read

Tofauti Kati Ya Mwanamke Na Mwanaume.

Hii inaonekana kuwa sentensi isiyofaa. Inaonekana kuwa japo tupo katika karne hii, bado kuna baadhi ya watu, hapa na pale, ambao wana mawazo ya kizamani, na bado wanang’ang’ania wazo lililopitwa na wakati la tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kama watu wa zama za kati (1500 A.D), watu hawa bado wanamuona mwanamke kuwa wa jinsia ya cheo cha chini na kwamba sio mwanadamu kamili na kamilifu. Yupo katikati si binaadamu wala si mnyama. Hafai kuishi maisha ya kujitegemea na lazima aishi chini ya uangalizi na udhibiti wa wanaume.

Lakini sasa tunajua kuwa mawazo yote haya yamepitwa na wakati na hayafai. Leo hii tunajua fika kuwa dai potofu la kudaiwa kuwa mwanamke sio mkamilifu lilizushwa na mwanaume katika enzi zile ambazo alikuwa anamtawala mwanamke. Sasa, habari iliyothibitishwa ni kwamba mwanamke anatokana na jinsia bora zaidi na mwanaume anatokana na jinsia duni.

Haya ni maoni ya baadhi ya Wamagharibi wa kisasa. Kwa ukweli kabisa, maendeleo ya sayansi ya karne ya 20 yamethibitisha wazi wazi kuwepo kwa tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kuwepo kwao sio uwasilishaji mbaya wa kijicho, bali ni ukweli wa kisayansi, uliotokana na uchunguzi na majaribio. Hata hivyo tofauti hizi hazipo ili kuthibitisha ni jinsia gani ni bora kuliko nyingine. Sheria ya maumbile imeziweka tofauti hizi ili mahusiano ya ndoa yawe imara zaidi na kuufanya msingi wa muungano kati ya mume na mke uwe mkubwa, imara na bora zaidi.

Maumbile yalitaka kugawa haki za kifamilia na majukumu yake baina yao kwa mikono yake (maumbile) yenyewe. Sheria ya maumbile umezifanya tofauti kati ya mwanaume na mwanamke sawa na tofauti ya viungo mbali mbali vya mwili. Imetoa nafasi mbali mbali kwa macho, masikio, mikono, nyayo na uti wa mgongo. Lakini haimaanishi kuwa imefanya dhulma na ubaguzi dhidi ya kiungo chochote.

Je Ni Uwiano Au Ukamilifu Na Kutokamilika?

Inashangaza kwamba baadhi ya watu wanasisitiza kuwa tofauti katika nguvu za kimwili na kisaikolojia za mwanaume na mwanamke hutokana na ukamilifu wa mwanaume na kutokamilika kwa mwanamke. Wanashikilia kuwa, kwa sababu fulani nzuri, kwa makusudi kabisa mwanamke ameumbwa akiwa sio mkamilifu.

Dhana ya kutokuwa mkamilifu kwa mwanamke imekuwa maarufu zaidi katika nchi za Magharibi kuliko Asia. Watu wa Magharibi wamemuonea. Wakati fulani wamekuwa wakitoa tafsiri mbaya ya maandiko ya kidini juu ya mwanamke, wanasema kwamba mwanamke ajione haya. Wakati fulani wanasema, ‘Mwanamke ni kiumbe mwenye nywele ndefu na ubongo usiofaa,’ ‘mwanamke ni nusu ya mnyama na nusu ya mtu’n.k.

Bado inashangaza zaidi kuona kwamba baadhi ya watu wa Magharibi wamebadilisha mwelekeo wao kwa nyuzi 180, hivi karibuni wameanza kuleta hoja elfu na moja kuthibitisha kwamba kwa mujibu wa maumbile, mwanaume ni duni na sio mkamilifu na kwamba jinsia ya mwanamke ni bora na mkamilifu.

Kama umeshakisoma kitabu, “Woman, the Superior Sex,’ cha Ashley Montague, unaweza kuona ni jinsi gani mwandishi huyu, kwa kupotosha ukweli na kuleta hoja zisikubaliana na ukweli alivyojaribu kuthibitisha kuwa mwanamke ni mkamilifu zaidi kuliko mwanaume. Katika fani za utabibu, saikolojia na takwimu za jamii kitabu hiki kinafaa sana, lakini pale mwandishi anapojaribu kutoa hitimisho lake kuthibitisha dai lake, ambalo ndio jina la kitabu anakwenda kwenye upuuzi mkubwa kabisa.

Haifahamiki kwa nini ni lazima kwa watu wa Magharibi kwamba siku moja wamuumbue mwanamke na kumuadhiri ili siku ya pili warekebishe yale ya nyuma, wanalazimika kumuondolea mapungufu na udhaifu waliokuwa wamembandikia na badala yake wanambandikia hayo mwanaume. Kuna umuhimu gani wa kuangalia tofauti kati ya mwanaume na mwanamke kwa matokeo ya ukamilifu wa jinsia mmoja na upungufu wa jinsia nyingine, ili kwamba wakati mwingine tulazimike kumuweka mwanaume upande na wakati mwingine mwanamke?

Mwandishi wa kitabu hiki anasisitiza kuwa mwanamke ni bora kuliko mwanaume na anaona kuwa utukufu alionao (mwanaume) ni matokeo ya sababu za kihistoria na kijamii na sio matokeo ya sababu za asili.

Kwa kusema kweli, tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ni suala la uwiano sio ukamilifu na kutokamilika. Sheria ya maumbile imeamua kuwa kwa kuwa mwanaume na mwanamke wameumbwa ili waishi pamoja, lazima wawe na uwiano mahususi wa vipaji vyao licha ya tofauti hizi. Nukta hii itafafanuliwa baadaye.

Nadharia Ya Plato.

Suala la tofauti kati ya mwanamke na mwanaume sio jipya ambalo tunaweza kusema kuwa limeibuka katika zama zetu. Lina umri wa miaka zaidi ya 2400. Lilijadiliwa katika sura yake ya sasa, na Plato katika kitabu chake ‘The Republic’.

Kwa uwazi anaelezea kwamba wanaume na wanawake wana vipaji sawa, na wanawake wanaweza kufanya kazi za kiume na kupata haki kama zile za wanaume.

Chanzo cha mawazo yote kuhusu mwanamke, ambayo yameibuka katika karne ya 20, na hata sehemu ya mawazo haya yanayoonekana kuwa ya ovyo na yasiyobadilika kwa watu wa karne ya 20, yamo katika mitazamo ya Plato. Hii ndio sababu watu wanavutiwa naye sana na kumuita ‘Baba wa Falsafa’.

Plato katika sura ya tano ya kitabu chake, ‘The Republic’ alizungumzia masuala kama vile ukomunisti wa wanawake na watoto, kuboresha kizazi (breed), kuwa hasi baadhi ya wanaume na wanawake, kuwaruhusu kuzaa wale tu wenye sifa zilizotukuka za kijenetiki, kulea watoto nje ya mazingira ya kifamilia na kuruhusu kuzaa katika miaka fulani tu ya uhai, katika kipindi ambacho nguvu (za uzazi) zipo kileleleni. Plato anaamini kuwa kama ilivyo kwa mwanaume, mwanamke anapaswa kupewa mafunzo ya kijeshi na kama mwanaume anavyoshiriki katika riadha, mwanamke ashiriki pia.

Hata hivyo, kuna mambo mawili ambayo Plato ameyasema. Moja ni kuwa anakiri kuwa kimwili na kiakili wanawake ni dhaifu kuliko wanaume. Kwa maneno mengine anaiona tofauti kati ya mwanaume na mwanamke kuwa ni ya kiasi (ukubwa), sio sifa (ubora) wa vipaji vyao. Anaamini kuwa wote mwanaume na mwanamke wana vipaji. Kitu pekee ni kuwa katika baadhi ya mambo mwanamke ni dhaifu kuliko mwanaume, lakini haoni sababu kwa nini awe na mfumo wa kipekee wa kuendesha mambo.

Kwa vile Plato anamuona mwanamke kuwa dhaifu kuliko mwanaume, anamshukuru Mungu kuwa alizaliwa mwanaume. Anasema; “Namshukuru Mungu kwa kuzaliwa kwangu Mgiriki (myunani) na sio vinginevyo, kwa kuzaliwa kwangu nikiwa huru na sio mtumwa na kuzaliwa kwangu mwanume na sio mwanamke.”

Nukta ya pili ni kuwa yote aliyoyasema Plato ya kuhusu kuboresha ukoo (uzazi), vipaji vya jinsia zote mbili na ukomunisti wa mwanamke na watoto yanahusiana na tabaka tawala, yaani wanafalsafa watawala, kwa sababu kwa mujibu wake, ni tabaka hili tu ndio linafaa kuwa watawala. Kama tunavyojua kisiasa, Plato alikuwa ni mpinga demokrasia na alikuwa akitetea utawala wa matabaka. Hivyo, alichokisema katika nukta hizo, kinahusiana na tabaka tawala. Kuhusiana na matabaka mengine, ana maoni tofauti.

Aristole Dhidi Ya Plato.

Mwanafunzi wa Plato, Aristole ni mwanafikra mwingine wa ulimwengu wa kale, ambaye maoni na mawazo yake tunayo. Ametoa maoni juu ya tofauti kati ya mwanamke na mwanaume na ameyapinga vikali maoni ya mwalimu wake. Anaamini kuwa mwanaume na mwanamke wanatofautiana sio kwa kiasi tu bali hata kwa sifa. Anasema kwamba jinsia hizi mbili zina vipaji vya aina tofauti na majukumu waliyopewa na sheria ya maumbile na haki walizopewa, vyote vinatofautiana sana.

Kwa mujibu wa Aristole, kanuni zao za maadili pia zinatofautiana katika mambo mengi. Inawezekana kuwa sifa ya maadili ikawa bora kwa mwanaume lakini isiwe hivyo kwa mwanamke na kinyume chake. Katika ulimwengu wa kale maoni ya Plato yaliondolewa, yakachukuliwa ya Aristole. Wasomi waliofuatia walipendelea maoni ya Aristole kuliko ya Plato.

Mtazamo Wa Ulimwengu Wa Sasa.

Hayo yalikuwa ya ulimwengu wa kale. Sasa hebu tuangalie ulimwengu wa sasa unavyosema. Ulimwengu wa sasa haubahatishi wala kukadiria. Unatumia njia za kisayansi. Hitimisho zake zimejengwa juu ya ukweli, takwimu na utafiti katika ulimwengu wa sasa. Kama matokeo ya elimu kubwa na sahihi zaidi katika medani za utabibu, saikolojia na maarifa ya jamii, tofauti nyingi na kubwa, zaidi kati ya mwanamke na mwanaume, zilizokuwa hazijulikani katika ulimwengu wa kale, sasa zimegunduliwa.

Watu wa kale walitathimini mwanaume na mwanamke kwa msingi wa kuwa mmoja ni mwenye kukwaruza sana, mrefu ana nywele nyingi zaidi mwilini, ana maungo makubwa zaidi na ana sauti nene zaidi wakati mwingine ana mwili nyororo zaidi, mfupi zaidi, na msafi zaidi, ana sauti nyembamba zaidi na ana maungo madogo zaidi. Waliozama zaidi walizingatia tofauti ya umri wao wa kukua (kubalehe na kuvunja ungo) na tofauti ya akili na hisa zao. Walimchukulia mwanaume kama alama ya busara, na mwanamke kama alama ya upendo na mihemko.

Lakini leo tofauti nyingi zaidi zinajulikana sasa kwamba ulimwengu wa mwanamke ni tofauti na ulimwengu wa mwanaume katika mambo mengi. Kwanza tutasimulia tofauti kati ya mwanaume na mwanamke, kwa mujibu wa tulivyozikusanya kutoka kwa wataalamu mabingwa wa fani hii. Kisha tutaeleza falsafa yake na tutaonyesha tofauti zipi ni za asili na zipi ni matokeo ya kihistoria, kiutamaduni na vipengele vya kijamii. Baadhi ya tofauti hizi ziko wazi mno kiasi cha kuwa huwezi kuzikana. Elimu ya wengine (juu ya hili) inaweza kupatikana kwa kusoma kidogo na uzoefu.

Uwili

Kimwili, mwanaume kwa wastani ana maungo makubwa na mwanamke ana maungo madogo. Mwanaume ni mrefu zaidi na mwanamke ni mfupi zaidi. Mwanaume ana ngozi inayo kwaruza na mwanamke ana ngozi laini zaidi. Sauti ya mwanaume inaparuza na ni nzito, na sauti ya mwanamke ni nyororo na inavutia.

Mwili wa mwanamke unakuwa haraka zaidi na wa mwanaume unakuwa pole pole zaidi. Inasemekana hata mimba ya mtoto wa kike inakua haraka ziadi kuliko mimba ya mtoto wa kiume. Mwanaume ana nguvu zaidi kuliko mwanamke, na ana misuli imara zaidi, lakini mwanamke ana uwezo mkubwa zaidi wa kustahimili kuliko mwanaume. Mwanamke huvunja ungo mapema na hufikia umri wa kuacha kuzaa mapema zaidi. Msichana huwahi kuanza kuzungumza kuliko mvulana.

Ubongo wa mwanaume ni mkubwa kuliko ubongo wa mwanamke lakini ukiwianishwa na mwili mzima (ukubwa wake ukigawanywa na ukubwa wa mwili mzima), mwanamke ana ubongo mkubwa zaidi. Mapafu ya mwanaume yanaweza kuvuta hewa nyingi zaidi kuliko mapafu ya mwanamke. Moyo wa mwanamke hupiga haraka zaidi kuliko moyo wa mwanaume.

Kisaikolojia, mwanaume anapenda zaidi mazoezi, kuwinda na maisha ya heka heka nyingi. Hisia za mwanaume ni changamoto na ugomvi ambapo mwanamke ni mwenye kupenda amani. Mwanamume ni mchokozi na mtu wa hima, mwanamke ni mtulivu na mkimya. Mwanamke huepuka mapigano na mambo ya nguvu nguvu na ndio maana kesi za wanawake kujinyonga ni chache zaidi.

Hata wakati wa kujinyonga wanaume hutumia njia za hatari kama vile kujipiga risasi, kujinyonga kwa kamba au kujirusha kwenye majengo marefu wakati wanawake hutumia, vidonge vya usingizi, madawa ya kulenya n.k. kwa ajili ya lengo hili. Mwanamke ana mihemko (jazba, hasira, furaha) ya haraka zaidi kuliko mwanaume na wanasisimka haraka zaidi. Mwanaume ni mtulivu wa akili zaidi.

Kwa asili mwanamke anapenda mapambo, manukato, vipodozi na vitu vya mitindo mipya mipya vya nguo, viatu n.k wakati mwanaume hayuko hivyo. Hisia za mwanamke sio thabiti (hazidumu), akili yake huwa inabadilika. Ni mwangalifu na huchukua tahadhari zaidi, ni mshika dini zaidi, mzungumzaji zaidi, muoga zaidi na anafuata taratibu zaidi kuliko mwanaume. Hisia zake ni za mfumo jike mama toka utoto wake. Hawezi kushindana na mwanaume katika maarifa ya kufasiri mambo yalivyo na masomo mengine makavu. Lakini katika fasihi na sanaa kama kupaka rangi, hayuko nyuma ya mwanaume.

Mwanaume ana uwezo mkubwa zaidi wa kuficha siri zake. Anaweza kuficha tukio baya lililomfika likabaki moyoni mwake tu na ndio sababu anakumbwa sana na magonjwa yanayosababishwa na undani (kuficha mambo moyoni). Mwanamke ni mwepesi kuhisi na mwenye moyo laini kuliko mwanaume, anaweza kuamua kulia kirahisi na wakati mwingine anaweza kupoteza fahamu.

Mtazamo Linganishi Wa Kila Mmoja

• Mwanaume ni mtumwa wa matamanio yake; mwanamke ni mtumwa wa mapenzi.

• Mwanaume humpenda mwanamke aliyempenda, mwanamke humpenda mwanaume aliyeitambua thamani yake (ya mwanamke huyo) na kutamka upendo wake kwake.

• Mwanaume hutaka kummiliki mwanamke, mwanamke hutaka kuutawala moyo wa mwanaume.

• Mwanaume hutaka kumzidi nguvu madaraka mwanamke, mwanamke hutaka kupenya katika moyo wa mwanaume.

• Mwanaume hutaka kumteka mwanamke; mwanamke hutaka kutekwa.

• Mwanamke hutaka mwanaume awe jasiri na shujaa na anayemjali, mwanaume hutaka mwanamke mwenye sura nzuri na mcheshi.

• Mwanamke hutaka ulinzi wa mwanaume, na huchukulia ulinzi huo kuwa ni kitu cha thamani zaidi anachoweza kukimiliki. Anaweza kuyadhibiti matamanio yake. Hisia za ngono za mwanaume ni kali na zenye nguvu za mwanamke ni baridi na zenye kusisimka.

Tofauti Kati Ya Mwanaume Na Mwanamke.

Mwana saikolojia wa kimarekani, Profesa Reek amechapisha matokeo ya utafiti wake juu ya mwanaume na mwanamke katika kitabu kikubwa. Anasema: Ulimwengu wa mwanaume ni tofauti kabisa na ule wa mwanamke. Ikiwa mwanamke hawezi kufikiri au kufanya mambo kama mwanaume, ni kwa sababu wanaishi katika dunia mbili tofauti.

Ameendelea kusema kuwa; “Kwa mujibu wa Agano la Kale, mwanaume na mwanamke wametokana na mwili mmoja. Hivyo ni kweli lakini ingawa wametokana na mwili mmoja, wana miili miwili tofauti, ambayo haifanani kabisa katika maumbile yake. Hawana hisia za aina moja na hawaonyeshi mwitikio wa aina moja katika matukio na ajali mbali mbali. Wako kama sayari mbili zinazozunguka katika njia mbili tofauti. Wanaweza kuelewana na wanaweza kukamilishana, lakini sio kitu kimoja (sawa). Hii ndio sababu wanaweza kukaa pamoja, kupendana na wanaweza wasichokane.

Profesa Reek analinganisha roho ya mwanaume na mwanamke na anagundua tofauti nyingi. Anasema; “Inakinaisha (chosha) kwa mwanaume kukaa na mwanamke anayempenda muda wote. Lakini hakuna kitu kizuri kwa mwanamke kuwa karibu na mwanaume anayempenda.

Mwanaume mara zote anataka kubaki vile vile. Lakini mwanamke anataka kuamka akiwa tofauti na mpya kila siku.

Sentensi bora kabisa ambayo mwanaume anaweza kumwambia mwanamke ni kuwa ‘Mpenzi wangu, nakupenda.’ Sentensi nzuri kabisa ambayo mwanamke hupenda kumwambia mwanaume ni, ‘Naona fahari kuwa na wewe.’

Mwanaume aliyepata kuwa na wanawake wengi katika maisha yake huwavutia sana wanawake wengine. Lakini wanaume hawapendi wanawake waliopata kuwa na wanaume wengine huko nyuma. Wanaume wanapokuwa wazee hukosa furaha kwa sababu wanapoteza kazi walizokuwa wanazitegemea. Wanawake wazee huwa na furaha kwa sababu, kwa mtazamo wao huwa wameweza kumiliki vitu bora kabisa ambavyo mtu anaweza kutamani, nyumba na wajukuu wachache.

Bahati nzuri kwa mwanaume ni kujipatia nafasi inayoheshimika katika jamii. Lakini kwa mwanamke bahati ni kuuteka moyo wa mwanaume na kubaki nao katika maisha yake yote.

Mwanaume mara zote hutaka kumbadilisha mwanamke wa chaguo lake ili afuate dini na utaifa wake.

Kwa mwanamke ni rahisi kubadilisha dini yake na uraia kwa ajili ya mwanaume aliyempenda ikiwa ni pamoja na kubadilisha ubini wake baada ya kuolewa.

Kazi Bora Ya Uumbaji

Bila kujali swali iwapo kutofanana kati ya mwanaume na mwanamke kunasababisha tofauti ya haki na majukumu yao au la, kutofanana kwenyewe ni moja ya kazi bora kabisa na ya ajabu mno ya uumbaji. Ni suala amabalo humuelekeza mtu katika kumtambua Allah na Umoja wake. Kunathibitisha kuwa mfumo wa dunia hii umepangiliwa kwa busara kubwa sana na ubora usio na mfano. Kunaonyesha kuwa uumbaji sio suala la bahati nasibu. Maumbile sio kazi ya upofu. Haiwezekani kutafsiri mambo ya ulimwengu bila kumtambua ‘Msababishaji Mkuu.’ Kwa nia ya kuhifadhi jamii ya viumbe, utaratibu mkubwa wa uumbaji umefanya mfumo wa uzazi kuwepo.

Wanaume na wanawake wanazaliwa kila siku. Kwa vile kuendelea kwa jamii ya wanaadamu kunategemea ushirikianao wao, maumbile yakaona mwanaume na mwanamke wanahitaji kuishi pamoja. Kwa ajili ya kusudio hili maslahi binafsi ambayo ni ya lazima kwa kila kiumbe yamebadilishwa na kuwa hisia za upendo, huduma, ushirikianao na uvumilivu. Ili kuufanya mpango huu uwezekane, na kuhakikisha kuwa miili yao na roho zao zinakubaliana vizuri na kwa raha, tofauti fulani za kiroho na kimwili zimewekwa kwa kila mmoja wao.

Tofauti hizi kati ya mwanamke na mwanaume zinawavuta wote kila mmoja kwa mwenzake. Kama mwanamke angekuwa na maumbile sawa kimwili, mihemko sawa na tabia sawa na mwanaume, isingewezekana kwake kumvutia mwanaume, kama ilivyo sasa. Kama mwanaume naye angekuwa na umbile la kimwili na kifiziolojia kama mwanamke, mwanamke asingemuona kuwa ndio sawa yake, asingefanya chochote kuuteka moyo wake. Mwanaume ameumbwa kuutawala ulimwengu, na mwanamke ameumbwa kumtawala mwanaume.

Sheria ya maumbile imepanga kwamba wote mwanamke na mwanaume wahitajiane na watafutane lakini uhusiano wao sio wa asili sawa na ile waliyo nayo kwa vitu vingine wanavyomiliki, uhusiano huo unatokana na ubinafsi. Wanataka kumiliki vitu kwa ajili ya matumizi yao, na wanavitafuta ili viwe chanzo cha raha na starehe yao. Lakini uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume una maana kila mmoja miongoni mwao anataka furaha na raha ya mwenzake, na hufurahi kujitolea kwa ajili ya mwenzake.

Muungano Mkubwa Zaidi Kuliko Uchu Wa Ngono.

Inashangaza kwamba baadhi ya watu hawawezi kutofautisha kati ya uchu wa ngono na mapenzi. Wanafikiri kuwa uhusiano kati ya mume na mke umejengwa juu ya tamaa, matamanio na hisia ya unyonyaji. Wanashikilia kuwa uhusiano huu ni wa aina moja na ule alionao mtu kwa vitu anavyokula, kunywa, kuvaa au kuendesha. Watu hawa hawajui kuwa katika maumbile, mbali na mahusiano hayo yaliyojengwa juu ya maslahi binafsi, kuna mahusiano mengine pia. Haya ndio mahusiano ambayo yanayoonyesha ubinadamu. Mahusiano haya, kwa kiasi fulani yapo kwa wanyama pia hususani linapokuja suala la majike/madume yao na watoto.

Watu hawa wanafikiri kuwa mwanaume mara zote humtazama mwanamke, kama vile mwanaume asiye na mke anavyomtazama mwanamke malaya. Wanaamini kuwa ni uchu na matamanio ya ngono tu yanayoweza kuwaunganisha mwanamke na mwanaume. Kwa kusema kweli muungano wa ndoa ni kitu kikubwa zaidi kuliko uchu wa ngono, na msingi wake ni ule uliotajwa katika Qur’ani.

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ

“Na miongoni mwa dalili zake ni kuwa amewaumbia wenza wenu kutokana na nyinyi ili mpate utulivu kwao na baina yenu ameweka mapenzi na huruma.” (Suratul Ruum; 30:21).

Ni kosa kubwa lilioje kuitafsiri historia ya uhusiano wa mwanaume na mwanamke kwa mtazamo wa ajira na unyonyaji au kwa msingi wa kupambana ili uishi. Lakini bado kuna watu wanaofanya hivyo na wanatoa hoja zisizo na msingi kutetea mawazo yao. Kwa kweli tunashangazwa sana kwa msingi wa migogoro na ukinzani, kana kwamba mwanaume na mwanamke ni matabaka mawili tofauti ya kijamii ambayo mara zote yapo katika migogoro. Kama inawezekana kuielezea historia ya uhusiano wa akina baba na watoto wao kwa msingi wa ajira na unyonyaji, basi hapo itawezekana pia kuielezea historia ya uhusiano wa waume na wake zao kwa msingi huo.

Ni kweli kwamba mwanaume amekuwa na nguvu zaidi kuliko mwanamke, lakini sheria ya maumbile imemuamrisha katika namna ambayo kwa silika hajaweza kumtendea vibaya au kwa ukatili mke wake kama ambavyo amekuwa akifanya kwa watumwa wake, walio chini ya cheo chake au miliki yake na wakati fulani hata kwa majirani zake.

Hatukatai kwamba mwanaume hajapata kufanya ukatili kwa mwanamke. Tunachopinga ni jinsi ukatili wake unavyoelezewa katika kipindi chote cha historia, wanaume wamewakandamiza wanawake, lakini pia waliwatendea vibaya watoto wao, licha ya upendo wote waliokuwa nao kwao. Sababu za ukatili huu zilikuwa ujinga, mila na kujipendelea wenyewe lakini sio kwa ajili ya kumnyonya mwanamke. Sababu hizi ndio hizo hizo zinazomfanya hata yeye mwenywe mwanaume ajikandamize na kujidhulumu, sababu hizi ni ujinga, desturi na tabia zilizozoeleka, na upendeleo (chuki) na sio tamaa binafsi zaidi.

Uwili Na Hisia Za Mwanamke Na Mwanaume Kwa Kumhusu Kila Mmoja

Sio tu kwamba mahusiano ya kifamilia ya mwanaume na mwanamke kwa mwenzake ni tofauti lakini pia hisia na mielekeo ya kila moja kwa mwenzake ni tofauti. Kwa maneno mengine, asili ya uhusiano wa mwanaume kwa mwanamke ni tofauti na uhusiano wa mwanamke kwa mwanaume, ingawa kila mmoja anavutiwa na mwenzake, lakini tofauti na ilivyo kwa viumbe visivyo hai, hapa kitu kidogo hukivutia kitu kikubwa kwake. Mwanaume ameumbwa kama udhihirisho wa kusubiri kwa hamu, mapenzi na mshughulikaji, na mwanamke kama udhihirisho wa mvuto na kutamanika. Hisia za hawa wawili ni tofauti lakini zinazokamilishana. Mmoja humtafuta mwenzake na mwingine huhitaji kutafutwa.

Wakati fulani uliopita, gazeti lilichapisha picha ya msichana mdogo wa Kirusi aliyekuwa amejinyonga. Msichana huyu aliacha ujumbe kuwa hakuna mwanaume aliyepata kumbusu hivyo maisha yake yamekuwa hayavumiliki tena.

Kwa msichana ni jambo la kukatisha tamaa sana kwamba hakuna mwanaume aliyepata kumbusu. Lakini mvulana mdogo haimsumbui kama msichana hajawahi kumbusu.

Will Durant katika mjadala wake mrefu, anasema msichana ambaye sifa yake kubwa ni elimu na uwezo mkubwa wa kufikiri tu, lakini hana ucheshi wa asili na ujanja wenye akili kidogo, haelekei kufanikiwa kupata mume. Asilimia sitini ya wanawake wenye elimu ya chuo Kikuu hubaki bila waume.

Amesema kwamba mwanamke mmoja mashuhuri na msomi alilalamika kuwa hakuna mtu aliyekuwa tayari kumuoa. Alikuwa akisema; “Kwa nini hakuna anayenipenda? Ninaweza kuwa mke bora kuliko wanawake wengine wengi. Lakini bado wanawake wasio na elimu na umuhimu wowote kijamii wanatafutwa na kuolewa lakini mimi sitafutwi.”

Inaweza kuonekana hapa kuwa hali ya kuvunjika moyo kwa mwanamke huyu ni tofauti na kwa mwanaume yeyote. Analalamika kwamba kwanini hakuna anayempenda.

Mwanaume huvunjika moyo tu pale ambapo anapokuwa hawezi kumpata mwanamke wa chaguo lake au anamtaka lakini anashindwa kumpata.

Hisia za mwanaume na mwanamke zimepangwa hivi, kwa makusudio maalumu ya kuufanya muungano wa mke na mume uwe mzuri zaidi, imara zaidi na wenye furaha zaidi. Katika maisha yao kwa kusema kweli, msingi wa jamii ya watu na malezi ya kizazi kijacho yamejengwa juu ya muungano huu.

Mwanasaikolojia wa kike anaandika; “Kama mwanasaikolojia shauku yangu kubwa imekuwa kujifunza juu ya roho (akili) za wanaume. Siku za nyuma huko nilipewa kazi ya kuchunguza sababu za kisaikolojia za mwanaume na mwanamke. Mwisho nilihitimisha kuwa; Wanawake wote wanapenda kufanya kazi chini ya uangalizi wa mtu mwingine. Wanapenda kufanya kazi katika vyeo vya kawaida sio kama bosi.

Wanawake wote wanapenda kuhisi kuwa kuwepo kwao kunatambulika na kunahitajika.

Mwanasaikolojia huyu anaeleza maoni yake kuwa; “Ninaamini kuwa mahitaji haya mawili ya kiroho yanatokana na ukweli kwamba wanawake wanaongozwa na mihemko (emotions) wakati wanaume huongozwa na akili. Mara nyingi inaonekana kwamba wanawake sio tu kwamba wana akili sawa na wanaume, bali wakati fulani hata huwazidi (wanaume).

Udhaifu wao pekee ni kuwa wana jazba sana (mno). Kufikiri kwa wanaume kunatekelezeka zaidi, wanahukumu vizuri zaidi, wanapanga mambo vizuri zaidi na wanawaelekeza wengine (ni wakurugenzi) vizuri zaidi. Ubora wa roho (akili) ya wanaume (kuizidi ya wanawake) ni kitu kilichopangwa na maumbile yenyewe. Jitihada yeyote mwanamke atakayofanya kubadilisha ukweli huu, itakuwa ni kujisumbua bure.

Wanawake lazima waukubali uhalisia kuwa kwa vile wao wana mhemuko sana wanahitaji usimamizi wa wanaume katika maisha yao. Lengo kubwa la maisha ya mwanamke ni ‘Kujihakikishia’ hatima yake ya baadaye. Akishalipata, huziambia kwa heri shughuli zake nyingine. Ni mwoga kufanya mambo ya hatari (ambayo haijulikani kama matokeo yake yatakuwa mazuri au mabaya). Uoga ni hisia za moyoni, na ili kuzishinda mwanamke anahitaji msaada wa mwanaume. Kazi zote zinazohitaji kufikiri muda wote zinamchosha.

Harakati Za Papara (Pupa).

Harakati za wazungu za kurejesha haki za wanamke zilikuwa ni suala la papara lililofanywa kwa uharaka usio wa lazima. Mpango wenyewe wa mageuzi ulikuwa mzuri, lakini ukweli wa kisayansi haukuzingatiwa katika utekelezaji wa mageuzi haya, na matokeo yake yakawa ni mchanganyiko wa nukta za maana na za ovyo.

Hakuna shaka kwamba mlolongo wa masaibu na taabu za wanawake uliondolewa, walikubaliwa na kupewa haki nyingi na milango sasa kwa ajili yao ikafunguliwa na harakati za haki za wanawake. Lakini wakati huo huo mageuzi haya yalileta mikosi na balaa kubwa. Sio kwa mwanamke tu, bali kwa wanaadamu wote. Kama papara na pupa visingepewa nafasi, haki za wanawake zingekuwa zilirejeshwa kwa namna bora zaidi na kusingekuwa na mayowe na vilio vya wasomi dhidi ya matokeo yake maovu.

Hata hivyo, tunatarajia kuwa ushauri mzuri utashinda na kuenea na katika mageuzi yatakayofuatia, badala ya kuwa na jazba, watayatumia na kutanguliza maarifa (elimu) na uelewa. Maoni ya wasomi yanaashiria wema na heri siku za usoni. Inaonekana kwamba watu wa Magharibi bado wanataabishwa na madhara ya mageuzi haya ambayo yanaonekana kuwasisimua na kuwafurahisha waigaji wao wa nchi za Mashariki (Asia).

Mtazamo Wa Will Durant.

Will Durant, katika kitabu chake, ‘Pleasures of Philosophy’ anaeleza vizuri kabisa masuala ya kijisia na familia. Hapa tutachagua baadhi ya mawazo yake ili wasomaji wetu waelewe uelekeo wa mkondo wa fikra miongoni mwa wasomi wa Kimagharibi na kuepuka hitimisho la papara.

Chini ya sura ya Love (mapenzi) anasema, ‘Utaratibu wa kwanza wa wazi huanza wakati wa kubalehe. Kubalehe kwa kiingereza ni ‘Puberty’ neno ambalo ni la kilatini lenye maana ya zama za nywele, yaani ni kipindi cha kuota nywele katika miili ya wavulana, hasa kifuani, jambo ambalo huwa ni la fahari kwao, na ndevu huota usoni, ndevu ambazo huzinyoa kila baada ya muda fulani. Ubora na uwingi wa nywele na vitu vingine unahusiana na nguvu ya uzazi na asili (chimbuko). Nywele huwa katika ubora wa juu kabisa katika zama za kilele cha urijali (nguvu za kiume). Kukua huku kwa nywele, pamoja na sauti kuanza kuparuza, ni sehemu ya tabia za awamu ya pili ya jinsia zinazotokea kwa wavulana wakati wa kubalehe.

Kwa upande wa wasichana wakati wa kuvunja ungo, maumbile huifanya tabia mienendo yao kuwa mizuri mno kiasi cha kuwavutia wanaowatazama. Matako yao huanza kuwa bapa ili kurahisisha kubeba mimba. Matiti yao hukua na kuchomoza kwa ajili ya kumnyoyesha mtoto. Hakuna anayejua kwa yakini kinachosababisha kuonekana kwa tabia za awamu ya pili za jinsia (secondary sex characteristics).

Hata hivyo nadharia ya Profesa Starling, katika siku za hivi karibuni imepata wafuasi wengi. Kwa mujibu wa nadharia hiyo seli za via vya uzazi, wakati wa hatua hii ya ukuzi, hazizalishi manii na mayai ya kike peke yake, bali pia huzalisha homoni ambazo huingizwa katika damu na kusababisha mabadiliko ya kimwili, kiroho na mengineyo. Katika umri huu, sio tu kwamba mwili hupata nguvu mpya, bali pia roho, tabia na mwenendo huathirika kwa namna nyingi.

Romain Rolland anasema kuwa katika miaka ya mtu, huja wakati ambapo mabadiliko mengi ya polepole ya kimwili husababisha maendeleo zaidi ya mwanaume au mwanamke. Mabadiliko muhimu kabisa huwa ni ukakamavu na nguvu kwa wanaume na uzuri unaovutia pamoja na ulaini wa ngozi na mwili kwa mwanamke.

Damoseh anasema kuwa kwa asili ‘wanaume wote ni waongo, walaghai, wanafiki, wana hila, na ni wagomvi; na wanawake wote ni wabinafsi, wanajishaua na sio waaminifu. Lakini kuna kitu kimoja duniani ambacho ni kitukufu na kitakatifu, na kitu hicho ni muungano wa watu hawa wawili ambao sio wakamilifu... kuelekea kwenye ukamilifu.

Taratibu za kutafuta mwenza kwa wakubwa zinakuwa na uanzishaji kwa mwanaume kupata mkono wa kheri, lakini kujiondoa kwa mwanamke kwa ajili ya ushawishi na udanganyifu (kama mambo yalivyo, kuna hali za kipekee). Kwa vile mwanaume, kwa asili ni kama mpiganaji na mnyama anayewinda, matendo yake ni ya hakika na halisi na pia yeye ndiye muanzaji (mchokozi). Mwanamke kwake (kwa mwanaume) ni zawadi ambayo lazima ichukuliwe na imilikiwe. Kutafuta mke/mwenzi ni juhudi na mapambano na ndoa ni umiliki na utawala, kuwepo kwa usafi thabiti (kutozini) kwa mwanamke husaidia maslahi ya uzazi, kwa vile kujizuia (kuzini) kwa mwanamke kutokana na aibu kunamsaidia mwanamke katika kuchagua mwenzi wake.

Usafi (kutozini) huwazuia wanawake kutokuwa waangalifu katika kuchagua wenzi (wanaume) wao, ambao ni baba wa wana wao watakaowazaa. Mwanamke huzungumza kwa maslahi ya wote lakini mwanaume hujizungumzia maslahi yake peke yake. Mwanamke anaujuzi zaidi wa kufanya uchunguzi kwa vile matamanio yake sio makubwa kiasi cha kufanya ashindwe kutumia akili yake vizuri.

Darwin amegundua kwamba katika jamii za viumbe wengi, majike hayapendi sana kufanya mapenzi. Wanaviumbe wengine wanaochunguza mimea na wanyama, kama Lemberzo, Cash na Kraft Ebing nao pia wana maoni kuwa wanawake wanapendelea zaidi kuonekana wanavutia, pamoja na kupokea sifa za juu juu (wakati fulani za uongo) na za jumla za wanaume, na wanapendelea pia kuona wanaume wanajali mahitaji yao halisi ya ndani kuliko kutaka kufanya ngono.

Lemberzo, na wengine wanasema kwamba ‘Msingi wa asili wa mapenzi ya mwanamke ni kuwa mama (na kuwajali watoto) ndio tabia na sifa ya kwanza ya mwanamke, kisha mapenzi ndio yanafuatia. Hisia zote na michomo ya moyoni inayomuunganisha mwanaume na mwanamke haitokani na mahitaji yake ya kimwili lakini inatokana na silika yake ya unyenyekevu (kujiweka chini ya uangalizi wa mwanaume). Silika hii ina kazi ya kutimiza na kutekeleza majukumu ya nafasi yake halisi.

Will Durant katika sura aliyoiita ‘Man and Woman’ (mwanaume na mwanamke), anasema; ‘Kazi kubwa ya mwanamke ni kuhakikisha kwamba jamii ya watu inaendelea kuishi na kudumu, na kazi kubwa ya mwanaume ni kuwatumikia mke na watoto wake. Wanaweza kuwa na kazi nyingine pia, lakini kwa misingi ya busara na kuangalia manufaa, hizo kazi nyingine ziko chini ya majukumu haya mawili. Haya ni majukumu mawili ya msingi ya binadamu anayoyafanya bila kujijua, ambayo utekelezaji wake ndio utakaoleta furaha kwa wanaadamu. Mwanamke kwa asili hutaka amani, sio vita. Inaonekana kwamba katika jamii nyingi za viumbe, mwanamke hana silika ya ugomvi na ukorofi kabisa. Akiamua kupigana, basi ni kwa ajili ya watoto wake.

Mwanamke ana subira zaidi kuliko mwanaume ingawa mwanaume ni jasiri zaidi katika kukabiliana na kazi za hatari na matatizo katika maisha. Ana uvumilivu mkubwa zaidi, na anaweza kukabiliana na ugumu na kero ndogo ndogo nyingi tu vizuri zaidi. Roho yake ya kupenda vita au ujasiri inaishia katika kupenda kuiona sifa hii kwa wengine. Anawapenda askari na wanaume wenye nguvu na majabari, kwa sababu hii anaweza kushawishiwa na fikra ya kufurahia au kupata ashiki kutokana na kuumia (masochism) na anaweza kuwa mhanga wa nguvu za kiume.

Moyo wa kupenda nguvu na ushujaa wakati fulani huyafunika hata maslahi yake ya kiuchumi, na wakati mwingine huchagua kuolewa na mtu shujaa (na kumuacha tajiri). Humkubali kwa furaha mwanaume ambaye hutoa amri kwa wengine kwa njia ya haki na uadilifu. Kama wanawake sio watii kiasi hicho siku hizi, tofauti na walivyokuwa zamani, ni kwa sababu wanaume siku hizi ni dhaifu, hawana nguvu kama zamani na mazingira yanayowazunguka. Silika yake humfanya apende desturi za zamani. Kimwili na kiakili hapendi kujaribujaribu vitu kama vile kuzini kabla ya ndoa n.k ingawa baadhi ya wanawake wanaoishi katika miji mikubwa wanaweza kuwa tofauti. Akiamua kufanya mapenzi (ngono) nje ya ndoa, si kwa sababu anataka uhuru katika hilo (ngono), bali ni kwa sababu bado hajapata mume mwaminifu na muwajibikaji.

Ikiwa katika ujana wake alipata kuvutiwa na shughuli za siasa na akawa anatamani kufanya kazi katika fani mbali mbali na tofauti za kazi, kwa kawaida huachana na kazi hizo baada ya kupata mume mwaminifu na mara moja hujiondoa yeye na mume wake katika mambo ya umma. Humkumbusha mume wake kuwa uaminifu na uwajibikaji wake aurudishe nyumbani kwake kwa kuwa mwanamke hahitaji kufikiri sana kujua kwamba mageuzi yote huanzia nyumbani. Anapofanikiwa kumrudisha mwanaume mbunifu na mzururaji nyumbani na kumfanya aiangalie nyumba na watoto wake, basi kusalimika na kuendelea kuishi kwa mwanadamu kunamtegemea yeye. Kwa asili hahusiki na mambo ya sheria na serikali. Nyumba na watoto ndio vitu anavyovipenda. Akishafanikiwa kuvitazama na kuvitunza vizuri, hajali ni serikali gani inaingia madarakani na ni serikali gani inaondoka madarakani.

Maumbile hayajali juu ya sheria za serikali. Vitu vya maana kabisa kwa maumbile (nature) ni nyumba (familia) na mtoto. Yakifanikiwa kuvihifadhi hivi vitu viwili, hayashughulishwi tena na mambo ya serikali, na huwacheka wale wanaojaribu kubadili sheria za msingi. Kama leo maumbile yanayoonekana kushindwa kuihifadhi familia (nyumba) na mtoto, hii ni kwa sababu mwanamke tangu siku nyingi ameyasahau maumbile. Lakini kushindwa kwa maumbile sio kwa kudumu. Yanaweza kuwapatia mamia ya manufaa yalionayo, yakiruhusiwa na kupewa nafsi ya kufanya hivyo. Kuna mataifa na watu wa rangi nyingi sana kuliko tulivyo na maumbile yanayohakikishia kuendelea kuishi na kudumu kutokana na faida ambazo maumbile yanazo.