa unamsaidia mume wako katika kazi yake. Kwa msaada wako huo, mume wako atapata hadhi kubwa na wewe utashiriki katika hadhi hiyo.

Msaidie Mume Wako Kupata Maendeleo

Wanadamu kiasili wanazo nguvu zisizo dhihirika za kuwawezesha kupata maendeleo. Kupenda kupata ubora ni hali ambayo kila mmoja wetu anayo; na tumeumbwa ili tuweze kufanikisha ubora.

Kila mmoja, ambaye anayo kazi yoyote katika umri wowote na katika hali yoyote anaweza kuendelea na kukomaa. Mtu hatakiwi kutosheka na hali ya yeye kuwepo tu na asisahau makusudio ya kuumbwa. Mtu lazima ajaribu kupata ubora katika kipindi cha uhai wake.

Licha ya kwamba kila mtu anafuatilia maendeleo, si wote wanaofanikiwa kupata maendeleo yanayohitaji malengo ya juu na juhudi kubwa ya kufanya kazi. Mtu lazima atayarishe uwanja na kuondosha vigingi na baada ya hapo anachukua hatua muhimu za kuelekea kwenye mkondo wa maendeleo. Umashuhuri wa mwanaume unategemea sana utashi wa mke wake. Mwanamke anaweza kumsaidia mume wake kupata maendeleo kama vile ambavyo pia anaweza kuwa mwenye kusababisha hasara kuhusu maendeleo ya mume wake.

Mpendwa Bibi! Wakati ambapo unafikiria uwezekano, fikiria hadhi ya juu zaidi ya mume wako na umtie moyo wa kufanikiwa. Kama bado anataka kuendelea na masomo yake au kama anataka kuongeza ujuzi wake kwa njia ya kusoma na utafiti, basi usimsitishe. Mpe moyo wa kufanikisha matakwa yake Panga maisha yako kwa namna ambayo hayatakuwa kipingamizi cha maendeleo yake.

Jaribu kumsaidia ili apate maendeleo kwa kutengeneza mazingira ya kuburudisha na kuliwaza ndani ya nyumba yenu. Kama mumeo hakusoma, mshawishi kwa unyenyekevu, mwambie aanze masomo yake ya usiku.

Kama mumeo ni msomi, mtie moyo wa kuongeza ujuzi wake kwa kusoma zaidi.Kama mume wako ni daktari wa tiba, mhamasishe asome majarida ya tiba na makala zingine zinazohusiana na tiba.

Kama mumeo ni mwalimu, mhandisi au jaji, basi mwambie awe anasoma vitabu na makala mbali mbali zinazohusiana na utaalamu wake. Unatakiwa kukumbuka kwamba katika kazi yoyote ambayo anafanya mumeo, ipo fursa ya kuendelea.

Usimruhusu mume wako aache mkondo ambao umewekwa na mpangilio kwenye muumbo. Mtumainishe asome vitabu. Usiruhusu umashuhuri wake usiendelee kuongezeka.

Kama hana muda wa kununua au kupata vitabu basi kwa kutumia ufawidhi wake wa rafiki yake, pata vitabu anavyo vipenda yeye. Mpe vitabu hivyo na mpe matumaini ya kusoma. Wewe pia unatakiwa kusoma vitabu na majarida yenye manufaa. Kama katika kusoma kwako unasoma makala ambayo ina manufaa kwa mume wako, basi mtaarifu. Kitendo hiki kina manufaa kadhaa:

Kwa kufanya hivi mara kwa mara, mume wako atakuwa mtu mwenye kuelimika ambaye atakujengea heshima wewe na yeye. Aidha, atakuwa bingwa mzuri sana ambaye huduma zake zita mnufaisha yeye na jamii yake.

Kwa kuwa amekubaliana na sheria za muumbo, kupitia kwenye masomo na utafiti wake, hapatakuwepo na uwezekano yeye kupata maradhi ya akili na kuchanganyikiwa.

kwa kuwa yupo kwenye mkondo wa kuelekea kwenye maendeleo na anaonesha kupendelea kusoma, basi ataambatana zaidi na wewe na watoto, hatavutiwa kwenye uovu na hatanasa kwenye mtego wa mazoea ya hatari.

Kuwa Mwangalifu Mume Wako Asipotoshwe

Wanaume wanatakiwa kuwa na uhuru wao na ushirikiano wao katika shughuli ili waweze kufanya kazi na kuendelea kwa namna inayowafaa. Kama wanaume watawekewa masharti katika shughuli zao, basi, hawatakuwa na furaha. Mke mwenye busara hawezi kuingilia mambo ya mume wake.

Mke hatakiwi kufuatilia nyendo za mume wake; kwa sababu lazima atambue kwamba kwa kumnyima mume wake uhuru anaouhitaji na kujaribu kumdhibiti katika shughuli zake anaweza kujibu kwa ukali sana.

Wanaume wenye busara na uzoefu hawahitaji kudhibitiwa.Wanaume kama hao kila mara kufanya mambo yao kwa busara; si rahisi kuwa danganya; wao wanawajua marafiki zao na maadui zao. Hata hivyo, wapo watu ambao ni wa kawaida; watu hawa wanaweza kudanganywa kwa urahisi na kuvutiwa kwa urahisi na watu wengine.

Wapo watu ambao ni laghai na wanangoja kuwadanganya watu wa kawaida. Mtu laghai, licha ya kujifanya kuwa mwema, humtega na kumnasa mtu mwingine na kumwelekeza kwenye uovu. Jamii iliyojaa uovu na tabia ya binadamu isiyokubali kushindwa haisaidii kurekebisha hali. Mtu wa kawaida anaweza asijue hali yake kwa kipindi fulani, lakini siku moja anashtuka na kujikuta yupo kwenye kina cha mtego na hawezi kujinasua.

Ukiangalia kila mahali pale ulipo, utaona watu wengi wa aina hiyo wenye bahati mbaya. labda hakuna hata mmojawao aliye nuia kuanguka kwenye mtego au kuwa mwovu. Lakini kupitia kwa urahisi wao, ujinga na uamuzi wa pupa sasa wamekuwa mawindo ya waovu katika jamii.

Kwa sababu hii, watu wepesi wanatakiwa kusimamiwa. Kwa kufuatilia shughuli zao, watu wenye busara na wenye kuwatakia mema wenzao watakuwa wamewafanyia huduma kubwa.

Watu wazuri sana kwa kazi hii, hata hivyo, ni wake wa wanaume hawa. Mke mwenye busara na mwerevu anaweza kufanikiwa kazi kubwa sana kuhusu mume wake, kwa msimamo wa kumsaidia na busara.

Wanawake wa aina hii, hata hivyo, lazima wakumbuke kwamba hawatakiwi kuingilia moja kwa moja mambo ya waume zao, au kuwaambia “Wafanye hivi” na “wasifanye vile”. Sababu yake ni kwamba wanaume mara nyingi hawataki kabisa kutumiwa kama kitendea kazi mikononi mwa wengine vinginevyo watajibu kwa ukali. Lakini mwanamke mwenye hekima angefuatilia shughuli za mumewe na kuwaangalia washirika wake bila kudhihirika, na mume asitambue.

Pia hutokea kwamba baadhi ya wanamume, wakati mwingine huchelewa kurudi nyumbani isivyo kawaida. Endapo jambo hili linatokea na idadi ya siku anazochelewa kurudi nyumbani imo katika kiwango kinacho kubalika, basi hapana haja ya kuwa na wasi wasi, kwa sababu upo wakati ambapo wanaume hujikuta wanajaribu kushughulikia mambo ambayo hawakuyategemea baada ya kazi zao. Hata hivyo, endapo idadi ya siku anazochelewa kurudi nyumbani inazidi kiwango kisicho kubalika, basi, mke wake atalazimika kufanya upelelezi. Lakini, upelelezi si jambo rahisi, unahitaji uvumilivu na busara, mtu lazima aepuke hasara na malalamiko.

Kwanza kabisa, mke anatakiwa azungumze na mume wake kwa upole na wema: Mke amuulize mume wake kwa nini alirudi nyumbani kwa kuchelewa kuliko jana yake na alikuwa wapi. Mke anatakiwa kufuatitilia jambo hili kwa busara na uvumilivu katika nyakati mbali mbali na fursa tofauti. Kama atagundua kwamba mumewe huchelewa kurudi nyumbani kwa sababu ya kazi yake au kuhudhuria mkutano wa kisayansi, kidini na kimaadili, basi amwache aendelee hivyo. Kama mke anahisi kwamba mume wake amepata rafiki mpya, anatakiwa ajue rafiki huyoni nani. Kama rafiki yake mpya ni mtu mwenye tabia njema na mwenendo safi, basi, asiwe na wasi wasi, kwa sababu rafiki mzuri ni neema kubwa.

Ukihisi kwamba mume wako anaingia kwenye upotofu au ameshirikiana na watu waovu na wasiofaa, basi unatakiwa umsitishe haraka sana. Katika hali kama hii, mwanamke anao wajibu mkubwa sana.

Kosa dogo tu katika kushughulikia jambo hili, kwa kufanya uzembe, linaweza kuharibu maisha ya familia yao.

Hii ni hali ambapo busara na werevu wa baadhi ya wanawake hutumika na kudhihiri. Mtu lazima akumbuke kwamba ugomvi na ubishi si suluhu na huweza kusababisha kinyume chake. Mwanamke nayepitia kwenye tukio hili anazo kazi mbili za kufanikisha: kwanza anatakiwa kutathmini hali ya nyumbani; na ajipime yeye mwenyewe na msimamo wake. Lazima agundue sababu ya tabia ya mume wake.

Lazima afanye uamuzi usio na upendeleo kwa nini haoneshi uchangamfu kwa familia yake na kuelekea kwenye upotofu. Mke anaweza akang’amua kwamba msimamo wake mwenyewe ndio umekuwa sababu; au labda alikuwa ndio sababu; au labda alikuwa hajali vyakula anavyo vipenda mumewe, jinsi anavyoonekana au mambo ya nyumbani. Mambo kama haya huwafanya wanaume wafarakane na familia. Wanaweza wakafuatilia mambo ya upotofu ya nje ili wasahau matatizo yao. Mke anaweza kumuuliza mume wake kuhusu matatizo yake na ajaribu kusaidia kuyatatua.

Kama mwanamke alijisahihisha na kuibadilisha nyumba kulingana na matakwa yake, basi, awe na matumaini kwamba mume wake atarudi tena kwenye familia yake na kwamba ataepuka sehemu zenye uovu.

Pili, mke lazima amwoneshe mume wake wema mwingi kadiri iwezekanavyo. Lazima amshauri mume wake na kumkumbusha matokeo mabaya na matendo yake. Anaweza hata kulia na kumwambia awaache marafiki zake wabaya. Lazima amwambie: Nina kupenda kwa dhati ya moyo wangu. Ninajivuna kuwa na wewe. Ninaona heri kuwa na wewe kuliko vitu vyote na nipo tayari kujitolea kwa ajili yako. Lakini nina huzunishwa na kitu kimoja; kwa nini mwanamume kama wewe, awe na marafiki kama, au ahudhurie dhifa ya aina hiyo? Matendo kama haya hayastahili kufanywa na wewe. Tafadhali acha kufanya mambo haya.

Mke lazima aendelee na msimamo huu hadi aushinde moyo wa mume wake. Inawezekana kwamba mume amezoea kuendekeza tabia zisizofaa na kwamba hawezi kuathiriwa kwa urahisi, lakini mke asikasirike. Lazima afuatilie lengo lake kwa juhudi na uvumilivu zaidi.

Wanawake wanao uwezo mkubwa kwa wanaume. Mwanamke anaweza kufanya lolote atakalo kama akili yake itamwelekeza kufanya hivyo. Kama mwanamke anaamua kumwokoa mume wake kutoka kwenye kinyaa cha maovu, anaweza kufanya hivyo. Upo uwezekano wa asili mia themanini kushinda, almuradi utekelezaji wake uwe wa busara. Kwa vyovyote vile, mke hatakiwi kutumia nguvu au msimamo wa ukali; isipokuwa tu kama haoni matokeo yoyote ya kuonesha wema na upole kwake. hata hivyo, hatakiwi agombane, aondoke nyumbani au atumie njia nyingine yoyote ile ya upole kadiri iwezekanavyo na si kulipize kisasi.

Ndio, kutunza mume ni kazi ya kila mke. Ni kazi ngumu na ndio maana Mtume (s.a.w) alisema: “Jihadi ya mwanamke ni kumtunza mume ipasavyo.”

Wanawake Wenye Dhana

Si vibaya mwanamke kuwa na tahadhari kuhusu mume wake, lakini ni pale tu ambapo haitavuka kiwango cha dhana na kutokuaminiana. Dhana ni maradhi yenye uharibifu na yasiotibika. Bahati mbaya baadhi ya wanawake huathiriwa na ugonjwa huu (wa dhana).

Mwanamke mwenye dhana hudhania kwamba mume wake, hawi mwaminifu kwake kihalali au isivyo halali. Anadhani kwamba ameoa mke mwingine au anataka kuoa mke mwingine. Mke anatuhumu kwamba mume wake anao uhusiano wa kimapenzi na katibu mukhtasi wake au mwanamke mwingine. Hupoteza imani kwake kwa sababu huchelewa kurudi nyumbani au alionekana anaongea na mwanamke.

Endapo atamsaidia mjane na watoto wake, mke anaweza kufikiria kwamba mume wake anavutiwa na mwanamke huyo, na si tendo la msaada.

Kama mwanamke yeyote anampongeza mume wake, kwa kumwambia kwamba sura yake inapendeza au tabia yake ni njema, anamalizia kwa kusema kwamba yeye anavutiwa na mwanamke huyo. Kwa kuona unywele wa mwanamke ndani ya gari yake, mke anadhani yupo mwanamke mwingine katika maisha yake. Wanawake wa aina hii wenye fikira kama hizi na uthibitisho usio kamili, polepole kimakosa hupata uhakika kuhusu waume zao kutokuwa na uaminifu.

Huwaza kuhusu suala hili usiku na mchana.

Pia huwaambia wengine, marafiki, na maaadui kuhusu suala hili; ambao kwa jina la huruma, wanaongezea nguvu shutuma zao na kuanza kuwaambia wanawake wahusika habari za wanaume wengine wasio waaminifu.

Ubishi na ugomvi huanza kutokeza. Mwanamke huanza kudharau mambo ya nyumbani na watoto na anaweza hata kwenda kwa wazazi wake.

Atamfuatilia na kupekua mifuko yake. Atasoma barua zake na ataelezea kila jambo dogo kuwa ni kwa sababu ya yeye kutokuwa mwaminifu.

Kwa msimamo huu, atayafanya maisha ya familia kuwa magumu na kuigeuza nyumba kuwa jahanamu iwakayo moto na ambamo yeye pia atateseka. Kama mume wake angeleta uthibitisho wa yeye kutokuwa na hatia au kuapa kwamba hajafanya jambo lolote baya, au alie, bado hataridhika.

Msomaji bila shaka amekwisha waona wanawake wa aina hii, lakini inafaa kujua mifano ifuatayo:

“Mwanamke alisema kwenye mahakama: “msishangae kwa nini nimeamua kutengana na mume wangu baada ya maisha ya ndoa ya miaka kumi na mbili na watoto wadogo watatu. Sasa ninao uhakika kwamba mume wangu si mwaminifu kwangu. Siku chache zilizopita nilimwona anatembea mtaani na mwanamke wa kuvutia. Nikasoma gazeti la kila wiki lenye ukurasa wa utabiri wa nyota.

Kila wiki, utabiri wa nyota ya mume wangu unasema kwamba angefurahia maisha na watu waliozaliwa mwezi wa juni. Mimi nimezaliwa mwezi wa Februari; Kwa hiyo mimi si mmojawapo wa watu waliotajwa kwenye utabiri. Zaidi ya hayo ninahisi mume wangu hanipendi kama alivyokuwa ananipenda zamani.”

Mume wa mwanamke huyu akasema: “Tafadhali niambie nifanye nini. Ningependa magazeti haya yangewafikiria wasomaji kama mke wangu, na hayangesema uwongo mwingi sana. Naomba kuaminiwa ninaposema kwamba huu utabiri wa nyota umeyafanya maisha yangu na yale ya watoto wangu kuharibika. Kama mojawapo ya utabiri huu unasema kwamba wiki hii nitapata kiasi kikubwa cha fedha halafu mke wangu huja kwangu na kuniuliza fedha nilizopata nimezifanyia nini? Au endapo utabiri wa nyota unasema kwamba ningepokea barua, basi Mwenyezi Mungu na anikoe! nadhani labda ni vizuri zaidi tutengane kwa sababu mke wangu hataki kukabiliana na ukweli.”

Mwanaume alisema mahakamani: “Ilikuwa mwezi uliopita nilipokuwa narudi kutoka kwenye karamu, mfanya kazi mwenzangu aliniomba nimpe lifti yeye na mke wake hadi nyumbani kwao. Siku moja mke wangu aliniomba nimnpeleke kwa wazazi wake. Wakati tupo njiani, mke wangu alipotazama nyumba ya gari akaona unywele wa mwanamke kwenye kiti cha nyuma. Akauliza unywele huo ulikuwa wa nani. Nilihangaika na sikuweza kumpa maelezo yanayo faa. Nilimfikisha nyumbani kwa wazazi wake na mimi nilikwenda kwenye kazi yangu. Nilipokwenda kumchukua usiku huo akakataa kuondoka na mimi. Nilimuuliza kwa nini? Aliniambia kwamba afadhali niendelee kuishi na mwenye huo unywele.”

Mwanamke mwenye umri mdogo alilalamika mahakamani na akasema: “mume wangu huchelewa kurudi nyumbani kila siku usiku kwa sababu ya kufanya kazi saa za ziada.

Nina wasi wasi kuhusu hili na tuhuma yangu imeongezeka kwa sababu ya hayo yanayo semwa na majirani zetu. Wanasema kwamba mume wangu anadanganya na hafanyi kazi usiku na kwamba huenda kwenye starehe zake.

Matokeo yake ni kwamba sipo tayari kuishi na mwongo.”

Katika nukta hii, mume alichukua barua chache kutoka mfukoni mwake na akaziweka kwenye kaunta mbele ya jaji na akamwomba azisome ili athibitishe kwamba yeye hana hatia na kumsitisha mkewe asiendelee na msimamo usiofaa.

“Jaji alianza kusoma barua kwa sauti. Mojawapo ya barua hizo ilionesha kwamba yeye hufanya kazi saa za ziada kuanzia saa 10 hadi 2 usiku. Barua nyingine pia zilihusiana na kazi yake ambapo aliombwa kuhudhuria semina fulani.

Mke wake alikuja mbele na baada ya kuona barua hizo alisema; “Nilikuwa nikipekua mifuko yake lakini zikuziona barua hizi.”

Jaji alisema; “Inawezekana aliziacha ofisini kwake.”

Mume akasema: “Tuhuma ya mke wangu kwangu imekuwa kubwa mno hivyo kwamba ninamtuhumu yeye. Kila siku usiku ninapatwa na majinamizi, ninadhani kwamba mke wangu anaye bwana mwingine na anataka tutengane ili akaolewe na bwana huyo.”

Kufikia hapo, mke alimkimbilia mume wake kwa haraka huku analia kwa furaha, alimwomba msamaha na wote wakaondoka mahakamani.

Mtaalamu wa meno alilalamika mahakamani na kusema: “Mke wangu ana wivu kupita kiasi. Mimi ni mtaalamu wa tiba ya meno na wapo wagonjwa wanawake ambao huja ofisini kwangu kwa ajili ya matibabu. Hali hii imeamsha wivu wa mke wangu na kila siku tunabishana kuhusu jambo hili. Mke wangu anaamini kwamba nisingewatibu wagonjwa wanawake. Lakini haiwezekani mimi nipoteze wateja wangu na yeye ananipenda mimi, lakini matumani yake yasio na maana yanaharibu maisha yetu.

Siku chache zilizopita alikuja kwenye chumba changu cha upasuaji na akanilazimisha tuondoke.

Tulikwenda na tukagombana. Aliniambia: ‘Nilikwenda kwenye chumba chako cha upasuaji na nikaketi karibu na msichana mdogo kwenye chumba cha wanaosubiri. Mimi na msichana huyu tukazungumza kuhusu wewe bila kujua kwamba mimi ni mke wake, alisema; Huyu bwana mganga wa meno ana sura nzuri na anatabia njema.” ’

Mganga wa meno aliendelea kusema: “Kwa sababu ya maoni ya msichana, mke wangu aliniburuza nje ya sehemu yangu ya kazi kwa njia ya kunivunjia heshima.”

Mwanamke alilalamika mahakamani na alisema: “Mmojawapo wa marafiki zangu aliniambia kwamba mume wangu huenda kwenye nyumba ya wageni wanawake. Siku moja nilimfuata na kugundua kwamba ilikuwa kweli. Sasa nataka mahakama imwadhibu.” Mume katika kukubali yale yaliyosemwa na mke wake, aliiambia mahakama: “Siku moja nilikwenda kwenye duka la dawa kununua dawa. Nilimuona mwanamke humo kwenye duka la madawa ananunua maziwa ya unga. hakuwa na fedha ya kutosha kununua maziwa, kwa hiyo nikajitolea kumsaidia. Baadaye nilitambua kwamba ni mjane ambaye alikuwa masikini. Kwa hiyo niliamua kuendeleza msaada wangu.” Majaji walitambua ukweli baada ya kuchunguza jambo hili na wakawasuluhisha wanandoa.”

Matukio kama haya hutokea kwenye familia nyingi. Hali ya familia hubadilika na huwa na mazingira ya kutazamia taabu tuhuma na uadui.

Watoto watapata mateso na athari za kisaikolojia ni mbaya sana.

Kama wanandoa wanaendelea katika hali hii, basi wote watateseka na wakioneshana kiburi, hakika wataelekea kutalikiana.

Inapotokea kutalikiana, wote wawili mume na mke watahasarika, kwa sababu kwa upande moja mume hatawaza kupata mke mwingine ambaye atakuwa bora zaidi kuliko wa kwanza. Kwa upande mwingine, watoto watateseka na hawatafurahia maisha mazuri. Watoto wanaweza hata kupata matatizo mapya kwa sababu ya baba wa kambo au mama wa kambo.

Mwanamume anaweza kudhani kwamba kwa kumtaliki mke wake, anaweza akamuoa mke, ‘bora’ ambaye ataishi naye kwa amani. Lakini hii ni ndoto tu na kuitambua ni vigumu sana. Kwa kumtaliki mke wake, anaweza akakutana na matatizo mapya kutoka kwa mke mpya.

Kutalikiana si njia ya kuielekea kwenye faraja na furaha kwa mwanamke. Licha ya kwamba anaweza kuhisi kwamba amelipiza kisasi, kuolewa tena haitakuwa rahisi kwake. Anaweza kuishi peke yake katika maisha yake yote na labda hatafurahia hata kuwa nao watoto wake. Hata kama ataolewa tena, hakuna uhakika kwamba mume wake mpya atakubaliana na matarajio yake. Anaweza hata akajikuta analea watoto wa mume wa mke aliyefariki. kwa hiyo wala si talaka ama ubishi na ugomvi vinaweza kuwaokoa wanandoa. Lakini ipo njia inayoweza kuwakomboa.

Msimamo mzuri kushinda yote ni kwamba mwanamume na mke wake wanaacha kubishana na kujaribu kuwa na mantiki. Wanamume wanayo wajibu mkubwa zaidi katika jambo hili na kwa kweli ufunguo wa suluhu upo mikononi mwao. Kwa kufuatia uvumilivu na usamehevu, wanaume wanaweza kujiokoa kutoka kwenye matatizo na pia kusaidia kuondoa kabisa dalili za tuhuma kwa wake zao.

Sasa maneno machache kwa wanaume:

Kwanza, mpendwa bwana! Lazima ukumbuke kwamba mkeo hata kama anakutuhumu, anakupenda. Anavutiwa sana na watoto wako na nyumba yenye familia.

Anaogopa kutengana. Kwa hakika atateseka kwa sababu ya hali yako ya maisha ya kusikitisha. Kama angekuwa hakupendi, hangekuonea wivu. Kwa hiyo mkeo hapendezwi na hali ya sasa, lakini atafanya nini endapo yeye ni mgonjwa? Wagonjwa wengine wanayo maradhi ya baridi yabisi na wengine wanaugua saratani. Mke wako anaumwa maradhi ya kuvurugikiwa na akili na kama huamini, basi mpeleke kwa mtaalamu wa maradhi ya akili. Unatakiwa kuwa na huruma na mpole. Usimkasirikie au kubishana na mkeo. Hapana mtu anayeweza kugombana na mtu mgonjwa. Usiwe mkali kwa ajili ya matendo yake yasio na adabu au madai. Usiishie kupigana naye.

Usimpeleke kwenye mahakama yoyote. Usimdharau. Usizungumze habari ya talaka au kutengana. Baina ya matendo haya, hakuna mojawapo linaweza kutibu maradhi yake, kwa kweli maradhi hayo yanaweza kuwa mabaya zaidi. Kutokuwa mwema kwake inaweza kuwa chanzo cha tuhuma yake.

Lazima uwe mwema kwa mkeo kadiri iwezekanavyo. Unaweza kumkasirikia mkeo sana kwa sababu ya msimamo wake, lakini hakuna njia nyingine yoyote. Lazima umtendee kwa namna hivyo kwamba anakuwa na uhakika wa wewe kutokuwa na hatia.

Pili, unatakiwa kujaribu kutengeneza uelewano baina yenu. Usimfiche kitu chochote. Mruhusu asome barua zako hata kabla wewe hujasoma. Usifiche funguo za meza yako ya faragha au sefu, Mruhusu apekue mabegi na mifuko yako. Mruhusu akufuatilie. Usioneshe kutokufurahishwa na mambo yaliyotajwa hapo juu, lakini yafikirie kama utaratibu wa kawaida katika maisha ya familia iliyo imara na kuelewana.

Baada ya kazi, kama hauna shughuli nyingine, rudi nyumbani haraka iwezekanavyo. kama jambo la haraka linajitokeza ambalo linahitaji kushughulukiwa, basi mwambie mkeo na mjulishe unakokwenda na wakati ambao atakutarajia kurudi nyumbani. Halafu jaribu kurudi muda huo. Endapo unachelewa kurudi nyumbani, basi haraka mwambioe mkeo sababu ya kukuchelewesha.

Uwe mwangalifu, usidanganye, vinginevyo ataanza kukutuhumu. Omba ushauri wake kuhusu mambo yako. Usimfiche kitu chochote. Mpe uhuru wa kukuuliza kuhusu suala lolote lisiloeleweka na kumtatiza yeye.

Tatu, wewe unaweza kuwa huna hatia ya jambo ambalo anakutuhumu, lakini pia tuhuma za wanawake zilizo nyingi si kwamba hazina uthibitisho. Labda, kwa kutokuwa mwangalifu umefanya jambo ambalo limemwathiri kiakili na kumfanya akutuhumu. Lazima utafakari kwa uangalifu kuhusu matendo yako ya nyuma. Inawezekana ukatambua sababu ya tuhuma yake. Kwa njia hii unaweza kutatua tatizo vizuri zaidi. Mathalani, kama wewe unataniana sana na wanawake wengine, jaribu kusitisha tabia hiyo kabisa.

Kuna umuhimu gani wewe kusifiwa kuwa unayo sura nzuri na tabia njema kwa hasara ya kutuhumiwa na mkeo na kutokukuamini? Kwa nini uchokoze tuhuma ya mke wako kwa kutaniana na katibu muhtasi wako au mfanyakazi mwenzako mwanamke? Kwa nini umwajiri mwanamke? Usitaniane na wanawake wengine, kwenye karamu.

Kama unataka kumsaidia mwanamke mjane, kwa nini usimjulieshe mke wako? Unaweza hata kumsaidia mjane kupitia kwa mke wako. Usijifikirie kwamba wewe ni mtumwa, au mtu aliyefungwa minyororo. Hutakiwi kuwa mtumwa, lakini mwanamume mwenye busara baada ya kufanya mkataba na mke wake, ana mtunza. Unatakiwa umsaidie aondokane na tatizo hili. Kwa uvumilivu na busara, unatakiwa uondoe hatari zinazo tishia msingi wa maisha safi ya familia yenu. Hapo utakuwa umetibu maradhi ya mke wako na kuwaokoa watoto wenu kutoka kwenye huzuni. Utakuwa umetoa huduma kubwa kwako kiakili na kimwili. Zaidi ya haya, Mwenyezi Mungu huwapa thawabu wanamume ambao wapo tayari kujitoa mhanga kwa nyakati muhimu kama hizi.

Imamu Ali (a.s) alisema: “Kila wakati wafanyieni wanawake wastani katika mambo yenu. Semeni nao kwa wema ili matendo yao yawe mazuri”

Imamu Sajjad (a.s) alisema: “Mojawapo ya haki za mwanamke kwa mume wake ni kwamba mume anatakiwa kusamehe ujinga na upumbavu wa mkewe (na kinyme chake).”

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Mwanamume yeyote anayeweza kuvumilia upungufu wa mkewe, kwa uvumilivu wake (kwa mke wake) wa kila mara, Mwenyezi Mungu Mweza wa yote, atampa thawabu za uvumilivu wa Hadhrat Ayub (a.s)”

Sasa wanawake wanakumbushwa kuhusu mambo machache:

Kwanza: Mpendwa Bibi! Suala la mume wako kutokuwa mwaminifu, kama masuala mengine yoyote, linahitaji kuthibitishwa.

Almuradi hajathibutishwa kuwa anahatia, huna haki ya kumtia hatiani. Wala si sheria ama dhamira ya mtu humruhusu mtu kumshtaki mtu kwa sababu ya welekeo wa uhalifu kufanyika. Wewe hungehisi uchungu kama mtu angekushtaki kuhusu kitu fulani bila ya uthibitisho wowote? Inawezekana kufikiria nadharia zako za kipumbavu na zisizo na msingi kama ndio uthibitisho wa uhalifu mkubwa kama zinaa?

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ {12}

“Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani baadhi ya dhana ni dhambi…” (Quran 49:12).
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Uzito wa kumshitaki mtu asiye na hatia kwa kumsingizia ni mzito zaidi ya milima mirefu.”

Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Mtu yeyote anayemshitaki muumini kwa kumsingizia, Mwenyezi Mungu, siku ya Ufufuo atamweka kwenye lundo la moto ili apate adhabu anayostahili.”

Mpendwa Bibi! Usiwe mpumbavu na usifanye haraka kuamua mambo. Unapokuwa na wakati, keti na andika uthibitisho wote na hoja kuhusu mumeo kuvunja uaminifu kwako. Halafu mbele ya kila jambo, andika vipengele vingine kwenye tatizo hilo na uwezekano wa mambo hayo kujitokeza tena. Kitakachofuata, jiweke wewe katika nafsi ya jaji na utafakari kwa undani sana kuhusu mambo yaliyoandikwa. Kama hazikushawishi kwamba ana hatia, basi ama unaweza kusahau jambo hilo au ufanye uchunguzi zaidi.

Mathalani kuwepo kwa unywele wa mwanamke kwenye gari ya mume wako ni jambo ambalo linaweza kuelezeka kwa urahisi kwa mojawapo ya haya yafuatayo: Unywele huo unaweza kuwa ni wa mmojawapo wa ndugu za mumeo kama vile dada yake, mama yake, changazi yake au watoto wao.

Unywele huo unaweza kuwa ni wako.

Inawezekana alimpa lifti rafiki au ndugu yake akiwa na mke wake na unywele huo ukawa ni wake.

Inawezekana alimpa lifti mwanamke ambaye alikuwa hajiwezi.

Inawezekana mmojawapo wa maadui zake ameangusha unywele huo kwenye gari lake kwa makusudi ili kukufanya wewe uwe na wasiwasi na mumeo.

Inawezekana aliyempa lifti ni mmojawapo wa wafanyakazi wanawake kwenye gari lake.

Pia uwezekano upo kwamba alitoka nje kimatembezi na hawara yake. Lakini mfano huo upo mbali mno kuliko ile iliyo tangulia kwa hiyo si wa kuzingatiwa sana. Si lazima mtu aufikirie kama ushahidi madhubuti wa kumtia mtu hatiani wakati ambapo anasahau uwezekano mwingine katika orodha hiyo hapo juu.

Kama mumeo anachelewa anarudi nyumbani, inawezekana alikuwa anafanya kazi za ziada; au labda alikuwa nyumbani kwa rafiki yake; au alikuwa anahudhuria semina au mkutano wa kidini; au inawezekana alitembea kwa miguu kurudi nyumbani.

Kama mwanamke anamuona mumeo kuwa ana sura ya kuvutia, hilo si kosa la mumeo. Kuwa na tabia njema si uthibitiosho wa kuwa na hatia!

Je, ungependa mumeo kuwa mtu mkali na kukimbiwa na kila mtu?

Kama mume wako anamhudumia mjane na watoto wake, mfikirie kuwa ni mtu mwenye kupenda kusaidia ambaye anafanya hili kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Kama mume wako anayo meza ya faragha au sefu nyumbani; na kama hakuruhusu kusoma barua zake usimfikirie kuwa anaye kimada. Kwa kawaida wanamume wanayo tabia ya usiri na wastani. Hawapendi watu wengine wajue mambo yao, labda wanayo mambo ya siri yahusuyo kazi zao. Labda hakuona wewe kama mtu unayeweza kuweka siri. Kwa vyovyote vile, uwezekano ni huo tu na usifikirie kuwa uthibitisho madhubuti.

Pili: Wakati wowote unapodhania jambo lolote ni lazima ulizungumze na mume wako kwa namna ambayo utapata ukweli wa jambo lenyewe, na si kwa njia ya ugomvi. Uwe muwazi kwake na muombe akueleze kuhusu suala la dhana yako ili usafishe moyo wako na utulie katika amani. Halafu msikilize kwa uangalifu. Tafakari kuhusu maelezo yake. Kama unaridhika nayo basi jambo hilo liishe.

Lakini kama bado una wasi wasi, basi chunguza jambo hilo wewe mwenyewe hadi ukweli ujulikane. Kama wakati wa kupeleleza unapata kipengele ambacho mumeo alidanganya, basi usikifikirie kama ndio uthibitisho wa kuwa na hatia. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa hana hatia, inawezekana kwa makusudi alikuwa hasemi kweli ili usije ukawa na wasi wasi zaidi. Tena ni bora zaidi kumwendea na kumhoji kwa nini hakusema kweli yote. Kama mambo yalivyo, si vema mtu kudanganya, lakini mumeo alifanya kosa hili, basi wewe usifanye upumbavu. Muulize kwa ushupavu akwambie ukweli.

Kushindwa kwake kukueleza kuhusu suala la tuhuma yako si dalili ya yeye kuwa na hatia. Inawezekana kwamba kwa hakika anaweza kusahau jambo au anaweza kuwa amehangaika. Wakati huu, usiendelee kufuatilia jambo hili tena na liache hadi wakati mwingine unaofaa. Akikwambia kwamba amesahau kitu fulani, kubali. Hata hivyo, kama bado unayo mashaka, fanya upelelezi kupitia njia nyingine.

Tatu: Usimwambie kila mtu unayemuona dhana yako kwa mumeo, kwani wanaweza kuwa maadui zako. Maadui mara nyingi huthibitisha madai yako na wanaweza hata kuongeza uwongo juu yako ili waharibu maisha yako.

Wanaweza kuwa si maadui, lakini kundi la watu wapumbavu wenye kuvutiwa kiakili kwa rahisi na watu wasiokuwa na uzoefu ambao wataimarisha madai yako kwa namna ya kukuhurumia. Watu hawa wanaweza kuwa ni ndugu zako au marafiki zako wa karibu. Ushauri unaofaa unatakiwa kutolewa na watu wenye busara, werevu na wenye huruma halisi. kama unataka kupata ushauri, basi waendee watu wanao stahiki na uwazungumzie jambo hili.

Nne: Kama ushahidi wa hatia ya mume wako si madhubuti; kama marafiki zako na ndugu zako wanadhani kwamba ushahidi huo hautoshi, endapo mume wako anajihisi kwamba hana hatia na hatimaye kama bado unamtuhumu, basi uwe na uhakika wewe unayo maradhi. Maradhi hayo ni kuvurugika kwa akili ambamo dalili za tuhuma zimeongezeka na kushindwa kuzidhibiti. Ni muhimu uende umuone mtaalamu wa magonjwa ya akili ambaye atakutibu ipasavyo.

Tano: Kwa hiyo, si busara wewe kubishana na mume wako au kupeleka malalamiko mahakamani. Usizungumze kuhusu talaka na usimshushe hadhi yake. Msimamo wa aina hiyo unaweza tu kuongeza hasira zaidi na ugomvi ambao unaweza kusababisha kuachana. Uwe mwangalifu usifanye mambo kipumbavu au kuamua kujiua. Kujiua mwenyewe si tu kwamba utapoteza maisha, lakini pia utaadhibiwa huko akhera.

Je, si jambo la kusikitisha kupoteza maisha yako kwa sababu ya fikra isiyo na msingi? Je, si vema kutatua matatizo yako kwa uvumilivu na busara?

Sita: Kama bado unamdhania mume wako au una hitimisha kwamba kwa hakika anaye mpenzi nje ya ndoa, bado wewe unalaumiwa, kwa sababu hujajaribu vya kutosha kuvuta moyo wake. Unaweka ufa katika maisha yake ambapo wanawake wengine wanaweza kuona ni mahali pa wazi na wakakaa hapo. Lakini, usikate tamaa; bado muda upo. Angalia upya msimamo wako na fanya mambo yako kwa namna ya kumvuta mume kwako.

Usisikileze mazungumzo ya uwongo

Mojawapo ya tabia hasi ya watu wengine ni kuwasema wengine kwa ubaya. Tabia hii si tu ni mbaya kwa jinsi ilivyo, lakini pia ni chanzo cha fitina. Husababisha dhana, kukosa rajua (kushutumu kila kitu), kutotangamana na migongano miongoni mwa watu. Huharibu mazingira ya kirafiki na kupanda mbegu ya kutokuelewana miongoni mwa familia. Huwatenganisha wanamume kutoka kwa wake zao na inaweza kusababisha mauaji.

Kwa bahati mbaya tabia hii imeenea miongoni mwa watu hivyo kwamba haionekani kuwa ni mbaya tena. Kwenye mkutano utawaona watu wanateta na kusengenya. Hususan kwenye mkutano wa wanawake, ishara za kuteta huwa zimejazana. Wanawake wawili wakikutana, huanza kuteta. Wanawasengenya wenzao kama vile ni mashindano. Wakati mwingine huwasema waume zao. Mathalani wanawasema jinsi waonekanavyo au kazi zao, na kuona dosari za mume wa nwanamke mwingine. Mwanamke mmoja anaweza kumlaumu mwenzake kwa kuolewa na makenika au fundi viatu. Kama mume ni dereva atasema; “Mumeo kila mara yupo safarini, unawezaje kuvumilia hali hiyo? Kama mume anauza nyama, atasema mumeo kila mara hunuka mafuta.”

Kama mume hana kipato cha kutosha, atasema; “Unaishi vipi kwa fedha ndogo kiasi hicho? Kwanini uliolewa naye? Si inasikitisha kwamba wewe na uzuri wote huo umeolewa na mtu mfupi na dhalili kama huyo? Wazazi wako walikuruhusu vipi kufanya hivi? Walichoka kuishi na wewe? Ungeweza kuolewa na mwanamume yeyote ambaye ungemtaka. Kwa nini ulimchagua mwanammume huyu? Hakupeleki mahali popote, hakupeleki sinema, popote.

Pamoja na hayo mumeo ni mtu mwenye uso wa kuotisha. Unawezaje kuishi naye? Ni vipi wewe, na elimu yako, ulikubali kuolewa na mkulima?”

Mazungumzo ya aina hii yanaweza kusikika katika asiliamia kubwa miongoni mwa vichimbakazi wa kike katika jamii yoyote. Wanawake wenye mazoea ya namna ya kuzungumza, kwa kweli, hawafikirii kuhusu matokeo mabaya sana yanayofuata baadaye. Hawafikiri kwamba kuteta kwao na kutafuta na kuona makosa ya watu ni tabia inayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa au hata mauaji.

Wanawake wa aina hii kwa kweli ni mashetani katika umbo la binadamu. Wao ni maadui wa familia. Hutengeneza migongano miongoni mwa familia na kuzibadili nyumba zao kuwa gereza la chini ya ardhi lenye giza na kutisha. Mtu anaweza kufanya nini? Hii ni sehemu ya jamii zetu. Licha ya kwamba Uislamu umetukataza kabisa kufanya vitendo kama hivi, hatupo tayari kuacha.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Enyi watu mnaodai kuwa ni Waislamu, lakini mlishindwa kuiruhusu imani iingie kwenye nyoyo zenu, msiwaseme Waislamu kwa ubaya na msitafute dosari zao.

Yeyote anayetafuta mapungufu ya watu, basi Mwenyezi Mungu Mweza wa yote atakuwa anafanya kama anavyofanya mtu huyo kwa wengine; na katika hali ile watafedheheshwa miongoni mwa watu, licha ya kuwa watakuwa majumbani mwao.”

Wanawake wenye tabia mbovu wanaweza kuwa wanafuatilia lengo moja au mengi. Wanateta kwa ajili ya kulipiza kisasi ili wavunje familia. Wanaweza wakafanya hivyo kwa sababu ya husuda au kujifaharisha wenyewe. Pengine walitaka kuficha upungufu wao wenyewe au kuwadanganya wanawake walio wepesi kudanganywa. Wanaweza kujifanya kuwa wanahuruma. Wakati mwingine wanateta kwa sababu ya kujifurahisha na hawafuatilii lengo lolote zaidi ya kuridhisha matamanio yao ya kuchukiza. Lakini mtu anachoweza kuwa na uhakika nacho ni kwamba matendo ya aina hii hayafanywi kwa lengo la kuwasaidia wengine na kwamba matendo kama haya yanaweza kusababisha athari za maangamizi.

Wasomaji kwa hakika wamekutana na matuko fulani ambayo yametokea kutokana na utesi. Ufuatao ni mfano wa matukio hayo: “Mwanamke alisema mahakamani: “Bwana… alikuwa na tabia ya kumteta mume wangu kwa lengo la kusababisha ugomvi baina yangu na mume wangu. Alikuwa akiniambia kwamba mume wangu hakuwa mtu mzuri vya kutosha na kwamba hakunielewa mimi au sikuwa na mshtuko wowote. Kila mara alitaka mimi nipewe talaka na niolewe na yeye…. matokeo ya ushauri wake wa udanganyifu nilipotoshwa na siku moja mimi na yeye tulimuua mume wangu.”

Bibi mpendwa! Sasa umetambua nia mbaya zilizojificha kwenye usengenyaji na kama unampenda mume na watoto wako, basi usije ukavutiwa na ndimi za mashetani yenye umbo la binadamu. Usikubali urafiki wao wa udanganyifu. Hakikisha wao si marafiki zako, ila ni maadui zako ambao wanataka kukuona wewe unatengana na familia yako. Usiwe mwepesi kudanganywa na usiwaamini.

Jaribu kupata malengo yao maovu kwa kutumia akili. Waambie waache haraka sana wanapoanza kumshutumu mume wako. Usione aibu kuwaambia: “kama mnataka muwe marafiki, basi acheni kuzungumza habari zinazohusu mume wangu. Si haki yenu nyinyi kumshutumu mume wangu. Ninampenda na hana dosari yoyote.”

Mara watakapo tambua kwamba unampenda mume wako na watoto wako kwa kutumia uimara wa ulimi wako, basi wanaweza wakatahayari kwa kukupotosha na hutasumbuliwa tena. Usidhani kwamba watakasirika, au kwamba utapoteza marafiki zako. Kama wao ni marafiki zako wa kweli, basi hawatakudhuru na sana watakushukuru. Kama ni maadui zako, basi, ni kipi kizuri zaidi cha kufanya kama sio kuwaepuka. Kama ukikutana na wale ambao wanang’ang’ania matendo yao maovu, vunja uhusiano wako nao.

Kumridhisha Mume Wako Na Si Mama Yako

Msichana anapokuwa nyumbani kwa wazazi wake anawajibika kuwaridhisha. hata hivyo, mara aolewapo, wajibu wake hubadilika.

Anapokuwa nyumbani kwa mume wake, mwanamke lazima ayapatie kipaumbele mahitaji ya mume wake. Hata hapo ambapo matakwa ya mume wake na wazazi wake yanatofautiana lazima amtii mume wake, hata kama wazazi wake hawakuridhika. Kutomtii mume ni kitendo ambacho kinaweza kuharibu uhusiano wa ndoa ya mtu, na kinyume chake. Aidha, kinamama wengi hawafaidi ilmu sahihi na busara.

Mama wengine, hawajatambua kwamba wanatakiwa kuwaacha mabinti zao wafikie maelewano na wanaume zao wenyewe.

Wanandoa lazima waachwe wapange mambo yao wenyewe na kama wakipata tatizo lolote walitatue wao kwa kutumia uwezo wao.

Kwa kuwa mama wa wake hawajui jambo hili, basi wao katika akili zao hujaribu kumfanya mkwe wao afuate wanavyotaka wao. Hujaribu kufanya hivyo moja kwa moja au kwa kuzunguka, kuingilia mambo yao ya familia. Wanawatumia mabinti zao ambao hawajapata uzoefu na hawafahamu vizuri hali yao, kwa lengo la kumvuta mkwe wao. Mama wakwe huwaambia mabinti zao kila wakati jinsi ya kutekeleza nini cha kufanya, kusema na asichotakiwa kusema.

Binti ambaye anamuona mama yake kama mwenye huruma na mwenye uzoefu anamtii na anajiingiza mwenyewe kwenye matamanio ya mama yake pia.

Kutakuwa hakuna matatizo yoyote kama mume atakubali matakwa ya mama mkwe wake. Hata hivyo, akionesha kukataa, basi ugomvi huanza kutokea. Kwa sababu ya ujinga wa mama mkwe anaweza kuwa jeuri ambayo inaweza kuharibu familia mabinti yake. Mama mjinga, badala ya kumpa matumaini binti yake kujitolea maisha yake kwa mume wake, anamfanya ampinge mume wake. Mama anaweza kumwabia binti yake: “Umeharibu maisha yako. Mume gani mbaya hivi! Wanaume wazuri kiasi gani walikuwa tayari kukuoa! maisha mazuri yalioje anayoishi binamu yako!

Bahati iliyoje ya dada yako! ni nini walicho nacho ambacho nyinyi hamnacho! Kwa nini uendeshe maisha ya namna hii? Binti yangu masikini!”

Mama ambaye maneno yake yanafikiriwa kama yenye huruma, husababisha ugomvi na ubishi baina ya binti yake na mume wake. Binti anawekwa katika hali ya kuanzisha ugomvi na mume wake. Wazazi wake binti watakuwa upande wake ili hatimaye washinde ugomvi, huonesha kuwa wako tayari mtoto wao apewe talaka.

“Mwanamke wa miaka thelathini alimshambulia mama yake mwenye umri wa miaka hamsini kwa sababu alisababisha kuvunjika kwa ndoa yake. Mwanamke alisema; ‘mama yangu alimsengenya mume wangu sana hivyo kwamba alisababisha mabishano mengi sana kati yangu na yeye. Hatimaye nikaachika lakini nilijuta baada ya muda mfupi. Lakini nilichelewa sana kwa sababu saa sita baada ya kutalikiana aliyekuwa mume wangu akamchumbia binamu yangu. Nilikasirika sana hivyo kamba niliamua kumpiga mama yangu.’ ”

“Mwanaume wa miaka thelathini na tisa alimkimbia mke wake na mama mkwe wake na akajiua, aliacha barua isemayo; ‘Kwa sababu ya msimamo wa mke wangu na kwa sababu hakuwa tayari kwenda Abdan na mimi, niliamua kuiaga dunia hii. Mke wangu na mama yake wanahusika na kifo changu.’ Hivyo mwanaume ambaye alichoshwa na uingiliaji wa mama mkwe wake, alijiua.”

Mwanamume ambaye alikuwa amechoshwa na uingiliaji wa mama mkwe wake, alimtupa nje ya teksi.

Bila shaka, mabinti ambao huwatii mama wa aina hii na kukubali matakwa yao, wanaweza kusababisha pigo lisiloweza kurudishwa kwao.

Kwa hiyo, mwanamke yeyote ambaye anajali familia yake, asivutiwe na matakwa ya mama yake na lazima asiyafikirie kwamba matakwa hayo ni sahihi asili mia kwa mia.

Mwanamke mwenye busara na mwerevu kila mara atapima ushauri na usemi wa mama yake kabla ya kutekeleza katika maisha ya familia yake. Anaweza kuyatekeleza kama hayakupingana au kuhatarisha mkataba wa familia yake. Kwa vyovyote vile binti atalazimika kukubali matakwa ya mama yake. Vinginevyo, kama binti akifikia hitimisho kwamba mama yake si mjuzi, na ushauri wake unaweza kusababisha ugomvi na mabishano, basi anaweza kuukataa ushauri wake.

Kwa vyovyote vile, upo uchaguzi wa aina mbili kwa binti: Kuendelea kutekeleza matakwa ya mama yake na katika hali hiyo,

kitakacho fuatilia ni mabishano ya kifamilia; au Ampuuze mama yake na kukubali kutekeleza matakwa ya mume wake.

Ni wazi kwamba, mtu hatachagua mfano wa (a) kwa sababu kama akichagua, basi ama itamlazimu aishi maisha ya kuteseka na mume wake au amtaliki. Kama ikitokea wakiachana labda mwanamke atakwenda kuishi na wazazi wake. Kwa vyovyote vile hawatamkubali kuwa kama mmoja wao wa familia na watajaribu kumfukuza. Atashushwa hadhi mbele ya watu wengine wa familia. Pia si rahisi kuishi peke yake. Pia haitakuwa rahisi kuolewa kwa mara nyingine. Anawezaje kuwa na uhakika kwamba ndoa nyingine itakuwa nzuri kuliko ya kwanza? Vipi watoto? Vipi watoto wa mume wa ndoa nyingine?

Anaweza kukata tamaa sana hivyo kwamba anaweza akajiua. Anaweza akawa mwanamke ambaye hatoweza kuishi naye hivyo kwamba mwanamume mwingine anaweza kumkimbia au hata kujiua. Mara mwanamke akitafakari matokeo ya kuendekeza matakwa ya ubinafsi na ya yasio na maana ya mama yake au watu wengine, basi lazima afanye uamuzi thabiti wa kudharau mazungumzo yote ili asihatarishe uhusiano wake na mume wake.

Angeweza akamwambia mama yake kwa hekima na adabu: “Sasa mimi nimeolewa, ni vema zaidi mimi nikijaribu kuilinda ndoa yangu na kumridhisha mume wangu. Ningependa kuwa mwema kwake, kwa sababu ni mwenzangu. Anaweza kunifurahisha na anaweza kunisaidia. Mazuri na mabaya ya maisha yanatupata tukiwa wote. Yeye ni chaguo langu na kama tukipata matatizo yoyote tutajaribu kuyatatua sisi wenyewe. Tunaweza kupanga sisi wenyewe, bila ya kupuuza ushauri wako mzuri mama. Kuingilia sana kwenye mambo yetu, inaweza kuwa sababu ya kuongeza ubaya juu ya hali mbaya ikawa mabaya zaidi.

“Kama unataka sisi kuwa na uhusiano mzuri na wewe, basi usiyaingilie maisha yetu, usimseme kwa ubaya mume wangu. (Mama naomba unielewe hivyo) vinginevyo nitalazimika kusitisha uhusiano wangu na wewe.”

Kama mama, yako kutokana na ushauri wako, anaacha kuingilia familia yenu, basi hutasumbuliwa tena. Hata hivyo, kama mama yako hayupo tayari kutilia maanani matakwa yako, punguza kumtembelea, na usiache kumshawishi mara chache hizo utakazomtembelea mpaka auone ukweli wa mambo.

Ambapo kutokana na wewe kuvunja uhusianao na wazazi wako, unaweza kupoteza kiasi fulani cha heshima yako miongoni mwa watu wa familia yako. Hivyo uwe na busara na hekima katika kumshauri mama yako, usiwe fedhuli kwake.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke mzuri zaidi miongoni mwa wanawake ni yule anayezaa watoto wengi, ana upendo na safi; ambaye hakubali kutekeleza matakwa ya ndugu zake lakini mtiifu kwa ajili ya mume wake tu na hujilinda mbele ya wageni, humsikiliza mume wake na kumtii, hutimiza matamanio yake ya faragha na hapotezi staha yake kwa namna yoyote ile.”

Mtume (s.a.w.w) aliongeza: “Mwanamke mbaya zaidi miongoni mwa wanawake ni yule anaye watii ndugu zake lakini hakubali kutekeleza matakwa ya mume wake, mgumba na asiye samehe, haogopi kufanya matendo maovu, hujiremba wakati mume wake hayupo, hatimizi matakwa ya mume wake katika faragha, mume wake akimwomba msamaha hataki kumsamehe makosa yake.”

Uwe Safi Na Mrembo Nyumbani Pia

Ni desturi ya wanawake wengi kwamba huvaa nguo zao nzuri na kujipamba sana, wakati wanapokwenda kwenye hafla au mikutanoni. Hata hivyo, wanaporudi nyumbani wanavua hayo mavazi mazuri na kuvaa nguo za zamani na chakavu. Wanawake hawa hawako makini na usafi nyumbani na hawajipambi. Wanapokuwa nyumbani nywele zao zinakuwa timtim, nguo zenye madoa na soksi zilizotoboka.

Kwa kweli hali inatakiwa ibadilishwe kabisa kwa kiasi kikubwa kabisa, kwamba mwanamke anatakiwa ajipambe akiwa nyumbani na awe mchangamfu kwa mume wake ili aweze kuvutia moyo wake na ili asiache ufa wowote ambao unaweza kujazwa na wanawake wengine. Kwa nini mwanamke aoneshe uzuri wake kwa watu wengine? Hivi inastahiki mwanamke kuonesha uzuri wake kwa wanaume wengine na kusababisha matatizo kwa vijana?

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema: “Mwanamke yeyote anayejipaka manukato na kuondoka nyumbani hawezi kupata neema za Mwenyezi Mungu Mweza wa yote hadi anaporudi nyumbani.”

Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Mwanamke bora zaidi miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mtiifu kwa mume wake, hujiremba kwa ajili ya mume wake lakini haoneshi urembo wake kwa wageni na mwanamke mbaya kuliko wote miongoni mwa wanawake wenu ni yule anayejipamba wakati mumewe hayupo.”

Bibi mpendwa! kuuteka moyo wa mwanaume hususan kwa muda mrefu si rahisi, Usifikirie hivi kwamba: “Ananipenda, hivyo Sihitaji kuonekana mrembo kwake au kujaribu kushinda moyo wake au kumshawishi.” Lazima udumishe mapenzi yako kwake kila siku. Uhakikishe mume wako atafurahi kuwa na mke safi na mrembo hata kama hawezi kutamka. Kama ukishindwa kuridhisha matamanio ya moyo wake na huvai nguo za kuvutia unapokuwa nyumbani, anaweza akawaona wanawake wazuri wenye kuvutia nje ya nyumba.

Anaweza akakatishwa tamaa na wewe na anaweza kuelekeza mapenzi yake nje ya njia iliyo nyooka. Akiwaona wanawake wazuri anawalinganisha na wewe. Kama wewe ni mchafu, mzembe, na nywele zako ni matimtim, anaweza akadhani kwamba wanawake wengine ni malaika ambao wameteremka kutoka mbinguni. Kwa hiyo jaribu kuonekana unapendeza na kuvutia wakati ukiwa nyumbani na uhakikishe kwamba atavutiwa na wewe kila wakati.

Soma barua ifuatayo iliyoandikwa na mume: “Mtu hawezi kubainisha mke wangu na mtumishi wangu wa ndani ya nyumba. Ninaapa kwa jina la Allah kwamba wakati mwingine hufikiri: natamaani angevaa nyumbani mojawapo ya mavazi haya yalioshonwa kwa ajili ya karamu. Natamani angetupa zile nguo zilizochakaa. Nimemwambia mke wangu mara kadhaa; Mpenzi angalau vaa zile nguo nzuri hapa nyumbani unapokuwa likizo. Akajibu kwa ukali ‘ Sihitaji kwa tofauti ninapokuwa nyumbani, lakini kama siku moja ninaonekana mchafu, mbele ya wafanyakazi wenzangu, nitaona aibu.’ ”

Msomaji anaweza kuamini kwamba wakati mwanamke anaangalia usafi wa nyumba na kupika hawezi kuvaa vizuri na kupendeza.

Hii inawezekana kuwa kweli lakini mama wa nyumba anaweza kuwa na nguo tofauti za kuvaa wakati wa kufanya usafi wa nyumba; na anaweza akabadilisha nguo zake za kufanyia kazi anapokuwa mbele ya mume wake au anapokuwa amerudi nyumbani. Wakati wote unaweza kuchana nywele zako na kujiweka katika hali ya usafi baada ya kufanya usafi wa nyumba.

Imamu Baqir (a.s) alisema: “Ni wajibu wa mwanamke kujipaka manukato na kuvaa nguo nzuri sana, kujipamba kadiri iwezekanavyo, na kukutana na mume wake katika hali hii mchana na usiku.”

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Wanawake hawatakiwi kuacha kujiremba iwe hata kuvaa kidani tu. Usiwe na mikono isiyo tiwa rangi kidogo, hata kama ni hina kidogo tu. Hata wanawake wazee wasiache kujipamba.”

Uwe Kama Mama Kwake

Wakati wa kazi nyingi na kuumwa maradhi, mtu anahitaji kutunzwa na watu wengine. Muuguzi anaweza kusaidia kupona kwa mgonjwa vizuri mno kwa sababu ya kumwangalia mgonjwa kwa wema na mapenzi. Wanamume ni watoto wadogo ambao wamekuwa. Watahitaji matunzo kama ya mama. Mwanamume akioa mwanamke, anatarajia mke wake kuwa kama mama yake kwake wakati akiugua na matatizo.

Bibi mpendwa! Kama mume wako anaugua, muangalie zaidi kuliko ilivyo kawaida.

Onesha huruma yako kwake na uoneshe kwamba umefadhaishwa sana na ugonjwa wake huu. Mliwaze, tayarisha mahitaji yake yote na wanyamazishe watoto ili mgonjwa apumzike. Kama anahitaji daktari au dawa, basi fanya atakavyo. Mpikie chakula anacho kipenda na ambacho ni kizuri kwake. Muulize kuhusu afya yake mara kwa mara. Jaribu kukaa karibu naye kadiri iwezekanavyo. Kama anaumwa sana hivyo kwamba hawezi hata kupata usingizi na wewe usilale kadiri iwezekanavyo. Mara utakapo amka, mwendee.

Muulize hali yake inaendeleaje. Kama usiku huo hakulala kabisa, basi onesha masikitiko yako. Hakikisha chumba chake kipo kimya wakati wa mchana. Matunzo yako kwake yatasababisha mgonjwa kupata nafuu haraka. Atafurahia juhudi zako na kukupenda zaidi. Zaidi ya hayo angefanya hivyo kwako endapo ungeugua.

Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Jihadi ya mwanamke ni kumtunza vizuri mume wake.”

Hifadhi Siri Za Familia

Wanawake mara nyingi kupenda kujua siri za waume zao, kipato chao, maamuzi yao kuhusu maisha ya siku zijazo, na kazi zao. Wanatarajia wanamume hawataficha chochote kutoka kwao.

Kinyume chake, wanaume hawapo tayari kuwaambia wake zao kila kitu. Matokeo yake ni kwamba waume wengine na wake wengine wakati wote huwa wanabishana kuhusu suala hili.

Baadhi ya wanawake wanasema kwamba waume zao hawana imani nao, hawataki wasome barua zao; hawataki wajue idadi ya kipato chao; wanaficha mambo mengi, hawajibu maswali yao inavyo stahili; na mara nyingine husema uwongo.

Katika hali ya kawaida, wanaume wanaweza kuwaambia wake zao siri zao.

Lakini wanaume wanamini kwamba wake zao hawafichi siri; kwamba huwaambia watu kila kitu wanacho jua na wanaweza hata kusababisha matatizo kwa waume zao.

Kama mtu anataka kujua siri za watu wengine inatosha kwenda kwa wake zao. Baadhi ya wake za watu, baada ya kujua siri za waume zao, huwasaliti na kwa hiyo hutumia vibaya imani ya waume zao kwao.

Ni dhahiri kwamba wanaume kwa kiasi fulani wanayo hoja. Wanawake, wakilinganishwa na wanaume, wanazidiwa zaidi na nguvu za mvuto wa hisia. Wanawake wanapo kasirika, hushindwa kujidhibiti, na kwa kuwa wanajua siri za waume zao, huwaingiza kwenye matatizo kwa kutoa siri zao.

Kwa hiyo, kama mwanamke anataka kujua siri za mume wake, lazima awe mwangalifu sana kwamba asiwaambie watu isipokuwa kwa idhini yake. Hatakiwi kuwaambia hata marafiki zake wa karibu sana au ndugu zake. Huko si kuweka siri kama ukimwambia mtu kuhusu siri hiyo, na kumwambia asiseme kwa mtu yeyote, vinginevyo kila mtu atajua siri hiyo.

Kwa hiyo mtu mwenye busara ni yule ambaye hasemi siri yake kwa mtu yeyote.

Imamu Ali (a.s) pia alisema: “Kifua cha mtu mwenye hekima ni kasiki ya siri zake.”

Imamu Ali (a.s) pia alisema: “Wema wa ulimwengu huu na ule ujayo umo katika mambo mawili; Kuwa msiri, na kufanya urafiki na watu wazuri; na maovu yote yamo kwenye mambo mawili kushindwa kuwa msiri na kufanya urafiki na watu wabaya.”

Kubali Uongozi Wake

Kila taasisi, kiwanda na shirika huhitaji meneja muajibikaji. Kwenye kila kitengo cha jamii na shirika, ushirikiano baina ya wafanyakazi ni muhimu. Hata hivyo, kuendesha mambo ya kitengo cha aina hiyo huhitaji meneja ambaye anaweza kuratibu kazi.

Mojawapo ya kitengo muhimu sana cha jamii ni familia; Kuendesha mambo ya kitengo hiki ni jambo la lazima na gumu.

Bila shaka, lazima pawepo na uelewano wa kina sana, na ushirikiano baina ya watu wa familia, lakini pia lazima pawepo kiongozi ambaye anaweza kuwajibika kwa ukamilifu kuhusu mambo ya familia. Ni wazi kwamba, kama familia haimfurahikii mtu anayeweza kuwapanga wengine, itapata usumbufu wa vurugu na ghasia.

Hivyo ama mume lazima awe kama mkurugenzi na mke awe chini yake au kinyume chake.

Hata hivyo, kwa kuwa kipengele cha mantiki ya wanaume kinatawala kipengele cha hisia za wanawake, wanaume wanaweza kuwa viongozi bora zaidi.

Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anasema kwenye Qurani Tukufu:


الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّهُ


ۚ


{34


}

“Wanamume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayotoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii ….” (Quran 4:34).

Hivyo, ni kwa manufaa ya jamaa wa familia kumheshimu mwanaume kama mlinzi wao na mkuu wao, na kutaka usimamizi wao katika matendo yao.

Hata hivyo, mtu asihitimishe kwamba hadhi ya mwanamke ndani ya nyumba inadunishwa, lakini ni kweli kwamba kudumisha utaratibu na nidhamu ndani ya nyumba ni majukumu yanayohitaji utendaji wa mume. Wanawake wanaoweza kufikiri bila upendeleo, wanaweza kuthibitisha tendo hili.

Mwanamke alisema: “Tulikuwa na desturi nzuri Iran ambayo kwa bahati mbaya imefifia pole pole. Kwenye mila hii mwanaume alikuwa ndiye mkuu wa mambo ya familia. Alikuwa ndiye msimamizi. Siku hizi hata hivyo hali imebadilika na familia haziwezi kufanya uamuzi kuhusu nani awe mkuu.

Ninaamini kwamba mwanamke wa leo, ambaye kwa namna moja au nyingine anayo hadhi sawa na ya mwanaume katika jamii, anaweza kukubali mume wake kama mkuu wa kaya…Desturi hii ya zamani inatakiwa ipendekezwe kwa mwanamke kijana wa leo, ambaye anayo nia ya kuolewa.

Anatakiwa kuingia nyumbani kwa mumewe akiwa amevaa vazi la harusi na kutoka ndani ya nyumba hiyo akiwa amevaa sanda.”

Ni kweli kwamba shughuli za maisha ya kila siku hazimruhusu mwanaume kushiriki katika mambo yote ya familia na kwamba kwa kawaida mke ndiye anaye endesha familia kufuatana na atakavyo, lakini hata hivyo haki ya kuamuru hubaki kwa mwanaume, na kwa hali hiyo lazima ahishimiwe.

Kwa hiyo, inapotokea mwanaume kutoa maoni yake kuhusu jambo lolote la familia au anashauri kitu chochote, mke hatakiwi kumpinga au kumnyima mume wake haki yake kuamuru kwa namna yoyote ile. Vinginevyo, mwanaume atajifikiria yeye hana mamlaka na kumuona mke wake kama mwanamke asiye na adabu na shukrani. Mwanaume anaweza kujenga kinyongo dhidi yake na katika hatua ya baadaye, anaweza hata kukataa matakwa ya halali ya mkewe.

Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Mwanamke mzuri atajali matakwa ya mumewe, na atafanya kwa mujibu wa apendavyo mumewe.”

Mwanamke alimuuliza Mtume (s.a.w): “Mwanamke anawajibu gani kwa mume wake?” Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke lazima amtii mume wake na asikiuke amri zake.”

Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Mwanamke mbaya sana miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mkaidi na sugu.”

Mtume (s.a.w.w) pia alismema: “Mwanamke mbaya zaidi miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mgumba, mchafu, sugu na asiye mtiifu.”

Bibi mpendwa! Kubali mamlaka ya mume wako. Taka usimamizi wake kuhusu mambo yenu ya familia. Usikiuke amri zake. Usikatae au kuweka pingamizi, yeye hushiriki katika mambo ya nyumbani na familia. Usikatae kushiriki kwake hata kwenye yale mambo ambayo wewe una utaalamu nayo. Usifanye vitendo vya kuonesha kwamba yeye hana mamlaka.

Mruhusu ashiriki katika kazi zako mara chache. Wafundishe watoto wenu kuhishimu mamlaka yake na waambie lazima waombe ruhusa kutoka kwa baba yao kuhusu mambo yao. Watoto wenu lazima watambue kwamba hawatakiwi kukiuka amri zake tangu utoto wao.

Kwa njia hii watoto wenu watakuwa na malezi ya kuwatii wazazi wao.

Uwe Muelekevu Wakati Wa Hali Ngumu

Maisha yamejaa hali ya kupanda na kushuka kuhusu kipato. Magurudumu ya bahati njema hayazunguki mara zote kufuatana na vile tunavyotaka. Mtu kupita kwenye hali ngumu mara nyingi. Kila mtu huugua maradhi. Hupoteza kazi zao na wengine wanaweza kupoteza utajiri wao wote. Mambo mengi yasiyo furahisha hutokea katika maisha ya kila mtu.

Mwanaume na mwanamke ambao wametoa kiapo cha kuaminiana wao wawili na kusaini makubaliano ya ndoa, wanatakiwa kupita kwenye njia ya maisha kwa kuelewana. Makubaliano yanatakiwa kuwa imara sana hivyo kwamba yanaweza kuwawoka pamoja katika hali ya maradhi na afya njema, katika hali ya neema na shida ya kipato na wakati wa raha na shida.

Bibi mpendwa! Kama mume wako anafilisikia na kuwa fukara, hivi ni lazima uongeze kwenye matatizo yake kwa kuwa na tabia isiyo kubalika.

Kama anaugua, na kulala kitandani, ama nyumbani au hospitalini, ni hatua ya kupendeza wewe ukizidisha wema kwake. Lazima umuuguze, shughulikia mahitaji yake, na tumia fedha kwa ajili yake. Kama unazo fedha za kwako mwenyewe, lazima ulipie matibabu yake. Kumbuka kama wewe ungekuwa mgonjwa, angelipa fedha yake kwa ajili ya afya yako. Je, ni haki wewe uzuiye mali yako kwa kuipendelea zaidi kuliko afya njema ya mume wako? Kama ukishindwa kumridhisha katika wakati mgumu kama huu, basi utamkasirisha, na anaweza hata kupendelea kukutaliki.

Hapa kuna kesi ifaayo kusoma: “Mtu alikuja mahakamani kumwacha mke wake. Alisema: ‘Siku chache zilizopita niliugua na daktari wangu aliniambia kwamba nilitakiwa kufanyiwa upasuaji. Nilimwomba mke wangu anikopeshe fedha alizokuwa nazo kwenye akiba yake. Alikataa na aliondoka nyumbani kwangu. Matokeo yake nilifanyiwa upasuaji kwenye Hospitali ya taifa. Sasa nimepona na afya yangu ni njema sitaki kuishi na mwanamke ambaye anapenda zaidi fedha yake kuliko mume wake. Mtu atamwitaje mwanamke huyu, mke?”

Kila mtu aliye makini katika mambo yake atakubali kwamba kwenye mfano uliotajwa hapo juu, mwanaume ndiye aliyekuwa na haki. Mwanamke kama huyo ambaye hataki kutumia fedha yake kwa ajili ya tiba ya mume wake, hastahili kuwa kwenye nafasi inayo heshimiwa ya ‘mke wa mtu.’

Bibi mpendwa! Uwe mwangalifu, usiwe katili wakati mume wako akiumwa maradhi ya kudumu; hivi ni lazima umwache yeye na watoto wenu kwa sababu hii? Unawezaje kumkimbia mwanamume ambaye umekuwa naye mchana na usiku wa starehe ya siku nyingi? Unajuaje kwamba labda hatima ya aina hii inakungojea wewe? Unawezaje kuwa na uhakika kwamba mwanamume mwingine atakuwa bora zaidi kuliko huyu? Usiwe sugu na mbinafsi. Ujitolee mhanga na uwe na moyo wa kumuabudu Mwenyezi Mungu, uilinde heshima yako na watoto wako.

Uwe mvumilivu na uwafundishe watoto wako somo la moyo wa upendo, mapenzi na ustahamilivu.

Unaweza kuwa na uhakika kwamba, katika dunia hii na ile ijayo, utapata thawabu nyingi sana. Moyo wako wa kujitolea ni njia bora sana ya kuonesha unamjali mume wako tabia ambayo inawekwa kwenye kiwango sawa na Jihadi.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Jihadi ya mwanamke ipo katika kumtunza mume wake.”

Usikatae Kusema Na Usinune

Ni kawaida ya wanawake wengine kwamba, wanapo tibuliwa na waume zao, hununa, hukataa kusema, hukataa kushughulikia kazi za nyumbani, hawataki kula, huwapiga watoto, au hulalamika. Wanaamini kwamba kuacha kusema au kuanzisha ugomvi ndizo njia nzuri sana kulipiza kisasi kwa waume zao. Msimamo huu si tu unashindwa kumwadhibu mwanaume, lakini unaweza kusababisha naye kulipiza kisasi. Maisha huanza kuwa magumu kwani hugeuka kuwa na mfululizo wa ugomvi. Mwanamke hupiga kite, halafu mwanamume naye hufanya hivyo. Mwanamke hukataa kusema na mwanamume hulipa kisasi. Mwanamke hufanya kitu kingine, na mwanamume hufanya hivyo hivyo hadi wanachoka na kupitia upatanishi wa ndugu au marafiki, huelewana. Lakini hii si mara ya kwanza wao kugombana. Watagombana tena na tena na patakuwepo na siku chache za machungu.

Kwa hiyo, kuishi maisha yenye ugomvi wa familia litakuwa si jambo la kufurahisha kwa ama wazazi au watoto. Vijana wengi waliozikimbia familia zao wanatoka kwenye familia za aina hii ambao baadaye huingia kwenye uhalifu na uovu.

Kijana ambaye alikamatwa kwa tuhuma ya wizi, aliwalaumu wazazi wake kwa uhalifu wake na alisema: “Wazazi wangu walikuwa wakibishana kila siku na baadaye kwenda kwa ndugu zao na mimi nilikwenda kuzurura mitaani. Halafu nikadanganywa na vijana wengine na hatimaye nikafanya uhalifu wa wizi.”

Msichana mwenye umri wa miaka kumi aliwaambia wafanya kazi wa usitawi wa jamii: “Sina uhakika lakini nakumbuka kwamba siku moja wakati wa usiku wazazi wangu walibishana kuhusu kitu fulani. Kesho yake, mama yangu aliondoka na baada ya siku chache, baba alinipeleka kwa shangazi yangu. Baada ya kipindi fulani mwanamke mkongwe alinichukua kutoka kwa shangazi na akanileta Tehran. Ni miaka michache iliyopita hadi sasa, ambapo nimekuwa ninaishi naye na niliteseka sana hivyo kwamba sitaki kurudi kwake.”

Mwalimu wa msichana huyo alisema; Huyu msichana ni mmojawapo wa wanafunzi wangu. Hana maendeleo mazuri katika masomo yake na inaonesha kama vile anaumizwa na jambo fulani. Wakati wote anafikiri. Amekuwa hata anakaa kwenye ua wa shule na kuonekana hayuko tayari kurudi nyumbani. Siku mbili zilizopita nilimuuliza kwa nini hataki kwenda nyumbani? Akajibu kwamba alikuwa anaishi na mwanamke mzee ambaye alikuwa mbaya sana kwake na kwamba hakutaka kurudi nyumbani kwa bi kizee huyo. Nilimuliza kuhusu wazazi wake na akasema walitengana.”

Bibi mpendwa! Lazima ukumbuke kwamba kama mume wako anakuwa mkali sana kwako na hataki kusema na wewe, halafu anaweza hata kuchukua hatua kali zaidi kama vile kukupiga.

Inawezekana labda utaondoka kwenda kwa wazazi wako kwa sababu ya ukali wake. Kitakachofuatia ni kwamba wazazi wako wanaweza wakaingilia kati, na ugomvi wako na mume wako utazidi kupanuka. Hatimaye labda unaweza kuachika ambapo wewe utapata hasara zaidi kuliko mume wako. Inawezekana ukaendelea kuishi peke yako katika uhai wako wote. Kwa hakika utajuta kutalikiwa.

Mwanamke alisema: “Kipindi fulani kilichopita niliolewa. Sikuwa na uelewa mzuri kuhusu kumtunza mume wangu na yeye hakuwa na ujuzi wa kutosha kunitunza mimi. Ilikuwa tabia yetu kugombana kila siku. Wiki moja nilikiwa sisemi naye na wiki moja baadaye alikuwa hataki kusema na mimi.

Mnamo siku za Ijumaa tu, tulikuwa tunaelewana, kupitia kwa upatanishi wa marafiki na ndugu. Pole pole mume wangu alikasirishwa na mimi na alifikiria kunitaliki na kuoa mke mwingine. Kwa kuwa nilikuwa na umri mdogo, sikuwa tayari kubadilika na sikukataa kutalikiwa. Tuliachana na mimi nilipanga nyumba ya kwangu mwenyewe. Baada ya muda mfupi nikatambua hatari. Watu wengi niliokutana nao lengo lao kubwa lilikuwa kunidanganya. Niliamua kupatana na mtaliki wangu na nilikwenda nyumbani kwake. Huko nilimkuta mwanamke ambaye alijijulisha kwangu kama mke wa mtalaka wangu. Nililia njia yote nilipokuwa narudi kwangu. Nilijuta kwa nini nilikubali kuachika, lakini nilichelewa sana.”

Mwanamke mwenye miaka ishirini na mbili, alimpeleka mtoto wake kwa wazazi wake, baada ya kuachika, alijaribu kujiua muda wa usiku, siku ya harusi ya dada yake.

Mama mpendwa! Lazima kwa kweli uepuke kumnunia na kukataa kusema na mumeo. Kama mumeo amekutibua uwe mvumilivu. Ukisha tulia na kuwa makini, ongea naye kwa upole kuhusu kukasirika kwako. Mathalan, unaweza kumwambia: “Ulinifedhehesha jana, au ulikataa kusikiliza matakwa yangu… Hivi ni haki kwamba unaweza kunitendea hivyo?”

Njia kama hivyo, si tu inakupumzisha kwenye hisia zako, bali pia itampa onyo. Kwa hiyo, mumeo atajaribu kurekebisha tabia yake na atakuheshimu kwa tabia yako njema. Matokeo yake atapitia upya tabia yake, na atajaribu kuwa na nidhamu.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wakati Waislamu wawili wakikataa kusemeshana na wasipopatana kwa muda wa siku tatu, wote wawili watakuwa wamevua joho la Uislamu, na hapatakuwepo na urafiki wowote baina yao. Halafu yeyote miongoni mwao ambaye ataanza kupatana na mwenzake, siku ya ufufuo ataishia Peponi (haraka kuliko mwenzake.)”

Mume Wako Akikasirika, Wewe Nyamaza

Mwanaume hukutana na watu wengi anapokuwa katika shughuli zake na hukabiliana na matatizo mengi. Anaporudi nyumbani, huwa amechoka na anapokutana na tukio dogo sana lisilofurahisha hukasirika na anaweza kuwa mkali kwa. familia yake.

Mwanamke mwenye busara atanyamaza wakati mume wake anajitapa kwa makelele yenye matusi. halafu mwanaume atanyamaza na kutulia na kujuta kwa matusi yake. Akiona kwamba hakuna jibu lolote kuhusu hasira yake, anaweza hata kuomba msamaha. Kwa msimamo huu, familia hurudi kwenye hali yake ya kawaida baada ya saa moja au mbili tu.

Hata hivyo, kama mwanamke wa nyumbani hakuelewa nafasi nyeti ya mume wake basi anaweza kupiga makelele, kuapa laana na kukasirika kwa ukali.

Kwa njia hii, mume na mke wanaweza kupigana na hatimaye kuchukua hatua ya kuachana. Familia nyingi huvunjika kwa sababu ya matukio madogo kama haya. Ipo hata mifano ambapo wanaume hukasirika sana hivyo kwamba hulipuka kama volcano na kufanya mauaji.

Mwanaume alimpiga risasi mke wake na mama wa kambo, na yeye mwenyewe akajipiga hadi kufa. Inafahamika kwamba wanandoa hao wana ugomvi mwingi na mabishano tangu mwanzo wa ndoa yao.

Usiku wa tukio hilo mume alirudi nyumbani kutoka kwenye shughuli zake ambapo wanandoa hao walianza tena ubishi mwingine.

Mume akampiga mke wake na mwanamke aliamua kwenda polisi. Haraka mwanaume alichukua bunduki, akamuua mke wake, mama yake wa kambo na halafu akajiua yeye mwenyewe kwa risasi.”

Si ingekuwa bora zaidi kama mwanamke angenyamaza wakati mume wake alikasirika? Kama mwanamke angevumilia, maisha ya watu watatu wangepotea? Wewe ungependelea vipi? Dakika chache za kimya au matokeo yote mabaya kwa kuendeleza ubishi na mume wako? Unadhani hata kwa dakika moja kwamba nafasi ya mwanaume inalindwa na kwa hiyo hana hatia. Si hivyo kabisa. Kama mambo yalivyo, anayo hatia.

Hakutakiwa kumaliza hasira yake kwa kumaliza familia yake. Kwenye sura ijayo, jambo hili litazungumziwa kwa kina zaidi lakini hapa tunasema kwamba mwanamke anatakiwa kuwa na busara na asijibu hasira ya mume wake hata kama mume yupo sawa au si sawa. Katika hali kama hii, mwanaume atashindwa kuthibiti hasira yake, kwa hiyo ni muhimu kwamba mke, anyamaze kimya ili aokoe familia yake.

Kwa kawaida wanawake hudhani kwamba kunyamaza kimya wanapokabiliana na hasira za waume zao, ni namna ya kudhalilishwa, na kwa hiyo wangepoteza hishima yao. Hata hivyo, hali hii ni kinyume chake. Mwanaume asiyeona jibu lolote anapomtukana mke wake, kwa hakika atajuta. Atamfikiria mke wake kuwa anampenda, ambaye licha ya uwezo wake wa kulipa kisasi alipendelea kusamehe. Mapenzi yake kwa mke wake yataongezeka mara nyingi. Ataomba msamaha na kwa hiyo mkewe atapata heshima zaidi.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke yeyote ambaye huvumilia hasira mbaya ya mume wake Mwenyezi Mungu atampa thawabu zinazolingana na zile Alizompa Asiya binti Muzahim.”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke aliyebora zaidi miongoni mwa wanawake zenu ni yule ambaye, akiona hasira ya mume wake humwambia; Nina jisalimisha kwako. Siwezi kulala hadi utakaporidhika na mimi.”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Usamehevu na uvumilivu ungeongeza heshima na hadhi ya wahusika. Uwe msamehevu ili Mwenyezi Mungu akuhifadhi.”

Burudani Za Wanamume

Baadhi ya wanamume hupenda kuwa na burudani zao nyumbani. Wanapenda, kwa mfano, kukusanya stampu au vitabu, kushughulikia bustani au kupiga picha wakati wa muda wao binafsi nyumbani.

Burudani kama hizo zimeainishwa kuwa ni shughuli bora zaidi. Burudani za aina hiyo zinafaa sana kwamba huwavutia wanaume kuwa nyumbani mwao, na halikadhalika husababisha akili na mwili kutulia. Mtu anaweza kufadhaika na kuchukizwa kwa sababu ya kukaa bila kufanya kazi. Ni ukweli kwamba njia mojawapo ya kuwatibu watu wenye maradhi, ya akili ni kuwashughulisha na kazi fulani. Wale miongoni mwetu wanaofanya kazi zaidi ya wengine, kwa ujumla hawaathiriwi na kuvurugikiwa na akili na hawaathiriwi na kazi za hatari.

Kwa hiyo, mwanamke lazima ahishimu burudani nzuri za waume wao na wasidhani kwamba burudani za kupitisha muda ni za kipumbavu, duni na zisizofaa. Wanawake lazima wawatie moyo waume zao kujishughulisha na burudani hizi na inapowezekana na wao washiriki.

Utunzaji Wa Nyumba

Nyumba, licha ya kwamba ni eneo dogo, ni neema yenye thamani kubwa. Ni hifadhi ya mwanamume ambaye hukimbilia humo baada ya kazi. Ni mahali pa kupata faraja hata wakati wa likizo, mtu huhisi kupumzika nyumbani kwake.

Hakuna mahali panapolingana na nyumbani na hakuna mahali ambapo mtu anaweza kupata amani kama nyumbani kwake. Ni mahali pa urafiki, upendo, uaminifu, faraja, mapumziko na ambapo wanaume na wanawake wenye maadili mema huelimishwa na kuelekezwa.

Ni karakana ya kuelekeza wanadamu na kuwasomesha na kuwalea watoto. Ni jamii ndogo ambayo humo jamii kubwa zaidi huundwa.

Nyumba inayo dhamana kubwa zaidi. Mazingira ya familia ndogo, licha ya kwamba ni sehemu ya jamii kubwa kufurahia uhuru wa ndani, ndio maana kazi ya kurekebisha taifa lazima ianzie kwenye familia.

Jukumu la elimu, uelekezaji na uendeshaji wa msingi huu nyeti wa jamii upo mikononi mwa wanawake. Kwa hiyo, kupitia kwenye matendo yao na tabia zao kwa familia zao, ni sifa zinazoweza kuashiria kudumaa au kuendelea kwa taifa. Hivyo, kazi ya mama wa nyumbani ni nyeti, yenye kuhishimiwa na inayostahili kutukuzwa.

Watu wanaoshindwa kupima nguvu ya kitengo cha familia na wanaona aibu kufanya kazi hii, kwa kweli hawajui thamani na manufaa yake. Mama wa nyumbani anatakiwa kujivunia nafasi yake. Anayo nafasi ya heshima na kujitoia mhanga kwa manufaa ya jamii.

Wanawake wasomi wanayo dhamana kubwa zaidi katika kazi hii na hivyo wanatakiwa kuwa mifano kwa wengine. Wanatakiwa kuthibitisha kwa vitendo kwamba kusoma si pingamizi ya mwanamke kuwa mama wa nyumbani, lakini ni kwamba pia husaidia kuwa mama wa nyumba bora zaidi.

Mwanamke msomi anatakiwa kuongoza maisha ya familia kwa jinsi iliyo nzuri kadiri iwezekanavyo. Anatakiwa kujivunia kazi ya kuwa mama wa nyumbani na athibitishe kwamba mke msomi ni bora zaidi kwa asiye msomi.

Sio sahihi yeye kuacha kazi ya kutunza familia kwa kisingizio cha kuwa msomi. Elimu haikusudiwi kumfanya mtu aliye nayo akwepe wajibu wake, lakini lengo lake ni kumsaidia mtu atimize wajibu wake vizuri zaidi.

“Mwanaume alioa msichana aliyehitimu elimu ya sekondari ya juu, alisema mahakamani, Mke wangu hataki kufanya kazi yoyote ya nyumbani. Kila nilipolalamika alisema kwamba kazi ya kutunza familia si kazi ya mwanamke aliyesoma. Hayupo tayari kubadilika na hata ananiomba nimpe talaka na badala yake nioe mtumishi wa nyumbani! Siku mbili zilizopita niliwaalika ndugu na marafiki zake mke wangu kwa chakula cha jioni. Wakati wa chakula niliitandaza nguo ya meza na kuweka fremu ya cheti cha mke wangu cha sekondari ya juu katikati ya meza. Halafu nikamwambia kila mmoja wao aangalie kwa makini chakula cha jioni ambacho mke wangu hunitayarishia kila jioni!”

Sasa tusome maoni ya wanawake wasomi wachache kuhusu kuwa mama wa nyumba:

Bibi F.N Shamirani msomi mwenye digrii, alisema:

“Mke wa nyumbani anatakiwa kuwa stadi wa kushughulikia mambo haya, mwandani mwema wa mume wake, mama mwema kwa watoto wake na mwenyeji mwema kwa wageni.”

Mke wa Fasihi ambaye ni bingwa wa tiba ya maradhi ya watoto, alisema: “Ninaamini kwamba mama wa nyumbani halisi ni yule ambaye hafanyi kazi ofisini, kwa ssababu kazi za ofosi nchini mwetu hazina vifaa muhimu kuhusu mahitaji ya lishe na vyumba vya watoto.

Mwanamke anaye fanya kazi ofisini wakati wote anao wasi wasi kuhusu watoto wake au chakula cha mume wake.”

Mke wa S. Yakita, ambaye ni mrakibu wa Ufundi kitivo cha Tiba, alisema.: “Mama wa nyumbani anatakiwa awe na uwezo wa kutengeneza nyumba safi na inayovutia kwa kutumia bajeti za furaha na huzuni na mume wake. Asidharau hadhi ya mume wake kiakili na kijamii.”

Mke wa I. Naimi alisema: “Mama wa nyumbani ni yule anaye punguza sana burudani zisizo na umuhimu na ambaye atajaribu kuendeleza mambo ya nyumbani. Pia lazima awe na uwezo wa kulinganisha kipato na matumizi.”

Usafi

Mojawapo ya wajibu muhimu wa mama wa nyumbani ni kudumisha usafi ndani ya nyumba. Usafi ni ufunguo kwa elimusiha na afya. Huzuia maradhi mengi na huwavutia watu wa familia. Ni chanzo cha heshima kwa familia.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Dini ya Uislamu msingi wake ni usafi.”

Mtume (s.a.w) pia alisema: “Uislamu ni safi kabisa, kwa hiyo lazima ufanye jitihada kuwa safi kwa sababu ni watu walio safi tu ndio watakaoingia Peponi.”

Kila mara iweke nyumba yenu katika hali ya usafi na kupanga vizuri. Futa vumbi mara moja kila siku na ondoa madoa yote na uchafu wote kutoka kwenye kuta, milango, madirisha, fenicha na vitu vingine. Weka taka kwenye pipa la taka lenye mfuniko, liweke mbali na vyumba vingine na jiko. Takataka zikijaa kwenye pipa la taka zimwage panapostahili. Kila mara usiweke taka mbele ya nyumba yenu. Usiwaruhusu watoto wenu wakojoe kwenye bustani au ua, na wakifanya hivyo, safisha sehemu hiyo kwa maji haraka. Usilundike vyombo vichafu. Vioshe haraka iwezekanavyo. Usisahau kwamba virusi vya hatari hukua kwenye uchafu na vinaweza kuwa vya hatari kwako na familia yako. Osha vyombo kwa maji safi, na baada ya hapo viweke kwenye sehemu iliyo safi. Kusanya nguo zote chafu, hususan nepi za watoto kutoka kwenye vyumba vyote na jiko na uzifue haraka iwezekanavyo.

Weka nguo za familia zote hususan nguo za ndani, safi na nadhifu. Osha nyama na mboga za majani na mchanganyiko wote wa chakula kabla ya kupika. Osha matunda yote kabla ya kula kwa sababu baadhi yao hupuliziwa sumu ya kuua wadudu.

Nawa mikono kabla na baada ya kula na wafundishe watoto wenu kufanya hivyo. Baada ya kula chakula nawa mikono na modomo. Kama inawezekena piga mswaki meno kila baada ya mlo. Kupiga mswaki ni jambo muhimu, angalau mara moja kwa siku, ni vema zaidi kabla ya kulala.

Kata kucha zako mara moja kwa wiki. Kucha ndefu si elimusiha, kwa sababu virusi vinaweza kuishi kwenye kucha ndefu. Oga, angalau mara moja kwa wiki au kama inawezekana kila baada ya siku moja.

Lazima unyoe nywele kwenye kwapa pamoja na sehemu zingine. Nywele zilizojificha kwenye mwili ni mahali panapoweza kuishi virusi vinavyokua. Usiruhusu nzi watue kwenye chakula kwa sababu nzi ni wasafirishaji wa vijiumbe hatari vya maradhi.

Dini Tukufu ya Uislamu inapendekeza kwa kusisitiza watu waangalie usafi. Imam Sadiq (a.s) alisema:

“Mwenyezi Mungu Mweza wa yote hupenda mapambo, sura ya kuvutia na hapendezewi kuona hali ya kujifanya maskini. Hupenda kuona athari za neema zake kwa mja wake, yaani, kumuona akiwa safi, nadhifu na kutumia manukato, kuremba nyumba yake, kupangusa vumbi kwenye mazingira ya nyumba yake kuwasha taa kabla ya jua kuchwa kwa sababu kitendo hiki huondoa umasikini nyumbani na kuongeza riziki.”

Mtume (s.a.w) alisema: “Mtu mchafu ni mja mbaya (kwa Mwenyezi Mungu)”

Imamu Saiq (a.s) alisema: “Iweke nyumba yako katika hali ya usafi na kuondoa utando wa buibui kwa sababu utando wa buibui husababisha umasikini.”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Usiache uchafu ndani ya nyumba wakati wa usiku kwa sababu shetani huishi humo (yaani, kwenye uchafu na najisi).”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Nguo za mtu lazima ziwe safi kila mara.” 101

Akiongezea, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: Usiache nguo yenye mafuta ndani ya nyumba, kwa sababu shetani hufanya makazi yake hapo.”

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Kuosha vyombo na kusafisha mazingira ya nyumba huongeza riziki.”

Imam Sadiq (a.s) pia alisema: “Usiache vyombo bila kuvifunika, vinginevyo shetani huvitemea mate na kuvitumia.”

Kwa kuongezea Imam Sadiq (a.s) alisema: “Matunda hupulizwa madawa yenye sumu, kwa hiyo, yakosheni kabla ya kula.”

Imam Kazim (a.s) alisema: “Kuoga kila baada ya siku moja humnenepesha mtu.”

Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Usiache uchafu nyuma ya mlango wa mbele wa nyumba kwa sababu shetani hufanya masikani hapo.”

Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu pia alisema; Kama ingekuwa si jambo la usumbufu kwa wafuasi wangu, ningewaagiza kupiga mswaki meno yao kila wanapochukua wudhu kwa ajili ya sala (yaani mara tano kwa siku).”

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Kukata kucha kila siku ya Ijumaa huzuia maambukizi ya ukoma, kichaa na kupofuka macho.” 109 Imesimuliwa kwamba shetani hulala usingizi chini ya kucha ndefu.”

Imamu Ali (a.s) alisema: “Kunawa mikono kabla ya kuanza kula chakula, hurefusha maisha, huzuia nguo za mtu kuchafuka na kung’arisha macho ya mtu.”

Nyumba Nadhifu

Nyumba nadhifu hupendwa zaidi kuliko nyumba chafu katika njia nyingi:

Kwanza: unadhifu husaidia kuifanya nyumba ionekane safi, inavutia na mandhari ya kupendeza. Nyumba yenye mpangilio wa vitu, haimchoshi mtu, lakini itakuwa chanzo cha shangwe na furaha.

Mbili: kazi ya utunzaji wa nyumba ingekuwa rahisi kwenye familia inayofuata maagizo ipasavyo, na mama mwenye nyumba kwa kujua kwa usahihi mahali vilipo vitu vya nyumbani, haungepotezwa muda kuvitafuta. matokeo yake ni kwamba mwanamke hatachoshwa na kazi yake.

Tatu: humvutia mwanamume nyumbani kwake na mke wake. Nyumba yenye mpangilio mzuri ni mwakilishi wa sifa ya mwanamke.

Nne: nyumba nadhifu ni chanzo cha majivuno ya familia yote. Yeyote anayeitembelea, atapendezwa nayo, na kuvutiwa na ubunifu na ladha ya mwanamke.

Kuwa na vitu vya anasa si chanzo cha kuifanya nyumba kuwa nzuri, lakini ni jinsi ambavyo vitu vya ndani ya nyumba vilivyopangwa, huifanya nyumba iwe ya kuvutia. Lazima utakuwa umewaona watu matajiri ambao nyumba zao, licha ya kuwa na vitu vingi vya anasa, huchosha na wapo watu ambao ni masikini ambao nyumba zao, kwa sababu ya kuwa na mpangilio mzuri wa vitu, hufurahisha kuziangalia.

Kwa hiyo, kuipanga nyumba ni mojawapo ya wajibu wa mama wa nyumbani. Wanawake wenye vipaji na ladha nzuri wanajua namna ya kuziweka nyumba zao katika mpangilio mzuri, lakini kutaja mambo machache ni jambo linalofaa.

Ainisha vyombo vyako; usiviomekeze vyombo vyote pamoja. Weka vyombo vya kulia chakula yaani visu, vijiko, na kadhalika weka mahali pengine. Weka vyombo vinavyotumika wakati wageni wakiwepo, mahali tofauti na vyombo vinavyotumika kila siku. Fanya hivyo kwa kila kitu. Kila kitu lazima kiwekwe mahali pake hivyo kwamba watu wote wa familia wanaweza kuvipata kwa urahisi hata kwenye giza.

Baadhi ya wanawake wanaweza kuamini kwamba utaratibu wa namna hiyo ni kwa ajili ya watu matajiri. Lakini hii si sahihi hata watu masikini lazima wapange vyombo vyao pamoja na vyombo vya jikoni, vitanda, nguo na vitu vinginevyo.

Mathalani, mke lazima awe na mahali pa kuweka nguo zake tu na nguo za mume ziwekwe mahali pengine na nguo za watoto mahali pengine. Nguo za kuvaa wakati wa baridi lazima ziwekwe mahali tofauti na zile za kuvaa wakati wa joto. Nguo chafu lazima ziwekwe mahali pake. Mapambo kama vile; bangili, vidani, heleni, vibanio vya nywele na kadhalika lazima viwekwe sehemu yake. Wafundishe watoto wenu wawe nadhifu kuhusu nguo zao, vitabu vyao, wanasesere na kadhalika. Unaweza kuwa na uhakika kwamba kwa kuwa nadhifu, watoto wenu watajifunza na kuwaiga nyinyi wazazi wao.

Wanawake wachafu huwalaumu watoto wao kwa uchafu wa nyumba, ambapo watoto wanatakiwa kujifunza kutoka kwa wazazi wao.

Kama wazazi ni nadhifu, basi watoto watajifunza, na watoto kwa kawaida wapo tayari kukemewa kinidhamu.

Weka fedha yako yote, hati muhimu mapambo ya vito na vyeti mahali pa salama au mahali ambapo watoto hawafikii. Si sahihi kumwadhibu mtoto kwa sababu ya kugusa, kuharibu au kupoteza kitu chochote cha thamani ambavyo umeviweka mahali ambapo watoto wanaweza kufika. Wazazi ndio wenye hatia na wanatakiwa kutambua vema zaidi.

Mwanamume aliacha fedha na akamwambia mkewe aziweke mahali pa salama na akaziweka kwenye maungio ya shubaka na akaondoka.

Baada ya muda mfupi mwanamume akarudi na hakuzikuta fedha hizo alizoziacha. Aliangalia sehemu mbali mbali ndani ya nyumba kwa shauku lakini hakuzipata na akamuona mwanae wa umri wa miaka mitano alikuwa anachoma kitu bustanini. Mama wa mtoto huyo alimwendea kwa hasira, akamnyanyua juu, na halafu akamtupa mtoto huyo chini kwa nguvu sana hivyo kwamba mtoto huyo alikufa papo hapo. Mama aliogopa sana alipokuwa anaiangalia maiti ya mtoto wake. Mwanamke huyo alipotoka bustanini, mumewe alianza kumpiga na halafu akaamua aende polisi. Akapanda pikipiki yake lakini alipokuwa anaelekea polisi alipata ajali. Sasa yupo kwenye chumba cha wagonjwa mahututi!

Unadhani ni nani mwenye makosa kwenye tukio hili? Unaweza kuamua wewe mwenyewe. Lakini unajua tukio lingine linalofanana na hili.

Dawa, mafuta ya taa, petroli na vitu vingine vyenye asili ya sumu lazima viwekwe mahali ambapo watoto hawawezi kuvipata. Watoto hunywa na kula chochote kinachoonekana kama chakula au maji. Usihatarishe maisha yao kwa uzembe wako. Wapo watoto wengi ambao hufa kwa sababu ya uzembe wa wazazi wao.

Watoto wawili, kaka na dada, wenye umri wa miaka 6 na 4 walikunywa

D.D.T ya kuyeyushwa. Mtoto wa kike wa miaka minne alikufa na kaka yake alipona. Watoto hao walikuwa peke yao ndani ya nyumba. Walikunywa myeyuko huo kwa sababu ya kukata kiu. Mama yao watoto hao alisema hospitalini kwamba myeyuko huo ulitengenezwa kwa lengo la kuua panya ndani ya nyumba yake.”

Watoto wawili walikunywa mafuta ya taa kwa makosa wakidhani kwamba ni maji. Mtoto mwingine alimeza vidonge kumi miongoni mwa vidonge vya mama yake. Watoto hawa wote walipelekwa hospitalini kutibiwa.

Hatimaye unakumbushwa kwamba nidhamu inafaa tu hadi kiwango fulani ili isiwe sababu ya kukunyang’anya faraja. Usije ukashikwa sana na shauku kuhusu unadhifu, kwa sababu kuwa na shauku sana kwenyewe ni tatizo.

Mwanaume alisema: “Nimechoshwa na tabia ya mke wangu kushikilia usafi na unadhifu. Kila siku ninaporudi nyumbani saa 10:30 alasiri, mke wangu huniamuru ninawe mikono na miguu mara kadhaa. Anataka niweke nguo zangu mahali panapostahili. Haniruhusu nivute sigara kwenye vyumba vyote. Wakati wote nilikuwa naishi kwa uhuru, lakini wakati wa miaka minne ya ndoa, nimekuwa ninaishi jela. Kwa nini mtu ajali sana kuhusu usafi na unadhifu. Hii ni shauku iliyozidi mno, nami siipendi tabia hii.”

Tabia ya wastani ni bora sana katika vipengele vyote vya maisha ya mtu.

Mtu hatakiwi kuwa na vurumai sana hivyo kwamba inakuwa haiwezekani kuishi maisha ya kawaida, na pia si lazima mtu adekeze usafi hadi kwenye kiwango cha shauku iliyozidi mpaka.

Kutayarisha Chakula

Wajibu mwingine muhimu sana wa mama wa nyumba ni kutayarisha chakula cha familia yake. Mama mwenye nyumba mzuri, pia ni mpishi mzuri ambaye anaweza kutayarisha chakula kitamu kwa fedha kidogo, ambapo mama wa nyumba mbaya hupika chakula kibaya kwa kutumia viungo vya gharama kubwa. Chakula kitamu ni njia ya kumvutia mume wako aelekee kwako. Mwanaume ambaye mke wake hupika vizuri, hafurahii zaidi kwenda kula nje.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke bora zaidi miongoni mwa wanawake zenu ni yule anayejipuliza manukato, hutayarisha chakula kwa ustadi na hadekezi tabia ya kutumia fedha kwa israfu. Mwanamke wa aina hii ni kundi la wafanyakazi wa Mwenyezi Mungu na mtu anayefanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kamwe hatapatwa na majuto au kushindwa.”

Haiwezekani kuandika orodha ya aina za mapishi, lakini vipo vitabu vingi vizuri kuhusu somo hili ambavyo vinaweza kupatikana na kutumiwa kupika chakula kitamu.

Lakini mambo machache ya kukumbuka: Nia ya kula chakula si kujaza tumbo lakini pia kwamba hugawia mwili lishe yote inayohitajika kuendeleza kazi yake. lishe muhimu inayohitajiwa na mwili ipo kwenye nyama, matunda, mboga na nafaka na inaweza kuainishwa katika makundi sita: Maji.

Madini; kama vile kalisi/chokaa,fosforasi, chuma, shaba na kadhalika. Vitu vyenye wanga yaani kabohaidreti. Mafuta. Protini. Vitamini kama A, B, C, D, E na K.

Sehemu kubwa ya uzito wa mtu ni maji. Maji huyeyusha chakula kigumu ili kiwe tayari kufyonzwa na utumbo mdogo. Maji pia hurekebisha joto la mwili.

Madini ni muhimu kwa kukua mifupa, meno, na kurekebisha utendaji wa misuli.

Kabohairdate hutengeneza nguvu na joto.

Protini husaidia mabadiliko ya seli mpya kushika nafasi ya zilizozeeka au zilizokufa na kusababisha kukua kwa mwili.

Vitamini pia ni muhimu kwa kukuza na kuimarisha mifupa, kurekebisha majibizo ya kemikali kwenye mwili na ni muhimu kudumisha mfumo mzuri wa neva nzuri.

Kila kitu kilichotajwa hapo juu ni muhimu kwa mwili. Utapiamlo husababisha maradhi mengi na unaweza kuua. Ubora wa chakula ni muhimu na upo uhusiano wa uwiano wa urefu wa kipindi cha maisha ya mtu, furaha na huzuni, uzuri na ubaya na neva zenye afya au maradhi ya akili.

Tunaonekana tulivyo kufuatana na tulicho kula. Kama mtu anafuatilia chakula chake na kujali mazoea ya ulaji wake, hatapata maradhi mara kwa mara. Si busara kula chakula kitamu bila kutafakari ubora wake. Mara afya ya mtu inapoharibika kwa sababu ya chakula kibaya, lazima atafute daktari wa kumtibu, lakini bahati mbaya mwili wa binadamu kamwe hautarudi katika afya yake ya ya mwanzo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Tumbo ni kituo cha maradhi yote.”

Kwa kuwa chaguo la chakula ni jukumu la wanawake, kwa hiyo, wanao wajibu wa afya ya familia. Uzembe mdogo sana kwa upande wa mwanamke, utaiweka afya ya familia yote katika hali ya kushambuliwa na maradhi mengi.

Kwa hiyo, mama mwenye nyumba, pamoja na yeye kuwa mpishi mzuri, lazima awe na uwezo wa kutambua ubora wa chakula.

Kwanza: Atalazimika kutayarisha chakula ambacho kina lishe muhimu kwa mwili wa binadamu kufanya kazi inavyostahili. Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema:

Wajibu wa mwanamke kwa mume wake ni kuwasha taa ndani ya nyumba na kutayarisha chakula kizuri na kinachofaa.”

Mwanamke alimuuliza Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu: “Ni thawabu nzuri kiasi gani zinazomngoja mwanamke anayetimiza wajibu wake kwa mume wake?” Mtume (s.a.w) alisema: “Kwa kila shughuli anayoifanya ambayo inahusu mambo ya familia, Mwenyezi Mungu humtazama kwa jicho la wema, na yeyote anayefurahia neema za Mwenyezi Mungu hatateswa.”

Pili: Mahitaji ya chakula ya watu hutofautiana. Umri, saizi ya mwili na vipengele vingine hubainisha kiwango cha mahitaji yetu ya lishe. Mathalani mtoto ambaye anakua huhitaji kalisi/chokaa zaidi ikilinganishwa na mahitaji ya madini ya aina hiyo ya mtu mwenye umri wa utu mzima. Vijana wanahitaji lishe yenye kuongeza nguvu zaidi kwa sababu wana shughuli nyingi zaidi.

Kazi ya mtu pia ni kipengele kinachobainisha aina ya chakula ambacho mtu anatakiwa kula. Mathalani, anayefanya kazi ngumu anahitaji chakula cha mafuta zaidi, sukari na wanga kwa sababu anashughulika sana.

Hali ya hewa ni kipengele kingine. Mahitaji ya lishe yetu kutofautiana kufuatana na msimu wa joto na baridi. Pia mtu mgonjwa chakula chake hutofautiana na kile cha mtu mwenye afya njema. Mpishi mzuri lazima akumbuke mambo yote haya.

Tatu: Ni kweli kwamba mtu anapofika umri wa miaka arubaini na zaidi, upo uwezekano wa kunenepa. Labda baadhi ya watu huona kuwa na kitambi ni dalili ya afya njema, lakini fikra hiyo si sahihi. Kuota kitambi ni ugonjwa ambao unaweza kusababisha athari mbaya sana kwenye moyo, shinikizo la damu, mafigo, kibofu cha nyongo, ini, na huweza kusababisha maumivu kifuani na kisukari.

Takwimu kutoka kwenye vyanzo vya tiba na kampuni za bima hushauri kwamba watu wembamba huishi kwa muda mrefu kuliko wanene.

Baada ya miaka arobanini, mtu hupunguza shughuli kwa hiyo anahitaji mafuta, sukari na wanga kidogo. Kalori hazigeuzwi kuwa nishati kwa wingi kama mwanzo kwa hiyo huchangia mwili kunenepa. Kwa hiyo ni bora kupunguza kula vitu hivi.

Mwanamke anayejali afya ya mume wake anatakiwa amtengenezee lishe maalum ili asinenepe. Lazima apunguze kula vitu vitamu, vinono na, lakini azidishe kula mayai, ini nyama ya kuku, nyama isiyo na mafuta, samaki na jibini. Bidhaa za maziwa pia zinazo manufaa.

Akiruhusiwa na daktari mtu mwenye uzito mkubwa anatakiwa kula matunda na mboga kwa wingi.

Kama umechoshwa na mume wako, kama unataka kuwa mjane, au kama unataka kumuua mume wako bila hatari ya kushtakiwa na polisi - basi unatakiwa kufanya jambo dogo tu. Mpe chakula kingi kitamu na cha kunenepesha. Mhimize ale mkate, wali na keki kwa wingi iwezekanavyo. Matokeo yake utamwondoa na si tu kwamba utakuwa mjane bali atakuwa amekushukuru kwa kumlisha vyakula vyote hivi vitamu.

Unaweza kushauri kwamba utaratibu wa aina hii unaweza kutekelezwa na watu matajiri ambao wanaweza kununua aina yoyote ya chakula wanachotaka. Unaweza kufikiria haiwezekani kwa watu wasio matajiri kuweka utaratibu kama huu.

Lakini mtu asisahau kwamba manufaa yote ya lishe yamejificha kwenye vyakula rahisi vya kawaida. Mwanamke ambaye amejifunza kuhusu mapishi atakwambia kwamba mtu anaweza mahitaji yote ya lishe ya mwili kutoka kwenye vyakula kama vile matunda, nafaka, mboga na bidhaa za maziwa.

Mtu anaweza kupika mlo kwa viambato hivi ambavyo vinaafikiana na elimusiha, afya na bila gharama.

Kupokea Wageni

Mojawapo ya kazi isiyoepukika ya kila familia ni kuwafurahisha wageni wakati moja au mwingine. Hii ni mila inayofurahisha kwani matokeo yake ni kwamba urafiki huwa karibu zaidi na watu husahau matatizo yao kwa kipindi kifupi. Kuwa na marafiki na ndugu ni jambo bora sana kwa kupitisha muda.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Riziki ya mgeni huteremka kutoka mbinguni na baada ya kuliwa, dhambi za Mwenyeji husamehewa.”

Imam Raza (a.s) alisema: “Mtu mwema hula chakula alichopewa na wenzake ili na wao wale chakula chake. Lakini mtu bahili hatakula chakula alichopewa na wengine kwani wasije kula chakula chake.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) alisema: “Ushirikiano na marafiki husababisha wema (miongoni mwao).”

Imamu Muhammad Taqi (a.s) alisema: “Kushirikiana na marafiki hukomaza akili ya mtu kuchangamsha moyo wa mtu hata ni kidogo tu.”

Kwenye bahari ya maisha yenye ghasia, roho ya mtu huhitaji utulivu, na amani ya akili inaweza kupatikana mtu anapokuwa na marafiki zake.

Watu husahau matatizo yao wakati wapo kwenye mkusanyiko wa kirafiki si tu urafiki unaweza kuimarika, lakini unaweza kutia nguvu hamasa yake.

Kukirimu wageni ni desturi njema na mara chache mtu anaweza kukanusha sifa zake lakini yapo matatizo mawili humo ambayo huyafanya familia zingine kusita kushiriki kwenye mila hii ya muda mrefu.

Kwanza: Vitu vya anasa na kuonana ana kwa ana vimefanya maisha ya wengi kuwa magumu miongoni mwa wengi wetu.

Bidhaa za familia ambazo kazi yake ni kuhudumia faraja yetu zimegeuka kuwa namna ya maonesho kwa wengine na majivuno. Hivyo, watu wamepunguza nyakati za kushirikiana na wengine. Licha ya kwamba wengi ambao wapo tayari kukusanyika, hukataa kufanya hivyo, kwa sababu wanayo fikira potofu kwamba hawana vitu vingi vya anasa nyumbani kwao, kwamba ni vema wakae mbali na wengine na wajiokoe na aibu. Tafakari ya namna hii huharibu hali ya mtu baada ya maisha ya hapa duniani, pia humweka katika hali ngumu katika dunia hii.

Bibi mpendwa! Hivi marafiki zako hukutembelea nyumbani ili waone vitu vyako vya anasa? Kama ndivyo, washauri waende kwenye maduka yanayouza vitu hivyo na majumba ya makumbusho badala ya kukutembelea wewe. Kushirikiana na watu wengine inamaanisha kuongeza urafiki na watu wengine pamoja na kufurahi nao. Maana yake si kujionesha au kujaza tumbo la mtu. Kila mtu anachukizwa na uanasa na mashindano ya aina hiyo. Lakini hawathubutu kuitupa mila hii yenye makosa.

Kama ulikuwa tayari kuwakirimu wageni wako kwa jinsi iliyo rahisi, ungeona kwamba wangekufuata. Kwa njia hii unaweza kushirikiana na marafiki zako kwa urahisi na bila usumbufu mkubwa. Hivyo, ufumbuzi wa tatizo hili ni rahisi. Badala ya kujaribu kulinganisha vyombo vyako na vile vya wengine, fanya juhudi kuzidisha nguvu ya mshikamano wa urafiki na wao kwa kuwafanyia wema.

Mbili: Tatizo lingine ni kuhusu kukirimu wageni wako. Mama wa nyumbani anajisumbua kutengeneza chakula cha wageni wachache kwa muda wa saa chache. Wakati mwingine mwanamke hawezi kutayarisha chakula kitamu, ambacho kitamtibua mume baadaye. Mume wake anaweza kuonesha kutokupendezwa na mapishi yake. Kwa hiyo, karamu zingine hufuatana na wasi wasi, wa wanandoa wenyeji na matokeo yake ni kwamba watu wanakuwa na mazoea ya kutokutayarisha karamu.

Kama mambo yalivyo, ni kweli kwamba kutayarisha karamu si jambo rahisi, lakini tatizo kubwa zaidi ni kutokeza pale ambapo mama wa nyumba hana ujuzi wa kutosha kuhusu namna ya kuwakirimu wageni wake.

Kuwakirimu wageni inakuwa rahisi kama mtu yupo tayari kujifunza ustadi muhimu. Hapa ni mifano miwili inaoneshwa unaweza kutumia wowote utakaopenda wakati wa kuwakirimu wageni wako:

Mfano wa (a) mwanaume anamtaarifu mke wake kwamba Ijumaa usiku kuna marafiki zake kumi watakuja kula chakula cha jioni.

Mke wake ambaye amepata kukutana na tukio lisilopendeza kwenye karamu zilizopita, ghafla hukasirika na kumpinga mume wake. Baada ya mazungumzo ya kina na mume kumwomba mke wake, hukubali kwa kusita kutayarisha chakula usiku kwa ajili ya wageni wake. Wanapitisha siku zao katika hali fulani ya wasi wasi na shauku hadi siku ya Ijumaa.

Siku hiyo ya Ijumaa mmojawapo anakwenda kununua vitu. Anakumbuka vitu vya muhimu vya kununua na baada ya kununua vitu vichache anarudi nyumbani.

mama wa nyumbani huanza kazi yake baada ya chakula cha mchana. Ghafla anakutana na matatizo mengi. Anatakiwa apike, aoshe vyombo, afagie, afute vumbi, apange chumba cha wageni na kadhalika. Pia, anatakiwa afanye yote haya yeye mwenyewe au mtu mmoja tu wa kumsaidia. Anaanza kushughulika akiwa na wasi wasi sana.

Anatafuta kisu cha kukata vitunguu, anatafuta chumvi kila mahali na kadhalika. Anatambua kwamba hakuna hata nyanya moja hapo nyumbani kwa hiyo anamtuma mtu kwenda kununua. Lazima sasa akaange nyama, aloweke mchele, aoshe mboga… na kadhalika.

Mke anakuwa na hamaki na fadhaa na halafu anamuita mtumishi kwa kelele, anamlaani mtoto wake wa kike, anampiga mtoto wake wa kiume na halafu anaishiwa gesi au mafuta ya taa. “Ee Mungu! Nitafanyaje?”

Ghafla kengele ya mlangoni inagonga wageni wamefika! Wanafika moja baada ya mwingine. Mume ambaye anatambua wasi wasi wa mke wake, anawakaribisha wageni ndani ya nyumba na kuwapeleka kwenye chumba cha wageni. Sasa anataka kuwahudumia kwa kuwapa chai, lakini haijawa tayari. Anamwita binti yake au mtoto wake wa kiume kwa kupiga kelele akihoji kwa nini birika la chai halijawekwa kwenye jiko. Chai inapokuwa tayari, anagundua kwamba hakuna sukari ya kutosha. Baada ya kununua sukari nyingine ya nyongeza, anachukua vikombe vichache vya chai na kuwapelekea wageni. Anawatazama wageni lakini akili yake ipo jikoni. Anajua nini kinachoendelea hapo.

Hawezi kukaa kwa raha au kuzungumza na wageni kwa amani. Ana wasi wasi kuhusu chakula. Inakuwa mbaya zaidi endapo miongoni mwa wageni wapo wanawake ambao wanauliza kila mara kuhusu mama wa nyumba. Mwanaume lazima ajibu kwamba mke wake anashughulika na mapishi na baada ya muda mfupi atatokea na kuwa nao.

Mke, mara kwa mara anakwenda kwa wageni lakini hawezi kuketi na kuwa nao. Wakati anaomba msamaha kutoka kwao kwa mara ngingine anarudi jikoni. Haiwezekani mke kutayarisha chakula kitamu hasa katika hali kama hii.

Mara chakula kikiwa tayari, lazima atafute vyombo, atangeneze kinywaji, lazima atafute vyombo atenge vinywaji, atafute gilasi ajaze pilipili na chumvi kwenye vitikiso na kadhalika.

Baada ya wageni kula chakula chao hatimaye wanaaga ‘kwa heri’ kwa wenyeji wao na kuondoka.

Hitimisho: Ama chakula kilikuwa na chumvi sana au hakina chumvi, kiliungua au kuliwiva nusu. Pia baadhi ya vitu labda vilisahauliwa na mama mwenye nyumba na kwa hiyo havikuwekwa mezani ili viliwe na wageni.

Sasa ni katikati ya usiku na mke amechoka. Amekuwa hana hata dakika ya kupumzika tangu adhuhuri. Pia hakuweza kuwahudumia wageni inavyostahili.

Mume amekuwa na wasi wasi sana ametumia fedha nyingi sana kwa karamu lakini jioni hiyo haikumfurahisha inawezekana hata akamlaumu mke wake.

Wana ndoa, si tu kwamba hawakufurahia karamu, lakini inaezekana pia kwamba watakuwa na mabishano kuhusu suala hili na inawezekana hata wasitengeneze karamu tena.

Wageni hawakufurahia karamu, kwa sababu walihisi kwamba walisababisha usumbufu mkubwa kwa wenyeji wao na labda walitamani kwamba hawangekuja kabisa.

Bila shaka, wasomaji hawangependa hali kama hiyo na hawangekuwa tayari au kuwa radhi kupitia kwenye hali kama hii.

Unajua chanzo cha tatizo hili? Vema, sababu halisi, moja tu ni mke kutokuwa na uzoefu na ujuzi kuhusu jinsi ya kukirimu wageni wake.

Vingenevyo, kutayarisha karamu si kazi ngumu kiasi hicho.

Sasa chaguo la pili: Mfano (b), mwanamume anamwambia mke wake kwamba marafiki kumi miongoni mwa marafiki zao watakuja kula chakula cha usiku Ijumaa. mke anakubali kwa kusema: “Sawa kabisa, tutayarishe nini chakula cha usiku siku hiyo?”

Wanandoa hawa wanaamua kuhusu jambo hili wote pamoja na wanaorodhesha vitu vyote vya muhimu kwa maandishi. Wanaangalia kwa makini mahitaji yao kwa mara nyingine na kwa kuweka alama vile vitu ambavyo tayari wanavyo nyumbani, wanaandika orodha nyingine ya vitu vinavyotakiwa kununuliwa.

Siku ya Alhamisi, siku moja kabla ya karamu, wanamaliza baadhi ya kazi kama vile kukata vitunguu, kuosha viazi, kuweka chumvi na pilipili mahali pake, kutayarisha vyombo vya mezani na kadhalika.

Siku ifuatayo, asubuhi, mama wa nyumba baada ya kustaftahi, anafanya baadhi ya kazi zake kama kuosha, kukata na kukaanga nyama, nyama ya kuku na viazi. Baada ya chakula cha mchana anaweza kumpumzika na baadaye anamalizia kazi zilizobakia.

Kwa hiyo anaweza kumaliza kazi yote ya mapishi, kupanga nyumba ionekane nadhifu bila ya mkurupuko au wasi wasi. Kusingekuwa na mabishano yoyote au kuchanganyikiwa. Angekuwa na muda wa kutosha wa kutayarisha chai baada ya wageni kuwasili. Anaweza kuwakaribisha wageni akiwa na mume wake na hata kuketi na kuzungumza nao. Angekwenda jikoni kwa sababu ya kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama ilivyo pangwa.

Anaweza kumuomba mume wake na watoto kumsaidia kutenga chakula mezani. Kwa hiyo, kila mtu angeweza kufurahia chakula chao kitamu kwa starehe.

Hitimisho: Wageni wamefurahia fursa ya kuwa na wenyeji wao. Wamezungumza na urafiki wao umezidi kuwa imara. Wamefurahia mlo na wamevutiwa na uwezo wa mama mwenye nyumba wa kuwakirimu wao. Hatimaye, wamefurahia jioni ambayo wangeikumbuka kwa muda mrefu ujao.

Mume ameweza kushirikiana na wageni. Amekuwa na muda mzuri na marafiki zake na amefurahi mke wake hakumshusha hadhi. Wametiwa moyo wa kuendelea kuwaalika marafiki zao mara kwa mara.

Hatimaye, mwanamke ambaye kwa uvumilivu na ujuzi wake, ameweza kuwakirimu wageni kama kawaida na bila ya tatizo, ameridhika na alivyo fanya. Anahisi furaha na mume wake na amethibitisha kwamba yeye ni mama wa nyumba bora.

Sasa unaweza kuchagua kufuata mfano wowote kati ya hiyo miwili.

Mdhamini Wa Nyumba

Kwa kawaida wanaume ni wafadhili wa familia. Hufanya bidii na hutumia mapato yao kwa wake zao na watoto wao. Wanaona huu ni wajibu wao na hawako tayari kuonesha kutokupendezwa na tatizo hili. Lakini pia wanaume wanategemea wake zao kutumia fedha zao kwa uangalifu na si kwa kufuja. Wanawake wanategemewa kuainisha mahitaji muhimu na kutumia fedha zao kwa uangalifu na si kwa kufuja. Wanawake wanategemewa kuainisha mahitaji muhimu na kutumia fedha kwa ajili ya vitu kama chakula, nguo, dawa, pango la nyumba, umeme, simu, moto wa gasi na maji.

Kuweka vitu kama hivyo kama mahitaji ya anasa katika orodha ya vitu muhimu hufikiriwa kuwa ni ufujaji. Wanaume hawapendi wake zao kutumia vibaya fedha zao katika kununua vitu visivyo vya muhimu au matumizi yanayo zidi kiasi.

Kama mwanaume anamuona mke wake mwaminifu katika kutunza fedha yake, kama anao uhakika, mke wake hatumii fedha kupita kiasi na kama anao uhakika kwamba fedha yake inayo patikana kwa shida haipotei bure, kwa hiyo, atafanya bidii zaidi na hatafuja fedha zake.

Kwa upande mwingine, kama mwanamke hutumia fedha za mume wake kununua nguo zake na mapambo yake au kama mke anatumia fedha katika kununua vitu visivyo muhimu na hadi waanze kukopa ili waweze kukidhi maisha, au kama familia, kama adui kafiri, hufuja utajiri wake basi mwanaume atakata tamaa. Hatapendelea kufanya kazi na kufadhili familia yake. Atadhani hakuna mantiki ya kufanya kazi na kusaidia watu ambao hawavutiwi na juhudi zake. Anaweza hata kukengeuka na kufuata njia yenye uovu. Tabia ambayo inaweza kuvunja misingi ya familia.

Bibi Mpendwa! Licha ya kwamba fedha za mume wako zimo katika utumiaji wako, usifikirie kwamba ni zako binafsi. Utajiri huo ni wa mumeo kisheria na wewe ni mdhamana. Kwa hiyo, kuchukua kitu chochote na kukifanya chako binafsi, kutoa kitu chochote, kutoa zawadi au kuuza kitu cha mumeo chochote, unahitaji ruhusa yake. Wewe unawajibika kwa mali ya mume wako na kwa vyovyote vile unatakiwa kuilinda. Ukikwepa wajibu wako, utakuwa na hoja ya kujibu Akhera.

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke ni mlinzi na mdhamini wa mali ya mume wake na katika hali hiyo anawajibika.”

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) pia alisema: Mwanamke bora kuliko wote miongoni mwa wanawake wenu ni yule anayejipuliza manukato, hutayarisha chakula kitamu na hatavuka mpaka katika matumizi. Mwanamke wa aina hii ni mwakilishi na yu katika kundi la wafanyakazi wa Mwenyezi Mungu na mtu anayefanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kamwe hatapatwa na majuto au kushindwa.”

“Mwanamke alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): “Ni zipi haki za mume kwa mke wake?” Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mke lazima awe mtiifu kwa mumewe, asikiuke amri zake na asitoe kitu chochote bila ya ruhusa yake.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu pia alisema(s.a.w.w): “Mwanamke bora kuzidi wote baina ya wanawake zenu ni yule anayetumia fedha kwa uangalifu.”

Kazi Za Wanawake

Ni sahihi kwamba kutafuta na kupata kipato cha familia ni wajibu wa mwanaume na kwamba wanawake hawaruhusiwi na sheria ya Kiislamu kuwajibika kwa kitendo hiki. Hata hivyo, wanawake pia wanatakiwa kufanya kazi. Katika Uislamu kukaa bure ni fedheha na hukemewa.

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anachukia kulala sana na kupumzika sana.”

Imam Sadiq (a.s) pia alisema: “Kulala sana hupoteza na kuharibu maisha ya mtu hapa duniani na Akhera.”

“Hadhrat Zahra (a.s) pia alikuwa akifanya kazi nyumbani”

Mtu yeyote mwenye kuhitaji na asiye hitaji, anatakiwa kuwa na kazi. Asipoteze bure maisha yake kwa kutofanya lolote, lakini anatakiwa kufanya kazi na kutoa mchango wake katika kujenga dunia iliyo bora.

Kama ni muhimu, mtu anatakiwa kutumia kipato chake kwa ajili ya familia yake na yeye mwenyewe, lakini kama kipato hicho hakihitajiki basi atoe msaada kwa wale wanao hitaji. Kukaa bure huchosha na mara nyingi husababisha maradhi ya kiakili na kisaikolojia na pia ufisadi.

Kazi iliyo bora zaidi kwa wanawake walioolewa ni kutunza nyumba. Utunzaji wa nyumba na watoto na kadhalika ni kazi nzuri na rahisi zaidi ambazo zinaweza kufanywa na wanawake.

Mwanamke aliyeolewa mwenye kipaji na bidii kwenye kazi anaweza kuibadili nyumba yake na kuwa mahali pa Pepo kwa watoto na mume wake; na hii ni kazi inayofaa na yenye thamani.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Jihadi ya mwanamke ni hapo ambapo humwangalia na kumtunza mume wake vema.”

Umm-e-Salamah alimuuliza Mtume (s.a.w.w.w): “Ni thawabu kiasi gani zimekadiriwa kwa kazi ya nyumbani kwa mke wa mtu?” Mtume (s.a.w.w) alijibu: “ Mwanamke yeyote ambaye anaipanga nyumba ionekane nadhifu, anachukua kitu fulani kutoka mahali fulani na kukiweka mahali pengine atafurahia neema za Mwenyezi Mungu, na mtu yeyote mwenye mvuto wa neema za Mwenyezi Mungu, hatateswa na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.”

Umm-e-Salamah akasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Wazazi wangu na watolewe muhanga kwa ajili yako, tafadhali taja thawabu zingine kwa ajili ya wanawake.” Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke anapokuwa mja mzito, Mwenyezi Mungu humpa yeye thawabu nyingi kama zile ambazo angepata mtu anayepigana vita vya Jihadi kwa kutumia utajiri wake na uhai wake. Halafu mwanamke anapojifungua mtoto wake, wito humfikia na kusema, ‘dhambi zake zote zimesamehewa; anza maisha mapya tena.’ Kila anapomnyonyesha mtoto wake maziwa yake, Mwenyezi Mungu humpa thawabu sawa na zile anazompa mtu anapomwacha huru mtumwa katika kipindi anacho mnyonyesha.”

Hata hivyo, hata wanapokuwa hawashughuliki na kazi za nyumbani, wanatakiwa kutafuta kitu cha kufanya, wanaweza kusoma vitabu, kufanya utafiti wa kitu chenye manufaa, ili wajiongezee ujuzi na kustadi wao. Wanaweza kuandika makala na hata vitabu. Wanaweza kuwa wachoraji, mafundi wa kupaka rangi, ufundi cherehani na kadhalika. Matokeo yake ni kwamba wanaweza kusaidia familia zao kiuchumi na pia kutoa mchango kwa jamii yao kwa kudhihirisha mafanikio yao kwa umma.

Kufanya kazi huzuia kuendelea kuwepo kwa maradhi ya akili.

Imam Ali (a.s) alisema: “Mwenyezi Mungu humpenda mchamungu ambaye kwa uaminifu anajishughulisha na kazi.”

Wakati ambapo baadhi ya wanawake hufanya kazi nyumbani, wapo wengine ambao hupenda kazi ya nje. Upendeleo huu ama unaweza kuwa kwa sababu ya kiuchumi au zingine. Kwa vyovyote vile, kazi nzuri kuliko zote ni zile za kitamaduni au uuguzi. Shule za vidudu, msingi, sekondari na sehemu zinazofaa kwa wanwake kufundisha na kuongoza wanafunzi wanawake. Mahospitali pia ni sehemu ambazo zinafaa kwa wanawake kutoa huduma ya uuguzi na udaktari.

Kazi kama hizi zinakubalika kwa maumbile ya kike; na pia mara chache sana, inapobidi wao kukutana na wanamume ambao si mahram (wanaume ambao sio ndugu wa karibu na ambao imeharamnishwa kufunga ndoa nao).

Yafuatayo ni mapendekezo kwa wanawake wenye nia au wanaofanya kazi nje ya nyumba zao:

Pata ushauri kutoka kwa mumeo kabla ya kuanza kufanya kazi. Ni haki ya mueo kukabali au kukataa kukupa ruhusa ya kufanya kazi. Kuanza kufanya kazi bila ruhusa ya mumeo inaweza kusababisha madhara kwenye mazingira tulivu ya kupendana katika familia yenu. Wanaume pia wanashauriwa kuwa wagumu kukubali wake zao kufanya kazi nje ya nyumba zao, isipokuwa kazi husika iwe haifai kwa wanamume.

Wanawake lazima wawe waangalifu kuhusu vazi la Hijabu ya kiislamu wanapokuwa nje ya nyumba zao. Lazima waende kazini bila kujipodoa na wavae nguo zisizo na urembo. Lazima waepuke kuchanganyika na wanaume ambao si mahram kwao kadiri iwezekanavyo. Ofisi ni mahali pa kazi si mahali pa kujionesha au mashindano.

Sifa njema na heshima ni sifa zisizoletwa na kivazi chako, lakini husababishwa na matendo yako, na matendo hayo unayafanua vema kiasi gani. Matendo yako yawe kama mwanamke wa kiislamu anaye heshimika. Dumisha tabia ya kujiheshimu mwenyewe, na usiziumize hisia za mume wako; mapambo yako na nguo zako nzuri sana, vaa unapokuwa nyumbani kwa ajili ya mume wako.

Wanawake wanatakiwa kuwa na tahadhari kwamba licha ya wao kufanya kazi nje ya nyumba zao, bado wanategemewa na waume zao na watoto wao kutoa huduma za shughuli, kama utunzaji wa nyumba, kupika, kufua na kadhalika.

Shughuli hizi zinaweza kufanywa kwa ushirikiano wa kifamilia. Kazi ya nje ya nyumba isiwe sababu ya kuitibua familia yote. Wanaume pia wanashauriwa kuwasaidia wake zao kuhusu utunzaji wa nyumba. Waume wasiwategemee wake zao kufanya kazi nje na nyumbani pake yao. Matumaini ya aina hii wala si halali ama haki. Wanaume na wanawake lazima wagawane kazi za nyumbani.

Kama mwanamke, ambaye anafanya kazi nje ya nyumba anaye mtoto, basi anatakiwa amwache mtoto kwenye shule ya chekechea au mtu anayeaminika na mwema. Wala si haki au busara kuwaacha watoto nyumbani bila mtu wa kuwatunza, kwani watoto wengi huwa waoga au kujihisi hawana msaada wanapo kabiliana na hali ya hatari.

Kama mwanamke anahisi kwamba, zaidi ya kazi zilizotajwa hapo juu na wajibu uliotajwa hapo juu, lazima afanye kazi nyingine, basi ni lazima aelewane na mume wake wazi wazi na aanze kufanya kazi hiyo kwa ruhusa yake na ushauri wake. Kama mume atakataa, mke lazima aache mpango huu. Kama mume atakubali mke wake afanye kazi, lazima achague kazi ambayo itamkutanisha na wageni wanaume wachache sana. Hii ni kwa manufaa yake na jamii. Kwa vyovyote vile, anapokuwa nje ya nyumba yake, lazima awe makini kufuata kanuni za vazi la kiislamu la Hijabu na asijipodoe kabisa.

Usipoteze Muda Wako Wa Akiba

Kazi za nyumbani huwa za aina nyingi mbali mbali. Kama mke anayo nia ya kufanya kazi kwa ubora zaidi hatoweza kuwa na muda wa kutosha wa kufanya kitu kingine. Huu ni ukweli hususan ambapo pia mama wa nyumbani anatakiwa kuwatunza watoto. Lakini wanawake walio wengi ambao wameolewa hupata muda wa akiba.

Kila mtu hutumia muda wake wa akiba kwa njia moja au nyingine. Wanawake wengine hupoteza muda wao wa akiba. Wanaweza tu kutembea mtaani au anazungumza na mwanamke mwingine. Mara nyingi mazungumzo yao ya saa chache hayana thamani yoyote. Wanaweza kusikiliza maneno ya kurudia rudia ambayo huthibitisha ni ya kupoteza muda na fadhaa.

Porojo za bure kama hizo husababisha kuvunjika heshima na maadili. Wanawake wanaopitia maisha ya namna hii, hakika wanapata hasara katika dunia hii na ile ijayo. Ni ajabu ilioje kwamba kama mtu yeyote anapoteza fedha, anatibuka sana, lakini watu hawafikirii hata kidogo kuhusu kupoteza muda wao wenye thamani katika maisha yao.

Mtu mwenye busara hujitahidi sana kutumia saa zenye thamani za maisha yake kwa manufaa. Ni mafanikio ya thamani kiasi gani mtu anaweza kuwa nayo!

Uvivu una madhara na husababisha maradhi ya akili na kuchanganyikiwa. Mtu mvivu wakati wote huwa katika mawazo na hutafuta njia za kuhisi huzuni.

Hupata aina nyingi za wasi wasi na baadaye akili yake huvurugika. Mtu mwenye furaha ni yule ambaye wakati wote anashughulika kufanya kitu fulani. Mtu mwenye bahati mbaya ni yule ambaye ni mvivu sana na hutumia muda wa ziada wa kutosha kufikiri raha na taabu za maisha yake. Kujishughulisha ni jambo la kufurahisha na uzembe ni chanzo cha mfadhaiko.

Je, si jambo la kusikitisha kwamba mtu anaweza kupoteza maisha yake yenye thamani au kutumia kiasi cha muda wake bila kunufaika kwa namna yoyote?

Bibi mpendwa! Unaweza kutumia kwa manufaa makubwa muda wako wa akiba. Unaweza kufanya kazi za kisayansi. Unaweza kununua vitabu vinavyo husiana na taaluma hiyo na kwa msaada wa mume wako, utaongeza ujuzi. Masomo ya kozi yoyote inawezekana, fizikia, kemia, Qur’ani, falsafa, historia, fasihi, saikolojia na kadhalika. Ungefurahia muda huo na labda siku moja ungetoa mchango wako kwa jamii kwa ujuzi wako. Unaweza kuandika makala au hata vitabu ambapo baadaye jina lako litaendelea kudumu. Pia unaweza kujipatia fedha.

Usidhani ya kwamba wanawake wote mashuhuri katika historia wanakuwa wakizembea. Wao pia waliolewa lakini ni hao ambao hawakupoteza bure muda wao wa akiba.

Bibi Dorothy Carnegie, alikuwa ameolewa na ambaye aliandika kitabu kizuri. Alikuwa akifanya kazi za nyumbani na pia alimsaidia mume wake (Dale Carnegie) kuandika kitabu chake maarufu; “How to make friends and Infuluence People.” Ameandika kwenye kitabu chake kuhusu kanuni za kumtunza mume: “Nimeandika kitabu hiki wakati mwanangu anapolala kwa muda wa saa mbili. Nilikuwa nasoma sana wakati ambapo nywele zangu zilikuwa zinakaushwa kwenye chumba cha kutengeneza nywele.”

Wapo wanawake wengi ambao wameandika vitabu maarufu wanapata mafanikio mengi katika uwanja wa sayansi.

Kama wewe ni mtu mwenye shauku, ungekuwa mmojawao. Kama mume wako ni mtafiti basi msaidie katika taaluma yake. Je, si jambo la kusikitisha kwa mwanamke msomi kutokutumia ujuzi wake wote?

Imamu Ali (a.s) alisema: “Hakuna hazina iliyo bora zaidi ya ujuzi.”

Imamu Baqir (a.s) alisema: “Yeyote anayetumia mchana na usiku kwa kutafuta ujuzi, kwa hakika ataunganishwa na neema za Mwenyzi Mungu.”

Kama wewe hupendelei kusoma au kutafiti basi jishughulishe na kazi za mkono au uchoraji kama kushona nguo, kupaka rangi, kufuma, mapambo ya maua, na kadhalika.

Unaweza kujifunza sanaa za aina hii na kuzifanyia mazoezi. Itikadi hizi zinaweza kukusaidia kiakili na kiuchumi. Uislamu pia umependekeza kazi za mikono zifanywe na wanawake wakati wa muda wao wa akiba. “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Kusokota na kufuma ni burudani nzuri kwa wanawake.”

Umama (Utunzaji Wa Watoto)

Mojawapo ya wajibu wa wanawake ni kutunza watoto wao. Hii si kazi rahisi lakini ni nyeti na muhimu. Ni wajibu wenye heshima na thamani kubwa uliowekwa kwa wanawake kwa amri ya muumbo. Yapo mambo machache ambayo yametajwa hapa kuhusu suala hili:

Tunda la Ndoa - licha ya kwamba mwanaume na mwanamke wanaoana kwa sababu chache kama vile kwa sababu ya ushawishi wa kijinsia, mapenzi na kadhalika, kupata mtoto si sababu mojawapo muhimu ya ndoa.

Lakini huwa haipiti muda mrefu kabla ya nia ya kweli ya maumbile ya asili kudhihirika na mapenzi ya kupata mtoto hukua ndani ya nyoyo zao. Kuwepo kwa mtoto ni tunda la mti wa ndoa na matamanio ya asili ya wanaume na wanawake. Ndoa isiyokuwa na mtoto ni sawa na mti usiokuwa na tunda. Mtoto huimarisha mfungamano wa mapenzi baina ya wanandoa. Huwa kama msukumo kwa maisha ya mwanamume kufanya kazi na hutia moyo wazazi kutunza familia yao.

Wakati mwingine ndoa hutokana na matamanio ya kijinsia ya papo kwa papo. Msingi wa aina hiyo si sahihi na haudumu na kila mara huelekea kwenye uharibifu. Kipengele kinachoimarisha msingi huu ni kuwepo kwa mtoto. Matamanio na msukumo wa kijinsia hufifia haraka sana. Kumbukumbu moja tu inayoendelea kuwepo kuhusu matamanio ya kijinsia ingekuwa watoto, ambao kuwepo kwao huchangamsha nyoyo za wazazi.

Imamu Sajjad (a.s) alisema: “Furaha ya mtu ni kupata watoto wachamungu ambao anaweza kupata msaada kutoka kwao.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Mtoto mcha Mungu ni mmea unao nukia harufu tamu kutoka miongoni mwa mimea ya Peponi.”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Ijumlishe kwenye idadi ya watoto wenu, kwa sababu mimi, Siku ya Hukumu, nitahisi nimeheshimiwa kuhusu ukubwa wa idadi yenu kuzidi umma zingine.”

Ni wajinga kiasi gani wale ambao, wakiwa na udhuru mbali mbali hukataa kupata watoto, na hivyo hupinga kanuni ya uumbaji!

Kumwelimisha mtoto: Wajibat ambazo ni nyeti kuliko zote za mama ni kazi ya kumwelimisha mtoto na kuwaelekeza. Licha ya kwamba wazazi wote wawili wanatakiwa kugawana wajibu huu, uzito mkubwa zaidi upo kwa mama. Hii ni kwa sababu mama anao uwezo wa kumlinda na kumfuatilia mtoto wakati wote. Kama mama, kwa kupitia kwenye utaratibu ulio sahihi hujaribu kulea watoto wao, halafu taifa lote na hata dunia ingepita kwenye mabadiliko ya kimapinduzi.

Hivyo, maendeleo au kutokuendelea kwa jamii ni mambo ambayo yapo mikononi mwa wanawake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Pepo iko chini ya nyayo za mama.” Watoto wadogo wa leo ndio wanaume na wanawake wa kesho. Masomo yoyote wanayo jifunza sasa, watayafanyia mazoezi katika jamii zijazo. Kama familia zinaendelea, jamii itaendelea kwa sababu jamii itaendelea kwa sababu jamii ni mkusanyiko wa familia nyingi. Dunia ya kesho itaumia kwa sababu ya kuwepo watoto wenye hasira, jeuri, wajinga, woga, wapenda dunia, wabaya, wazembe, wachoyo na katili.

Kinyume chake dunia ya kesho itafaidika kwa sababu ya kuwepo leo watoto ambao ni waaminifu, wenye tabia njema, wema, jasiri, wapenda haki, wa kutegemewa na kadhalika.

Kwa hiyo, kwa ujumla, wazazi na hasa zaidi mama wanao wajibu kwa jamii zao. Wanaweza kuhudumia jamii zao kwa kulea na kukuza watoto wachamungu. Kwa upande mwingine, uzembe katika utekelezaji wa wajibu wao utahojiwa Siku ya Hukumu.

Imamu Sajjad (a.s) alisema: “Haki ya mtoto wako ni kwamba unatakiwa kutambua kwamba anatoka kwako.

Awe mzuri au mbaya anao uhusiano na wewe. Wewe unawajibika kumlea, kumsomesha na kumuonesha njia inayo elekea kwa Mwenyezi Mungu na kumsaidia awe mtiifu.

Unatakiwa kumshughulikia kwa namna ambayo kwamba ukimtendea wema, utakuwa na uhakika wa kupata thawabu na kama ukimfanyia ubaya, uwe na uhakika wa kuadhibiwa.”

Kama mambo yalivyo, si mama wote ambao wanatambua umuhimu wa stadi za kumwelekeza mtoto na ndio sababu wanatakiwa kujifunza na kuzijua stadi hizo.

Si katika eneo la kitabu hiki kuweka maelezo ya kina kuhusu malezi ya mtoto. Kwa bahati nzuri, vipo vitabu vingi ambavyo vimeandikwa na waandishi na wasomi kuhusu somo hili. Wanawake wanaweza kununua vitabu hivi na kwa msaada wa uzoefu wao wenyewe, wanaweza kuwaelimisha watoto wao na hata kuwa mabingwa katika fani ya malezi ya mtoto. Mama mmoja bingwa anaweza kuwasaidia mama wengine katika kazi zao kuhusu watoto wao.

Hapa linatakiwa kutajwa jambo moja. Watu wengi hufanya kosa kuhusu maneno mawili: ‘elimu’ na ‘maelekezo,’ au hudhani yana maana moja. Lakini mtu anatakiwa kujua kwamba kumfundisha mtoto masomo mbali mbali kama vile hadith zinazo faa, mashairi, Qur’ani, Hadith za Mtume

(s.a.w.w) na Maimamu (a.s) si kumwelimisha. Masomo kama haya yanafaa lakini mtoto si tu ajifunze kuhusu watu waaminifu, lakini yeye mwenyewe anatakiwa kuwa mwaminifu.

Hivyo, lazima tutengeneze hali ya mazingira ya maisha ambayo mtoto kwa kawaida atakuwa mtu mwaminifu na mchamungu. Kama mtoto atakuwa mtu mwaminifu na mchamungu. Kama mtoto atakuwa kwenye mazingira ya uaminifu, ukweli, ujasiri, nidhamu, usafi, wema, upendo, uhuru, haki, uvumilivu kutegemewa, utiifu na kujitoa muhanga, basi hujifunza yote hayo. Kwa upande mwingine, mtoto anayepata makuzi akiwa katika mazingira ya uovu, udanganyifu, hasira, chuki, uaminifu na uasi hataepuka kuathiriwa na mambo hayo. Mtoto kama huyu anaweza kujifunza hadith nyingi, lakini hatanufaika nazo.

Wazazi wasio waaminifu kulea na kukuza watoto waaminifu kwa kuwafundisha Qur’ani na Hadith.

Mama na baba waovu kwa kweli humfundisha mtoto wao kuwa muovu. Mtoto huzingatia zaidi matendo ya wazazi wake na si maneno yao.

Kwa hiyo, wale miongoni mwetu ambao wapo makini kulea watoto waaminifu na wema, lazima kwanza warekebishe tabia zao wenyewe. Hii ndio tu njia ya kumwelimisha mtoto anufaike yeye mwenyewe na jamii yake.

Lishe Na Afya

Wajibu mwingine muhimu wa mwanamke aliye olewa ni kuwapa chakula watoto. Afya nzuri au ugonjwa, uzuri au ubaya, hata tabia njema au mbaya na ujanja wa watoto, vyote hivi vina uhusiano na lishe wanayopewa.

Watoto wana mpangilio tofauti wa kula kulinganisha na watu wazima.

Watoto wanayo mahitaji mbali mbali katika umri tofauti na kwa hiyo mama wanatakiwa kulifikiria jambo hili wanapo wapa chakula watoto wao.

Chakula kizuri sana na chenye kurutubisha sana ni maziwa. Maziwa yana kila kitu kinachohitajiwa kwa ajili ya mwili wenye afya. Hivyo, hakuna chakula kinachomfaa mtoto mchanga isipokuwa maziwa ya mama yake. Kwa kuwa maziwa yana viambato ambavyo vinafaa kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mtoto mchanga, kwa hiyo hakuna matatizo ya kumlisha mtoto mchanga maziwa ya mama yake. Zaidi ya hayo, mama hahitaji kuchemsha, kuondoa, vijidudu au kuyasafisha kabisa maziwa hayo. Hakuna wasi wasi wa uhalisi wake.

Imamu Ali (a.s) alisema: “Hakuna chakula kizuri zaidi na kingi zaidi kuliko mazia ya mama kwa mtoto mchanga.”

Daktari A.H. Mkuu wa Eastern Maditeranean Region of World Health Organization wa zamani alisema: “Mojawapo ya kipengele muhimu ambacho husababisha mtoto apatwe na maradhi mengi ni kutokupata maziwa ya mama yake ambayo ndio tu bima ya maisha ya mtu.”

Hivyo, mama wanao nyonyesha watoto wao maziwa yao lazima wakumbuke lishe muhimu kwa watoto wao imo kwenye maziwa hayo.

Lakini maziwa yenye lishe bora ni yale tu yanayotokana na lishe bora ya mama, ubora wa maziwa yake yanahusiana na ubora na wingi wa chakula cha mama. Mama akipata chakula bora zaidi ndivyo na maziwa yake yatakavyokuwa. Mama wanao wanyonyesha watoto wao maziwa yao, kutokana na uzembe wao kuhusu lishe bora wanaweza kuharibu afya zao na zile za watoto wao.

Baba wanaolea watoto wachanga pia wanao wajibu wa kuwapa wake zao chakula cha kutosha na kilicho bora. Utapiamlo ni tatizo kubwa kwa watu wengi kuboresha na mtu hatakiwi kudharau jambo hili au vinginevyo awe tayari kulipa, kugharamia tiba ya maradhi yanayosababishwa na hali hii.

Unaweza kupata taarifa ya kutosha kuhusu somo hili kutoka kwa daktari wako wa tiba au vitabu vinavyo husiana nalo. Lakini kama sharti la ujumla mama anaye nyonyesha anatakiwa kula aina zote za vyakula kuanzia nyama, matunda, vyakula vitokanavyo na maziwa… mpaka mboga za majani.

Ukweli ulio muhimu ni kwamba maziwa ya mama huathiri tabia ya mtoto na ndio sababu Imamu Ali (a.s) alisema: “Msichague wanawake wapumbavu kunyonyesha watoto wenu maziwa yao, kwa sababu maziwa hufanya asili ya ubora wao kupenyezwa kwa mtoto.”

Imam Baqi (a.s) alisema: “Chagueni wanawake waungwana kunyonyesha watoto wenu maziwa yao, kwa sababu asili ya ubora wa maziwa unapitishwa kutoka kwa mnyonyaji hadi kwa mtoto.”

Lazima umnyonyeshe mtoto kwa vipindi. Mtoto wako hupata mazoea kutokana na ulinganifu huu na kumsaidia kuwa mvumilivu. Pia humsaidia kuhusu kuboresha mpangilio wa mmeng’enyeo wa chakula na tumbo. Kwa upande mwingine, kama utamnyonyesha mtoto kila anapolia basi, hatajifunza kuwa na nidhamu. Kama mtoto akizoea kupata atakacho kwa njia ya kulia basi ataichukua tabia hii na kuutumia hata atakapokuwa mtu mzima.

Hatakuwa na umuhimu wa kuvumilia atakapo kabiliwa na shida. Ama atatumia nguvu ili afanikishe matamanio yake au atafadhaika akipatwa na matatizo.

Usidhani kwamba kumfundisha mtoto nidhamu ni kazi ngumu. Lazima uwe mvumilivu na utaratibu unaofaa wa kumwelekeza kufuatana na kiwango chako. Wataalam wa lishe ya mtoto wanasema kwamba mtoto mchanga lazima anyonyeshwe kila baada ya saa tatu au nne.

Mpakate mtoto unapomnyonyesha. Kwa kumkumbatia mtoto anahisi mapenzi yako na inaweza kuathiri hata utu wake. Usimnyonyeshe mtoto mchanga wakati umelala chini kwa sababu imeonekana kwamba mama wengine hulala usingizi wakati wa kunyonyesha na matokeo yake watoto wengine wamekosa hewa kwa sababu matiti ya mama zao yaliwazuia kupumua.

Kama wewe mwenyewe huna maziwa kabisa unaweza kutumia maziwa ya ng’ombe ni mazito zaidi ya binadamu, pia lazima uongeze maji kiasi fulani. Pia unaweza kutumia maziwa yaliyosafishwa, ambayo lazima uyachemshe kwa muda wa dakika ishirini au hadi yanapokuwa salama kutumiwa na mtoto.

Usimnyonyeshe mtoto mchanga maziwa ya baridi au moto, lakini yanatakiwa yawe na joto sawa na yale ya binadamu.

Kila baada ya kunyonya lazima chupa na nyonyo zichemshwe kwenye maji na uangalifu wa ziada lazima ufanywe wakati wa majira ya joto. Uwe mwangalifu usitumie maziwa yaliyobakia au yaliyochacha. Ni vema kupima wingi wa maziwa katika kila kipindi cha kunyonya ili kuhakikisha kwamba mtoto wako anapata maziwa ya kutosha.

Katika kutumia maziwa ya unga unatakiwa upate ushauri kutoka kwa bingwa wa magonjwa ya watoto. Kila mara lazima utumie maziwa ya unga mapya.

Baada ya mwezi wa nne wa umri wa mtoto, unaweza kuanza kumyonyaesha maji ya matunda. Baada ya umri wa miezi sita, pia unaweza kuanza kumlisha vyakula vikavu na supu. Unaweza kumlisha bisikuti na mkate mtamu. Maziwa mtindi na jibini hufaa. Pole pole unaweza kuanza kumpa mtoto kiasi kidogo cha chakula chako.

Kumbuka kwamba mtoto wako mchanga huhisi kiu mara nyingi kama wewe. Kwa hiyo, mnyweshe maji, lakini sio chai au kahawa. Matunda, mboga na supu ni vyakula vyenye manufaa maalum kwa mtoto mchanga anayekua.

Usisahau kuwa safi kuhusu malazi ya mtoto, nguo zake na nepi zake. Mnawishe uso na mikono yake mara nyingi. Muogeshe katika vipindi vya kawaida, kwa sababu watoto wachanga ni rahisi sana kuugua kwa sababu ya uchafu na vijidudu.

Lazima watoto wapate chanjo ya kinga dhidi ya maradhi ya ndui, tetekuwanga, kifadulo, kiharusi cha watoto (polio), homa ya vipele

vyekundu, surua, dondakoo. Kwa bahati nzuri chanjo zipo zinapatikana kwenye hospitali na vituo vya afya kwa urahisi. Unaweza kuwa na watoto wenye afya njema kwa kushika kanuni za elimusiha na usafi.