read

Talaka – IV

Ni dhahiri kutokana na majadiliano tuliyoyafanya kuwa Uislamu unachukia talaka na kuvunja maisha ya ndoa. Umechukua kila hatua ya kimaadili na kijamii ili kuiokoa ndoa kutokana na hatari ya kuvunjika, lakini haukutumia mbinu ya kulazimisha wala nguvu ya sheria. Uislamu unapinga matumizi ya nguvu ya sheria ili kumzuia mwanaume asimtaliki mkewe na kumlazimisha mwanamke kuendelea kuishi na mume wake. Uislamu unaona kuwa hatua hizi haziafikiani na nafasi ya mwanamke katika familia, kwani hisia za moyoni na mihemko ndio nguzo za maisha ya familia.

Ni mwanamke anayepokea fukuto la hisia za upendo wa mume wake na yeye hulipeleka kwa watoto wake. Ikiwa mwanaume atapoteza upendo wake kwa mke wake, mazingira ya nyumbani huwa baridi na ovyo ovyo. Hata hisia za kimama kwa watoto wake hutegemea kwa kiasi kikubwa upendo wa mumewe. Kwa mujibu wa mwanasaikolojia mashuhuri, hisia za kimama sio silika kwa maana kwamba haiwi kuwa hisia hizi haziongezeki au kupungua. Upendo na kujali anakokuonyesha mwanaume kwa mkewe kuna athari kubwa kwenye hisia zake za kimama.

Kwa kifupi, mwanamke huhamasishwa na kuchochewa na hisia za ndani na upendo wa mumewe katika kuzisafirisha hisia zake kwa wanawe.

Mwanaume anaweza kulinganishwa na mlima, mwanamke kama mto na watoto kama mimea. Mto lazima upokee maji kutoka milimani ili uyafyonze na kuyatoa katika hali ya maji yanayotoa uhai kwa ajili ya umwagiliaji wa mimea na maua. Mvua isiponyesha mlimani au yakinyong’onyea ardhini, mto utakauka na mimea itanyauka.

Kama ilivyo kuwa ni muhimu kwa rutuba ya ardhi na kwa kustawi kwa mimea, hisia za ndani na upendo wa mwanaume kwa mke wake ni muhimu sana kwa maisha ya ustawi, mafanikio na furaha ya watoto na mama yao.

Inapokuwa hisia za moyoni na upendo wa mume ni muhimu kiasi hicho kwa mafanikio ya maisha ya familia, ni vipi sheria inaweza kutumika kama silaha dhidi yake?

Uislamu unapinga vitendo vya aibu na udhalilishaji vinavyofanywa na baadhi ya wale wanaowataliki wake zao wa zamani na kuoa wapya. Lakini kwa maoni ya Uislamu, sio dawa kumlazimisha mwanaume aliyepoteza mapenzi kuendelea kuishi na mkewe dhidi ya matakwa na utashi wake. Kitendo hicho hakiendani na sheria ya maumbile ya maisha ya familia.

Ikiwa mwanamke atajaribu kurudi katika nyumba ya mumewe kwa nguvu ya sheria na kwa msaada wa mamlaka za kiutawala, nafasi yake katika nyumba itakuwa sawa na utawala wa kijeshi. Katika hali hii hataweza kuwa malikia wa nyumba, wala hawezi kuwa kiunganishi cha hisia kati ya mume wake na watoto wake. Pia hataweza kukidhi hitajio lake la upendo na kutazamwa vyema.

Uislamu umechukua hatua ili kuondoa kesi za talaka, lakini Uislamu ukiwa kama mtunga sheria, hautaki kumlazimisha mwanamke ambaye ni kitovu cha mfumo wa familia, kuishi na mwanaume mkorofi asiyemtaka (yaani mwanaume asiyemtaka mwanamke huyo).

Hatua iliyochukuliwa na Uislamu ni kinyume cha kilichofanywa na kinachofanywa na ulimwengu wa Magharibi. Uislamu unapiga vita mambo yote yanayosababisha hali ya kutokuwa na uaminifu na uasherati lakini hauko tayari kumlazimisha mwanamke kuishi na mume asiyekuwa mwaminifu. Lakini kinyume chake ulimwengu wa Kimagharibi unapalilia mambo yanayosababisha kutokuwepo kwa uaminifu, na wakati huo huo unataka kumlazimisha mwanamke kuendela kuishi na mume asiyekuwa mwaminifu na mwasherati.

Uislamu umetumia rasilimali zake zote ili kutunza uhai wa roho ya ubinadamu na uchangamfu na ingawa haumlazimishi mwanaume asiye mchangamfu kwa mkewe kuendelea kuishi na mke wake, kiuhalisia umefanikiwa sana kupunguza kesi za talaka zinazotokana na kutochangamkiana. Wengine hawazingatii nukta hizi na wanataka furaha kwa nguvu na katika ncha ya sindano na hivyo hawajafanikiwa.

Mbali na kesi za talaka zinazotokea katika nchi za Magharibi kwa madai ya wanawake kwa sababu ya kutoshabihiana (incompatibility) na kama ilivyoelezwa na gazeti la Newsweek, kupenda starehe, idadi ya matukio ya talaka kwa sababu ya uasherati wa mwanaume ni kubwa mno kuliko idadi ya matukio kama hayo katika nchi za Mashariki (Asia).

Asili Ya Amani Ya Familia Ni Tofauti Na Zile Aina Nyingine Za Amani.

Hapana shaka yoyote kuwa inapaswa pawepo amani na maeleweno kati ya mume na mke, lakini amani na maelewano yanayopaswa kuwepo katika maisha ya ndoa ni tofauti sana na amani inayopaswa kuwepo kati ya marafiki wawili, wenzi wawili, majirani wawili na nchi mbili majirani.

Amani na maelewano katika maisha ya ndoa ni sawa na amani na maelewano yanayopaswa kuwepo kati ya wazazi na watoto. Yanahusisha uvumilivu, kujitolea, kujali maslahi ya mwenzako, kuvunja ukuta wa uwili (hivyo kuwa mwili mmoja) na kushiriki katika furaha na huzuni ya mwenzi wake. Lakini kinyume chake, amani na maelewano kati ya marafiki wawili, wenzi wawili, majirani wawili au nchi mbili majirani ina maana kutoingilia haki za mwenzako katika nchi mbili zinazogombana, hata amani iliyopatikana kwa mtutu inatosha. Hata dola ya tatu ikiingilia na kuweka kizuizi ili kuzuia mashambulizi ya moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili, amani itakuwa tayari imepatikana, kwa amani ya kisiasa inamaanisha kutokuwepo vitendo vya uchokozi na migongano (kuparuana).

Lakini amani ya familia ni tofauti na amani ya kisiasa. Hapa kutoingilia haki za mwenzako hakutoshi. Amani ya mtutu wa bunduki haifai chochote. Kinachotakiwa ni muungano wa roho, jambo ambalo ni la juu zaidi na la msingi zaidi. Mambo yako hivyo hivyo katika amani na maelewano kati ya wazazi na watoto. Hapa pia panahitajika kitu kikubwa zaidi kuliko kutokuwepo kwa uchokozi peke yake. Kwa bahati mbaya, kwa sababu za kihistoria na wakati fulani za kimkoa, nchi za Magharibi hazitambui umuhimu wa hisia za moyoni. Wao hawaoni tofauti yoyote kati ya amani ya familia na amani ya kisasa au amani ya kijamii.

Watu wa Magharibi wanafikiri kuwa kwa vile amani kati ya nchi mbili inaweza kufikiwa kwa kurundika majeshi ya dola ya tatu katika mpaka wa nchi hizi mbili, halikadhalika amani kati ya mume na mke inaweza kuimarishwa kwa kuweka nguvu ya kisheria (kimahakama) katika mpaka wa maisha yao. Wanasahau kuwa mafanikio ya maisha ya familia hutegemea kutoweka au kuondolewa kwa mipaka yote (baina yao).

Watu wa Mashariki wenye akili za Kimagharibi, badala ya kujivunia mfumo wao na kuwaonyesha watu wa Magharibi ubovu na mapungufu ya mfumo wa Kimagharibi, wamebobea katika kuiga kibubusa kiasi cha kushindwa kutofautisha kati ya wema na uovu. Lakini muda si mrefu nchi za Mashariki zitaondokana kabisa na minyororo ya magharibi, zitaigundua haiba (Shaksia) yao na zitajifunza kujitegemea. Hapa ni muhimu kutaja nukta mbili.

Uislamu Unakaribisha Jambo Lolote Litakaloondosha Hatari Ya Talaka.

Kutokana na tulivyoyaandika baadhi ya watu wanaweza kwa makosa kuhitimsiha kuwa tunaunga mkono wazo la wanaume kuwataliki wake zao kwa ridhaa zao na kwa raha zao. Kwa hakika hivi sivyo. Tunachomaanisha ni kuwa Uislamu hautaki kutumia nguvu ya sheria dhidi ya mume. Uislamu unakaribisha jambo lolote litakalofanikiwa kumshawishi mume kuachana na wazo la kutoa talaka, na zaidi ya hayo talaka sio sahihi mpaka itamkwe mbele ya watu wawili waadilifu, ambao wanatarajiwa kutumia jitihada zao zote kuwapatanisha wanandoa.

Mila ya sasa ambayo mara nyingi talaka inatolewa mbele ya watu wawili waadilifu, ambao hata hawafahamu wanandoa zaidi ya kuyajua majina yao, sio ya Kiislamu kabisa.

Ulazima wa kuwepo mashahidi wawili wajuzi ni moja ya mambo yanayoweza kumshawishi mume kuachana na mpango wa kutoa talaka, ikiwa sharti hili litazingatiwa kikamilifu kwa maana iliyokusudiwa. Uislamu hauchukulii kuwepo kwa mashahidi wawili kuwa ni jambo la lazima wakati wa ndoa (ili ndoa isihi), ambayo ni mwanzo wa mkataba wa ndoa, kwa sababu hautaki kuchelewesha amali njema. Lakini unaona kuwa ni sharti la lazima kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu na wajuzi ili talaka iweze kusihi (kuwa sahihi), jambo ambalo ni mwisho wa mkataba wa ndoa.

Halikadhalika kwa mujibu wa Uislamu talaka sio sahihi (valid) kama itatolewa wakati mwanamke yupo hedhini ingawa hakuna kikwazo cha kufunga ndoa katika kipindi hicho. Ilivyo hedhi kwa vile ni kikwazo cha kufanyika tendo la ndoa, ilipaswa kuwa ni kikwazo cha ufungaji wa ndoa sio talaka. Lakini kwa vile Uislamu unahimiza usalama wa ndoa na unakataza utengano, umeruhusu ndoa ifungwe hata kama mwanamke yupo hedhini na umekataza talaka katika kipindi hicho. Katika baadhi ya hali, ni lazima kusubiri kwa miezi mitatu kabla ya talaka kuruhusiwa kutolewa.

Vikwazo vyote hivi vinakusudiwa kutoa muda wa kutosha wa kuruhusu hasira, iliyosababisha uamuzi wa kutoa talaka, ipoe na kuwawezesha mume na mke kurejea maisha yao ya kawaida.

Aidha, katika talaka rejea mume anaruhusiwa kumrejea mke wake ndani ya kipindi cha eda.

Uislamu umemuwekea mwanaume kikwazo kingine kwa kumtaka azikabili gharama za ndoa pamoja na matunzo ya mke na watoto katika kipindi chote cha eda. Ikiwa mwanaume anataka kumtaliki mke wake na kumuoa mwanamke mwingine, kwanza anapaswa kulipa gharama za matunzo ya mke wa kwanza, na kubeba gharama ya matunzo ya watoto na kulipa mahari ya mke mpya. Na pia anapaswa kubeba jukumu la matunzo ya mke wa pili pamoja na watoto atakaomzalia.

Mbali na jukumu la kuwalea watoto, majaaliwa yao yenye mashaka humhofisha na kumzuia mume kuchukua uamuzi wa kutoa talaka.

Pamoja na yote haya, Uislamu unaona kuwa ni lazima pindi ndoa inapovunjika mahakama ya familia yenye wasuluhishi wawili, mmoja kutoka upande wa mume na mwingine upande wa mke, hupaswa kuwasuluhisha wanandoa.

Wasuluhishi wanapaswa kufanya kila liwezekanalo kusuluhisha ugomvi baina ya mume na mke na ikibidi wanaweza kuwataka ushauri wanandoa ili kufikia lengo hili. Wanaweza tu kuvunja ndoa ikiwa wataona kuwa usuluhishi hauwezekani kabisa. Ikiwa kuna uwezekanao, wasuluhishi wanapaswa kuwa ni ndugu wa wanandoa, ikiwa upo uwezekano wa kupatikana watu wenye ujuzi miongoni mwa ndugu zao.

Qur’ani Tukufu inasema:

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِنْ أَهْلِهَا إِنْ يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا {35}

“Ikiwa mna hofu ya kuvunjika kwa ndoa baina yenu wawili (mke na mume), chagueni msuluhishi mmoja kutoka kwa mume na mwingine kutoka kwa mke. Ikiwa wote wanataka mapatano, Mwenyezi Mungu atawawezesha. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yote, Mwenye habari.” (Suratul Nisa, 4:35).

Mwandishi wa Kashshaf, neno ‘msuluhishi’ anasema kuwa ni mtu anayechaguliwa kusuluhisha anayepaswa kuwa mwaminifu, fasaha na mwenye uwezo wa kuleta maelewano na kuzitendea haki pande mbili. Anasema pia kuwa inafaa zaidi kuteuwa msuluhishi kutoka miongoni mwa ndugu zao kwa vile wanatarajiwa kujua sababu za mgogoro vizuri zaidi na pande zote zinaweza kuzungumza nao kwa uhuru zaidi na wanaweza kuwa na imani nao zaidi.

Mafakihi wanatofautiana juu ya suala la usuluhishi, iwapo usuluhishi ni wajibu au unapendekezwa tu. Wazo lililo mashuhuri zaidi ni kuwa ni jukumu la serikali kuteuwa wasuluhishi. Shaheed Thani, katika kitabu chake, ‘Masalik’ ametoa rasmi rai ya kisheria kuwa usuluhishi ni wajibu na unapaswa kuratibiwa na serikali.

Sayyid Muhammad Rashid Riza, mwandishi wa Tafsiri ya Qur’ani, AlManar, baada ya kutoa rai kuwa usuluhishi ni wajibu, anazungumzia khitilafu ya maoni ya mafakihi (wajuzi wa sheria za Kiislamu) juu ya suala hili na anasema kuwa, kivitendo, Waislamu hawafuati kanuni hii ya busara na hivyo wanakosa fursa ya kufaidika na faida zake nyingi. Wanavyuoni wanapoteza nguvu zao katika kubishana tu, wakati hakuna anayechukua hatua kuitekeleza. Kama kanuni haitekelezwi, kuna tofauti gani ikiwa kanuni hiyo ni wajibu au inapendekezwa tu?

Juu ya sharti ambalo wasuluhishi wanaweza kumuwekea mume ili kufanikisha usuluhishi, Shahid Thani anasema kuwa wanaweza kwa mfano, kumlazimisha mume kumweka mke wake katika mji fulani au nyumba fulani na asimuweke mama yake au mke wake mwingine katika nyumba hiyo hata kama ni kwenye chumba tofauti; kulipa malipo yote ya mahari aliyopangiwa wakati wa ndoa kwa mkupuo na kulipa mkopo wote kwa mkupuo mmoja kwa mke wake.

Kwa kifupi, hatua yoyote inayofaa kumshawihsi mume kuachana na mpango wa kutoa talaka inafaa na inakaribishwa.

Hili ni jibu kwa swali tuliloliibua awali kuwa mahakama inayoiwakilisha jamii ina haki ya kuingilia kati na kuzuia kuvunjika kwa ndoa au haina.

Mahakama inaweza kuingilia kati kwa sababu uamuzi wa mume wa kumtaliki mke si mara zote unakuwa ni dalili ya kuvunjika kabisa kwa ndoa. Anaweza kutoa uamuzi huo kwa sababu ya hasira au hali ya kutoelewana. Hatua yoyote itakayochukuliwa na jamii kuzuia utekelezaji wa uamuzi huo inakaribishwa na Uislamu.

Mahakama ya usuluhishi, ikiwa ni mwakilishi wa jamii, inaweza kuziamuru ofisi zinazohusika na utoaji wa talaka kutohitimisha kesi ya madai ya talaka, mpaka mahakama iwahakikishie kuwa imeshindwa kuwapatanisha na kuleta amani na maelewano kati ya mume na mke.

Huduma Alizotoa Mke Katika Familia

Talaka, mbali na kuvunja maisha matakatifu ya familia, husababisha matatizo mengine makubwa kwa mke, matatizo ambayo hayawezi kupuuzwa. Jaalia mke ameishi katika nyumba na mumewe kwa miaka, ameichukulia nyumba kuwa ni yake na kwa dhati na uaminifu mkubwa, anafanya bidii kubwa kuijenga na kuitengeneza. Anapunguza bajeti ya chakula na mavazi, ukiachilia mbali wanawake wa mijini (ambao hawafanyi hivi), kiasi cha kumkera hata mumewe (kwa jinsi anavyobana matumizi), na anasita hata kuajiri msaidizi wa kumsaidia kazi za ndani. Anajitolea ujana wake, nguvu zake, afya yake kwa ajili ya mumewe na nyumba yake. Sasa mume wa mke huyu, baada ya miaka ya kuishi pamoja, anataka kumtaliki mke mwingine, sio tu kuwa anataka kuziharibu jitihada zote za mke wake, bali pia anataka kujiingiza katika raha za mapenzi kwa kutumia maumivu ya mke wake (anayemuacha).

Huku sio kuvunjika tu kwa ndoa, na haiwezi ikadaiwa kuwa, kwa asili ni jambo la aibu kwa staha ya mwanamke kung’ang’ania kwa mwanaume huyu ambaye hampendi.

Hapa maswala mengine pia huibuka – suala la kutokuwa na nyumba kwa mke, suala la kuikabidhi nyumba yake kwa hasimu wake na suala la kupoteza jitihada zake zote na huduma alizozitoa huko nyuma katika nyumba yake.

Kila mwanadamu anataka kuwa na nyumba yake na huhisi kushikamana na nyumba aliyoijenga kwa mikono yake mwenyewe hasa. Ukijaribu kumfukuza ndege katika kiota alichokijenga, bila shaka atakataa na kujilinda. Kwa maoni yetu, tatizo hili linastahili kujadiliwa kwa umakini. Katika hali hizo, talaka inakuwa sio kuvunjika kwa ndoa peke yake, bali huwa ni kuangamia kabisa kwa mwanamke.

Hata hivyo, suala la nyumba ni tofauti na lile la talaka, na haya masuala mawili yanapaswa kujadiliwa tofauti tofauti. Kwa mtazamo wa Uislamu, tatizo hili halipaswi kutokea. Linatokea kutokana na kutojua kanuni za Kiislamu na taratibu zake na wanaume kuzitumia vibaya dhamira njema za wake zao.

Watu walio wengi wanadhani kuwa matunda yote ya jasho la mwanamke ni mali ya mume wake. Wanafikia hata kufikiri kuwa mume ana haki ya kumlazimisha mke wake kumfanyia kazi na kwamba anapaswa kutii amri zote kama mtumwa. Fikra hii potofu ndio chanzo cha matatizo yote. Kama tulivyosema mwanamke ana uhuru kamili kuhusiana na kazi na shughuli. Chochote anachopata huwa ni mali yake peke yake. Uislamu umempa uhuru wa kiuchumi. Na bado umemuwajibisha mume kubeba gharama zote za mke na watoto wake.

Hivyo Uislamu umempa mwanamke fursa nyingi za kujipatia fedha za kumwezesha kuishi maisha ya heshima na yasiomtegemea mwanaume (baada ya kuachika). Talaka na kutengana hakukupaswa kumhofisha kwa upande wa uchumi. Vitu vyote ambavyo anaweza kuwa amekusanya ili kuijenga nyumba yake ni mali yake na mume wake hana haki ya kuvichukua. Mwanaume kuvichukua vitu hivyo kunaweza tu kuhalalishwa na mifumo ambayo inamlazimisha kufanya kazi katika nyumba ya mumewe. Masaibu yanayowapata watu wetu huenda yanasababishwa na kutojua kwao sheria.

Sababu nyingine ya tatizo hili ni tabia ya baadhi ya wanaume kuunyonya uaminifu wa wake zao. Baadhi ya wanawake wanajitolea sio kwa sababu hawaielewi sheria ya Kiislamu, bali kwa sababu wanawaamini waume zao kupita kiasi. Hawataki kuitumia fursa waliyopewa na Uislamu. Ghafla huzinduka usingizini na kukuta kwamba wamepoteza maisha yao kwa kujitolea kwa mwanaume asiyekuwa mwaminifu na wamepoteza fursa waliyopewa na dini yao.

Ikiwa mke atasamehe haki yake ya kisheria ya kujiwekea akaunti yake tofauti ya fedha na mapato mengine, mume pia anatarajiwa kwamba, kwa kuzingatia kujitolea na huduma alizotoa mke wake atatoa zawadi na hidaya kwa mkewe. Qur’ani inasema;

وَإِذَا حُيِّيتُمْ بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ

“Mnaposalimiwa kwa salamu, itikieni kwa salamu iliyo bora kuliko hiyo au angalau kama hiyo.’ (Suratul Nisa, 4:86).

Imekuwa ni mila ya watu wema kumpa mke zawadi za vitu vya thamani kama vile nyumba au mali nyingine kama hidaya.

Hata hivyo, tunachomaanisha ni kuwa suala la kutokuwa na nyumba(makazi) halihusiani na talaka na haliwezi kutatuliwa kwa kurekebisha sheria. Tatizo hili linahusiana na suala la uhuru wa kiuchumi wa mwanamke na tatizo hilo tayari limeshatatuliwa na Uislamu. Tatizo hili limeibuka kutokana na ujinga (kutojua) wa baadhi ya wanawake na wengine kwa sababu ya kuwaamini mno waume zao, tatizo hili litamalizika kabisa ikiwa wanawake watayajua mafundisho ya Uislamu juu ya jambo hili na kuacha kuwaamini mno waume zao.