read

Talaka II

Katika zama zetu, talaka imekuwa tatizo la dunia kwani wote wanalinung’unikia na kulilalamikia. Wale ambao sheria zao zinazuia talaka kabisa wanalalamikia kutokuwepo kwa njia ya kuepuka ndoa zisizo na mafanikio. Halikadhalika wale walioruhusu talaka, wanaume na wanawake, wanalalamikia ongezeko la talaka na kuyumba kwa maisha ya familia na madhara yake. Wale waliotoa haki ya kutoa talaka kwa wanaume peke yao, wanaeleza kutoridhishwa kwao na mambo mawili.

Kwanza baadhi ya watu wa ovyo, baada ya miaka ya maisha ya ndoa, ghafla huwataliki wake zao wa zamani ambao wameishi nao katika kipindi bora kabisa cha ujana wao (hao wanawake) kwa sababu tu sasa wanatamani kuwa na mke mpya.

Pili baadhi ya watu wakorofi wanakataa kuwataliki wake zao, na ilhali hakuna uwezekano wowote wa kufikia maelewano na kuendelea na maisha ya ndoa pamoja.

Mara nyingi hutokea kuwa, kwa sababu mbali mbali tofauti kati ya mume na mke hufikia hatua ambayo hakuna uwezekano wowote wa usuluhishi, na kiuhalisia wanatengana. Katika hali hiyo, njia pekee ya maana ni kuvunja uhusiano wao kisheria, uhusiano ambao kiuhalisia tayari umeshavunjika na kumruhusu kila mmoja wao kutafuta mwenzi mpya maishani. Lakini baadhi ya wanaume ili kuwatesa wake zao na kuwanyima haki ya kufurahia unyumba, hukataa kuwataliki wake zao. Wanamuacha mwanamke, kwa mujibu wa Qur’ani, katika hali ya kuning’inia (talaka ya kuangika). Watu hawa wako mbali kabisa na mafundisho ya Uislamu, ingawa wanatumia mamlaka ya sheria ya Kiislamu kwa tabia yao isiyofaa. Mwenendo wao huwapa maoni wale wasiojua Uislamu vyema kuwa hivi ndivyo Uislamu unavyotaka talaka iwe.

Wakosoaji wanauliza kwa kejeli kuwa iwapo ni kweli kwamba Uislamu umeruhusu wanaume kuwatesa wake zao kadri wapendavyo wakati fulani wanawapa talaka na wakati fulani wanaibatilisha na bado wakati huo huo wanajiridhisha mioyoni mwao kuwa wametumia haki yao halali na ya kisheria.

Wakosoaji wanasema kuwa kitendo hiki ni mfano mzuri wa dhuluma na ukatili. Wanauliza: “Kama ni kweli, kama Waislamu wanavyodai kuwa sheria za Kiislamu zimeundwa kwa kuzingatia msingi wa haki na uongofu, je ni hatua gani ambazo Uislamu umechukua kuzuia aina hii ya dhulma?”

Juu ya ukatili na dhulma ya matendo hayo, hakuna shaka yeyote kuwa ni matendo yasiyofaa. Uislamu, kama tutakavyoonyesha hapa, umezingatia hali hii na una njia za kukabiliana na tatizo hili. Swali muhimu ni: ipi njia bora ya kuzuia dhulma na ukatili huu? Je vitendo vya dhulma vinatokana na ubovu wa sheria ya talaka? Au sababu zake zitafutwe sehemu nyingine? Je matendo haya yanaweza kukomeshwa kwa kurekebisha sheria au hatua nyinginezo zinapaswa kuchukuliwa?

Uislamu una njia zake za kutatua matatizo ya kijamii. Baadhi wanafikiri kuwa yanaweza kutatuliwa kwa imma kuunda sheria mpya au kurekebisha zilizopo. Lakini Uislamu unaelewa kuwa sheria ina mipaka yake. Inaweza kufaa tu katika mahusiano makavu ya kimikataba. Lakini katika mahusiano ya hisia za moyo (kama mapenzi), sheria peke yake haiwezi kufanya mambo mengi, na lazima tuangalie hatua nyingine pia.

Kama tutakavyoonyesha baadaye Uislamu unaitumia vyema nguvu ya sheria pale tu ambapo kweli sheria inaweza kufanya kazi. Haujashindwa katika hili.

Talaka Za Aibu/Za Kuumbua.

Kwanza tuliangalie tatizo la talaka za kuumbua na kuaibisha katika zama hizi.

Kimsingi, Uislamu unapinga kabisa talaka. Unataka talaka isiwepo. Umeiruhusu talaka kama njia ya mwisho ambapo kutengana hakuepukiki. Wale wanaoowa wake wapya kila mara na kuwaacha wa zamani, Uislamu unawakana na umewaita kuwa ni maadui wa Mwenyezi Mungu.

Kitabu maarufu cha hadithi, alKafi, kinasimulia kisa kifuatacho;
Mtukufu Mtume alimuuliza mtu mmoja; “Umemfanya nini mke wako?” Akasema “Nimemtaliki,’ Mtume akamuuliza; “Je ulimuona anafanya jambo lolote baya?” “hapana sikuona.” Mwanaume yule alioa tena. Mtume akamuliza, ‘Je umeoa mke mwingine?” “Ndio”

Baada ya muda fulani Mtume akamuuliza tena, “Umemfanya nini mke wako?” Nimemtaliki” Je amefanya kosa lolote?” “Hapana” Mtu yule alioa mara ya tatu. Mtume akamuliza tena kama alikuwa ameoa mke mpya. Akajibu ndio, Baada ya muda fulani Mtume akamuuliza tena, “Umemfanya nini mke wako?”

“Nimemtaliki” “Je amefanya kosa lolote?” “Hapana”.

Mtume akasema kuwa Mwenyezi Mungu hampendi na anamchukia mtu ambaye hubadilisha wake kila mara, na wanawake wanaobadilisha waume kila mara. Watu hao ni maadui wa Mwenyezi Mungu.

Iliripotiwa kwa Mtume kuwa Abu Ayub Ansari alikuwa ameamua kumtaliki mke wake. Mtume alikuwa akimjua mwanamke huyo vizuri. Alijua pia kuwa uamuzi wa Abu Ayub haukuwa na sababu za maana.

Mtume akasema, “Kumtaliki Umme Ayub (mke wa Abu Ayub) ni dhambi kubwa.”

Mtume alisema kuwa Jibril alimuusia mno juu ya kuwatendea wema wanawake mpaka akahisi kuwa hairuhusiwi kumtaliki mwanamke isipokuwa kama amezini.

Imam Ja’far Sadiq (a.s) amesema kuwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) amesema; “Hakuna kitu kinachopendeza kwa Mwenyezi Mungu kama nyumba ambayo ndani yake ndoa inafungwa na hakuna jambo linalochukiza mbele ya Allah kama nyumba ambayo ndani yake talaka inatolewa.”

Imam Ja’afar Sadiq (a.s) pia amesema kuwa neno ‘Talaka’ limetajwa tena na tena katika Qur’ani na maelezo yake ya kina yametolewa kwa sababu Allah anachukia kutengana kwa wanandoa.

AlTabarisi katika kitabu chake “Makarim alAkhlaq” amemnukuu Mtume akisema: “Oeni lakini msitoe talaka kwani talaka huitikisa Arshi ya Mwenyezi Mungu”.

Hadithi kama hizi pia zimo katika vitabu vya Kisunni. Abu Daud katika kitabu chake, Sunan amesimulia kwamba Mtume amesema: “Mwenyezi Mungu hajaruhusu jambo lolote lenye kuchukiza kama talaka.” Kwa maneno mengine, ingawa Allah ameruhusu talaka, bado talaka ndilo jambo analolichukia mno.

Viongozi wakubwa wa kidini (Maimamu) walikuwa wakijiepusha mno kutoa talaka kwa kadri inavyowezekana. Katika maisha yao matukio ya talaka yalikuwa na sababu za msingi sana. Kwa mfano, Imam Baqir (a.s) alimuona mwanamke. Alikuwa akimpenda sana mke huyo, lakini wakati fulani aligundua kuwa mwanamke huyu alikuwa na chuki na uadui mkubwa dhidi ya Imam Ali ibn Abi Talib. Ilimbidi amtaliki.

Alipoulizwa kwa nini alimtaliki na ilhali alikuwa akimpenda sana, Imam alisema kuwa hakutaka kuishi na kaa la moto wa Jahanamu pembeni yake.

Uvumi Usio Na Msingi.

Inafaa kuelezea hapa uvumi usio na msingi uliotungwa na makhalifa wa ukoo wa Abbas. Uvumi huu ulienea mno kiasi cha kuweza kurekodiwa na waandishi mashuhuri katika vitabu vyao. Kwa mujibu wa uvumi huo, Imam Hassan Mujtaba (a.s), mtoto wa Imam Ali ibn Abi Talib (a.s) ni mmoja wa wale waliooa wake wengi na kuwataliki. Uvumi huo ulienezwa karne moja baada ya kufariki kwa Imam. Uvumi huu ulienezwa mno kiasi cha kuwa hata wafuasi wake waliuamini bila kuzingatia ukweli kuwa kitendo hicho cha kuchukiza sio stahili ya Imam Mtukufu na kisingetarajiwa kwake, mtu aliyekuwa akienda Hija kwa miguu, na aligawa nusu ya mali yake kwa maskini zaidi ya mara ishirini.

Kama tunavyojua, tofauti na watoto wa kizazi cha Imam Husayn (a.s) ambao waliongozwa wakati ule na Imam Sadiq (a.s.) watoto wa kizazi cha Imam Hassan (a.s) walishirikiana na Bani Abbas wakati wa kuuangusha utawala wa kiukoo wa Bani Umayya. Awali Bani Abbas walielezea imani na utii wao kwa watoto wa kizazi cha Imam Hassan (a.s), lakini walipofanikiwa kupata madaraka waliwasaliti na wengi wao waliwatenga, ama kwa kuwaua au kwa kuwafunga gerezani.

Katika kuendeleza sera yao hii, Bani Abbas walianzisha kampeni za propaganda dhidi ya kizazi cha Imam Hassan (a.s). Moja ya hila walizozifanya ilikuwa ni kumshutumu babu yake na Imam Hassan ambaye pia ni ami yake na Mtukufu Mtume, Abu Talib (a.s), kuwa hakupata kusilimu na alikufa kafiri. Walitaka kujenga hoja kuwa wao kwa vile ni kizazi cha ami mwingine wa Mtume, aliyekuwa amesilimu, wanastahili zaidi kuwa makhalifa. Ili kufikia lengo lao walitumia fedha nyingi sana na walibuni visa vingi vya uongo.

Idadi kubwa ya Masunni ambao walishawishika na propaganda hizi, bado wanaamini kuwa Abu Talib alikuwa kafiri. Ingawa utafiti wa hivi karibuni kabisa uliofanywa na wanazuoni wa Kissuni umebainisha ukweli wa jambo hili kwa kiasi kikubwa, lakini hata hivyo bado baadhi yao wanatia shaka.

Uzushi mwingine uliozushwa na Bani Abbas, ulikuwa kwamba Imam Hassan (a.s) alirithi ukhalifa baada ya baba yake, lakini kwa vile alikuwa mtu muasherati, hakuweza kutawala vizuri na akalazimika kuusalimisha ukhalifa kwa adui yake makini, Muawiya ambaye alimpatia fedha na kwa kutumia fedha hizo Imam Hassan alijishughulisha na kuoa na kutoa talaka.

Kwa bahati nzuri, utafiti wa wanazuoni wa zama zetu umekiweka wazi chanzo cha uzushi huu. Mtu wa kwanza kutamka uzushi huu alikuwa ni Kadhi (Qazi) aliyeteuliwa na khalifa Mansur aliyemwelekeza kubuni na kusambaza uzushi dhidi ya Imam. Mwanahistoria mmoja, alipokuwa akitoa maoni yake dhidi ya uongo huu, anahoji kuwa ikiwa Imam Hassan (a.s) alioa wanawake wengi kiasi hicho mbona watoto wake hatuwaoni? Kwa nini idadi ya watoto wake ni ndogo? na ilhali tunajua kuwa Imam hakuwa tasa na njia za kuzuia mimba au kutoa mimba hazikuwa mila ya zama hizo?

Tunashangaa wepesi wa kuamini wa baadhi ya wakusanyaji wa hadithi za Kishia. Wanaweza vipi kuandika kuwa Imam Hassan (a.s) alikuwa na tabia ya kutaliki wanawake, wakati wao wenyewe wanaripoti kuwa Mtukufu Mtume na Maimamu wamesema kuwa Allah anaichukua talaka na anamkana mwanaume ambaye ana tabia ya kuwataliki wake zake. Kamwe haikutokea kwa mabwana hawa kuchagua moja katika haya mambo matatu; (i) Talaka si kitu kibaya, (ii) Imam Hassan (a.s) hakuwa na ada ya kuwataliki wakeze au (iii) Imam Hassan (a.s) hakuambatana na mafundisho ya Uislamu. Lakini cha ajabu ni kuwa si tu wanaamini juu ya usahihi wa hadithi inayosema talaka inachukiza mbele ya Allah, lakini pia wakati huo huo, licha ya kuwa wafuasi waaminifu kwa Imam, wananukuu ripoti kuwa, Imam alikuwa na tabia ya kuwataliki wanawake mara kwa mara. Wanaziruka ripoti hizi bila kuzitolea maelezo.

Baadhi ya wanahadith (Muhadithina) wamekwenda mbali zaidi kiasi cha kusimulia kwamba Imam Ali (a.s) hakuwa akifurahia tabia ya mtoto wake. Katika hotuba yake ya hadhara aliwaomba watu wasimuozeshe binti zao kwa vile alikuwa na tabia ya kuwataliki. Lakini inasemekana kuwa watu walijibu kuwa lilikuwa ni jambo la fahari kwao kwamba binti zao walipata kuwa wake za mtoto (mjukuu) wa Mtume hata kwa muda mfupi.

Inaelekea kuwa baadhi ya watu walikuwa na fikra kuwa talaka si jambo baya ikiwa mwanamke mwenyewe na familia yake walikuwa radhi. Wanafikiri kuwa talaka inachukiza tu iwapo upande wa pili haikuridhia, lakini hakuna tatizo kabisa kama mwanamke ameridhia kuishi na mwanaume anayejifaharisha naye kwa siku chache.

Hata hivyo huu sio uhalisia. Ridhaa ya mwanamke au wazazi wake haibatilishi ubaya wa talaka. Talaka inachukiza kwa vile Uislamu unataka ndoa idumu na familia iwe imara. Ridhaa ya wanandoa pia haibadilishi ubaya wa talaka. Uislamu hauioni talaka kuwa inachukiza kwa baadhi tu ya tabaka la wanawake. Ni suala la kanuni.

Tumelijadili suala hili la Imam Hassan (a.s) si tu kwa nia ya kuurudia uongo wa kihistoria dhidi ya mtu mwenye umuhimu wa kihistoria, lakini pia kuwaonya wale watu waovu ambao wanaweza kujiingiza kwenye vitendo vya namna hii na kuhalalisha tabia yao hii kwa kutumia mfano wa Imam Hassan (a.s) kama kiigizo chao.

Hapana shaka yoyote kuwa talaka ni jambo lenye kuchukiza sana katika Uislamu.

Kwa Nini Uislamu Haukuharamisha Talaka?

Hapa maswali kadhaa yanaibuka. Kama talaka haipendezi na inachukiwa kiasai hicho na Allah, kwa nini haikuharamishwa moja kwa moja na Uislamu? Uislamu ungekuwa angalau umeweka masharti ya kuthibitisha usahihi wa talaka (yaani yawepo mambo ambayo hayo yakifanywa yatachukuliwa kuwa ni sababu tosha ya kutoa talaka). Katika hali hiyo mtu yeyote ambaye angetaka kumtaliki mke wake angelazimika kisheria kueleza sababu zake za msingi mbele ya mahakama ya sheria za kutaka kutoa talaka.

Swali la pili ni kuwa; “Sentensi hii ina maana gani?: Katika vitu vyote vilivyoruhusiwa, talaka ndio kitu kinachochukiwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu.” Kama inaruhusiwa haiwezi kuchukiza na kama inachukiza haiwezi kuruhusiwa. Kuruhusiwa na kuchukiza ni maneno mawili yanayokinzana.

Mwisho, je idara ya mahakama inayoiwakilisha jamii, ina haki ya kuingilia suala la talaka kiasi cha kuweza kuibatilisha? Au kuweza kusikiliza mashauri mpaka idhihirike kuwa usuluhishi hauwezekani na hivyo hakuna namna isipokuwa kuvunja ndoa?