read

Mahari na Matunzo I

Ni moja ya desturi za zamani za mahusiano ya kifamilia ya mwanadamu kwamba wakati wa kuoa mwanaume hulipa mahari kwa mwanamke (anayemuoa) au kwa baba yake (huyo mwanamke). Na mbali na hili, hujitolea kugharamia gharama zote za mke wake na watoto katika kipindi chote cha uhai wake.

Ni nini msingi wa desturi hii? Ni kwa nini na ni kwa namna gani? Ni nini mantiki ya mahari? Je mahari na matunzo bado ni mambo yanayofaa kuendelezwa hadi sasa, hata kama mwanaume na mwanamke wana haki sawa za kibinadamu na za asili na mahusiano baina yao yamejengwa kwa msingi wa uadilifu na usawa? Au ni mabaki (masalia) yaliyobakia ya enzi zile ambapo mwanaume alimmiliki mwanamke? Je uadilifu na usawa wa haki, hasa katika karne hii unaamrisha kuwa desturi hizi zilizopitwa na wakati zipigwe marufuku? Na kwamba ndoa ifungwe bila mahari? Na mwanamke ajitunze mwenywe? Na kwamba jukumu la kulea watoto (gharama zake) liwe jukumu la kuchangia wote wawili, mke na mume?

Tunataka kujibu maswali haya, na tutaanza na swali la mahari. Hebu tuangalie jinsi hii desturi ilivyoanza, falsafa yake ni nini na jinsi wanasosholojia wanavyoeleza chanzo /asili yake:

Historia Fupi Ya Mahari.

Inasemekana kwamba zamani kabla ya historia kuanza kuandikwa, mwanadamu aliishi maisha ya kishenzi, yaliyokuwa na muundo wa kikabila. Kwa sababu zisizojulikana ndoa kati ya ndugu wa damu moja ilikatazwa. Hivyo vijana wa kiume wa kabila waliotaka kuoa, walilazimika kuchagua wake zao kutoka katika kabila jingine. Mara nyingi waliyatembelea makabila mengine kwa madhumuni haya. Enzi hizo mwanaume hakuwa anajua jukumu lake katika kusababisha mimba (yaani hakujua kama tendo lake la ndoa ndilo linalosababisha mimba). Alifikiri kuwa mtoto alikuwa ni mali ya mama kwa asilimia mia moja. Ingawa aliona watoto wakifanana naye sana. hakujua sababu ya kufanana huko. Kwa hali hii watoto nao walifikiri kuwa walikuwa ni mali ya mama yao na sio baba yao. Wakati huo ukoo ulitambulishwa kwa kupitia mfumo jike.

Wanaume walionekana kuwa ni wagumba na tasa. Baada ya ndoa, waliishi na watu wa kabila la mke wake kama kiambatanishi tu, kwa sababu mwanamke alihitaji uswahiba wa mume wake. Kipindi hiki kinajulikana kama kipindi cha mfumo jike (matriarchy).

Haikuchukua muda mrefu, mwanaume akagundua jukumu lake katika uzazi (utungaji mimba) na akaamini kwamba kumbe kiuhalisia watoto walikuwa ni wake. Kuanzia wakati huo na kuendelea, alimtawala mwanamke na akajipa cheo cha ukuu wa familia. Hivyo, kipindi cha mfumo dume, kikaanza.

Katika kipindi hiki pia ndoa ya ndugu wa damu moja ilikatazwa. Mwanaume alipaswa kuchagua mke kutoka katika kabila (au ukoo) mwingine, na kumleta katika kabila lake. Kwa vile kulikuwa na hali ya kutokuelewana baina ya makabila kutokana na vita vya kikabila, njia pekee ya kupata mke ilikuwa ni kumdaka na kumbeba kwa nguvu binti wa kabila jingine.

Pole pole maelewano na amani yakachukua nafasi ya mapigano na magomvi, na makabila mbali mbali yakaweza kuishi pamoja kwa amani. Katika kipindi hiki mila ya kuwadaka na kuwabeba kwa nguvu wasichana ilipigwa marufuku. Ili kumpata mke aliyempenda, mwanaume alipaswa kwenda kufanya kazi kwa baba wa msichana huyo kwa muda fulani. Kwa kuzingatia kazi alizozifanya hapo ukweni, baba wa msichana alimuozesha kwa huyo mwanaume, naye alimchukua na kwenda naye kwenye kabila lake.

Mfumo wa malipo wa fedha ulipoenea, mwanaume aligundua kuwa badala ya kufanyakazi kwa baba wa bibi harusi kwa miaka, ilikuwa ni bora zaidi kupeleka ukweni zawadi maridhawa na kumchukua msichana mara moja. Huu ndio ukawa mwanzo wa mahari.

Kwa mujibu wa nadharia hii, katika siku za mwanzo mwanaume aliishi kama kiambatanisho cha mwanamke na alimtumikia (mwanamke). Katika kipindi hiki mwanamke alimtawala mwanaume. Katika hatua inayofuata, madaraka yalipohamia mikononi mwa mwanaume, aliteka nyara wanawake kutoka katika kabila jingine. Wakati wa hatua ya tatu, ili kumpata mwanamke, mwanaume alikwenda kwa baba wa mwanamke na kumhudumia kwa miaka kadhaa. Wakati wa hatua ya nne, mwanaume aliwasilisha kiasi cha fedha kwa baba wa mwanamke. Na hivyo ndio desturi ya mahari ilivyoanza.

Inasemekana kwamba tangu wakati mtu alipofutilia mbali mfumo jike na kuweka msingi wa mfumo dume, alimpa mwanamke hadhi ya utumwa au zaidi kama mfanyakazi au mtumishi wake. Alimchukulia kama chombo cha uchumi, ambacho kwa njia nyingine ataweza kukidhi matamanio yake vile vile. Hakumpa uhru wa kijamii au wa kiuchumi. Mapato ya kazi ya mwanamke yalikuwa ni mali ya baba au ya mumewe. Hakuwa na haki ya kujichagulia mume wake, wala kuendesha shughuli yoyote ya kiuchumi kwa ajili yake mwenyewe. Fedha ambayo mwanaume amelipa kama mahari na gharama ambazo anatoa kama matumizi (nafaqah) zilikuwa kabisa zinatokana na pato la uchumi ambalo amelipata kutoka kwa mwanamke katika kipindi cha wakati wa mahusiano ya ndoa.

Mahari Katika Mfumo Wa Haki Wa Kiislamu.

Kuna hatua ya tano pia ambayo wanasosholojia na wasomi wengine hawakuisema. Katika hatua hii mwanaume humpa zawadi mwanamke. Wazazi wote wawili wa mwanamke hawana haki ya kuidai zawadi hiyo. Mwanamke hupokea zawadi, lakini hubaki na uhuru wake wa kiuchumi na kijamii. Humchagua mume kwa hiari yake mwenyewe, bila kulazimishwa na baba wala kaka. Na zaidi ya hayo, si baba wala mume wake mwenye haki ya kumnyonya. Matunda ya kazi na jasho lake ni mali yake binafsi, na hakuna mwenye haki ya kumuingilia juu ya mali hiyo. Katika masuala ya kifedha hahitaji uangalizi au usimamizi wa yeyote.

Mume ana haki moja tu. Anaweza kufurahia tendo la ndoa na mke wake. Katika muda wote wa ndoa yao, mwanaume anawajibika kumtimizia mkewe mahitaji yote ya halali kwa mujibu wa uwezo wake.

Hii ndio hatua inayotambuliwa na Uislamu na ambayo juu yake Uislamu umejenga msingi wake wa mahusiano ya ndoa. Aya nyingi za Qur’ani zinasisitiza kuwa mahari ni mali ya mwanamke. Na mbali na mahari, mwanaume anapaswa kumtunza na kubeba gharama zote za mkewe. Na wakati huo huo chochote anachokipata mwanamke ni mali yake peke yake na sio ya mtu mwingine yeyote, sio ya baba yake wala mume wake.

Hapa ndipo suala la mahari na matunzo linapotatanisha kidogo. Maadamu mahari inalipwa kwa baba wa msichana na anakwenda kwenye nyumba ya mume kama mtumwa na mume akawa na mamlaka ya kumnyonya, hapa suala lingekuwa rahisi kueleweka. Mahari ililipwa kama bei ya msichana na alipaswa kutunzwa kama mtumwa mwingine yeyote. Sasa kwa vile baba wa msichana hakulipwa chochote, mume haruhusiwi kumnyonya mke wake, mwanamke ana uhuru kamili wa kiuchumi, na kuhusiana na haki zake hahitaji usimamizi, udhibiti au uangalizi wa mtu yeyote. Sasa kwa kuwa mambo yako hivi kuna maana gani ya kulipa mahari na kugharamia matunzo?

Tuitazame Historia Kidogo.

Ili tuweze kuelewa falsafa ya mahari na matunzo katika hatua hii ya tano, tunapaswa kuitazama kiumakinifu nadharia ya vipindi vinne iliyotajwa hapo juu. Ukweli ni kwamba yote yaliyosemwa juu ya vipindi hivi si chochote zaidi ya nadharia tete iliyojengwa juu ya dhana na makisio tu. Hayana taarifa za kihistoria wala ukweli wa kisayansi. Hatuna elimu ya uhakika juu ya mwanadamu aliyeishi kabla ya kuanza kuandikwa kwa historia. Yote yaliyosemwa juu ya kipindi cha mfumo jike, akina baba kuwauza binti zao, na wanawake kunyonywa kiuchumi na waume zao, si ya kuaminika sana.

Kuna mambo mawili yaliyoisumbua akili juu ya dhana na makisio. La kwanza ni kuwa mtu duni (wa kale) amewakilishwa kama mtu mshenzi, mgomvi na asiyekuwa na hisia za kibinadamu. Jambo la pili ni kuwa mpangilio wa ajabu wa maumbile katika kufikia malengo yake umepuuzwa.

Tafsiri hii ya asili ya mwanadamu pengine inaweza kutolewa na watu wa Magharibi na sio watu wa Mashariki isipokuwa wale watu wa Mashariki ambao wanafuata mila za Kimagharibi kwa sababu fulani fulani, mzungu hazifahamu vizuri hisia na mawazo ya kibinadamu. Hawezi kukiri kuwa ana mchango wa msingi katika historia. Kutokana na uchu wake wa kiuchumi, akili yake yote iko kwenye mkate na siagi. Huitazama historia kama mashine, ambayo huwa haitembei mpaka iwekewe mafuta. Kama mwelekeo wake ni ngono huwaona wanaadamu wote na historia ya mwanadamu, pamoja na utamaduni wao, sanaa, maadili na dini kama miundo iliyorekebishwa ya mchezo wa ngono. Kama maoni yake ni ya kisiasa, basi huiona historia yote ya mwanadamu kuwa ni mfululizo wa vita, umwagaji damu na vitendo vya ukatili.

Mzungu aliteswa mno kwa kutumia jina la dini katika zama za kati, ambapo watu mara nyingi walikuwa wakichomwa moto wakiwa hai, kiasi cha kuwa amekuwa na mzio na jina la Mungu, dini na vitu vyote vinavyowakilisha dini. Hii ndio sababu, licha ya ushahidi wote wa ukweli kwamba maumbile yana makusudio na mfumo wa ulimwengu haufanyi kazi kwa bahati nasibu hajathubutu kukiri kuwepo kwa ‘Sababu Sababishi’ (yaani Mwenyezi Mungu).

Hatuwaombi wafasiri wa historia wa Kimagharibi kukiri kuwepo kwa mitume, waliokuwa wakitokea katika historia yote ya mwanadamu kuja kutangaza ujumbe wa uadilifu na ubinadamu na kupiga vita ufisadi, mambo ambayo waliyafanikisha kwa ukamilifu. Tunachowataka ni angalau wasipuuzie jukumu la utambuzi waliopewa na maumbile.

Hakuna shaka kwamba katika historia ya uhusiano wa mwanaume na mwanamke, kumekuwa na matukio mengi ya ukatili uliopindukia, na mengine yakiwa ni maovu mno, ambayo yamesimuliwa katika Qur’ani pia, lakini hatuwezi kusema kwamba historia yote ya mwanadamu ilikuwa imejaa vitendo vya ukatili na mapigano.

Falsafa Ya Kweli Ya Mahari

Kwa mujibu wa imani yetu, mahari ilikuja kutokana na mipangilio makini, iliyowekwa katika usanifu wa uumbaji ili kuweka sawa uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke. Mahari imetokea (imekuwepo), kwa sababu, kwa asili majukumu ya mwanaume na mwanamke kila mmoja kwa mwenzake yako tofauti. Kwa mujibu wa mafunzo ya dini sheria ya mapenzi na mvuto ipo kila sehemu ulimwengu. Kwa vile kila kitu kimetengenezwa ili kutekeleza kazi maalum, basi majukumu yake ni tofauti na vitu vingine vyote.

Tulipokuwa tukijadili tofauti kati ya mwanaume na mwanamke, tulishaeleza tayari kuwa hisia na shauku zao kuhusiana na kila mmoja, hazifanani. Sheria ya uumbaji imeshaamuru kuwa mwanamke awe na sifa za urembo (uzuri), fahari na kutojali ambapo mwanaume awe na sifa za kubembeleza na kushughulika. Hivi ndiyo udhaifu wa kimwili wa mwanamke ulivyofidiwa, na kwa sababu hii mara zote mwanaume ndiye amekuwa akimtaka mwanamke pamoja na kutoa pendekezo la kuoa. Kama tulivyoona huko nyuma kwa mujibu wa wanasosholojia katika vipindi vyote vya mfumo jike na mfumo dume, ni mwanaume ndiye amekuwa akimtaka mwanamke.

Wanasayansi wanasema kwamba mwanaume ana uchu (tamaa) zaidi (ya ngono) kuliko mwanamke. Baadhi ya hadithi za Kiislamu zinasema kuwa mwanaume hana tamaa (uchu) zaidi. Ilivyo, mambo ni kinyume chake lakini mwanamke ana uwezo zaidi wa kujizuia. Kivitendo, maoni yote mawili yanaleta kitu kimoja. Hata hivyo, ni jambo la hakika kwamba mwanaume ana uwezo mdogo zaidi wa kujizuia. Sifa hii imemuwezesha mwanamke asimfuate (asianze kumtaka) mwanaume, wala kujipeleka kwake kirahisi. Silika ya mwanaume humlazimisha kumwendea na kumtaka mwanamke, na huchukua hatua kadhaa ili ampate. Moja ya hatua hizi ni kumpa zawadi.

Wanaume mara zote wamekuwa wakichuana kumpata mwanamke (msichana). Wamekuwa hata wakipigana ili kufikia lengo hili. Lakini wanawake kamwe hawajapata kuonyesha umakini na shauku kama hii ya kumpata mwanaume. Mambo yako hivi kwa sababu majukumu ya mwanaume na mwanamke kila mmoja kwa mwenzake sio sawa. Mwanaume mara zote humfukuzia mwanamke wakati mwanamke humuonyesha hali fulani ya kutokumjali.

Mahari yanahusiana sana na staha na usafi wa kimaadili (hususan kutozini). Mwanamke anafahamu kwa silika kuwa heshima na staha yake vinataka asijitoe bure kwa mwanaume.

Hivi ndivyo mwanamke alivyo, licha ya udhaifu wake wa kimwili aliweza kuwapigisha magoti wanaume, kuwalazimisha kuchuana vikali na kuwafanya akina Romeo kuwakimbilia akina Juliet. Mwanamke anapokubali kuolewa na mwanaume, hupokea zawadi kutoka kwa huyo mwanaume kama ishara ya urafiki, furaha na dhamira njema.

Inasemekana kwamba miongoni mwa makabila ya kishenzi, msichana alipokuwa na waposaji zaidi ya mmoja alikuwa akiwashawishi wapigane mapigano rasmi ili kutetea hadhi yao. Aliyeshinda au kumua mwenzake (mpinzani wake) alionekana ndiye anayefaa kumuoa msichana huyo.

Kulikuwa na habari kwenye gazeti kwamba msichana mmoja katika mji wa Tehran aliwashawishi wavulana wawili kupigana ili kutetea hadhi yao mbele yake. Kwa wale wanaofikiri kuwa nguvu ni mabavu ya kikatili na wanashikilia kuwa historia ya uhusiano wa mwanaume na mwanamke haina chochote zaidi ya vitendo vya ukatili na unyonyaji, si jambo linaloaminika kwamba jinsia dhaifu na ya kike inaweza kuwashawishi watu wawili wa jinsia yenye nguvu kushambuliana/kupigana. Lakini kwa wale wenye elimu kidogo juu ya nguvu ya ajabu ambayo maumbile yamempa mwanamke, hapa hakuna kitu cha ajabu.

Mwanamke ana ushawishi mkubwa sana kwa mwanaume. Ushawishi wa mwanamke kwa mwanaume umekuwa mkubwa zaidi kuliko ule wa mwanaume kwa mwanamke. Mwanaume anamhitaji sana mwanamke, na pia anauhitaji sana ucheshi wake, usafi wake wa kimaadili na staha ili apate mafanikio katika sanaa na medali za ujasiri. Sifa ya kujenga watu wenye haiba kubwa na wenye vipaji vikubwa inamrudia yeye. Mwanamke anamjenga mwanaume na mwanaume anaijenga jamii. Mwanamke akipoteza sifa ya usafi wa kimaadili, staha na kujizuia, na akajaribu kufanya majukumu ambayo ni ya mwanaume, kwanza mwanamke huyu anaweza kujishushia hadhi, kisha mwanaume anaweza kupoteza uanaume wake, na mwisho wa safari jamii inaweza kuangamia.

Ustadi ule wa mwanamke, umemuwezesha kudumisha haiba yake katika kipindi chote cha historia, kumlazimisha mwanaume kwenda katika mlango wake, kama mchumba, kumshawishi mwanaume kuingia katika uadui na hata kupigana kwa ajili yake, kudumisha staha na usafi wa kimaadili kama nembo yake ya ubora, kuuficha mwili wake usionekana kwa wanaume, kumhamasisha mwanaume apende kufanya matendo magumu ya kishujaa, kama rasilimali takatifu, kufanya vizuri katika mambo ya kiakili na matendo ya ubunifu, kuimba nyimbo za mapenzi na kunyenyekea mbele ya jinsia dhaifu kwa unyenyekevu mkubwa. Kwa hiyo tabia hii imemlazimisha mwanaume kutoa zawadi kwa bibi harusi wakati wa ndoa kama mahari.

Mahari ni sehemu ya sheria ya maumbile, ambayo imeanzishwa na maumbile yenyewe.

Mahari Katika Qur’ani

Muundo wa mahari ulioelezwa hapo juu kuhusiana na hatua ya tano sio ubunifu wa Qur’ani. Qur’ani ilichokifanya ni kuurejesha katika muundo wake wa asili na mzuri kabisa. Qur’ani inasema kwa ufasaha:

وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً ۚ

“Wapeni wanawake mahari yao, hali yakuwa ni hadiya (zawadi)…” (Suratul Nisa 4:4).

Hii ina maana kwamba mahari ni haki ya wanawake (hao wanaoolewa) na ni zawadi wanayopewa wao moja kwa moja. Haiwahusu baba na kaka zao. Katika sentensi hii fupi Qur’ani imetaja nukta tatu za msingi:

Kwanza: imetumia neno Saduqatihinna (yaani ukweli na uaminifu) badala ya neno mahari. Hivyo mahari ni alama ya ukarimu na wema wa mwanaume anayeilipa. Nukta hii imeelezwa na wafasiri mbalimbali mashuhuri wa Qur’ani Tukufu, kama vile Zamakhshari, mwandishi wa tafsir mashuhuri ya Qur’ani iitwayo Kashshaf. Halikadhalika mwanasayansi wa asili na maendeleo ya lugha, Righib Isfahani amesema katika kamusi yake ya Qur’ani kuwa mahari imeitwa Saduqah kwa sababu ni alama ya uaminifu wa imani.

Pili: ni dhahiri kutokana na |Aya hiyo ya Qur’ani kuwa mahari inapaswa kulipwa kwa mwanamke moja kwa moja, na wazazi wa mwanamke hawapaswi kudai chochote katika mahari hiyo. Mahari sio fidia ya jitihada walizozifanya wazazi katika kumlea binti yao.

Tatu: ni dhahiri pia kuwa mahari si chochote zaidi ya hadiya na zawadi.

Sifa Ya Hisia (Za Kimapenzi) Miongoni Mwa Wanyama.

Sheria ya mahusianao ya kimapenzi haiwahusu binadamu peke yao bali hata wanyama. Ingawa jinsia zote mbili zinahitajiana, jinsia ya kiume huhisi haja kubwa zaidi kwa ajili ya mwanamke, na huanzisha jitihada za kumpata. Hii ndio sababu mwanaume/dume huwa hatumii vibaya nguvu nyingi alizonazo (kumuonea mwanamke /jike), na huonyesha wema kwa mwanamke.

Zawadi Katika Mahusiano Haramu

Hata mwanaume na mwanamke wanapotaka kufurahia ngono katika mahusiano haramu (nje ya ndoa), ni mwanaume ambaye humpatia mwanamke zawadi. Wanapopata chai, kahawa au chakula pamoja ni mwanaume ambaye huona kuwa ni juumu lake kulipa bili. Mwanamke huona kuwa ni matusi kutakiwa kumlipia mwanaume. Baadhi ya watu hudai kuwa mvulana anahitaji uwezo wa kifedha ili kujiingiza katika zinaa ambapo kwa msichana hiyo ni njia ya kujipatia zawadi. Mila hizi ambazo tunazikuta katika mahusiano halali (ya ndoa) na haramu (ya nje ya ndoa) zinatokana na kutofautiana kwa hisia za mwanaume na mwanamke za kila mmoja kwa mwenzake.

Mzungu Ana Mahusiano Ya Asili Zaidi Katika Kufanya Mapenzi Ya Haramu Kuliko Katika Ndoa.

Katika nchi za Magharibi ambako hali za kifamilia zimeharibiwa kwa jina la usawa wa haki za binadamu, na jitihada inafanyika kugawa majukumu sawa ya kazi za ndani (kama kupika, kudeki n.k) lakini bado mwanaume anatekeleza majukumu yake ya asili katika mahusiano ya nje ya ndoa. Katika mahusiano ya nje ya ndoa, bado mwanaume hutoa zawadi kwa mwanamke na hubeba gharama za huyo mwanamke, lakini katika ndoa, sio tu kwamba hakuna mahari, lakini mwanamke pia hubeba mzigo mkubwa wa gharama za matumizi ya nje ya nyumbani. Hii ina maana kuwa kwa wazungu mapenzi nje ya ndoa ni ya asili zaidi kuliko mapenzi ndani ya ndoa ya kizungu.

Mahari ni mfano unaoonyesha kuwa mwanaume na mwanamke wameumbwa kwa vipaji tofauti na sheria ya maumbile imewapangia haki za asili zisizofanana.