read

Mirathi

Zama za kale mwanamke alikuwa harithi kitu na, hata aliporithi, alitendewa kama mtoto. Alikuwa hana haiba ya kisheria inayojitegemea. Kwa mujibu wa baadhi ya mifumo ya kisheria ya kale, mtoto wa kike alipata urithi lakini watoto wake hawakupata. Kwa upande mwingine, mtoto wa kiume sio tu anapata urithi yeye mwenyewe, bali pia watoto wake walirithi mali iliyoachwa na mababu zao. Baadhi ya mifumo mingine ya sheria ilimruhusu mwanamke kurithi lakini si kwa kupata asilimia maalum au kwa lugha ya Qur’ani ‘gawio lililopangwa.’ Walichokifanya ilikuwa ni kumruhusu mzazi kuusia kuwa apewe, kama muusiaji anataka.

Wanahistoria na wachunguzi wameeleza kwa kina aina mbali mbali za sheria zilizokuwepo kale, lakini kwa sasa hatutaki kwenda kwa undani zaidi. Kwa sasa ufupisho tulioueleza hapo juu unatosha.

Kwa Nini Mwanamke Alinyimwa Urithi?

Sababu kuu ya kumnyima mwanamke urithi ilikuwa ni kuzuia kuhama kwa mali kutoka familia moja kwenda nyingine. Kwa mujibu ya imani za kale, mchango wa mwanamke katika uzazi haukuwa wa thamani sana. Akina mama walitumika kama mifuko tu ambamo mbegu ya baba ilikua na kuwa mtoto. Kwa sababu hii waliamini kuwa watoto wa mtoto wa kiume walikuwa sehemu ya familia lakini watoto wa mtoto wa kike hawakuwa sehemu ya familia yake, kwa vile walikuwa sehemu ya familia ya babu yao mzaa baba. Hivyo kama binti angepata urithi, hiyo ingemaanisha kuhamisha mali kwenda kwa watoto wake (binti), watoto ambao hawahusiani na familia ya marehemu.

Marehemu Dr. Musa Ameed anasema kuwa katika siku za kale dini na sio mahusiano mengine yoyote ya asili, ndio ilikuwa msingi wa uundwaji wa familia. Babu, mbali na kuwa mkuu wa kijamii wa watoto na wajukuu wake, pia alikuwa mkuu wao wa kidini. Utekelezaji wa sherehe za kidini na matendo ya ibada yalikabidhiwa kwa kizazi kinachofuatia kupitia kwa watoto wa kiume tu. Wahenga waliwaona wanaume peke yao kuwa ndiyo njia ya kuhifadhi na kuendeleza kizazi. Baba wa familia mbali na kumpa maisha mwanaye wa kiume, pia alimkabidhi imani na matendo ya kidini. Kwa mujibu wa Maveda wa Kihindi na Wagiriki na sheria za kirumi, nguvu ya kizazi ilikuwa kwa wanaume tu, na hivyo dini za familia zilikuwa ni miliki ya wanaume pekee, na wanawake hawakuwa na usemi wowote isipokuwa kupitia kwa baba zao au waume zao. Kwa vile hawakuweza kushiriki katika utekelezaji wa sherehe na shughuli za kidini, basi walikosa faida na manufaa yote ya kifamilia. Hivyo mfumo wa urithi ulipokuja wanawake walitengwa.

Kutengwa kwa wanawake katika urithi kulikuwa na sababu nyingine pia, mojawapo ikiwa ni kuwa hawakuwa wakakamavu vya kutosha kuwa askari. Katika jamii ambazo ziliweka umuhimu mkubwa katika matendo ya kishujaa na nguvu ya kupigana, na mpiganaji alionekana kuwa bora kuliko watu laki moja wasio wapiganaji, mwanamke alinyimwa urithi kwa vile hakuwa na uwezo wa kupigana.

Kwa sababu hii, Waarabu wa zama za kabla ya Uislamu, walikuwa hawakubali suala la mwanamke kurithi mali, maadamu kulikuwepo wanafamilia wa kiume hata kama kiukoo walikuwa ni ndugu wa mbali. Hii ndio sababu walishangazwa sana Qur’ani iliposema wazi wazi kuwa;

لِلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِمَّا اكْتَسَبُوا ۖ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِمَّا اكْتَسَبْنَ ۚ

“Wanaume wana sehemu katika kile kinachoachwa na wazazi na ndugu wa karibu, kiwe kikubwa au kidogo gawio lililopangwa.” (Suratul Nisa, 4:32).

Ilipata kutokea wakati fulani ndugu yake na Hasan bin Thabit, mshairi maarufu, alifariki katika siku hizo, huku akiacha mke na binti zake wengi. Binamu zao wa mfumo dume waligawiana mali zote na hawakuwapa chochote mjane na binti zake. Mjane alilalamika kwa Mtume ambaye aliwaita ndugu wa mume. Walisema kuwa mwanamke hakuwa na uwezo wa kubeba silaha na kupigana na adui. Ni wanaume waliojilinda wao na wanawake. Hivyo ni wao tu waliokuwa na haki ya kurithi mali. Walipofikia hapo Mtume akawasomea amri ya Allah, kama ilivyo katika Aya hiyo hapo juu.

Urithi Wa Mtoto Wa Kiume Wa Kupanga.

Waarabu wa kipindi cha kabla ya Uislamu wakati fulani walimfanya mtu fulani kuwa mtoto wao wa kiume wa kupanga. Mtoto huyu wa kupanga kama mtoto halisi, alichukuliwa kuwa mrithi. Mila ya kujipatia watoto wa kupanga ilikuwepo katika mataifa mengine pia kama vile Urumi na Iran. Mtoto wa kiume wa kupanga, kama ilivyo kwa mtoto halisi alikuwa na haki zote ambazo mabinti halisi wa kuzaliwa hawakuwa nazo. Haki hizi zilikuwa ni pamoja na haki ya kurithi. Halikadhalika kumuoa mke wa mtoto wa kupanga hakukuwa kunaruhusiwa. Qur’ani Tukufu ilipiga marufuku mila hizi.

Urithi Wa Mshirika

Mila nyingine, iliyokuwa ya kawaida miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu ilikuwa ni ile ya ushirika (alliance). Watu ambao hawakuwa na uhusiano wa damu walikula yamini ya undugu kuwa; “Damu yako ni damu yangu, uchokozi wowote dhidi yako utakuwa ni uchokozi dhidi yangu; utarithi mali yangu na mimi nitarithi mali yako.” Kwa mujibu wa ushirika huu, makundi yote yalikuwa yakiwajibika kumlinda mshirika wake katika kipindi chote cha uhai wao, na mmoja wao alipokufa, mshirika aliyebaki alichukua mali za marehemu.

Mke Kama Sehemu Ya Mirathi.

Wakati fulani zama za kabala ya Uislamu, Waarabu walikuwa wakimhesabu mjane kuwa sehemu ya mali ya mume aliyefariki na hivyo, yeye pia alirithiwa. Ikiwa marehemu alikuwa na mtoto wa kiume kutoka kwa mke mwingine, huyo alikuwa na uwezo wa kumrushia mjane kipande cha nguo kama ishara ya kumrithi. Baada ya hapo alikuwa na uhuru wa kumwamulia atakavyo au kumfanya vyovyote apendavyo kwa raha zake. Alikuwa na hiari ya ama kumuoa yeye mwenyewe au kumuozesha kwa mtu mwingine na yeye kuchukua mahari. Mila hii ambayo haikuwepo miongoni mwa Waarabu peke yao ilipigwa marufuku na Qur’ani.

Kuhusiana na suala hili la mirathi katika madaraja mbali mbali, sheria za jamii za kale za Wahindi, Wajapan, Warumi, Wagiriki (wayunani) na Wairani zilikuwa ama haziruhusu wanawake kurithi au zilikuwa zinawabagua (yaani walikuwa wanapewa kidogo sana). Kutokana na uchache wa nafasi hatuwezi kuyaandika hapa yote yaliyoandikwa na wataalamu wa fani hii.

Mila Ya Kuwarithi Wanawake Katika Kipindi Cha Sasania.

Hayati Saeed Nafisi katika kitabu chake, ‘Social History of Iran from the Sasanian times to the end of the Ummayad period’ ameandika kuwa; “Tabia nyingine ya kuvutia au kushangaza ya utamaduni wa Wasasania ilikuwa ya kwamba mvulana alipobaleghe, baba yake alimuozesha mwanae huyo mmoja wa wake zake wengi (wa baba huyo). Katika zama hizo mwanamke hakuwa na haki yoyote ya kisheria. Baba na mume walikuwa na madaraka makubwa sana juu ya mali ya mwanamke.

“Lilikuwa ni jukumu la baba au mkuu wa familia kumuoza binti yake alipofikia umri wa miaka 15. Lakini umri wa kuoa kwa wavulana ulikuwa miaka 20. Baada ya kuolewa binti huyo hakuwa na haki ya kurithi mali ya baba yake au mlezi wake. Hakuwa na haki ya kuchagua mume, lakini alikuwa na hiari ya kufanya ndoa ya haramu ikiwa baba yake alishindwa kumuoza baada ya kuwa amevunja ungo. Katika hali hiyo, pia hakuruhusiwa kurithi chochote kutoka kwa baba yake.

Hapakuwa na kikomo cha idadi ya wanawake ambao mwanaume angeweza kuoa. Kumbukumbu za Wagiriki zinaonyesha kuwa mume alikuwa akimiliki mamia ya wanawake katika nyumba yake. Vitabu vya kidini vya Wazoroastria vinaonyesha kuwa kanuni za ndoa katika zama za Sasania zilikuwa tata na zilizokorogeka.

Urithi Wa Mwanamke Katika Uislamu.

Sheria ya mirathi ya Kiislamu imeepukana na mapungufu yote ya huko nyuma. Kitu kinachopingwa na wale wanaodai kutetea usawa kati ya mwanaume na mwanamke, ni kwamba gawio la mwanamke ni nusu ya gawio la mwanaume. Kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu mtoto wa kiume hupata mara mbili ya mtoto wa kike, kaka hupata mara mbili ya dada yake na mume hupata mara mbili ya kile anachopata mke wake. Gawio la baba na mama ndio halifuati utaratibu huu.

Ikiwa marehemu ana watoto, na wazazi (wa huyo marehemu) wako hai, kila mmoja wa wazazi wawili atapata moja ya sita ya mali iliyoachwa na marehemu. Ni kutokana na nafasi maalum ya mwanamke katika mahari, matunzo, huduma za kijeshi na baadhi ya sheria za jinai ndio maana gawio lake limefanywa kuwa nusu ya lile la mwanaume.

Kwa sababu zilizotajwa hapo awali, Uislamu unachukulia matunzo na mahari kuwa ni mambo muhimu na ya lazima katika kuiimarisha ndoa. Yanatoa hakikisho la maelewano na masikilizano. Kuyaondoa ni kulitikisa jengo zima la familia na kumsukumia mwanamke katika umalaya. Kwa vile mahari na matunzo ni wajibu wa lazima wa mume, basi ni wazi kuwa majukumu ya kifedha ya mwanamke yamepunguzwa sana na mzigo wa mwanaume umeongezwa. Ili kufidia jukumu zito alilonalo mwanaume, gawio lake la urithi limepangwa kuwa mara mbili ya lile la manamke. Ni mahari na matunzo yaliyopunguza gawio la mwanamke.

Pingamizi La Wamagharibi.

Baadhi ya watu wa Magharibi wanapokosoa udogo wa gawio la mwanamke la urithi na wanapolitumia hili kama silaha ya propaganda dhidi ya Uislamu, wanadai kuwa hakuna ulazima wowote wa kupunguza gawio la mwanamke ili kuja kulifidia kwa mahari na matunzo. Je, kuna haja yoyote ya kupita vichochoroni na kuzunguka vichaka? Kwanini gawio la mirathi la mwanamke lisilingane na gawio la mwanaume ili tusilazimike kulifidia kwa mahari na matunzo?

Hawa mabwana ambao wanaonekana kumpenda mfalme kuliko mfalme mwenywe anavyojipenda wamechanganya habari. Sababisho wamelipeka kwenye matokeo na matokeo wameyapeleka kwenye sababisho. Wanafikiri kuwa mahari na matunzo ni matokeo ya nafasi ya pekee kuhusiani na urithi, wakati ambapo ukweli ni kinyume chake.

Aidha, wanaelekea kuwa na mawazo kuwa kipengele cha fedha ndio kitu pekee kinachozingatiwa, kama hiki kingekuwa ndio kigezo pekee basi kusingekuwa na haja ya mfumo wa mahari na matunzo wala mfumo unaotoa tofauti ya gawio kati ya mwanaume na mwanamke.

Kama tulivyoeleza mwanzo, Uislamu umezingatia vipengele vingi, vingine ni vya asili na vingine ni vya kisaikolojia. Umezingatia mahitaji maalumu ya mwanamke, yanayotokana na jukumu lake la uzazi. Kimsingi mwanaume hana mahitaji hayo. Mbali na hayo, kwa upande mwingine, uwezo wa mwanamke wa kuzalisha ni mdogo kuliko wa mwanaume na kwa upande mwingine matumizi yake ni makubwa kuliko ya mwanaume.

Kwa nyongeza, kuna vipengele vingine mbali mbali vya kujirembesha kuhusiana na mfumo wa akili zao. Kwa mfano mwanaume mara zote hupenda kutumia fedha zake kwa ajili ya mwanamke anayempenda. Vipengele vingine vya kisaikolojia na kijamii, vinavyosaidia kuimarisha mahusiano ya kifamilia pia vimezingatiwa. Kwa kuzingatia nukta zote hizi, Uislamu umefanya mahari na matunzo kuwa ni wajibu wa lazima. Hivyo sio suala la pesa, ambalo inaweza kusemwa kwamba kuna haja ya kupunguzwa mgao wa mwanamke sehemu moja na kumfidia sehemu nyingine.

Pingamizi La Waasi Wa Kipindi Cha Awali Cha Uislamu.

Tumesema kuwa mahari na matunzo ni sababisho na nafasi ya pekee ya mwanamke na tofauti zilizopo katika mirathi ni matokea yake. Nukta hii haijaanzishwa leo. Ilikuwepo hata katika siku za awali za Uislamu.

Katika karne ya pili Hijria alikuwepo mtu mmoja aliyeitwa Ibn Abi alAwja, ambaye hakuwa akiamini juu ya dini. Kwa kutumia fursa ya uhuru wa kidini (imani) ya wakati ule alikuwa akielezea waziwazi mawazo yake ya kikafiri. Wakati fulani alikuwa akija katika Masjid alHaram (Makka) au Masjid Nabawi (Madina) na alikuwa akijibizana na wanavyuoni wa wakati ule juu ya kanuni za Uislamu.

Moja ya pingamizi lake dhidi ya Uislamu lilihusu mirathi. Alikuwa akisema; “Ana kosa gani huyu mwanamke maskini anayepata sehemu moja wakati mwanaume anapata sehemu mbili.” Kwa mujibu wake yeye hii ilikuwa ni dhulma kwa mwanamke. Imam Jafar asSadiq (as) katika kumjibu alisema kuwa hali iko hivyo kwa sababu mwanamke amesamehewa kazi za jeshi. Na zaidi ya hilo Uislamu umemuamrisha mwanaume kulipa mahari na kumtunza mkewe na katika baadhi ya kesi za jinai ambapo ndugu wa mhalifu walipaswa kulipa fedha za damu (kufidia mtu aliyeuliwa) mwanamke aliondolewa (alisamehewa) katika malipo hayo. Hizi ndio sababu zilizofanya gawio lake lipunguzwe.

Hivyo Imam Jafar Sadiq (as) alieleza wazi wazi nafasi ya pekee ya mwanamke juu ya mirathi, sheria ya mirathi na matunzo, kusamehewa kwake kutoa huduma ya jeshi na malipo ya fedha za damu.

Maimamu wengine pia walijibu hivyo hivyo walipoulizwa swali hilo.