(28). Utetezi Wa Bahlul Mahakamani

Katika mji wa Baghdad kulikuwapo na mfanyabiashara aliyekuwa mtu mwema na mwadilifu katika biashara yake. Yeye alikuwa akiagiza mali kutoka mbali na kuuza kwa bei nafuu, na kwa hayo, alikuwa maarufu na alipendwa na wakazi wa mji huo.

Vile vile kulikuwapo na mfanyabiashara mmoja Myahudi ambaye alikuwa akiuza mali yake kwa bei ghali mno na vile vile alikuwa akiendesha shughuli za kukopesha fedha kwa riba. Alikuwa akiwapa watu fedha kwa kutaka riba kubwa na alikuwa akitoa masharti magumu mno.Ikatokea kuwa yule mfanya biashara mwema na hivyo alimwendea huyo Myahudi na kumtaka deni. Kwa kuwa Myahudi alikuwa na uadui wa siku nyingi, basi alimwambia kuwa atampa kwa sharti moja nayo ni iwapo atashindwa kulipa kwa tarehe maalum basi akubali kukatwa nyama mwilini mwake kiasi cha kilo moja, sehemu yoyote ile. Kwa hayo mfanyabiashara huyo alikubali sharti hilo na hivyo akafanya mapatano hayo katika njia ya maandishi.

Ikatokea huyo mfanyabiashara akashindwa kulipa deni lake kwa tarehe ya mapatano, hivyo, Myahudi akapeleka mapatano yao kwa Hakimu kwa kupatiwa hukumu ya kutekeleza kukatwa kwa nyama. Naye alikuwa amekwisha panga kukata nyama sehemu ile ambayo itamfanya huyo mtu afe tu. Lakini Hakimu amekuwa daima akiichelewesha hiyo kesi au Myahudi akaghairi mawazo yake.

Lakini Myahudi akawa anamwendea kila siku kutaka kuharakishwa kwa hukumu. Kesi hiyo ikawa mashuhuri hapo Baghdad, na siku ya kesi ilipotolewa, watu walijazana Mahakamani kusikiliza kesi na yatakayotokea.

Siku hiyo Bahlul pia alifika kujionea. Aliweza kusikiliza kwa makini mno maneno ya pande zote mbili.

Hakimu alisoma karatasi ya mapatano na mwishoni alimwambia Mfanyabiashara:"Kwa mujibu wa waraka huu, wewe unatakiwa kumlipa Myahudi kwa mjibu wa mapatano, nyama ya sehemu yoyote ile aitakayo yeye. Sasa je unalo lolote la kusema au kujitetea?

Mfanyabiashara akasema:"Ewe Mwenyezi Mungu! Wewe ndiye uelewaye zaidi. Basi!"
Na hapo Bahlul akasema kwa sauti: "Ewe hakimu! Je inawezekana kwangu mimi kumtete binadamu mwenzangu katika kesi hii kama wakili wake?

Hakimu alimjibu: "Naam inawezekana. Hivyo tutolee dalili zako za utetezi."
Bahlul alijitosa baina ya mfanyabiashara na Myahudi na akasema: "Kwa mujibu wa mapatano haya Myahudi anayo haki ya kumkata nyama huyu bwana lakini atakapokata nyama ya huyo mfanyabiashara basi kusidondoke hata tone moja la damu na anapomkata nyama aikate kwa kipimo tu - yaani isizidi wala kupungua. Na iwapo huyo Myahudi atakiuka masharti hayo mawili basi ahukumiwe adhabu ya kifo, mali na milki yake yote itaifishwe!"

Hakimu kwa maneno ya Bahlul, alibakia kimya huku akifurahi. Na Myahudi yule ilimbidi achukue fedha alizomkopesha bila ya riba yoyote."