Dibaji

Imepokewa kutoka katika hadithi kwamba kabla ya kurejea kwa Imam Al-Mahdi (a.s), jina lake na kutajwa kwake kutazidi katika ndimi za watu. Kama ambavyo tunaamini kwamba sasa tunaishi katika zama zenye baraka za kabla ya kurejea kwake, na kwamba ni wajibu wetu kushiriki huko ‘kuendelea kumtaja’ kama sehemu ya kuendelea kutimiza ahadi zetu tulizojiwekea katika kutoa maarifa bora ya Uislamu katika jumuia yetu hususan kwa vijana, tunakitambulisha kitabu hiki kwako, “Safari ya kuifuata nuru.” Ni kitabu cha tatu kutolewa baada ya vitabu vilivyotangulia; Tukio la Karbala” (An Emergence over Karbala) na, “Njia ya kuufikia ukamilifu” (Your Way to Perfection).

Kitabu hiki si kipya kwa maudhui yake, kwani fikra zilizotolewa humu zimo katika vitabu vingine. Hata hivyo, namna yake ya uandishi imeelekezwa kwa uangalifu kwa mtu yeyote yule anayetaka kupata habari za kweli juu ya Imam Mahdi (a.s), ni utaratibu mpya na utamfanya muda wote awe anafuatilia kuisoma kwa mazingatio.

Sayyid Abbas Noor Eddine ameweza kumuelezea Imam Mahdi (a.s) katika kurasa hizi chache katika namna ambayo ameweza kulifikia lengo lililokusudiwa na pia inaweza hata kuanzisha mwenendo mpya wa jinsi ya kuyafumbua masuala yaliyo tete kama haya.

Ni vyema ifahamike kwamba kitabu hiki kimewalenga zaidi vijana ambao wanajitahidi kuujenga utamaduni wao wa Kiislamu katika njia nyepesi kwa kadri iwezekanavyo. Hata hivyo, hii haina maana kwamba kitabu hiki kitakosa manufaa kwa wengine, na hasa hata kwa wale ambao wana maarifa makubwa juu ya mada hii muhimu.

Mwisho tungependa kumshukuru mwandishi, Sayyid Abbas Noor Eddine, mtarjumi Zaid Al-Salaami, na mtangazaji, dada Nada Haidar, kutokana na Juhudi zao kubwa mno

Pia tunawashukuru wote ambao wametusaidia katika kipindi chote ambacho kitabu hiki kilikuwa kinatayarishwa.