Du’a Al–Ahad

Imepokewa katika hadithi kwamba yeyote atakayeisoma dua hii kwa kila asubuhi zipatazo arobaini atakuwa miongoni mwa wafuasi wa Al Qa’im (a.s). Na endapo atakufa kabla ya Imam (a.s) kutokea, basi Allah (s.w.t) atamfufua toka kaburini mwake ili amsaidie Imam (a.s), na atampa kwa kila neno moja atakalolitamka thawabu elfu moja, na atamfutia madhambi elfu moja.

Yaa Allah!
Ewe Mola wa Nuru yenye kuhifadhika Milele.
Mola wa Arshi iliyo juu zaidi.

Mola wa bahari zinazokupwa na kujaa, ziendazo mbele na zirudizo nyuma kwa mstari mmoja.

Aliyeiteremsha Taurati, Injili na Zaburi.

Mola wa nyakati za Usiku kwa ajili ya mapumziko, na nyakati za Mchana wenye joto kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Aliyeiteremsha Qur’ani yenye Kupambanua.
Mola wa Malaika na Mitume na Manabii wateule.

Ee Mola! Ninakuomba Wewe, Kwa Jina lako la Ukarimu na Nuru yako iliyo Bora Mno na Ufalme Wako Unaodumu Milele.

Ee! Uliye Hai Daima! Mwenye Kujitosheleza Mwenyewe!
Ninakuomba Wewe kwa jina lako (kati ya Majina Yako), Ambalo hutoa Nuru Mbinguni na Ardhini.
Na Kwa Jina lako (Kati ya Majina Yako), Ambalo huwaongoa wa zama zote kuwa katika Njia Sahihi tangu Mwanzo hadi Mwisho.
Ee! Uliye Hai Daima Ulikuwepo kabla ya Uhai kuumbwa.
Ee! Uliye Hai Milele Utakayekuwa Hai Daima wakati maisha ya aina zote yatakapokoma.
Ee Mola! Uliye Hai Milele, Ambaye Daima Yu Hai wakati ambapo hakuna Uhai utakaokuwepo
Ee ! Ambaye Huwafufua wafu na Kuwafisha walio hai.
Ee Mola! Uliye Hai Daima! Hapana Mola Mwingine isipokuwa Wewe.

Ee Mola! Fikisha kwa Mawla (Kiongozi) wetu, Imamu aliyeongozwa katika Njia Sahihi, Baraka za Allah Ziwe Juu yake na kwa Babu zake Watoharifu, toka kwa Waumini wote wanaume na Waumini wote wanawake waishio katika sehemu za Mashariki na waishio katika sehemu za Magharibi, waishio mabondeni na waishio milimani, waishio ardhini na waishio baharini, na vile vile toka kwangu na wazazi wangu.

Baraka zil zo Tukufu kama ambavyo Arshi ya Allah ilivyo (Tukufu) na bayana kama ambavyo maneno ya Allah yalivyo ndani ya kitabu chake.

Ee Mola! Namgeukia tena yeye (Kiongozi wetu), Asubuhi ya leo hii. Siku zote nimekuwa thabiti katika kuahidi, kutoa ahadi na kulalamika kwake nikimuelekea yeye na kujitoa kwake katika kumsaidia, bila ya kupepesa macho yangu, wala kuiacha ahadi hii ipotee hivi hivi.

Ewe Mola! Nijalie niwe miongoni mwa wasaidizi wake na watumishi wake na wenye kujitolea kwake katika kukidhi haja zake, niwe miongoni mwa wenye kutekeleza amri zake na wenye kumuhami, wenye kutangulia katika atakalo na wenye kujitoa muhanga mbele yake.

Ee Mola! Endapo kifo kitakuja mapema kati yangu mimi na yeye, kwa sababu kifo ni jambo lisiloepukika kwa waja wako, nifufue nikiwa nimevaa sanda yangu na upanga wangu mkononi na nikiwa na hoja za kutosha za kumtii Allah nikiitikia wito wa Mamlaka inayoita, ikiwaita watu wote waishio karibu na waishio mbali.

Ee Mola! Unipe fursa ya kuuona uso wa Kiongozi Aliyeongozwa katika Njia Sahihi, na Mwanzo wa zama mpya inayosubiriwa, na kuiona sura ya Kiongozi mwema. Chondechonde, mfikishe sasa hivi, mfanyie wepesi Kurejea Kwake, na Umpe Nguvu zote zitakazomwezesha aweze kutekeleza Lengo Lako. Zieneze habari zake, na uuimarishe Utawala wake. Uiimarishe Dhamira yake, na Itikadi yake.

Ee Mola! Ijaze ardhi yako kwa kumleta yeye, wafufue waja wako, hakika Umesema, na maneno Yako ni kweli na sahihi. “Ubadhirifu na uharibifu waonekana ardhini na baharini kwa sababu ya uovu wa ilivyofanya mikono ya watu.

Ee Mola! Yaweke wazi kabisa kwetu Mamlaka uliyoyateua, Mwana wa Binti wa Mtume wako, aitwaye Muhammad, kutokana na jina la Mtume Wako, ili asipumzike ila baada ya kuyashinda majeshi ya waovu, mpaka awachanechane wawe vipandevipande na kuuweka ukweli na kutimiza lengo la wajibu wake katika kuweka mambo yote ya hukumu za kidini na kiroho.

Ee Mola! Mfanye awe ndiye kimbilio pekee la wanaodhulumiwa (Mustaadhafina), msaidizi wa wale ambao hawana msaidizi asiyekuwa Wewe, muhuishaji wa yale yaliyowekwa kando miongoni mwa maamrisho ya Kitabu Chako, mtiaji nguvu wa yale yaliyopatikana miongoni mwa maarifa ya dini yako na taratibu za maisha ya Mtume Wako, Baraka za Allah ziwe juu yake na Aali zake.

Ee Mola! Muweke salama dhidi ya Uadui na Maadui. Ee Mola! Mpe furaha Mtume Wako, Muhammad (saw), Baraka za Allah ziwe juu yake na Aali Zake, Kwa kumfanya mrithi wake aliye mbora kabisa afahamike, na uwafanye waitikiao wito wake wafurahi pamoja naye, na kujumuika pamo- ja katika kumtii yeye mara tu atokeapo hapa Ulimwenguni.

Ee Mola! Yakomeshe mateso ya watu wakati ambao yeye akiwa yupo, na utupeleke haraka kwenye Ufalme wake uliouahidi (Zuhur). Hakika watu wengine wanaona kuwa ni mbali mno kuja kwake lakini sisi tunaona kuwa ni karibu sana.

Kwa Baraka Zako.
Ewe Mwingi wa Rehema.
(Sasa soma Du’a ifuatayo mara tatu)**
Njoo Haraka, Njoo Haraka, Njoo Haraka, Ewe kiongozi wetu, Imam Sahibuz Zamani.

**Katika baadhi ya vitabu msomaji wa dua hii anashauriwa kupiga paja lake la kulia kwa kiganja cha mkono wa kulia mara amalizapo kusoma.

Imam Ja’afar Bin Muhammad Al Sadiq (a.s) anasema kwanza usomaji wa mara kwa mara wa dua hii humfanya mtu awe katika nafasi nzuri ya kuteuliwa kuwa mfuasi wa Imamu Sahibuz Zamaan (a.t.f.s). Ikiwa msomaji atakufa kabla ya Imam kutokea hapa ulimwenguni, Allah atamfufua ili aweze kumsaidia Imam katika kazi yake hiyo Tukufu ya ki-Mungu.