read

Mahari Na Matunzo –II

Katika sura hii tumeelezea falsafa na asili ya mahari. Tumeonyesha kuwa sheria ya maumbile imeweka mahusiano kati ya jinsia hizi mbili na imeweka majukumu tofauti ya watu wa jinsia hizi mbili katika maisha. Ilionyeshwa pia kuwa mahari ilitokana na hisia za upendo na upole wa mwanaume, na sio kutokana na hisia zake za kutawala na ukatili. jukumu la mwanamke katika jambo hili limetokana na utambuzi wake wa pekee wa kujizuia, (yaani kujizuia kujitoa kirahisi kwa mwanaume) na sio kwa sababu ya udhaifu wowote au kutokuwa na uwezo wowote.

Malipo ya mahari ni zana iliyoamuriwa na sheria ya maumbile ili kuonyesha thamani ya mwanamke. Thamani yake ya kimaadili ni kubwa sana kuliko thamani yake ya kimwili.

Mila Za Kabla Ya Uislamu Ziliondolewa Na Uislamu.

Qur’ani iliondoa mila nyingi za Waarabu zilizokuwepo kabla ya Uislamu zilizokuwa zikihusiana na mahari, na ikairejesha mahari katika nafasi yake ya asili na inayostahili.

Katika kipindi cha kabla ya Uislamu wazazi walifkiri kuwa mahari ni mali yao wanayopewa kama hadiya ya taabu walizopata katika kumlea na kumkuza msichana. Imetajwa katika Kashshaf (Tafsiri ya Qur’ani inayosikifa sana) n.k kuwa pindi msichana alipozaliwa na mtu alipotoka kumpongeza baba wa msichana huyo basi alitoa pongezi hizo kwa kusema, “Mkoba huu unaonukia uzuri uwe na manufaa kwako”, msemo wenye maana, “Mungu ajalie umuozeshe na upokee mahari yake”.

Katika kipindi cha kabla ya Uislamu, akina baba au kama wao hawakuwepo makaka, kama walinzi na walezi wa asili wa msichana walimuozesha kwa mwanaume waliyemtaka wao sio ambaye msichana mwenyewe alimtaka. Na wakati huo huo waliona mahari yake kuwa ni mali yao.

Wakati mwingine walibadilishana mabinti. Mwanaume alikuwa akimtoa binti yake au dada yake na kumpa mwanaume mwingine kwa matarajio ya yeye pia kupewa binti au dada wa huyo ambaye yeye amemuozesha. Katika ndoa ya aina hii iliyokuwa ikiitwa ndoa ya Shighar, waolewaji wote wawili walikuwa hawapokei mahari yoyote. Uislamu ulipiga marufuku aina hii ya ndoa. Mtukufu Mtume alisema; “Hakuna Shighar (kubadilishana mabinti au akina dada) katika Uislamu.”

Kwa mujibu wa desturi ya Kiislamu, sio tu kwamba baba hapaswi kudai chochote katika sehemu ya mahari ya binti yake, lakini pia hairuhusiwi kuingiza katika mkataba wa ndoa sharti la kwamba mbali na mahari, malipo mengine ya ziada yatalipwa kwa baba wa binti. Kwa maneno mengine, baba haruhusiwi kunufaika kifedha kwa namna yeyote kutokana na ndoa ya binti yake.

Uislamu pia ulipiga marufuku mila ambayo ilimlazimisha muoaji kufanya kazi kwa baba mkwe mtarajiwa kama mahari katika kipindi ambacho kulikuwa hakuna fedha. Mila hii haikuja tu kuwepo kwa sababu mababa walitaka kunufaika kupitia kwa mabinti zao. Kulikuwa na sababu nyingine pia, ambazo zilikuwa ndio ada ya zama hizo ambazo kiumuhimu hazikuwa za uonevu. Hata hivyo, hakuna shaka yeyote juu ya kuwepo kwa mila hii katika zama za kale.

Kisa cha Musa na Shu’aib, kilichosimuliwa katika Qur’ani kinaonyesha kuwepo kwa mila hiyo. (Nabii) Musa alipokuwa akitoroka kutoka Misri, alipofika katika kisima cha Madyan aliwahurumia binti zake Shuayb, waliokuwa wamesimama pembeni na kondoo zao na hakuna aliyekuwa akiwajali. Musa aliwachotea maji. Wasichana wale walimsimulia baba yao kisa hicho (cha kusaidiwa na Nabii Musa) na baba yao alimtuma mmoja wao kwenda kumwita Musa nyumbani kwake.

Baada ya kujitambulisha, Shuaib alimwambia Musa; “Ningependa nikuozeshe binti yangu mmoja kwa sharti kwamba utanifanyia kazi kwa miaka minane. Ukipenda unaweza kunifanyia kwa miaka miwili zaidi na hivyo jumla kuwa miaka kumi.” Musa aliikubali pendekezo hilo na akawa mkwe wa Shuaib. Mila hiyo ndio ilikuwa utamaduni wa zama hizo.

Kulikuwa na sababu mbili zilizosababisha mila hii. Kwanza, fedha hazikuwepo wakati huo na huduma pekee ambayo bwana harusi angeweza kuitoa kwa mke wake au baba mkwe wake ilikuwa ni kuwafanyia kazi. Sababu ya pili ilikuwa ni kuwepo kwa mila ya mahari. Wanasosholojia wanaamini kuwa mila ya kumpa baba (mkwe) mahari ni moja ya desturi ya zamani sana. Ili kutoa mahari, imma baba mkwe alimpa muoaji kazi za kufanya au alichukua fedha kutoka kwake. Kimsingi alichokichukua kutoka kwa mume wa binti yake ilikuwa ni kwa ajili ya manufaa ya binti yake.

Hata hivyo, tayari Uislamu umeshapiga marufuku mila hiyo, na sasa baba wa mwanamke hapaswi kudai chochote katika mahari ya binti yake, hata kama anataka aitumie kwa ajili ya binti yake. Ni mwanamke mwenyewe tu ndiye mwenye haki ya kuitumia apendavyo.

Katika zama za kabla ya Uislamu, kulikuwepo mila nyingine pia, ambazo kimsingi zilimnyima mwanamke mahari yake. Moja ya mila hizo ilikuwa ni kurithi haki za unyumba. Ilikuwa mwanaume akifa, mtoto wake wa kiume au kaka yake alirithi haki za unyumba (yaani alimrithi mke wa marehemu) pamoja na mali za marehemu. Mtoto au kaka wa marehemu alikuwa na haki ya ama kumuozesha mjane kwa mwanaume mwingine na mahari kuichukua yeye au yeye mwenyewe kujitangaza kuwa ni mume wa mjane tena kwa kutumia mahari ile ile aliyoitoa marehemu.

Qur’ani Tukufu ilipiga marufuku mila hii pia. Inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَنْ تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا ۖ

“Enyi mlioamini! Sio halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu.” (Suratul Nisaa; 4:19).

Katika Aya nyingine, Qur’ani Tukufu imepiga marufuku kabisa ndoa ya kumuoa mke wa baba (mama wa kambo) hata kama ataridhia. Qur’ani inasema;

وَلَا تَنْكِحُوا مَا نَكَحَ آبَاؤُكُمْ مِنَ النِّسَاءِ

“Msiwaoe wanawake waliopata kuolewa na baba zenu.” (Suratul Nisa; 4:22).

Qur’ani Tu kufu ilipiga marufuku mila zote zilizomnyima mwanamke mahari yake. Moja ya mila hizo ilikuwa ni kwamba mwanaume alipomchoka mke wake, alimtesa kwa matarajio kuwa mwanamke huyo atakubali kupewa talaka kwa sharti la kurudisha mahari yote au nusu aliyopewa. Qur’ani Tukufu inasema;

وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ

“Wala msiwazuie wanawake kuolewa ili mpate kuchukua sehemu ya yale mliyowapatia.” (Suratul Nisaa, 4:19)

Mila nyingine mbaya ilikuwa mwanaume alimuoa mwanamke na hata kulipa mahari kubwa, lakini baada ya kumchoka alikuwa akimchafulia jina lake, kwa kumshutumu kwa uzinifu na kudai arudishiwe mahari yake. Mila hii pia ilipigwa marufuku na Uislamu.

Uislamu Una Mfumo Wake Wa Mahari.

Ni kanuni ya Uislamu isiyo na ubishi wowote kuwa mwanaume hana haki yoyote juu ya mali au fedha ya mke wake, wala hana haki ya kumlazimisha kumfanyia chochote. Mapato ya mke anayefanya kazi hayawezi kutumiwa na mume wake bila ruhusa yake ( ya mke). Katika hili hakuna tofauti kati ya mwanaume na mwanamke.

Kinyume na mila ya kikristo iliyoenea huko Ulaya hadi mwanzoni mwa karne ya 20, mwanamke kwa mtazamo wa Uislamu, hayuko chini ya udhibiti wa mume wake katika masuala ya kifedha. Ana uhuru kamili na fedha zake. Ingawa Uislamu umempa mwanamke uhuru kamili wa kiuchumi na umezuia mume wake asimuingilie mke wake katika mali zake bado umebakisha mfumo wa mahari. Hii inaonyesha kuwa kwa mtazamo wa Uislamu mahari hailipwi kwa mwanamke ili mwanaume aje kunufaika na nishati yake ya mwili au kumnyonya kiuchumi. Uislamu una mfumo wake wa mahari, ambao hautakiwi kuchanganywa na mfumo mwingine wowote. Vipingamizi vinavyotolewa dhidi ya mifumo mingine, havina mwanya wowote katika mfumo wa Kiislamu.

Kama ilivyoelezwa katika sura hii, Qur’ani Tukufu imelezea mahari kama, ‘hadiya.’ Kwa mujibu wa Qur’ani, mahari ni wajibu (lazima).

Qur’ani imezingatia kwa uangalifu tabia zote za maumbile ya mwanadamu, na ili kuhakikisha kuwa si mwanaume wala mwanamke anayepewa nafasi ya kusahau majukumu na mchango wao wa asili, imehimiza umuhimu wa kupanga mahari. Mchango au jukumu la mwanamke ni kuitikia penzi la mwanaume. Ni vizuri ikiwa atampenda mwanaume lakini upendo wake unatakiwa kuwa ni mwitikio wa hatua za mwanzo zilizochkuliwa na mwanaume. Ikiwa atampenda mwanaume ambaye tangiapo hampendi, basi atakumbana na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kushindwa kulimiliki pendo hilo na hili litakuwa ni pigo kubwa sana kwa haiba yake. Lakini ikiwa upendo wake ni mwitikio wa upendo wa mwanaume, hapa kunakuwa hakuna suala la kushindwa au pigo kwa haiba yake.

Je, ni kweli kwamba mwanamke sio mwaminifu, kwamba hana msimamo katika penzi lake, na kwamba hawezi kutumainiwa? Ni kweli na pia sio kweli. Ni kweli kama atakayelianzisha penzi ni mwanamke. Kama yeye ndio wa kwanza kuanguka katika penzi, basi hilo sio la kuaminika. Muda si mrefu atapoteza penzi lake. Lakini sio kweli ikiwa penzi la mwanamke ni mwitikio wa penzi la dhati la mwanaume, katika hali hii, penzi halielekei kudumaa, isipokuwa kama mwanaume mwenywe atapoteza penzi lake kwa mwanamke huyo. Hapo ndio penzi litadumaa. Hili ndio penzi la asili la mwanamke.

Ni kutokana na penzi la aina ya kwanza ambapo mwanamke anabobea katika kutokuwa mwaminifu, na ni kutokana na aina ya pili ya penzi ambalo amepewa katika uaminifu. Ikiwa jamii inataka uimara wa familia, basi haina budi kuifuata Qur’ani ambayo imeweka kanuni tofauti kwa mwanaume na mwanamke. Sheria ya mahari inaafikiana na maumbile, kwa sababu ni ishara kwamba penzi lilianzishwa na mwanaume, na mwanamke aliitikia tu. Mwanaume hutoa zawadi kama ishara ya upendo na heshima kwa mwanamke. Hivyo sio jambo la maana kuifuta sheria hii ambayo huunda sehemu muhimu ya sheria iliyoundwa na maumbile yenyewe.

Kama tulivyoona, Qur’ani Tukufu ilipiga marufuku mila nyingi zilizokuwepo kabla ya Uislamu pamoja na desturi zilizokuwa zinahusiana na mahari, ingawa watu wa zama hizo walikuwa wamezizoea sana. Qur’ani ilichokiamrisha ni tofauti na mila zilizokuwepo katika siku hizo. Hivyo haiwezi ikadaiwa kuwa Qur’ani haijasisitiza kuwepo au kutokuwepo kwa mahari. Ingeweza kuwa ilipiga marufuku kabisa suala la mahari lakini haikuona kuwa ni jambo la busara kufanya hivyo.

Ukosoaji Wa Wanaopinga Kuwepo Kwa Mahari

Sasa baada ya kuona maoni ya Uislamu juu ya mahari, hebu tuangalie ukosoaji unaotolewa na wale wanaopinga sheria hii ya Uislamu.

Mkosoaji mmoja anasema; “Kama ilivyo kwa mtu anavyotumia fedha kupata bustani, nyumba, au farasi, halikadhalika fedha lazima itumike katika kumnunua mwanamke. Na kama ilivyo kuwa bei ya nyumba, bustani au farasi hutegemea ukubwa, uzuri na ubora wa matumizi yake halikadhalika bei ya mwanamke hutegemea uzuri au ubaya wake na mali au umasikini wake. Hio ndio falsafa ya mahari. Hakuna unyumba bila kutoa pesa na kutoa kulipa bei ya manunuzi.”

Kama ingekuwa ni mila ya Kimagharibi, je, watu wangezusha fitna za chuki dhidi yake? Ikiwa mtu mmoja atampa pesa mtu mwingine, je, hii ina maana kuwa amemnunua? Je mila ya kupeana zawadi ipigwe marufuku? Qur’ani inaeleza wazi wazi kuwa mahari si chochote zaidi ya zawadi. Na zaidi ya hili Qur’ani imeweka sheria za uchumi ambazo haziruhusu mwanaume kumnyonya mwanamke kiuchumi.

Unaweza kusema kuwa wanaume wengi wa Asia wanawanyonya wake zao kiuchumi. Hilo tunakubali. Lakini hakutokani na mahari. Wanaume hawa hawasemi kuwa wanafanya hivyo kwa kuwa waliwalipia wake zao mahari. Kuna sababu nyingine zilizosababisha kuwa mara nyingi wanaume wanawatawala wanawake. Kwanini sheria ya maumbile ichafuliwe badala ya kuwabadilisha wanaume wanaohusika? Lengo kuu la hoja zote hizi ni kuwafanya watu wa Mashariki wasahau falsafa yao ya maisha na kanuni za kibinadamu, ili waweze kumezwa kirahisi na wageni.

Mkosoaji huyu anaendelea kusema kuwa; “Ikiwa kuna usawa kamili wa kiuchumi kati ya mwanaume na mwanamke, hakuna sababu kwanini mwanaume ashikwe shati kumtunza mke wake na kumpatia chakula, mavazi na mahari. Hapa mwanamke analipwa mara mbili, jambo ambalo mwanaume hajawahi kufikiriwa kufanyiwa.”

Tukiichambua hoja hii kwa uangalifu, tutaona inamaanisha kuwa katika kipindi ambapo mwanamke hakuwa na haki ya kumiliki mali na hakuwa na uhuru wa kiuchumi, mahari na matunzo vilihalalishwa kwa kiasi fulani. Lakini katika hali ambazo mwanamke amepewa uhuru wa kiuchumi, kama Uislamu ulivyompa, hakuna uhalali wa kumtunza na kumpa mahari.

Mkosoaji huyu anaonekana kuwa na imani potofu kuwa mahari ilikuwa ikilipwa ili kufidia dhulma ya kiuchumi aliyokuwa akifanyiwa mwanamke. Ukweli ni kinyume chake. Tukiitazama Qur’ani falsafa halisi ya mahari inaweza kuthibitika.

Mkosoaji mwingine ameandika; “Kwa vile mwanaume na mwanamke wameumbwa sawa, mmoja kumlipia gharama au kumpa marupurupu mwingine hakuna sababu ya kiakili. Kama ilivyo mwanaume anavyomhitaji mwanamke, halikadhalika ndivyo mwanamke anavyomhitaji mwanaume. Hivyo katika hili wote wawili wanahitajiana. Hivyo itakuwa sio haki kumuamrisha mmoja wao kulipa gharama za mwenzake. Lakini kwa vile mwanaume alikuwa na haki ya kutoa talaka na mwanamke hakuwa na uhakika wa kuishi na mwanaume huyo kama mume wake katika uhai wake wote, hivyo alipewa haki ya kudai aina fulani ya usalama (kinga) kutoka kwa mwanaume.”

Anaongeza kuwa; “Katika mazingira ambapo mwanaume hana haki kabisa kutoa talaka, basi hakuna uhalali kabisa wa kuendelea kwa desturi hii.”

Ni dhahiri kuwa kutokana na tulivyoyasema hoja hizi hazina msingi wowote. Mahari sio bei wala mshahara. Hapana shaka kwamba mwanaume na mwanamke wanahitajiana, lakini nafasi zao hazifanani. Maumbile yamewaweka katika nafasi tofauti.

Pia ni upuuzi kuielezea mahari kuwa ni kinga ya kifedha dhidi ya haki ya talaka, na juu ya hilo, kudai kuwa hii ndio sababu iliyoufanya Uislamu uiamrishe, ni kilele cha upuuzi. Tungependa kuwauliza watu hao kuwa kwanini awali Uislamu ulimpa mwanaume haki ya kutoa talaka? Kama haki hii ya talaka isingekuwepo je kusingekuwa na haja ya usalama (kinga)? Na zaidi ya haya sentensi hii ina maana kuwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alipopanga mahari kwa ajili ya wake zake wenyewe, alikuwa na nia ya kuwapa kinga dhidi yake mwenyewe. Halikadhalika alipopanga mahari ya Bibi Fatima wakati wa ndoa yake kwa Imam Ali alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuweka kinga kwa bibi Fatima dhidi ya Imam Ali.

Ikiwa, kwa ajili ya kujenga hoja tu, tutakubali kuwa mahari ni aina ya kinga, sasa swali linaloibuka ni kuwa, kwa nini Mtume (s.a.w.w.) aliwashauri wanawake kusamehe mahari yao kwa waume zao kama ishara ya wema. Kwa nini alikielezea kitendo hicho kuwa ni cha heri na kina thawabu nyingi? Kwa nini alihimiza kuwa mahari iwe ndogo kwa kadiri inavyowezekana? Je hii haionyeshi kuwa Mtume aliichukulia mahari kuwa ni zawadi na alichukulia kuwa kuisamehe ilikuwa ni njia ya kuimarisha mapenzi baina ya mume na mke?

Kama Uislamu uliitazama mahari kuwa ni kinga, kwa nini basi Qur’ani inasema, “Wapeni wanawake mahari yao kama hadiya; kwa nini haikusema wapeni wanawake mahari yao kama kinga.”

Aidha, inaonekana kuwa mkosoaji huyu ana imani potofu kuwa, katika siku za awali za Uislamu, mahari ilikuwa na muundo sawa na wa sasa. Hivi sasa utaratibu uliozoeleka ni kuwa hulipa kiasi fulani cha mahari, lakini mke huwa hapati mahari yote, isipokuwa kunapokuwa na ubishani. Aina hii ya mahari huchukua sura ya kinga. Lakini katika kipindi cha awali cha Uislamu, utaratibu ulikuwa ni kulipa fedha ya mahari yote iliyokubaliwa. Katika mazingira haya haiwezi kudaiwa kuwa mahari ni mfumo fulani wa kinga.

Historia inaonyesha kuwa Mtume Mtukufu hakuwa akikubali kufungisha ndoa yoyote bila mahari kupangwa. Kisa kifuatacho kilichotajwa katika vitabu vya Shia na Sunni ni mfano wa desturi ya Mtume:
Mwanamke alikuja kwa Mtume akasema; “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Nikubali niwe mke wako.” Mtume Mtukufu alinyamaza kimya na hakusema kitu. Mwanamke alikaa chini.

Mmoja wa masahaba wa Mtume aliinuka na kusema; “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Kama hauko tayari, mimi niko tayari kumuoa.” Mtume akauliza ni mahari gani utakayotoa?” “Sina kitu.” Mtume akasema: “hiyo haitafaa. Nenda nyumbani kwako. Labda unaweza kupata kitu cha kumpa mwanamke huyu kama mahari yake. Mwanamume yule alienda kwenye nyumba yake. Mara akarudi na kusema; “Sikupata chochote.” Mtume akasema nenda tena ukatafute, hata pete ya chuma itafaa.”

Mwanaume yule alienda tena. Alirudi na kusema kuwa hakuweza kupata pete ya chuma. Alisema kuwa alikuwa tayari kutoa nguo alizovaa kama mahari kwa mwanamke yule.

Mmoja wa masahaba wa Mtume, aliyekuwa akimjua mtu huyo vizuri, alisema kuwa anafahamu kuwa mtu huyo alikuwa hana nguo nyingine. Hivyo alimuomba Mtume ampangie zile zile nguo alizovaa ndio ziwe mahari ya mwanamke huyo.

Mtume alisema; “Ikiwa nusu ya nguo zake zitapangwa kuwa mahari nani atakayezivaa? Yeyote kati ya hawa wawili atakayevaa nguo hizi atamuacha mwenzake bila nguo. Hilo haliwezekani.”

Mchumbiaji alikuwa amekaa kwenye sehemu yake. Mwanamke pia alikuwa akisubiri uamuzi wa mwisho. Wakati huo, Mtume na masahaba wake wengine walikuwa wamejishughulisha katika kuzungumza juu ya jambo jingine. Muda mrefu ulipopita, mwanaume yule aliinuka ili aondoke. Mtukufu Mtume alimwita kwa kumwambia, “‘Njoo hapa’ Akaja.

Mtume akamuliza “Unaikumbuka Qur’ani? “Ndiyo ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu!” Ninaikumbuka sura hii na ile.” “Je unaweza kuzisoma kutoka kichwani (bila kitabu)?” “Ndiyo, ninaweza” Mtume akasema; “Vizuri sana. Sasa ni sawa. Ninakuozesha mwanamke huyu na mahari yake ni kuwa umfundishe Qur’ani.”

Mwanaume yule aliushika mkono wa mwanamke yule na wote wawili wakaondoka!

Kuna nukta nyingine, pia zinazohusiana na suala la mahari kwa sasa tunaziacha.