Dibaji

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

Amesema Mwenyeezi Mungu (swt): "Niombeni nitawaitikia" (40:60).Mtume (saww) naye amesema: "Dua ni silaha ya muumin."

Kwa hakika dua ni miongoni mwa ibada, kwani ni utambulisho wa mja kumuhitajia Mola wake. Kuna Aya na Hadithi nyingi sana zinazohimiza kusoma dua. Kwa hiyo dua inatakikana wakati wowote; sio wakati wa shida tu. Ndio maana Mtume (saww) akasema: "Jijulishe kwa Mwenyeezi Mungu wakati wa raha, atakujua wakati wa shida"

Dua Kumayl ni maarufu sana. Ni dua ya Khidhr (a.s.) ambayo Imam Ali (a.s.) alimfundisha, Kumayl bin Ziyad ambaye alikuwa ni miongoni mwa sahaba zake. Ndio maana ikapata jina lake.

Imependekezwa sana kusomwa kila usiku wa kuamkia Ijumaa na usiku wa kuamkia nusu ya Mwezi Sha'abani au kwa mwezi mara moja au angalau mara moja katika maisha. Ni dua ya kuomba kufunguliwa mlango wa riziki, kughufiriwa dhambi nk.

Tunamshukuru sana ndugu yetu, Sayyid Ahmad Aqil, kwa kazi kubwa aliyoifanya kuitarjumu dua hii. Nasema kazi kubwa, kwa sababu dua ni kuzungumza na Mwenyeezi Mungu, huku ukimsihi akupe kila unachokiomba. Lugha yake, inahitajia unyenyekevu na usanifu wa hali ya juu sana; na kuihamisha lugha hiyo pamoja na usanifu wake nako kunahitajia usanifu.

Ndugu yetu Ahmad amejitahidi sana katika hili, kiasi ambacho nimemuomba aendelee na kazi hiyo katika dua nyingine Kwani dua hasanikujua kile unachokisema na unachokiomba. Bila shaka kazi hiyo itawasaidia sana wale wasiojua kusoma lugha ya kiarabu.

Na tawfiki ni ya Mwenyeezi Mungu

Hassan Ali Mwalupa