read

Dibaji

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu.

Matatizo Ya Mahusiano Ya Kifamilia.

Tatizo la mahusiano ya kifamilia katika zama zetu sio rahisi sana kiasi kwamba mtu anaweza kulitatua kwa kuandaaa kura za maoni ya vijana wa kike na wa kiume, au kwa kuendesha semina. Sio tatizo la nchi wala hakuna nchi iliyodai kulitatua kabisa.

Will Durant, mwanafalsafa anayejulikana vyema, na mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘History of Civilization’ anasema, “Tukijaalia kuwa tunaishi katika mwaka wa 2000 A.D na tunataka kujua tukio lililokuwa muhimu kabisa katika robo ya kwanza ya karne ya 20, tutaona kuwa haikuwa vita ya kwanza ya Dunia wala Mapinduzi ya Urusi. Lilikuwa ni badiliko la nafasi ya mwanamke. Historia haikuwahi kushuhudia badiliko la kusisimua kiasi hicho ndani ya muda mfupi kiasi hicho. Nyumbani, ambapo ndio ulikuwa msingi wa kiuendeshaji wetu wa kijamii, mfumo wa unyumba (ndoa), ambao ulizuia ufisadi na zinaa na kuleta utengamano wa maisha ya familia, na sheria madhubuti ya maadili iliyotusaidia kuondoka katika ushenzi kwenda katika utamaduni na tabia inayokubalika ya kijamii, yote haya yalisukumiziwa mbali na badiliko hili la kimapinduzi.”

Hata sasa tunapoishi katika karne ya 21, tunasikia malalamiko mengi kuliko kipindi kingine chochote kuwa mfumo wa familia unaporomka, msingi wa ndoa unadhoofika, wavulana wanakwepa kuoa, wasichana wanachukia kuzaa (kuwa mama), mahusiano baina ya wazazi hasa akina mama na watoto yanazidi kuwa mabaya, mwanamke wa dunia ya leo hana adabu, ngono ya bei nafuu inachukua nafasi ya mapenzi ya dhati, talaka zimeongezeka, idadi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa inaongezeka, mapenzi ya dhati, heshima na uchangamfu kati ya mume na mke vinazidi kupungua.

Je Tuige Wazungu Au Tujitegemee?

Inasikitisha kuona kuwa baadhi ya watu wasioelewa mambo wanafikiria kuwa suala la mahusiano ya kifamilia ni sawa na matatizo ya kuongoza watalii, kuendesha taksi, kuendesha basi na kuunganisha mtandao wa mabomba ya maji na umeme, mambo yaliyotatuliwa na wazungu miaka mingi iliyopita na hivyo tukipatwa na tatizo lolote tuwaige wao mara moja.

Hizi ni njozi tu. Wazungu wana matatizo makubwa sana ya kifamilia kuliko sisi. Wanataabika sana na wasomi wao ni waropokaji. Ukiacha elimu kwa wasichana, wana matatizo makubwa katika masuala mengine. Familia zao zina huzuni kubwa kuliko zetu.

Kulazimishwa Na Historia

Baadhi ya watu wanafikiri kuwa kuporomoka na kuchafuka kwa mfumo wa familia kunatokana na ukombozi wa wanawake, ambao kwa upande mwingine ulikuwa ni matokeo yasiyoepukika ya mapinduzi ya viwanda na maendeleo ya sayansi na ustaarabu. Ni suala la kulazimishwa na historia. Hatuna njia ya kufanya isipokuwa kukubaliana na ufisadi na vurugu hizi, na kusahau furaha ya maisha ya familia tuliyokuwa tukiyafurahia huko nyuma.

Kufikiri kwa staili hii ni kwa juu juu na kwa kitoto. Tunakubali kwamba maisha ya viwanda yameathiri mahusiano ya kifamilia na bado yanaathiri, lakini mambo makuu yaliyoathiri mfumo wa maisha ya familia huko Ulaya, ni mawili:

La kwanza ni mila katili na za kipumbavu, mazoea na sheria zilizokuwepo Ulaya hadi karne iliyopita. Ilikuwa ni mwishoni tu mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 ambapo wanawake wa Ulaya walipata haki ya kumiliki mali. Jambo jingine lililochangia ni kuwa, wale waliojitolea kurekebisha hali za wanawake walichagua njia potofu. Walikusudia kuziremba nyusi zake za macho lakini walimnyima uwezo wa kuona.

Mbali na maisha ya viwanda, sheria za zamani za Ulaya na mageuzi ya watu wa kisasa (modernists) yamechangia katika vurugu na mkanganyiko uliopo. Hivyo hakuna sababu inayotulazimisha sisi Waislamu kupita njia waliyopita na kuangukia katika utata na ugumu huu ambao wenzetu wameangukia. Tunapaswa kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari na maisha ya kimagharibi.

Tunapaswa kuyatazama maisha ya Magharibi kwa tahadhari. Huku tukitumia na kupata maarifa yao, viwanda vyao, mbinu zao na baadhi ya kanuni za kijamii zinazofaa kuigwa. Tunapaswa kujiepusha kuiga mila zao, mazoea (desturi) na sheria ambazo zimewaletea masaibu makubwa. Kwa mfano kurekebisha sheria za kiraia na mahusianao ya kifamilia ili ziafikiane na sheria za kimagharibi.