read

Talaka – III

Tumesema kwamba kwa mtazamo wa Uislamu, talaka ni jambo linalochukiza. Uislamu unataka ndoa iwe imara na idumu. Tuliibua swali kuwa ikiwa talaka inachukiza, kwa nini Uislamu haujaipiga marufuku? Je Uislamu haukupiga marufuku vitendo vyote vinavyochukiza kama vile kunywa pombe, kucheza kamari, ukatili n.k? Kama jibu ni ndiyo, sasa kwa nini Uslamu haujaiharamisha kabisa talaka kisheria? Kimsingi inapingana na mantiki kusema kuwa talaka inaruhusiwa na wakati huo huo inachukiza. Kama inaruhusiwa, vipi inaweza kuchukiza? Kama inachukiza vipi inaweza kuruhusiwa? Uislamu kwa upande mmoja unamkunjia uso mtu anayemtaliki mke wake na wakati huo huo haumuwekei kikwazo cha kisheria (cha kutoa talaka), kwa nini?

Ni swali la busara sana, na ni ufunguo wa siri zote za tatizo la talaka. Kwa kusema kweli, ndoa ni uhusiano wa asili na sio uhusiano wa kimkataba. Maumbile yameweka sheria maalum kwa ajili yake. Mikataba mingine ya kijamii kama vile ya mauzo, ya ajira, rehani ya amana, ya uwakili n.k. Si lolote zaidi ya makubaliano ya kijamii. Hayana mkono wa maumbile na silika. Sheria ya maumbile haiingilii mikataba hii. Lakini kinyume chake, mkataba wa ndoa una utaratibu maalum. Umeundwa na matamanio ya asili ya pande mbili.

Kwa hiyo, haishangazi kuona kuwa mkataba wa ndoa una kanuni zake maalum ambazo ni tofauti na zile za mikataba mingine yote.

Sheria Za Maumbile Katika Ndoa Na Talaka.

Katika jamii ya kiraia, sheria za asili pekee ni sheria ya uhuru na usawa, sheria ambayo juu yake hujengwa sheria nyingine zote za kijamii. Lakini katika mkataba wa ndoa, mbali na kanuni za jumla za uhuru na usawa, maumbile yametoa sheria nyingine pia, ambazo lazima zizingatiwe katika suala la ndoa, mahari, matunzo na mwisho talaka. Hakuna faida yoyote kuyapuuza maumbile. Kama Alexis Carrel alivyoonyesha, sheria za kibaiolojia na sheria nyingine za maisha (asili) ni ngumu, katili na zisizozuiliwa kama sheria za kinajimu.

Ndoa maana yake ni kuambatana na ni muungano, na talaka maana yake ni kutengana.

Maumbile yamesanifu sheria ya maumbile katika namna ambayo mwanaume hutenda mambo kwa nia ya kumpata mwanamke, na mwanamke hujiondoa (hukataa kataa) kwa nia ya kumvutia na kumpotosha mwanaume. Mwanaume hutaka kuumiliki mwili wa mwanamke na mwanamke hutaka kuuteka moyo wa mwanaume. Msingi wa ndoa umejengwa juu ya upendo, muungano na kuhurumiana na ushirikiano na uswahiba peke yake. Katika jengo la familia, jinsia ya kike huchukua nafasi muhimu na jinsia ya kiume huchukua nafasi ya pembeni. Kutokana na yote haya ni dhahiri kuwa maumbile lazima yatakuwa yameweka kanuni maalumu kwa ajili ya uvunjaji wa maisha ya familia pia.

Hapo awali tulimnukuu msomi mmoja akisema kuwa kutafuta mwenzi maana yake ni kushambulia (kwa upande wa mwanaume) na kuteka nyara na kujifaragua kwa mwanamke kwa nia ya kumpendeza na kumdanganya. Kwa mwanaume ambaye yeye kwa asili ni kama mnyama mwindaji, vitendo vyake ni vya kichokozi na kwake mwanamke ni medali ambayo lazima aipate. Kutafuta mwenzi ni mapambano na ndoa ni kunyakua na kumiliki.

Mkataba ambao umejengwa juu ya upendo na hisia za umoja hauwezi ukashinikizwa kwa nguvu. Sheria inaweza kuwalazimisha watu wawili kuuheshimu mkataba wao kwa msingi wa kushirikiana na usawa lakini haiwezi kuwalazimisha kupendana, kuwa waaminifu kila mmoja kwa mwenzake, kila mmoja kujitolea kwa ajili ya mwenzake na kila mmoja kushiriki furaha za mwenzake.

Kama tunataka kudumisha uhusiano huu kati ya watu wawili, tunapaswa kutumia mbinu na njia nyingine tofauti na sheria.

Kwa mujibu wa mpangilio wa asili wa ndoa, ambao juu yake ndio sheria za Kiislamu zimejengwa, mke hushika nafasi ya mtu anayestahiki upendo na heshima katika familia. Ikiwa kwa sababu fulani fulani atapoteza nafasi hii na akanyimwa upendo na mapenzi ya mume wake, msingi wa jengo la familia huanguka chini na utaratibu wa asili huparanganyika.

Uislamu huiangalia hali hii kwa huzuni, lakini Uislamu hauwezi kuendelea kufikiri kuwa ndoa bado iko hai hata baada ya kusambaratika kwa msingi wake wa asili.

Uislamu umechukua hatua maalum ili kuhakikisha kuwa maisha ya familia yanabaki katika hali yake ya asili, yaani mke atabaki katika hali ya kupendwa na kuhitajika, na mume abaki na hisia za kumpenda mkewe na awe tayari kumhudumia.

Uislamu umemhimiza mwanamke ajipambe na kujiremba sana ili kumridhisha mume wake, kuonyesha utimilifu wake kwa ajili ya mumewe, kumkidhia matamanio yake ya asili na kuepuka kumkera kwa ujeuri na kiburi. Pia umemhimiza mwanaume kumpenda mke wake, kuwa mpole kwake na kushikamana naye na asiufiche upendo wake kwa mkewe. Hatua hizi zimechukuliwa ili kuifanya furaha ya ngono ibakie katika wigo wa familia na kuifanya jamii ya nje ya familia kujishughulisha na kazi na shughuli nyingine badala ya ngono (yaani ngono iwe nyumbani tu, nje ya nyumbani iwe ni sehemu ya kazi na shughuli nyingine).

Uislamu unataka mahusiano ya jimai (ngono) yawe masafi na yasiyo na uchafu. Hatua zote hizi zimechukuliwa kwa nia ya kuifanya taasisi ya familia iepukane na hatari ya kuvunjika na kusambaratika.

Nafasi Ya Asili Ya Mwanaume Katika Maisha Ya Familia.

Kwa mtazamo wa Uislamu, ni matusi kabisa kwa mwanamke kwamba sheria imlazimishe kuishi na mwanaume asiyempenda. Sheria inaweza kumlazimisha mwanamke kuishi na mwanaume fulani lakini haiwezi kumhakikishia kuwa atapata nafasi muhimu kabisa katika familia, nafasi ambayo anastahili. Sheria inaweza kumlazimisha mwanaume kumhudumia mke wake lakini haiwezi kumlazimisha kuwa mume anayejali.

Hivyo, upendo wa mwanaume unapopoa, ndoa hupoteza mwelekeo kwa mtazamo wa maumbile.

Hapa swali jingine linaibuka. Je, upendo wa mwanamke ukipoa, maisha ya familia yataathirika? Je maisha ya ndoa yataendelea kama yalivyo au yatafikia kikomo. Kama yatabaki salama, sasa inakuwaje kwamba ukosefu wa upendo kwa upande wa mume huvunja ndoa lakini ukosefu wa upendo kwa upande wa mke hauvunji ndoa?

Je, kuna tofauti yeyote kati ya mwanaume na mwanamke? Kama ukosefu wa upendo kwa upande wa mke vile vile huvunja ndoa, basi ni dhahiri kuwa wanawake pia wanapaswa kuwa na haki ya kutoa talaka kama mwanaume.

Kwa kusema kweli, mafanikio ya maisha ya familia hutegemea maelewano na masikilizano ya wote wawili, mume na mke. Lakini kama tulivyosema hapo awali kuna tofauti ya tabia ya akili (mentality) ya mwanaume na ile ya mwanamke. Huko nyuma tumeshanukuu maoni ya wanasayansi juu ya hili. Maumbile yamepanga kuwa mapenzi ya kweli na ya dhati ya mwanamke huja tu kama mwitikio wa upendo wa dhati wa mwanaume. Hivyo mapenzi ya mwanamke kwa mwanaume ni matokeo ya upendo wa dhati wa mwanaume.

Maumbile yamemkabidhi mwanaume funguo za udhibiti wa mapenzi na maelewano yao. Ikiwa mwanaume anampenda mwanamke na ni mwaminifu kwake basi mwanamke pia humpenda na kubaki mwaminifu kwake, kwa kusema kweli uaminifu wa mwanamke ni mwitikio wa uaminifu wa mwanaume.

Maumbile yameweka funguo za kuvunja ndoa mikononi mwa mwanaume. Ni kutojali kwa mwanaume na kutokuwa kwake mwaminifu kunakopoozesha mapenzi ya mwanamke. Kwa upande mwingine, kutojali na kupuuzia kwa mwanamke hakumwathiri mwanaume lakini kinyume chake sio kweli.

Mwanaume kupoteza upendo ni mwisho wa ndoa, lakini kwa mwanamke sio hivyo. Ikiwa mwanaume anajali na ni mwaminifu, mara zote anaweza kurejesha upendo wa mke wake kwa kumuonyesha upendo, upole na kujali. Sio matusi kwa mwanaume kumlazimisha kipenzi chake kwa msaada wa nguvu ya sheria, kuendelea kuishi naye, na kumshawishi polepole. Lakini si jambo linalovumilika kwa mke kutumia nguvu ya sheria ili kumrejesha mlinzi na kipenzi chake.

Mambo huwa hivi inapokuwa kutojali kwa mwanamke hakutokani na ukosefu wa maadili na ukatili wa mwanaume. Hawezi kuruhusiwa kutumia vibaya nafasi yake kumtesa au kumtendea vibaya mke wake. Tutaijadili nukta hii baadaye.

Ilivyo, mwanaume anahitaji mwili wa mwanamke na mwanamke anauhitaji moyo wa mwanaume. Hiyo ndio tofauti kati ya hawa wawili. Ndoa huwa haina maana kwa mwanamke kama hapati ulinzi na mapenzi ya dhati ya mume wake.

Maoni Ya Mwanasaikolojia Wa Kike.

Hivi karibuni makala moja ilichapishwa na mwanamama mmoja mwanasaikolojia wa Kifaransa, Beatrice Maryo, ambaye ana shahada ya udaktari na anafanya kazi kama daktari wa akili katika hospitali ya Paris. Yeye mwenyewe ni mama wa watoto watatu.

Katika makala hii ameelezea vizuri sana ni jinsi gani mwanamke mwenye mimba au anayenyonyesha anavyohitaji upole na upendo wa mume wake. Anasema kwamba; “Kuanzia wakati mwanamke anapoanza kuhisi kuwa muda si mrefu atakuwa mama, huanza kuutafiti mwili wake. Huutazama kila mara na kuunusa, hasa inapokuwa ni mtoto wake wa kwanza. Huhisi udadisi mwingi juu yake mwenyewe kana kwamba yeye ni mgeni wa mwili wake na hutaka kujijua (kujigundua) kwa mara ya kwanza.

Anapohisi kutembea kwa mtoto kidogo katika tumbo lake, huanza kusikilizia kwa uangalifu kila sauti ya mwili wake. Kuwepo kwa mtu mwingine katika mwili wake humfanya asikie furaha sana kiasi cha kutaka kujitenga na kupumzika. Hutaka abaki peke yake na kitoto chake kidogo, ambacho bado hakijaja katika ulimwengu huu.

“Wanaume, katika kipindi cha ujauzito wa wake zao, wana majukumu muhimu ya kufanya, lakini kwa bahati mbaya sana, mara nyingi huyakwepa majukumu haya. Mama mtarajiwa huhitaji kuhisi kuwa mume wake anamwelewa, anampenda, na anamlinda. Vinginevyo, anapoona tumbo lake limevimba, kuvutia kwake kumetoweka, homa za asubuhi zimeanza, na anaogopa uchungu wa uzazi, atamlaumu mume wake, aliyempa mimba na kumsababishia matatizo na taabu zote. Ni jukumu la mume kujiweka karibu zaidi na mke wake mara nyingi zaidi kuliko kipindi kingine chochote katika miezi yake ya ujauzito. Familia yote inahitaji baba mpole na anayejali ambaye mke na watoto watamweleza matatizo yao, huzuni zao na furaha zao. Hata kama maongezi yao sio ya maana bado ni muhimu baba kuyasikiliza.

“Mwanamke mjamzito hutaka sana watu wote wamuongelee mtoto wake. Mwanamke huona fahari kuwa mama. Lakini anapoona mume wake hamjali mtoto, hisia yake ya fahari hubadilika na kuwa hisia ya dharau. Huchukia kuwa mama na kuwa mjamzito, na huwa ni aina ya udhalilishaji kwake. Inafahamika kuwa akina mama hawa hupata uchungu mkubwa wakati wa kujifungua… Uhusiano kati ya mama na mtoto sio wa pande mbili. Ni uhusiano wa pande tatu; mama, mtoto na baba. Hata kama baba hayupo (ikiwa wamepeana talaka), bado ana jukumu muhimu katika maisha ya ndani ya mama yaani fikra na hisia zake pamoja na hisia ya umama (motherhood)…”

Haya ndiyo aliyoyasema mwanasaikolojia wa kike ambaye pia ni mama.

Jengo Lililojengwa Juu Ya Msingi Wa Hisia Za Moyoni.

Mwanamke hutegemea sana uaminifu, upole na ulinzi wa mume wake kiasi kwamba bila ya kuwepo ushirikiano wake wa dhati, basi hata mtoto mwanamke huyu huwa hamjali sana. Anaweza kuvumilia ugumu wa maisha kwa msaada wake tu (mumewe). Katika hali hii inawezekanaje kumlazimisha, kwa kutumia nguvu ya sheria kubaki ameshikamana na mwanaume ambaye hamtaki?

Je, sio kejeli kwamba kwa upande mmoja tunajenga mazingira ambayo kwayo wanaume wanawajali wake zao kidogo tu na wanamalizia ujana wao sehemu nyingine na kwa upande mwingine tunawatupa wake zao juu yao kwa nguvu ya sheria? Ukweli ni kuwa, Uislamu unataka mwanaume mwenyewe amtafute mwanamke, na ampende. Uislamu hautaki kumtupia mwanamke (yaani kumpatia mwanamke asiyempenda).

Ni kanuni ya jumla kuwa palipo na suala la mapenzi, kujitolea na uaminifu, hapawezi kuwa na kulazimishana kwa nguvu ya sheria. Ikiwa mume hampendi mke wake, linaweza kuwa ni jambo la kusikitisha lakini hakuna nguvu inayoweza kumfanya ampende.

Hebu tutoe mfano mmoja. Kama tunavyojua, katika sala za jamaa kuna sharti kwamba kiongozi wa sala anaweza kuwa yule tu ambaye ni mchamungu na ambaye wafuasi wake wana imani juu ya uchamungu wake. Katika hali hii uhusiano kati ya kiongozi na wafuasi wake umejengwa juu ya uchamungu wa kiongozi na imani waliyonayo wafuasi wake juu yake. Ikiwa wafuasi wake watapoteza imani juu yake iwe kwa haki au kwa makosa, uhusiano huu huharibika. Sheria haiwezi kutumika kuurejesha.

Kwa vile ni suala la hisia za moyoni, hakuna yeyote anayeweza kulazimishwa kisheria kuwa na imani na mtu fulani. Hata kama kiongozi wa sala ana kiwango cha juu kabisa cha uchamungu na wema, hawezi kuwalazimisha wengine kusali nyuma yake. Itakuwa ni kichekesho sana kufungua kesi mahakamani kwa sababu watu fulani au wote hawakusali nyuma yake. Inaweza hata kuwa ni matusi kwa nafasi ya kiongozi wa sala kujaribu kuwalazimisha watu kusali nyuma yake.

Hali ni hivyo hivyo katika suala la uhusiano kati ya wapiga kura na mgombea katika uchaguzi. Watu watampigia kura mgombea yule tu ambaye wana imani naye. Wasipomchagua mgombea fulani, hata awe na sifa na anafaa kiasi gani, hawezi kuwashitaki wapiga kura.

Kitu pekee kinachoweza kufanyika katika hali hizi ni kuwaelimisha watu juu ya vigezo sahihi na kukuza kiwango chao cha uelewa ili watakapokuwa wakitekeleza jukumu lao la kidini, wampate mtu muongofu kabisa wa kumfuata na wanapotekeleza jukumu lao la kijamii wampigie kura mtu anayestahiki. Lakini ikitokea, kwa sababu yoyote iwayo, watu wakabadilisha maoni yao, linaweza kuwa ni jambo la kusikitisha tu, lakini hakuwezi kuwa na suala la kulazimishana au kuwachukulia hatua za kisheria wapiga kura.

Jukumu la kifamilia ni sawa kabisa na majukumu ya kidini na kijamii tuliyoyataja hapo juu, Uislamu huiona familia kuwa ni jamii ya asili ambayo imewekewa taratibu maalum ambazo zinapaswa kufuatwa kwa ukamilifu ili iweze kwenda vizuri.

Ni mafanikio makubwa sana kwa Uislamu kwa kuweza kuuweka utaratibu huu, kwani nchi za Magharibi bado hazijaweza kutatua matatizo yake ya kifamilia. Sio hivyo tu, bali kila siku matatizo yanazidi kuongezeka na kila siku matatizo mapya yanazidi kuongezeka juu ya matatizo ya zamani. Kwa bahati nzuri, kutokana na uchunguzi wa kisayansi, mambo yanazidi kuwa wazi pole pole. Tunashawishika kwa asilimia zote kuwa ulimwengu wa Kimagharibi pole pole utazikubali kanuni na mafundisho ya Kiislamu juu ya sheria za familia. Hata hivyo hatuamini kuwa mafundisho halisi ya Uislamu yanafanana kabisa na yale yanayofuatwa na kutekelezwa leo hii. (na waislamu – yaani mafundisho hayatekelezwi vilivyo)

Kinachoimarisha Jengo La Familia Ni Zaidi Ya Usawa.

Ulimwengu wa Kimagharibi wa leo umeleweshwa na neno usawa bila kujua kuwa suala la uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke lilitatuliwa na Uislamu karne 14 zilizopita. Katika suala la mfumo wa familia, kuna kitu kikubwa zaidi kuliko usawa. Kwa jamii ya kiraia, maumbile yameweka sheria ya usawa tu, lakini kwa jamii ya kifamilia maumbile yameweka sheria nyingine pia. Mahusiano ya kifamilia hayawezi kuongozwa kwa msingi wa usawa peke yake. Sheria nyingine zote za maumbile zinazoyaongoza mahusiano haya, lazima zitambuliwe na zifuatwe.

Usawa Katika Ufisadi

Kwa bahati mbaya neno ‘usawa’ limetumika sana na mara nyingi mno kiasi cha kuwa maana yake halisi imeshaharibika. Ni mara chache kutokea kwa yeyote kuwa neno usawa linapotumika humaanisha usawa wa haki. Kanuni ya usawa haiwezi kutumika kila sehemu bila kubagua. Inaweza kuwa dhihaka kubwa kusema kuwa kila kitu kimekuwa sawa kwa sababu huko nyuma ni wanaume tu waliowadanganya wake zao.

Je, tunaweza kufurahia na kutangaza kuwa sasa usawa umefikiwa kwa sababu huko nyuma ni 10% ya ndoa zilizokuwa zikiishia kwenye talaka na kutengana, na sasa katika baadhi ya sehemu za dunia, 40% ya ndoa zinaishia kwenye talaka, na katika 50% (nusu) ya talaka hizi zilianzishwa (ziliombwa) na wanawake? Zamani ni wanaume waliowasaliti wake zao kwa kujiingiza katika zinaa na wake zao walikuwa waaminifu sana kwa waume zao, lakini sasa hata wanawake nao wanawasaliti waume zao na hawazingatii tena usafi wa kimaadili (hawajiepushi na zinaa).

Je haya ni maendeleo? Je tunaweza kusema kuwa huu ni usawa? Zamani mara nyingi wanaume waliuonyesha ukatili na ugumu (wa hisia) kwa wake zao. Waliwatelekeza wake zao na watoto na kuwakimbilia vimada. Sasa hata akina mama wenye watoto wengi, baada ya kuwa wameolewa miaka mingi huko nyuma, wanazitelekeleza nyumba zao na kwenda kukidhi tamaa zao, kufuatia utambulisho mfupi aliopewa kwa mtu asiyejua katika hafla ya dansi. Je, hii inamaanisha kuimarika kwa usawa?

Hivyo ndivyo ambavyo badala ya kutibu maradhi ya kijamii na kuimarisha maisha ya kifamilia (ndoa), tunadhoofisha mfumo wa familia na kuitikisa misingi yake. Lakini vilevile, tunafurahia kuwa sasa usawa unazidi kuboreka. Kama hali hii itaendelea muda si mrefu mwanamke atamzidi mwanaume kwa ufisadi, upotofu na ugumu wa moyo.

Sasa ni dhahiri kuwa kwa nini Uislamu, licha ya kuichukia talaka, haujaiharamisha moja kwa moja. Ni dhahiri kuwa ni vipi kitu kinaweza kuruhusiwa na bado kikawa kinachukiza sana.