read

Talaka I

Hakuna zama kama hizi za kwetu ambapo uzingativu umefanywa sana kwenye hatari ya kusambaratika kwa familia na madhara yake. Na tena, hakuna zama kama hizi za kwetu ambapo mtu amekabiliana na hatari halisi ya kusambaratika huko.

Kuongezeka Kwa Talaka Katika Maisha Ya Kisasa.

Huko nyuma uzingativu sana haukuwekwa katika tatizo la talaka, sababu zake na madhara yake pamoja na mbinu za kulizuia vilikuwa havijadiliwi sana na bado idadi ya talaka ilikuwa ndogo sana. Hakuna shaka kuwa ongezeko la talaka hivi sasa ikilinganishwa na zamani linatokana na kuongezeka kwa sababu za talaka. Maisha ya kijamii yamebadilika mno kiasi cha kuwa sasa kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kuvurugika kwa familia, na hii ndio sababu jitihada za wasomi na watu wanaoshughulikia masuala ya kijamii zimeshindwa kuzaa matunda. Inasikitisha kuwa kizazi kijacho kinakubaliwa na hatari zaidi.

Gazeti la Kimarekani, ‘Newsweek’ katika makala inayovutia yenye kichwa cha habari ‘Divorce in America’ (Talaka katika Marekani) linaandika kuwa ukiwa Marekani ni rahisi zaidi kupata talaka kuliko kupata taksii.

‘Newsweek’ linaandika zaidi kuwa methali mbili kuhusu talaka zinajulikana zaidi miongoni mwa Wamarekani kuliko methali nyingine zozote zile. Mojawapo ni kuwa ‘Usuluhishi mgumu kabisa kati ya mume na mke ni bora kuliko talaka.’ Methali hii ina umri wa miaka 400 na zaidi.

Ya pili ambayo imebeba ujumbe ulio kinyume na hii methali ya kwanza imepata umaarufu katika nusu ya pili ya karne ya 20. Inasema kuwa ‘penzi la pili ni tamu zaidi kuliko la kwanza.”

Makala inaonyesha kuwa methali ya pili ndiyo inayofanya kazi zaidi nchini Marekani. Jinamizi la talaka linajivutia kwake, sio kwa ndoa mpya tu, bali hata za mama zao na za wanandoa waliooana zamani huko. Tangu wakati wa Vita vya pili vya Dunia na kuendelea, kwa wastani idadi ya talaka kwa mwaka si chini ya laki nne (400,000). Katika hizo ndoa zilizovunjika, 40% zilikuwa zimeweza kudumu kwa miaka kumi na zaidi na 13% ndizo zilikuwa zimeweza kudumu kwa zaidi ya miaka 20. Wastani wa umri wa talaka (umri wa wanawake wanaotalikiwa) wa wanawake milioni mbili ilikuwa ni miaka 45, 62% ya hao walikuwa na watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 wakati ndoa ilipokuwa inavunjika. Wanawake hawa, kwa kusema kweli, wanaunda kizazi maalum.

Ingawa mwanamke wa Kimarekani hujisikia huru kabisa baada ya talaka, lakini bado hao waliotalikiwa, wawe vijana au wa umri wa kati, huwa hawana furaha. Kutokuwa kwao na furaha kunaweza kupimwa kutokana na ongezeko la idadi ya wanawake wanaowaita madaktari wa akili au ambao ni walevi wa kupindukia.

Katika kila wanawake wanne, mmoja ni mlevi. Idadi ya wanawake waliotalikiwa wanaojinyonga ni kubwa mara tatu kuliko ya wale wenye waume. Kwa kifupi ni kuwa mara tu mwanamke anapoibuka mshindi katika mahakama ya talaka hugundua kuwa maisha baada ya talaka sio kitanda cha maua ya waridi. Ni vigumu ulimwengu kuwa na maoni mazuri juu ya mwanamke anayeivunja ndoa yake, nyumba thabiti kabisa ya mahusiano ya mwanadamu. Jamii inaweza kumheshimu mwanamke huyo na pengine kumuonea wivu, lakini haiwezi kumuona kuwa ni mtu aliyeingia katika maisha ya mtu na kumletea furaha (mumewe).

Katika makala hii ya gazeti la Newsweek suali limeibuka kuwa ongezeko hili la talaka linalozidi kukua linatokana na mwenendo usio kubaliana kati ya mume na mke, au sababu nyingine. Mwandishi wa makala hii amesema kuwa hata kama tofauti za tabia na kutopatana zitakubaliwa kuwa sababu ya kutengana kwa wanandoa waliooana hivi punde, nini tunaweza kusema juu ya talaka za wanandoa walioishi ndani ya ndoa kwa muda mrefu? Tukizingatia msaada wa kisheria unaotolewa na sheria ya Marekani kuhusiana na talaka, tunaweza kusema kuwa kutofautiana kwa mihemko na tabia sio sababu ya kutengana kwa wanandoa walioishi kwa miaka kumi au zaidi.

Katika zama za vidonge vya kuzuia mimba, mapinduzi ya ngono (ufuska) na kuboreka kwa hadhi yao ya kisheria, wanawake wengi wametokea kuamini kuwa furaha na raha ni bora kuliko uimara wa maisha ya ndoa. Mara nyingi unaweza kuona kuwa mume na mke wanaishi pamoja kwa miaka, wana watoto, kila mmoja anashiriki furaha na huzuni ya mwenzake lakini ghafla mke anaomba talaka bila ya kuwepo mabadiliko yoyote ya kimali au hadhi na makubaliano ya mume. Sababu ni kuwa, mpaka jana, mwanamke alikuwa tayari kuvumilia uchoshi wa maisha, lakini hayuko tayari kufanya hivyo leo.

Ongezeko la kesi za talaka haliko Marekani peke yake. Sehemu yoyote ambayo utamaduni wa Kimagharibi umejipenyeza kwa kiasi fulani, kiwango cha talaka kiko juu. Hata katika nchi za Mashariki, talaka imekuwa ni jambo la kawaida zaidi katika miji mikubwa ya kisasa kuliko katika miji midogo na vijiji.

Mazingira Yanayochangia Talaka Nchini Marekani.

Tayari tumeshalinukuu gazeti la Newsweek likisema kuwa mwanamke wa kimarekani hujali zaidi starehe na burudani kuliko uthabiti na uimara wa maisha ya familia. Sasa hebu tupige hatua moja mbele ili tuone kwanini amechukua mwelekeo huo. Hapana shaka kwamba tabia hii sio ya asili wala ya kuzaliwa nayo. Imetokana na sababu fulani za kijamii. Ni mazingira ya Marekani yaliyosababisha akili hii ya mwanamke wa Kimarekani. Baadhi ya watu wa Magharibi wanafanya jitihada kubwa kumsukumia mwanamke wa Mashariki katika mwenendo wanaoufuata wanawake wa Kimarekani. Kama wakifanikiwa majaaliwa ya mwanamke wa Mashariki na familia ya Mashariki hayatakuwa na tofauti na yale ya mwanamke wa kimarekani na familia ya Kimarekani.

Gazeti maarufu la Ufaranza litolewalo kila siku linaandika kuwa katika migahawa zaidi ya 200 na nyumba za kulala wageni katika jimbo la Califonia, wafanyakazi (wahudumu) wa kike wanavaa nguo za nusu uchi. Nguo hizo ambazo ni za kuogelea zinatambuliwa kuwa ndio sare za kazini katika miji ya SanFransisco na Los Angeles.

Katika jiji la New York kuna kumbi nyingi za sinema zinazoonyesha filamu za ngono tu, na picha za uchi za wanawake zinaweza kuonekana zikionyeshwa mbele ya milango ya kuingilia kumbini. Majina ya filamu za ngono ni ya aina hii; “Wanaume wanaobadilishana wake zao’, ‘Wasichana wasio na maadili,’ ‘Magauni ambayo hayafichi chochote.’ Maktaba kuna vitabu vichache sana vya hadithi za kubuni (fiction books) ambavyo katika majalada yake hakuna picha za wanawake walio uchi.

Majina ya vitabu kama vile ‘Tabia ya ngono ya wanaume wa kimarekani,’ ‘Tabia ya ngono ya wanaume wa Kimagharibi,’ Tabia ya ngono ya vijana walio chini ya miaka 20,’ ‘Mbinu mpya za ngono zilizotokana na habari mpya kabisa,” vimekuwa maarufu na vingi mno. Mwandishi wa makala katika gazeti hili la Kifaransa anauliza kwa mshangao na wasiwasi; “Marekani unakwenda wapi?’

Katika mazingira kama haya ikiwa mwanamke wa Kimarekani amepoteza mizania yake na anajali burudani na raha zaidi kuliko uaminifu kwa mume wake na familia, hawezi kulaumiwa. Ni mazingira ya kijamii ambayo yameharibu kila mzizi wa mfumo wa utakatifu wa familia.

Inashangaza kuwa viongozi wa zama zetu wanazipa nguvu na msukumo zaidi sababu zinazosababisha talaka na kusambaratika kwa maisha ya familia na kwa upande mwingine wanapiga mayowe na kelele kuwa kiwango cha talaka kimekuwa kikubwa mno. Hii ni sawa na kumwambia mtu afagie bohari na kuomba asichafue nguo zake.

Nadharia Tano.

Hebu tuangalie, iwapo kimsingi talaka ni nzuri au mbaya. Swali ni je ni jambo zuri kuuacha wazi mlango wa talaka, hata katika hatari ya kusambaratika kwa maisha ya familia? Ikiwa ni jambo zuri basi hakuna tatizo hata kama kiwango cha talaka kitakuwa kikubwa. Na ikiwa sio jambo zuri, je talaka ipigwe marufuku kabisa na ndoa ifanywe kuwa ya milele? Wazo la tatu ni kuwa talaka isipigwe marufuku kisheria, kwani katika baadhi ya hali haiepukiki, lakini wakati huo huo jamii ichukue kila hatua inayowezekana kuondosha sababu za mikwaruzano na kutengana kwa mume na mke na hivyo kuwanusuru watoto kukosa familia. Ni dhahiri kuwa sheria peke yake haiwezi kufanya chochote ikiwa jamii yenyewe inazipalilia sababu zinazosababisha talaka.

Ikiwa talaka haifai kupigwa marufuku kabisa, je iruhusiwe katika muundo gani? Je ni nani awe na mamlaka ya kutoa talaka? Mwanaume peke yake, mwanamke peke yake au wote? Na wazo la mwisho ni kuwa je mwanaume na mwanamke wote wafuate taratibu zinazofanana katiksa kutoa au kuomba talaka au kila jinsia iwe na utaratibu wake?

Yote kwa yote, hizi ni nadharia tano zinazohusiana na Talaka:

Talaka inayotolewa bila kikwazo chochote cha kisheria au kimaadili. Hawa ni wale wanaoitazama ndoa kwa mtazamo wa kupata raha tu, ambao hawaipi utakatifu wowote, na ambao hawajali thamani ya kijamii ya familia. Wanafikiri kuwa mara tu baada ya ndoa kuvunjika na ndoa mpya kuchukua nafasi ya ndoa ya zamani (iliyovunjilka) wanaume na wanawake walioachana hupata furaha zaidi. Yule anayesema kuwa penzi la pili ni tamu kuliko penzi la kwanza ndiye huiunga mkono nadharia hii. Katika nadharia hii, sio tu kwamba thamani ya kijamii ya kifamilia imesahauliwa lakini pia furaha na kuridhishana kunakosababishwa na ndoa kumepuuzwa pia. Hivyo nadharia hii ni ya kipuuzi na ya kitoto kabisa.

Ndoa ni taasisi takatifu. Ni muungano wa mioyo na roho, taasisi ambayo lazima itunzwe kwa usalama na isiharibiwe. Neno talaka linapaswa kuondolewa kutoka katika kamusi ya jamii ya wanaadamu. Mwanaume na mwanamke wanaooana lazima wajue kuwa hakuna kitakachowatenganisha zaidi ya kifo.

Hii ndio nadharia ambayo imekuwa ikitetewa na Kanisa Katoliki kwa karne nyingi na bado inatetewa.

Wanaoiunga mkono nadharia hii wanazidi kupungua dunaini. Hivi sasa ni Italia na Hispania tu wanoifuata. Ni mara nyingi tu tunasikia kwamba, hata Italia, wanaume na wanawake wanaipinga sheria hii na jitihada zinafanyika ili sheria ya talaka itambuliwe rasmi. Watu wengi hawako tayari kuendelea kutaabika na michosho ya ndoa zao zisizo na mafanikio.

Miaka kadhaa huko nyuma, gazeti la ‘The Daily Express’ lilichapisha makala yenye kichwa cha habari, ‘Ndoa Italia ina maana kifungo kwa mwanamke.’ Makala hii ilisema kuwa, hivi sasa kutokana na kutokuwepo kwa talaka, watu wa Italia wanajiingiza katika mahusiano ya haramu (zinaa). Zaidi ya Waitalia milioni tano walikuwa wakiamini kuwa maisha yao yamejaa madhambi.

Gazeti la Italia litolewalo kila siku liliandika kuwa kuzuia talaka kumesababisha tatizo kubwa sana kwa Waitalia. Wengi wao walilazimika kuukana uraia wa Italia kwa sababu hiyo. Taasisi fulani ya Italia ilipoitisha kura ya maoni, 97% ya wanawake wa Italia walijibu ‘hapana’ kwa swali lililoulizwa kuwa iwapo talaka ilikuwa ni jambo linalochukiza katika kanuni za dini.

Bado kanisa linashikilia msimamo wake na kuendelea kutoa hoja kuutetea (msimamo huo).

Hapana shaka yeyote kuwa ndoa ni taasisi takatifu na inatakiwa idumu. Lakini inaweza tu kudumu iwapo wanandoa wote wawili wanashirikiana. Kuna hali ambapo maelewano kati ya mke na mume huwa hayawezekani. Katika hali kama hizi nguvu za sheria haziwezi kuwapatanisha na kuwaunganisha kwa jina la muungano wa ndoa. Nadharia ya kanisa imeshindwa kabisa kufanya kazi. Sio ajabu muda si mrefu kanisa lenyewe likabadilisha msimamo wake. Hivyo hatuhitaji kuijadili nadharia hii zaidi.

Ndoa inaweza kuvunjwa na mwanaume sio mwanamke. Katika ulimwengu wa zamani watu wengi walikuwa na mtazamo huu, lakini sasa hatudhani kuwa una wafuasi. Hivyo hatuhitaji kuijadili pia.

Ndoa ni taasisi takatifu na mfumo wa kifamilia unaheshimika, lakini mlango wa kutoa talaka kwa masharti fulani, uwe wazi kwa wanandoa wote na taratibu za kuvunja ndoa zinapaswa zifanane kwa jinsia zote mbili. Watetezi wa kufanana kwa haki za familia ambao kwa makosa walikuita usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke, wanaiunga mkono nadharia hii. Kwa mujibu wa watu hawa, masharti yanayofanana, mipaka inayofanana na vikwazo vinavyofanana vinapaswa vitumike kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume wakati wa kuvunja ndoa. Wanapinga suluhishi jingine ambalo ni la kidhalimu na linalobagua.

Hapana shaka ndoa ni taasisi takatifu, mfumo wa familia unaheshimika, talaka ni jambo linalochukuza na ni jukumu la jamii kuondoa visababisho vyote vya talaka, lakini bado talaka haiwezi kuzuiwa moja kwa moja na kwamba mamlaka ya kutoa au kuomba talaka yapo kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume. Hata hivyo utaratibu wa kufuatwa katika uvunjaji wa ndoa uwe tofauti kati ya jinsia hizi mbili. Talaka ni moja ya haki zisizofanana (lakini zinazolingana) kati ya mwanaume na mwanamke.

Hii ndio nadharia inayowakilisha maoni ya Uislamu na nchi za Waislamu zinaifuata.