read

Kutafuta Riziki.

853. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 168:

“Amelaaniwa, amelaaniwa yule ambaye hawajali wale anaotakiwa kuwalisha ambao wanamtegemea, kwa hakika amelaaniwa kwa mara nyingi.”

854. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Man la Yahdharul Faqih, J. 4, Uk. 16:

“Mwanamme yule ambaye anafanya subira kwa hasira mbaya za mke wake, na anatafuta ile subira kwa Allah swt, basi Allah swt anamjaalia thawabu na ujira mkubwa sana kwa wale wenye kushukuru.”

855. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Amesema, Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 168 na Al-Kafi, J. 5, Uk. 88:

“Yeyote yule anayevumilia taabu za kutafuta pesa kwa ajili ya kumtimizia haja ya mke wake, ni sawa na yule anayepigana vita vya Jihadi katika njia ya Allah swt.”

856. Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s.,Manla Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 168:

“Ni dhambi moja kubwa kabisa kwa mtu ambaye anawapuuza wale wanaomtegemea yeye kwa kuwapatia riziki. (Dhambi hii kubwa inaweza kumteketeza huyo mtu).”

857. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Amesema, Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 168:

“Mtu mwenye furaha ni yule ambaye anasimamia na kuratibu maswala ya mke na watoto wake.”

Wake Kuwawia Wema Waume Zao.

858. Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura Ar-Rum, 30, Ayah ya 21.

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.

859. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipopata habari kutoka kwa Ummi Salama kuhusu Uthman ibn Mazu’un, basi aliondoka kuelekea wafuasi wake na huku akiwaambia kuwa, Bihar al-Anwaar, J. 93, Uk. 73:

“Je nyie mnajitenga na wake zenu ? Kwa hakika, mimi mwenyewe huwaendea wanawake, huwa ninakula chakula nao mchana, na kulala nao usiku. Kwa hakika yeyote yule anayejitenga na maisha ninavyoishi mimi basi hatakuwa miongoni mwangu (yaani atakayeipa mgongo).”

860. Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Man la YahdharulFaqih, J. 3, Uk. 385:

“Yeyote yule anayeikataa ndoa na kuipuuzia kwa hofu ya gharama itakayo mfikia, basi anaondoa imani yake juu ya Allah swt kwani inamaanisha kuwa yeye hamwamini Allah swt.”

861. Imeripotiwa kutoka kwa Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. kuwa, Bihar al-Anwaar, J. 103, Uk. 219:

“Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kwa kumjibu mwanamke ambaye alikuwa hataki aolewe ila abaki bila kuolewa, kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimjibu
“ usifanye hivyo, kwa sababu iwapo ndivyo ingekuwa ni kutukuka huko, basi Bi Fatimah az-Zahara a.s. angekuwa ni mwanamke wa kwanza kutokuolewa kuliko wewe (kwa sababu yeye alikuwa na wadhifa mmoja mkubwa sana akiwa ni binti wake Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.), na kwa hakika hakuna mwanamke yeyote duniani ambaye anaweza kuwa na utukufu zaidi ya Bi Fatimah az-Zahara a.s.”

862. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripotiwa kusema kuwa, Al-Kafi J. 5, Uk. 496:

Wanawake watatu walimwijia Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na kusema kuwa waume zao wamekataa kula nyama au kutumia manukato au kuwakaribia wake zao. Na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. (Akikaripia matendo yao) alikwenda haraka juu ya Mimbar na baada ya Kumhimidi Allah swt alisema: Je wamekuwaje baadhi ya watu kuwa hawataki kula nyama, na wala hawataki kutumia manukato, na wameacha kuwakaribia wake zao?.”

863. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Amesema, Al-Kafi J. 5, Uk. 494:

“Kuwa wakati mke wa Uthman ibn Mazu’un, alipomwelezea Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa bwana wake daima amekuwa akifunga saumu siku za mchana na kusali wakati wa usiku alikuwa hajali maisha yake na wala alikuwa hamjali mke wake pia, kwa kusikia hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliondoka akaenda moja kwa moja nyumbani kwake na akamkuta yuko anasali. Wakati Uthman alipomaliza sala zake, Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia: “Ewe Uthman, Allah swt hakunituma mimi kuwa Ruhbani (Kuwa kama Mapadre kwa kikirsto) bali amenituma mimi kwa ajili ya dini iliyo rahisi ambayo inalinda haki za mwili na roho. Mimi hufunga saumu, huwa nikidumisha sala, na huwa nikichanganyikana na kujumuika pamoja na familia yangu kwa ukamilifu. Na yeyote yule anayependa Sunnah yangu na mwenendo wangu basi lazima afuate mwenendo wa maisha yangu, na Sunnah yangu; Na kwa hakika ndoa ikiwa ni mojawapo ya Sunnah zangu.”