read

(29). Mbinu Za Bahlul.

Siku moja Bahlul alikuwa akipita njia moja na akamkuta mtu mmoja akilia, ambaye alionekana kama mgeni hapo mjini.

Bahlul alimwuliza: "Ewe ndugu! Je kitu gani kilichokusibu kiasi cha kukufanya uanze kulia hivi?"

Yule mtu akamjibu: "Mimi ni mgeni mjini humu. Nilifika ili nikae siku chache. Mimi nilikuwa na fedha na vitu vya thamani ambavyo kwa khofu ya waizi niliviwekesha kama amana kwa mwuza mafuta ya manukato ambaye nilipomwendea baadaye anirejeshee, alisema ati mimi ni mwehu na hivyo akafanikiwa katika kunigeuka.

Bahlul aliwambia: "Usihuzunike! Mimi nitahakikisha kuwa huyo Atar (mwuza mafuta ya manukato) atakurudishia amana yako kwa wepesi kabisa."

Akamwuliza ni Atar yupi, na baada ya kumfahamu, alisema: "Kesho saa fulani nitakusubiri dukani mwake na usinisemeshe kama kwamba haunijui. Na utawaambia kuwa nirudishie amana yangu!" Mtu huyo akakubali.

Hapo moja kwa moja, Bahlul alimwendea yule Atar na kumwambia: "Mimi nimepata safari ya ghafla ya kwenda khurasan na ninavyo vito na dhahabu vya thamani ya Ashrafi elfu thelathini ambazo ninataka kukuwekesha amana. Iwapo nitarudi salama basi nitachukua mali yangu na iwapo nitakuwa sikurudi hadi siku fulani fulani basi wewe utakuwa msimamizi wa mali hiyo na utaiuza na kujenga msikiti mmoja kwa fedha zake."

Atar alifurahishwa mno kwa hayo na akasema: "Usiwe na shaka! Je hiyo amana utaileta lini?"

Bahlul alimjibu: "Kesho saa fulani. "Na akaondoka zake. Na alishona mfuko mmoja wa ngozi na humo akaweka lakiri yake. Ulipofika wakati waliopeana Bahlul akatokezea na mfuko wake huo, wakati wanazungumza na Bahlul, akatokezea yule mgeni akamwambia mwenye duka "Ewe Bwana! Naomba amana yangu niliyokuachia."

Kwa kuwa mwenye duka, alikuwa na tamaa kubwa ya kifurushi cha Bahlul na ili kuonyesha uaminifu wake, alimwamuru mfanyakazi wake akamletee mfuko wa mgeni huyo.

Mgeni huyo alipoona kuwa amerudishiwa mfuko wake bila ya hata neno moja, alimshukuru Bahlul na kumwombea dua njema.
Akaondoka mjini.