read

Usamehevu

1386. Kwa upande mmoja Uislamu unawasisitiza Waislamu kutafuta nyenzo za kujipatia mahitajio yao ya kila siku katika maisha yao kwa njia zifuatazo:

1387. Ibada ni za aina saba, na mojawapo ni kule kujitafutia mahitaji ya kila siku kwa njia zilizo halalishwa katika Dini. 1

1388. Yeyote yule aliye na maji pamoja na ardhi katika uwezo wake, na wala halimi katika ardhi hiyo, na iwapo atakumbwa na hali ya kukosa chakula cha kujilisha yeye pamoja na familia yake, basi atambue wazi kuwa huyo amekosa baraka za Allah swt. 2

1389. Moja ya matendo yaliyo bora kabisa ni kilimo kwani mkulima anajishughulisha katika kilimo na upandaji wa mazao ambayo yanawafaidisha wote bila ya kuchagua iwapo huyu ni mwema au mwovu. 3

1390. Yeyote yule asiyejitafutia mahitaji yake ya maisha basi kamwe hatakuwa na maisha ya mbeleni kwani atateketea.

1391. Na yeyote yule anayejitahidi kwa bidii kubwa kwa kujipatia mahitaji kwa ajili ya familia yake basi huyo ni sawa na yule ambaye anapigana vita vya Jihad. 4

1392. Kwa upande wa pili, Islam inaamini kuwa iwapo mtu atakuwanavyo mali na milki, kilimo na viwanda, utajiri na starehe lakini bila ya Taqwa ya Allah swt kama vile imani juu ya Allah swt na Mitume a.s, Imani juu ya siku ya Qiyama, thawabu, na adhabu na bila ya kuwa na tabia njema na kuuthamini ubinadamu kama vile msamaha, ushirikiano katika mambo mema, moyo wa utoaji, kuonea huruma n.k. basi kamwe haviwezi kumpatia maendeleo.

1393. Allah swt anatuambia katika Qur’an Tukufu Surah Al A’S’R, 103 : Ayah 1-3

‘Naapa kwa alasiri.’
‘ Hakika mwanadamu yumo hasarani !’
‘ Ila wale ambao wameamini wakatenda mema na wakausiana kwa haki na subira.’

1394. Imam Hussein a.s. amenakiliwa akisema:

“Kama kwa kweli kuna milki ya mali ya mtu humu duniani, basi hiyo ni kuwa na tabia njema. Iwapo watu wote watakufa, basi kifo jema kabisa mbele ya Allah swt ni kule kujitolea mhanga katika njia ya Allah swt.”

1395. Usamehevu upo wa aina mbili:

• Sisi tunamsamehe mtu pale tunajikuta kuwa hatuna uwezo wa kulipiza kisasi. Kwa hakika aina hii ya usamehevu unatokana na subira na kuvumilia na kamwe si kusamehe. Kwa maneno mengine, ni aina mojawapo ya kutoweza kujisaidia na udhaifu.

• Sisi tunamsamehe mtu ingawaje tunao uwezo wa kulipiza kisasi. Aina hii ya usamehevu ndio unaofundishwa na Islam pamoja viongozi wetu.

1396. Amesema Al-Imam Ali as. :

“Mtu anayestahiki kusamehe wengine ni yule ambaye ni mwenye uwezo mkuu zaidi katika kuwaadhibu wengine.”5

1397. Katika wusia wake wakati akiongea na Harith Hamdani, Al- Imam Ali a.s. alisema:

“Tuliza ghadhabu zako na kumsamehe mtu aliyekukosea wakati wewe ukiwa na uwezo au cheo chako.” 6 “Wakati wewe utakapomzidi nguvu adui yako, basi zingatia kumsamehe ikiwa ndiyo shukurani ya kupata uwezo huo.” 7

1398. Amesema al-Imam as- Sadique a.s.

“Kuwasamehe wengine wakati mtu yupo katika madaraka ni sambamba na tabia na desturi za Mitume a.s pamoja waja wema.” 8

1399. 410. Baadhi ya Ayah za Qur’an tukufu zizungumziazo maudhui haya:

Qur'an Tukufu, Sura Al- A’araf (7) Ayah ya 199,

Uchukulie kusamehe na kuamrisha mema na kujiepusha na majaheli9

Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura A’araf ( 7 ) Ayah ya 200,

‘Na iwapo wasiwasi wa Shaitani utakusumbua basi jikinge kwa Allah, Yeye ndiye Asikiaye na Ajuaye yote.’

1400. Qur'an Tukufu, Sura Aali ‘Imran ( 3 ) Ayah 134

Wale wanaotumia wakiwa katika hali nzuri na dhiki na ambao huzuia ghadhabu zao na kusamehe (makosa ya) watu ; kwani Allah huwapenda wafanyao mema.10

1401. Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura Aali ‘Imran ( 3 ) Ayah ya 159 kuwa: 11

Hivyo kutokana na Rehema itokayo kwa Allah kuwa wewe umekuwa mlaini kwao na kama ungalikuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangalikukimbia. Basi uwasamehe wewe na uwaombe msamaha na ushauriane (kwa kuwaridhisha tu ) nao katika mambo. Na unapoazimia mtegemee Allah, Hakika Allah huwapenda wamtegemeao.

Aya hii tukufu imewateremkia kuhusu wale ambao walikwenda kinyume na amri ya Mtume Muhammad sa.w.w. katika Vita vya Uhud ambapo kulisababisha Waislamu kushindwa. Watu hao walikuwa ni hamsini na wawili (52) kwa idadi ambao waliwekwa na Mtume s.a.w.w. kulinda pakuingilia huko bondeni na aliwaambia : “ Iwapo sisi tutashinda au kushindwa, nyinyi kamwe musisogee wala kuondoka hata hatua moja kutoka sehemu hii iliyo nyeti.”

Mbinu hii ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ikiwa pamoja na baraka za Allah swt na moyo wa kujitolea mhanga wa vijana wa Kiislamu wenye imani halisi, iliwafanikisha kuwashinda maadui ambao walikimbia. Wailsamu baada ya maadui kukimbia, walianza kukusanya mali iliyopatikana vitani hapo katika uwanja wa mapigano.

Mara hawa watu hamsini na wawili walipopata habari kuwa Waislamu wameshinda na wanakusanya mali iliyopatikana vitani, wote, isipokuwa kumi na wawili tu, waliacha ngome zao wazi na kukimbilia mali huku wakiwa wamevunja amri ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. iliyokuwa imewakataza wasiondoke hapo walipo katika sura yoyote ile ama iwe ya ushindi au kushindwa. Kwa kuona haya, Khalid ibn Walid, ambaye alikuwa ni kamanda wa jeshi la makafiri, alikwenda hapo bondeni akiwa na jeshi la wapanda farasi mia mbili (200 ) wakiwa wamejiandaa kwa silaha. Makafiri hao waliwashambulia kwa ghafla Waislamu kumi na wawili na kuwaua wote na wakatokezea kwa nyuma kushambulia jeshi la Waislamu. Katika mapigano haya, Mashujaa sabini ( 70 ) wa jeshi la Waislamu waliuawa, akiwemo Hamzah Sayyid ush-Shuhadaa (kiongozi wa mashahidi). Na Mas’ab ibn Umair vile vile wapiganaji wengi walijeruhiwa akiwemo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Kwa hakika kuvunja amri ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kwa hao wachache kulileta maafa makubwa kwa upande wa Waislamu. Watu walitegemea kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. atatoa amri kali kabisa dhidi ya hawa wachache; lakini sivyo na badala yake kuliteremka Ayah tukufu ikisema:

Qur'an Tukufu, Sura Aali ‘Imran ( 3 ), Ayah ya 159, kuwa:

فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ

‘…Basi uwasamehe wewe na uwaombe msamaha na ushauriane (kwa kuwaridhisha tu ) nao katika mambo….’

Kwa kuiteremsha Ayah hii, Allah swt alimwamuru Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. atoe msamaha kwa waliokuwa wamekosa.

1402. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:

“Bora ya tendo lililo mbele ya Allah swt ni kusamehe mtu ambaye amekukosea, kuwapenda ndugu na jamaa ambao wameukata uhusiano pamoja nawe, na kuwa mkarimu kwa yule ambaye aliwahi kukunyima. “ Na hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliisoma Ayah hii ya Qur’an:

1403. Qur'an Tukufu, Sura Al- A’araf (7) Ayah ya 199,

‘Uchukulie kusamehe na kuamrisha mema na kujiepusha na majaheli’ 12

1404. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika mkataba aliokuwa amemwandikia Malik-i-Ashtar, aliandika:

Zijazeni nyoyo zenu kwa huruma, uwema na kuwapenda waliochini yenu. Na kamwe musitendee kama wanyama walafi na waroho, kujifanya kama munawalea kwa kuwatenga, kwani wao wapo wa aina mbili: ama wao ni nduguzo katika imani au wapo sawa katika kuumbwa. Wao wanapotoka bila ya kujua na kasoro zinawaghalibu, wanakosea ama kwa makusudi au bila kukusudia. Kwa hivyo nawe pia uwasamehe kwa kutegemea naye Allah swt atakusamehe, kwani wewe umekuwa na uwezo dhidi yao, na Yule aliyekuchagua wewe yu juu yako, na Allah swt yupo juu ya yule aliyekuweka katika wadhifa huu.” 13

1405. Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. :

Kusikitika baada ya kutoa msamaha ni afadhali ya kufurahi baada ya kuadhibu.” 14

1406. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Hadith ‘Arbain, ananakili Marehemu Deilami:

“Siku ya Qiyama, mpiga mbiu atasimama na kusema: ‘Yeyote aliye na malipo yake kwa Allah swt basi asimame.’ Lakini hakuna watakao simama isipokuwa wale tu ambao walikuwa ni wasamehevu. Anaendelea kusema ‘Je hao hawakusikia ahadi iliyokuwa imetolewa na Allah swt :

Qur'an Tukufu,Surah Ash-Shuura ( 42 ), Ayah 40, 15

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ

‘Na malipo ya uovu mfano wa huo. Lakini anayesamehe na kusahihisha; ujira wake uko kwa Allah swt. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.’

1407. Qur'an Tukufu,Sura An-Nahl (16) Ayah 126,

وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُمْ بِهِ ۖ وَلَئِنْ صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِلصَّابِرِينَ

Na mkilipiza, basi lipizeni sawa na vile mlivyoonewa, na kama mkisubiri basi hiyo itakuwa bora kabisa kwa wafanyao subira’.

1408. Baada ya ufunuo wa Ayah hiyo, Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema : “mimi nitakuwa mwenye subira.” 16

1409. Qur'an Tukufu, Surah Fat-h (48 ) Ayah 1-2,

إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُبِينًا

لِيَغْفِرَ لَكَ اللَّهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ وَيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكَ وَيَهْدِيَكَ صِرَاطًا مُسْتَقِيمًا

‘Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri. Kwamba Allah alinde kwa ajili yako (dhidi) ya yale yaliyopita kabla ya (wafuasi wako) kasoro zako na yale yanayokuja …’ 17

1410. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliisoma Ayah ifuatayo :

Qur'an Tukufu, Surah Bani- Israil (17 ) Ayah 81,

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا

‘Na sema: ‘Ukweli umefika; na uongo umetoweka; Kwa hakika uongo ndio wenye kutoweka.’18

1411. Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimsamehe mtumwa wa Kihabeshi, Wahshi, ambaye ndiye aliyekuwa amemwua Bwana Hamza, babake mkubwa wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. . Alimsamehe wakati ambapo alikuwa na uwezo kamili wa kumwadhibu na kulipiza kisasi. Kwa hakika hii ndiyo iliyokuwa kanuni ya mtu ambaye alikuwa akiwaambia watu wote kuwa huruma ipo imefungamana katika tabia tatu:

    • Kumsamehe yule aliyekutendea yasivyo sahihi.

    • Kudumisha mshikamano wa udugu pamoja na jamaa ambaye ameuvunja uhusiano pamoja nawe.

    • Kumsamehe yule ambaye amekudhulumu au kukunyima haki yako.

1412. Qur’an tukufu inawataka Wailsamu waigize tabia na mwnenendo kama Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na ndiye awe kiigizo chao :

1413. Qur'an Tukufu, Surah Ahzab (33 ) Ayah 21,

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

Kwa hakika mnao mfano mwema kwa Mtume wa Allah, … 19

Kwa mujibu wa Ayah hiyo, iwapo sisi tutapenda kuwa Waislamu wema, basi itatubidi kuzifuata tabia na mienendo yote ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. .

1414. Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s.

“Allah swt hakubakiza chochote kile ambacho waja Wake watakihitaji hadi Siku ya Qiyama, isipokuwa vyote vipo katika kitabu kitakatifu cha Qur’an na ambayo yote yamefikishwa kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.. Yeye amewekea mipaka kwa kila kitu, na kuweka uthibitisho kwa ajili yake. Kwa wale watakaopita mipaka yake, Allah swt ameainisha adhabu za kutubu za Kidini.” 20

1415. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema :

“Tofauti baina ya Waislamu na jamii zingine ni kwamba watu wote ni sawa mbele ya Shariah za Allah swt. Islam haitofautishi baina ya tajiri na masikini, au baina ya mwenye nguvu na mnyonge. Kwa kiapo cha Allah swt ! Lau Fatima binti ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. angalikuwa amefanya uizi, basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. angalimkata mkono wake pia.” 21

 • 1. Tuhaf ul-Qaul , uk.26
 • 2. Chuo cha Wananyumba ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , j.1, uk. 13
 • 3. Safinat ul-Bihar, j. 1, uk. 549
 • 4. Chuo cha Wananyumba ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , j.1, uk. 11
 • 5. Nahjul Balaghah, uk. 266
 • 6. Nahjul Balaghah, uk. 142
 • 7. Nahjul Balaghah, uk. 103
 • 8. Safinat ul- Bahar, j.2, uk. 207
 • 9. Al-Quran, Sura ‘Aaraf, Ayah 199 - 200
 • 10. Al-Quran, Sura Ali Imran, Ayah 134
 • 11. Al-Quran, Sura Ali Imran, Ayah 159
 • 12. Al-Mizan al - ‘i’tidal, j.8, uk. 402,
 • 13. Nahjul Balaghah, uk. 94
 • 14. Safinat ul- Bahar, j.2, uk. 207
 • 15. Safinat ul- Bahar, j.2, uk. 208
 • 16. Muntahi al-A’mal, j.1, uk. 62
 • 17. Surah Fath (48 ) Ayah 1-2
 • 18. Surah Bani-Israil (17 ) Ayah 81
 • 19. Surah Ahzab (33 ) Ayah 21
 • 20. Hudud Wasail, uk.311
 • 21. Islam na Fikara za kibinadamu, uk. 670