read

Zaka

1303. Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah al –Tawbah, Ayah 35 :

يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ

Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahannam , na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, “Haya ndiyo (yale mali) mliojilimbikia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya ) yale mliyokuwa mkikusanya.

1304. Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah Ali-Imran, 3 , Ayah 180 :

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَهُمْ ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allah swt katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao. La ni vibaya kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyoyafanyia ubakhili – Siku ya Qiyamah.

1305. Imeandikwa katika Minhaj-us-Sadiqiin kuwa imeelezwa katika Hadith kuwa :

‘Yeyote yule aliyebarikiwa na Allah swt kwa mali na utajiri, lakini kwa sababu za ubakhili wake hakutoa Zaka na malipo mengine yaliyofaradhishwa kwake, basi Siku ya Qiyamah mali hiyo itatokezea kwake katika sura ya nyoka, ambaye atakuwa mwenye sumu kali kwani hatakuwa na unywele wowote juu ya kichwa chake na atakuwa na alama mbili za rangi nyeusi chini ya macho yake na hii ndiyo dalili ya kutambulisha kuwa nyoka huyo ni mkali sana na hatari kabisa. Basi nyoka huyo atajiviringisha shingoni mwa mtu huyo kama mnyororo. Katika hali ya kumsuta, nyoka huyo atasema: ‘Mimi ni mali yako ile ambayo wewe ulikuwa ukijivuna na kujifakharisha duniani.’

1306. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema katika Wasail-as Shiah, mlango 3, J.6, Uk. 11:

“Mtu yeyote ambaye hatatoa na kulipa Zaka ya mali yake basi Siku ya Qiyamah Allah swt atamwadhibu kwa miale ya mioto katika sura ya nyoka wakubwa ambao watakuwa wakinyofoa na kula nyama yake hadi hapo hisabu yake itakapokwisha.”

1307. Vile vile Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema katika Tafsir Minhaj as-Sadiqiin kuwa :

“Iwapo mtu aliye na mali na utajiri atakapoijiwa na ndugu au jamaa yake kwa ajili kuomba msaada kutokea mali na utajiri huo alionao, na yeye kwa sababu ya ubakhili wake akimnyima, basi Allah swt atamtoa nyoka mkubwa kabisa kutokea mioto ya Jahannam ambaye huizungusha ulimi wake mdomoni ili kwamba mtu huyo amwijie ili aweze kujiviringa shingoni mwake kama mnyororo mzito.”

1308. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema katika Wasa’il as-Shiah, Zakat, mlango 3, Hadith 1, J.6, Uk. 11 na Al-Kafi :

“Mtu yeyote anayemiliki dhahabu na fedha na asipotoa Zaka yake iliyofaradhishwa (au Khums, kama vile inavyoelezwa katika Tafsir al-Qummi), basi Allah swt atamfunga kifungo katika mahala pa upweke na atamwekea nyoka mkubwa kabisa ambaye atakuwa amedondosha nywele zake kwa sababu ya sumu kali aliyonayo, na wakati nyoka huyo atakapotaka kumshika basi mtu huyo atakuwa akijairbu sana kukimbia lakini atkaposhindwa hatimaye na atakapotambua kuwa hataweza kujiokoa basi atamnyooshea mikono yake mbele ya nyoka huyo. Lakini nyoka huyo atazitafuna mikono hiyo kama vile anavyotafunwa mtoto mdogo wa ngamia na atajiviringisha shingoni mwake kama mnyororo. Na hapo Allah swt anatuambia kuwa ‘Yeyote yule anayemiliki mifugo, ng’ombe na ngamia na siyetoa Zaka ya mali yake, basi Allah swt Siku ya Qiyamah atamfunga kifungo cha upweke na kila mnyama atamwuma na kila mnyama mwenye meno makali atampasua na yeyote yule ambaye hatoi Zaka kutokea mitende, mizabibu na mazao yake ya kilimo, basi huyo siku ya Qiyamah basi atafungwa shingoni mwake kwa mnyororo wenye urefu wa takriban magorofa saba.”

1309. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema katika Wasa’il as-Shiah Mlango 3, J.6, Uk.11 :

“Allah swt amefaradhisha Zaka pamoja na Sala. Ameamrisha kutekeleza Sala na kutoa Zaka hivyo iwapo mtu atasali bila ya kutoa Zaka, basi atakuwa hakukamilisha Sala.”

1310. Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Wasa’il as-Shiah, Zakat, mlango 3, Hadith 13, J.6, Uk. 11: amesema kuwa :

“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliingia katika Masjid an-Nabawi, na aliwataja watu watano kwa majina yao na akasema kuwa inukeni na mtoke humu Msikitini na wala msisali kwani nyinyi hamutoi Zaka.
(Wasiolipa Zaka wamefukuzwa kutoka Msikitini !)

1311. Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema katika Wasa’il as-Shiah, ZAKAT,mlango 3, Hadith 24, J.6, Uk 14 :

“Mtu yeyote asiyelipa Zaka ya mali yake basi yeye wakati wa mauti yake atataka kurudishwa humu duniani ili aweze kutoa na kulipa Zaka, kama vile Allah swt anatuambia: ‘Ewe Allah swt nirudishe tena ili nikafanye mema niliyokuwa nimeyaacha !’ Yaani wakati wa kifo chake atasema kuwa arudishwe humu duniani ili akaitumie mali aliyoilimbikiza katika njia njema, lakini atajibiwa kuwa kamwe haitawezekana hivyo kurudi kwake.”

1312. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameelezea tafsir ya Ayah isemayo kuwa : ‘Allah swt atawaonyesha matendo yao katika hali ya kusikitisha mno kuwa wao hawatatoka nje ya Jahannam’ kama ifuatavyo katika Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 5, J.6, Uk 21 :

“Mtu yule ambaye anakusanya na kulimbikiza mali yake na anafanya ubakhili katika kuitumia katika mambo mema na kwa kutoa zaka n.k., basi anapokufa huku amewaachia mali hiyo wale ambao watatumia mali hiyo katika utiifu wa Allah swt au kwa kutenda madhambi, basi iwapo itatumiwa katika utiifu wa Allah swt basi atakuwa mtu wa kujivuna na iwapo itatumiwa katika maasi na madhambi basi itamdhalilisha.”

1313. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 5, J.6, Uk21 :

“Hakuna kitu kinachokimaliza Islam kama Ubakhili na njia ya Ubakhili ni sawa na njia ya sisimizi ambayo haionekani na yenyewe ipo kama Shirk ambayo inayo aina nyingi.”

1314. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Safinat al-Bihar, J.1 Uk. 155 :

“Watu watakapokataa kutoa Zaka, basi baraka itakuwa imeondolewa kutoka ardhini kwa kutoa mazao na matunda kutoka mashamba yao,na madini.”

1315. Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema katika Wasa’il as-Shiah, Mlango 1, Hadith 13 :

“Muwatibu wagonjwa wenu kwa kutoa Sadaka na mutokomeze balaa, maafa kwa Du’a na muhifadhi mali zenu kwa kutoa Zaka.”

1316. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 10, J.6, Uk23 :

“Allah swt anazo mahala pengi humu ardhini ambazo huitwa ‘kilipiza kisasi’ hivyo Allah swt anapomjaalia mtu mali na utajiri, na huyo mtu haitumii kwa kutoa malipo aliyofaradhishiwa, basi huwekewa nafasi mahala hapo. Mali ambayo anakusanya kwa mbinu zake zote,inapomtoka na anaiachia wengine.”

1317. Zipo riwaya nyingi ambazo zinazumngumzia kukufurishwa kwa mtu asiyetoa Zaka kwa sababu za ubakhili wake. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema katika Wasa’il as-Shiah,mlango 4, Hadith 2, J.6, Uk 18 :

“Bila shaka Allah swt amewawekea hisa mafukara na wenye shida katika mali za matajiri ambayo imefaradhishwa. Faradhi ambayo inapotimizwa inakuwa ni yenye kuwafakharisha matajiri hao na ni kwa sababu ya kutoa huko Zaka kunakoharamisha kumwagwa damu yao na wanaolipa zaka wanaitwa Waislamu.”

1318. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, Wasa’il as-Shiah,, J.6, Uk 18 :

“Mtu yeyote yule ambaye hatatoa Zaka hata lau kwa kiasi cha Qirat (1.20 Dinar yaani punje nne za Shayiri) basi huyo si Mumin wala si Mwislamu na watu kama hawa ndivyo alivyoelezea Allah swt kuwa watakuwa wakitaka warudishwe humu duniani ili watekeleze mema.”

1319. Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameeleza katika Wasa’il as-Shiah,, J.6, Uk 18:

“Mtu yeyote yule ambaye hatatoa Zaka hata kwa kiasi cha Qirat moja (sawa na punje nne za Shayiri) basi huyo atakuwa bila imani na kufa kwa mauti ya Myahudi au Mnasara.”

1320. Amesema vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. katika Wasa’il as-Shiah, Zakat, mlango 3, Hadith 1, J.6, Uk. 19 na Kafi :

“Allah swt ameruhusu kumwagwa damu ya watu wa aina mbili ambapo hukumu hii itatekelezwa pale atakapodhihiri Al-Imam Muhammad Mahdi, Sahibuz-Zamaan, a.s. na hivyo mmoja miongoni mwa watu hao wawili ni yule anayefanya zinaa ilhali anayo mke wake hivyo atauawa kwa kupigwa mawe hadi kufa kwake na wa pili ni yule asiyetoa Zaka, huyo atakatwa kichwa.”

1321. Vile vile amesema, katika Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 8, J.6, Uk 20 :

“Mali haipotei katika majangwa na Baharini isipokuwa ile isiyolipiwa Zaka na atakapodhihiri Al-Imam Muhammad Mahdi, Sahibuz-Zamaan, a.s. basi wale wote wasiolipa Zaka watasakwa na kukamtwa na watakatwa shingo zao.”

1322. Amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Fussilat, 41, Ayah 6–8 :

ۗ وَوَيْلٌ لِلْمُشْرِكِينَ

الَّذِينَ لَا يُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ

“Ole wao wanaomshirikisha, ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Aakhera.”

1323. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , katika Al-mustadrak :

“Kwa kiapo cha Allah swt ambaye anayo roho ya Mtume Wake katika kudura yake, kuwa hakuna mtu anayemfanyia khiana Allah swt isipokuwa Mushrikina kama hawa ambao hawatoi Zaka kutoka mali zao.”

1324. Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., katika Al-Khisal, Uk. 450, Mlango Kumi :

“Ya Ali ! Katika Ummah wangu wapo makafiri wa makundi kumi :
1. Mfitini na mchonganishi

2. Mchawi

3. Dayyuth yaani mwanamme yule ambaye anajua kuwa mke wake anazini lakini hajali bali anapuuzia,

4. Mwanamme yule ambaye anauroho wa kiharamu wa kutafuta wanawake mbalimbal kwa kulawiti,

5. Anayewalawiti wanyama

6. Anayezini pamoja na wale walioharamishwa kwake yaani ambao ni mahram kwake,

7. Anayechochea na kuzidisha moto wa fitina na chuki miongoni mwa watu,

8. Anayewasaidia makafiri kihali na mali kupigana dhidi ya Waislamu,

9. Asiyetoa Zaka

10. Asiye Hijji ilhali ana uwezo kamili na kutimiza masharti yake na akifa katika hali hiyo.”

1325. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema katika kuzungumzia faida za utoaji wa Zaka, katika Kafi na Wasail, Mlango 1, Hadith 9 :

“Bila shaka Zaka imefaradhishwa kwa ajili ya kuwajaribu (mtihani) matajiri na wenye mali na kuwatimizia mahitaji ya wenye shida na kwa yakini, iwapo watu wangalikuwa wakitoa Zaka ipasavyo, basi kusingalikuwapo na Waislamu masikini na wenye shida na wala kusingalikuwa na mmoja kumtegemea mwingine na wala kusingalikuwapo na wenye kuwa na njaa au wasiokuwa na nguo. Lakini taabu na shida zote walionazo masikini ni kutokana na wenye mali na utajiri kutotimiza wajibu wao wa kutoa Zaka na Sadaka. Hivyo Allah swt humtenga mbali na neeema na baraka Zake yule ambaye hatimizi wajibu wake huo. Nami naapa kwa kiapo cha Allah swt ambaye ameumba viumbe vyote na anawapatia riziki zao, kuwa hakuna kinachopotea katika mali katika nchi kavu au majini isipokuwa ile isiyotolewa Zaka.

Faida ya tatu, Nafsi yetu inatoharishwa kwa udhalilisho wa ugonjwa sugu wa ubakhili na hivyo inatubidi sisi lazima tuutibu ugonjwa huu unaoangamiza na kutumaliza.

1326. Hivyo Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah al-Tawba, Ayah 103 :

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِمْ بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَهُمْ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Chukua Sadaka katika mali yao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Sadaka zao na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Kwa hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu, na Allah swt ndiye asikiaye na ajuaye.”

1327. Vile vile Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah al – Hashri, 59, Ayah 9:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِنْ قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَنْ يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda waliohamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa waliyopewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.”

1328. Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah al –Baqarah, Ayah 28 :

“Allah swt huongezea katika Sadaka”

1329. Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu, Surah al – Sabaa, 34, Ayah 39 :

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنْفَقْتُمْ مِنْ شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ

‘Chochote kile mtakachokitoa (katika njia yake), basi Atawalipeni (humu humu duniani) malipo yake, Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.’

1330. Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah al –Rum, 30, Ayah 39 :

وَمَا آتَيْتُمْ مِنْ رِبًا لِيَرْبُوَ فِي أَمْوَالِ النَّاسِ فَلَا يَرْبُو عِنْدَ اللَّهِ ۖ وَمَا آتَيْتُمْ مِنْ زَكَاةٍ تُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُضْعِفُونَ

‘Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Allah swt . Lakini mnachokitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Allah swt, basi hao ndio watakaozidishiwa.’

1331. Amesema Bi. Fatimah az-Zahra a.s. bintie Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika hotuba aliyoitoa kuzungumzia Fadak katika Bihar al-Anwaar, J.8, Uk 109 :

“Kwa ajili ya kujitakasa na dhambi la Shirk, Allah swt ametufaradhishia kuikamilisha imani yetu (yaani mtu yeyote anayetaka kujitakasisha na unajisi basi inambidi kuleta imani kwa moyo wake kamilifu), na Sala inamwepusha na magonjwa ya kiburi na kujifakharisha, na Zaka inamwepusha mtu kwa magonjwa ya ubahili ili mwanadamu awe mkarimu na mpenda kutoa kwa ajili ya mema ili atakasike) na hii pia ndiyo sababu kuu katika kujiongezea riziki .”

1332. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akisema katika Al-Kafi:

“Yeyote yule anayetumia kutoka mali yake katika njia ya kheri, basi Allah swt anamlipa mema humu duniani na kumwongezea katika malipo yake.”

1333. Vile vile ameripotiwa akisema Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika Wasa’il as-Shiah : Mlango Sadaka, Hadith 19, J.6, Uk. 259 :

“Tafuteni riziki yenu kwa kutoa Sadaka.”

1334. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripotiwa katika Kitab ‘Uddatud-Da’i kuwa alimwuliza mtoto wake :

“Je nyumbani kuna kiasi gani kwa ajili ya matumizi?”

Naye alimjibu :
“Zipo Dinar arobaini tu.”
Imam a.s. alimwambia
“Dinar zote hizo zigawe Sadaka.”
Kwa hayo mtoto wake alimwambia Imam a.s.
“Ewe Baba ! Mbali na Dinar hizi arobaini, hatutabakia na akiba yoyote.”
Imam a.s. alimwambia :
“Nakuambia kuwa zitoe Dinar zote Sadaka kwani ni Allah swt tu ndiye atakayetuongezea kwa hilo. Je wewe hauelwei kuwa kila kitu kina ufunguo wake ? Na ufunguo wa riziki ni Sadaka (kutolea mema ).”

Kwa hayo, mtoto wake aliyekuwa akiitwa Muhammad, alizitoa Sadaka Dinar hizo na hazikupita siku kumi, Imam a.s. alitumiwa Dinar elfu nne.

Hapo Imam a.s. alimwambia mwanae :
“Ewe Mwanangu ! Sisi tulitoa Dinar arobaini tu na Allah swt ametupa Dinar elfu nne badala yake.”

1335. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Nahjul Balagha kuwa :

“Mtu anapokuwa masikini au mwenye shida basi fanyeni biashara pamoja na Allah swt kwa kutoa Sadaka.”

1336. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema :

“Zakat-i-Fitrah inakamilisha saumu za mwezi Mtukufu wa Ramadhani.”

1337. Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah al – Tawbah, 9, Ayah 60 :

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Wa kupewa Sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allah swt , na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaradhiwa na Allah swt . Na Allah swt ni Mwenye kujua Mwenye hikima.”

1338. Vitu saba vina Zaka Sunnah :

1. Mali ya biashara au mtaji

Mali ambayo mtu anataka kuitumia katika kufanyia biashara
2. Aina za nafaka :

Mfano mchele, dengu, dengu iliyoparazwa. Lakini mbogamboga kama vile biringanya, matango, matikimaji, maboga hayana Zaka.
3. Farasi jike

4. Vito vya dhahabu na mawe

Vitu vilivyotengezwa vya kuvaa na mawe kama almasi n.k.
5. Mali iliyozikwa au kufichwa

Iwapo mtu atakuwa na mali aliyoizika au aliyoificha ambayo hawezi kuitumia basi kwa misingi ya uwezo inambidi kutoa Zaka ya mwaka mmoja.
6. Kukwepa kutoa Zaka

Iwapo mtu atauza sehemu ya mali kiasi fulani kabla ya kuisha kwa mwaka kwa misingi ya kukwepa kulipa Zaka, basi itambidi uanzapo mwaka mpya, alipie Zaka sehemu hiyo aliyokuwa ameuza kwa ajili ya kukwepa Zaka yake.
7. Mali ya kukodisha

Mtu anayepokea malipo kutokana na kukodisha majumba, maduka, mashamba, mabustani au hamaam (mabafu yanayotoza malipo kwa kutumia ).