read

Ndoa Ya Muda II

Tayari tumeshaeleza tabia ya ndoa ya muda, ulazima wa kuwepo kwake na ndoa ya kudumu kushindwa kukidhi mahitaji yote ya wanaadamu. Sasa hebu tuangalie upande wa pili wa shilingi na kuona hasara na dosari zake. Kabla ya kujadili hilo hebu tuangalie kitu kimoja.

Historia Ya Imani.

Katika masomo yote ambayo watu mbali mbali wameyatolea maoni, hakuna lililo tata na gumu kama historia ya mawazo, imani, mila na desturi za mwanadamu. Hii ndio sababu kuwa japo mada hii ni maarufu sana, maoni yaliyo mengi yanayotolewa juu ya hili yamekuwa ni upuuzi.

Mtu yeyote mwenye elimu juu ya falsafa, mafundisho ya kumfikia Mungu kwa tafkira, irifan (mysticism) na falsafa ya uanazuoni (schalasticim) wa Kiislamu, na akasoma maandishi ya hivi karibuni katika nchi yetu juu ya masuala yanayohusiana na mada hii ataona kuwa mengi yanaazimwa kutoka kwa wageni au wananukuu na kuiga kila neno lao, pia anaweza kuelewa ninachomaanisha. Waandishi wetu wa zama hizi wanarudia au kuziegemeza kazi zao na mustashirik, wakati inaonekana kuwa mustashirik hawa na vibaraka wao hawafanyi lolote katika kuyachambua masuala haya kwa kina.

Kwa mfano, suala linalofahamika katika mafunzo ya Kiislamu ya irifan (mytcism) kama wahadat alWujud (Umoja wa Mwenyezi Mungu) limejadiliwa kutoka katika kila pembe, lakini hakuna jitihada ya maana iliyoelekezwa kufafanua maana halisi ya dhana (neno) hiyo wala kuelezea maoni ya vinara wa mafunzo haya ya irifan (Islamic Mysticism) kama vile Muhyiuddin ibn Arabi na Sadrul Muta’llihin Shiraz. Hivi karibuni maoni yaliyotolewa juu ya ndoa ya muda katika gazeti la Iran ‘ZaneImruz’ au “mwanamke wa leo” yamenikumbusha mada ya ‘Wahdat alWujud’

Katika makala haya kila kitu kilizungumzwa juu ya ndoa ya muda, lakini nia hasa ya sheria hii iliachwa. Watu hawajali sheria hii kwa kuwa ni sehemu ya urithi wa Mashariki. Ingekuwa ni zawadi kutoka Magharibi mambo yangekuwa tofauti kabisa.

Kama sheria hii ingekuwa inatoka Magharibi bila shaka makongamano na semina yangekuwa yanafanyika kutetea wazo kuwa ndoa ya kudumu haikidhi hali ya maisha ya karne hii na kwamba kizazi hiki hakiko tayari kubeba majukumu mazito ya ndoa ya kudumu. Kizazi hiki kinataka kuwa huru. Kinataka kuishi maisha ya uhuru. Kinataka ndoa huru ambayo masharti yake yataamuliwa na wanandoa wenyewe.

Sasa kwa kuwa tayari sauti zimeanza kupazwa huko Ulaya kuteteta ndoa ya muda na watu mashuhuri kama Bertrand Russel wanaihubiri kwa jina la ndoa ya wenzi inatarajiwa kuwa baada ya muda si mrefu ndoa ya muda itakuwa mashuhuri mno kiasi cha kuwa tutalazimika kuzindua kampeni za kutetea ndoa ya kudumu.

Pingamizi

Yafuatayo ndiyo yanayosemwa kuwa ni ubaya na mapungufu ya ndoa ya muda.

Msingi wa ndoa unapaswa kuwa wa kudumu tokea mwanzo wa mahusiano ya unyumba, mume na mke wanapaswa kujua kuwa kila mmoja ni mali ya mwenzake kwa kudumu. Wazo la kutengana halipaswi kuingi akilini mwao. Ndoa ya muda sio mkataba wa kudumu kati ya mume na mke.

Ni kweli kuwa msingi wa ndoa unapaswa kuwa wa kudumu. Hata hivyo, pingamizi hili linaweza kuwa sahihi tu kama tutaipinga ndoa ya kudumu na kuhimiza kuwa nafasi yake ichukuliwe na ndoa ya muda.

Kama pande mbili zinaweza kuimudu ndoa ya kudumu na kila mmoja ana imani ya kutosha na mwenzake na wakaamua kuwa kwa kudumu kila mmoja awe mali ya mwenzake hapana shaka kuwa wanapaswa kufunga ndoa ya kudumu.

Sheria ya ndoa ya muda imewekwa tu kwa vile ndoa ya kudumu peke yake haiwezi kukidhi mahitaji yote ya wanaadamu katika hali zote. Kuruhusu ndoa ya kudumu peke yake kutasababisha tu Ukomonisti wa ngono. Ni wazi kuwa hakuna mvulana au msichana ambaye ana rasilimali za kutosha kwa ajili ya ndoa ya kudumu anaweza kujiingiza katika mahusiano ya muda.

Wanawake na wasichana wa Kiirani, licha ya kuwa Shia, hawalipendi wazo la ndoa ya muda. Wanaliona kama tusi kwao. Hivyo maoni ya jumla ya Shia wenyewe yamelikataa.

Tunaweza kujibu kuwa kulichukia wazo hilo kijumla kunatokana na wanaume waasherati kulitumia vibaya. Ni jukumu la serikali kuzuia kutumiwa kwake vibaya. Pili sio jambo la maana kutarajia ndoa ya muda kuwa mashuhuri kama ndoa ya kudumu, kwa sababu ndoa ya muda inakusudiwa kukidhi mahitaji ya wahusika ikiwa wote au mmoja wao hayuko tayari kufunga ndoa ya kudumu.

Ndoa ya muda inashusha hadhi na utu wa mwanamke. Ni sawa sawa na kuukodi mwili wa mtu, na hata kuhalalisha uuzaji wa watu. Ni kinyume na staha ya mwanamke kumuweka kwa ajili ya mwanaume yeyote kwa kubadilishana na fedha.

Hili ni pingamizi linalostaajabisha zaidi. Kwanza ndoa ya muda, kama tulivyoeleza hapo awali, haina uhusiano wowote na uuzaji au ukodishaji. Je inaweza kuwa uuzaji au ukodoshaji kwa vile tu muda wa ndoa ni maalum? Je inakuwa ni kukodisha kwa kuwa mahari inapaswa kupangwa? Tunataka kulijadili suala la mahari tofauti.

Mafakihi wamekubaliana kuwa, kwa asili ya mkataba, hakuna tofauti kati ya ndoa ya kudumu na ndoa ya muda. Ni miundo miwili ya ndoa na mikataba yake inaweza kusihi tu kwa kuzingatia kanuni ya ndoa. Ikiwa mkataba wa ndoa ya muda utachukua sura ya uuzaji au ununuaji, basi itakuwa ni batili.

Pili, tangu lini ada ya kukodi (kuajiri) watu ilipigwa marufuku? Mafundi cherehani, vionyozi, wapishi, hata wataalamu mabingwa, waajiriwa wote wa serikali kuanzia kwa Waziri Mkuu hadi kwa afisa wa cheo cha chini kabisa na wafanyakazi wote wa viwandani wote ni wa kukodiwa.

Mwanamke ambaye kwa hiari yake anaingia mkataba wa ndoa ya muda na mwanaume fulani sio mwanamke aliyekodishwa na hafanyi jambo la aibu kwa staha yake. Kama unataka kuona wanawake waliokodishwa na waliofanywa watumwa na unataka kujua maana halisi ya mwanamke aliyeajiriwa (kodiwa), unapaswa kwenda Ulaya na Marekani na utembelee makampuni ya filamu. Huko utaona miondoko ya viungo vya mwanamke, ishara zake na mikao ya kingono ikiuzwa.

Tiketi za sinema na kumbi za starehe unazonunua ndiyo mishahara ya wanawake waliokodiwa. Unatambua ni kiasi gani mwanamke anajidhalilisha ili kupata fedha? Analazimika kujifunza kwa miaka mingi sanaa ya kuamsha na kuchochea hamu ya ngono chini ya usimamizi wa wataalamu bingwa wa fani hiyo na wenye uzoefu. Analazimika kuuweka mwili wake, roho yake na haiba yake rehani kwenye makampuni ya biashara ili kuvutia wateja zaidi na zaidi. Ukitembelea mikahawa na mahoteli, unaweza kuona ni heshima gani mwanamke aliyopata, ni jinsi gani analazimika kuuza heshima na utu wake kwa ajili ya fedha kidogo ili kujaza masanduku ya fedha ya mabepari na jinsi gani analazimika kujiuza mbele ya wageni.

Wanawake waliokodiwa ni wale wasichana wa mauzo katika maduka makubwa ambao wanaitoa mhanga heshima na staha yao ili kukidhi tamaa ya waajiri wao.

Wanawake waliokodiwa ni wale wasichana wanamitindo wanaoonekana katika TV wakitangaza bidhaa na wanaotumia mbinu zote kuwavutia wateja kwao.

Nani asiyejua kuwa leo hii huko Magharibi uzuri wa mwanamke, mvuto wake wa kingono, sauti yake, sanaa yake, mwili wake, roho yake na zaidi ya yote, haiba yake vinatumika kama njia nyenyekevu za kutumikia maslahi ya ubepari wa Ulaya na Marekani?

Ninashangaa ni vipi mwanamke aliyeolewa na mwanaume fulani kwa hiari yake lakini kwa muda maalum anachukuliwa kuwa mwanamke aliyekodiwa (kufanya ngono) wakati mwanamke ambaye katika sherehe ya harusi au kwenye hafla ya jioni, mbele ya maelfu ya macho yenye tamaa ya wanaume, anaimba mpaka koo lake linauma, haonekani kuwa ni mwanamke aliyekodiwa (kufanya mambo machafu).

Kwa kuruhusu ndoa ya muda, Uislamu umemkinga mwanamke dhidi ya kunyonywa na mwanaume. Pia Uislamu umemkataza kutumia njia dhalili ili kujipatia riziki. Je, ni Uislamu uliomdhalilisha mwanamke au Ulaya ya karne hii?

Ikiwa siku moja mwanamke atagundua mitego yote ambayo mwanaume wa karne hii ameiweka katika njia yake, bila shaka atapinga kwa nguvu zote uongo na udanganyifu huu. Hapo tu ndipo atakapobaini kuwa mlinzi pekee mwaminifu kwake na kimbilio lake ni Qur’ani. Siku hiyo haiko mbali sana!

Aidha, ndoa ya muda inahalalisha ndoa za mitala, ambazo ni mila mbaya. Kwa hiyo ndoa ya muda haifai. Mwisho wa sura hii tutaeleza ni kwa ajili ya nani sheria hii imewekwa. Na kuhusiana na ndoa za mitala, tutajadili hilo katika sura inayofuata.

Ndoa ya muda haidumu. Huwaacha watoto watakaozaliwa wakiwa hawana makazi. Wanakuwa hawana mtu anayewajibika kwao. Wananyimwa uangalizi wa baba na upendo wa mama.

Katika ndoa ya kudumu hakuna mwanandoa anayeweza kukwepa jukumu la kuzaa watoto, lakini katika ndoa ya muda, pande zote mbili ziko huru. Ni kweli kuwa mke hapaswi kumzuia mume wake kufurahia jimai, lakini anaweza kuchukua hatua za kuzuia mimba. Tatizo hili limetatuliwa kabisa kutokana na maendeleo ya njia za kisasa za kuzuia mimba.

Hivyo katika ndoa ya muda, ikiwa wote wawili, mume na mke wanapenda wanaweza kuzaa watoto, ikiwa wanalikubali jukumu la kuwalea. Ni wazi kuwa, kwa upande wa upendo wa asili, hakuna tofauti kati ya mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa ya kudumu na yule wa ndoa ya muda. Ikiwa baba au mama watakataa kutekeleza jukumu lao, ni jukumu la mahakama kuwalazimisha kama vile tu inavyoingilia katika suala la talaka. Ikiwa mume na mke hawataki kuzaa watoto na nia yao ni kukidhi haja zao tu, wanapaswa wajiepushe kuzaa watoto.

Kama tunavyojua, Kanisa haliruhusu njia za kuzuia mimba. Lakini kwa maoni ya Uislamu mume na mke wako huru kutumia njia za kuzuia mimba. Hata hivyo mimba ikishaingia hairuhusiwi kuitoa au kuiharibu.

Hili ndilo wanalolimaanisha mafakihi wa Kishia wanaposema kuwa lengo la ndoa ya kudumu ni kupata watoto na la ndoa ya muda ni kukidhi haja ya asili ya jimai.

Ndoa Ya Muda Maalum Na Nyumba Ya Wake Wa Mtu

Moja ya mada, ambazo nchi za magharibi zinaitumia kama silaha ya kuonyesha uovu wa nchi za Mashariki na ambayo nchi za magharibi zimeandaa filamu na tamthilia kwa ajili yake ni suala la uundaji wa nyumba za wake (harems). Kwa bahati mbaya, mifano hii ni ukweli uliopata kuwepo katika historia.

Maisha ya baadhi ya makhalifa na masultani yanatoa mfano kamili wa muundo wa ‘nyumba za wanawake’ wao, ambazo huelezewa kuwa ni alama mashuhuri ya uasherati wa mwanaume wa Mashariki.

Inadaiwa kuwa uhalali wa ndoa ya muda unafanana tu na uhalali wa nyumba ya wake, ambayo ni nukta dhaifu kwa upande wa nchi za Masharikii na imeleta aibu kwayo. Sio hivyo tu, bali pia ni sawa na kuhalalisha uasherati, miundo yote ambayo inakwenda kinyume na maadili na husababisha kuporomoka na kuangamia.

Kitu hicho pia kimesemwa juu ya ndoa za mitala na zimetafsiriwa kuwa ni uhalalishaji wa nyumba za wanawake wengi (walio chini ya mwanaume mmoja). Tutalijadili suala la ndoa za mitala peke yake. Hivi sasa tunabakia kwenye ndoa ya muda.

Suala hili linapaswa kujadiliwa katika pembe mbili:

Ni sababu gani za kijamii zilizosababisha uundwaji wa nyumba za wake (wa mtu mmoja) huko nyuma? Je, sheria ya ndoa ya muda ilikuwa na ushawishi katika hali hii?

Je sheria ya ndoa ya muda inakusudia kutoa fursa kwa wanaume waasherati kuunda nyumba za wanawake wao?

Sababu Za Kijamii Za Uundwaji Wa Nyumba Za Wake Wa Mtu (Harems).

Kulikuwa na sababu mbili zilizosababisha kuwepo kwa nyumba hizi. Ya kwanza ilikuwa ni uchamungu na staha ya mwanamke. Nyumba hizi zinaweza kuundwa tu katika mazingira ambayo mwanamke hawezi kufanya tendo la ndoa na mwanaume zaidi ya mmoja. Katika hali hiyo mwanaume muasherati hana namna ila kuwakusanya wanawake wengi na kuunda ‘nyumba ya wakeze’ (harem).

Ni wazi kuwa katika mazingira ambayo umuhimu hauwekwi katika staha na wanawake wapo wengi na bure hakuna anayeweza kuchukua taabu ya kuunda ‘nyumba ya wake’ kubwa kwa gharama kubwa na vifaa vingi.

Sababu ya pili ilikuwa ni kutokuwepo kwa uadilifu wa kijamii. Mazingira yanayofaa kwa uundaji wa ‘nyumba za wake’ ni kuwa wachache wamebobea katika kila aina ya starehe na raha, ambapo wengine hawawezi hata kupata mlo wa siku, na ambamo kuna wengi ambao hawawezi kumudu kuoa na kuwa na familia. Katika mazingira hayo, idadi ya wanawake ambao hawajaolewa huongezeka na hutengeneza mazingira mazuri ya uundwaji wa nyumba za wake.

Kwa upande mwingine, ikiwa kuna uadilifu wa kijamii na kuna uwezo wa kuunda familia na kuchagua mke/mume kwa wote, basi ni wazi kuwa kila mwanamke ataambatana na mume mmoja na kunakuwa hakuna fursa ya ufisadi na uundaji wa nyumba hizi.

Ikiwa kila mtu mzima ana nafasi ya kuwa na mume/mke, ni wazi kuwa hapatakuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaobaki kwa ajili ya matajiri kuunda nyumba za wake, kwani idadi ya wanawake kwa kawaida huwa sawa, huzidi au kupungua kidogo kuliko idadi ya wanaume.

Imekuwa ni mila kuwa historia inasimulia hadithi za nyumba hizi za makhalifa na masultani na kuelezea fahari na utajiri wa vitala (makazi na ofisi) vyao lakini hupuuzia kueleza dhiki, shida na taabu ya wale waliokufa katika tawala hizo na ambao hali zao hazikuwa zikiwaruhusu kuwa na mke.

Mamia ya wanawake waliomalizia maisha yao katika nyumba hizi walikuwa ni haki ya asili ya wanaume hawa fukara waliolazimika kubakia bila kuoa mpaka walipokufa.

Bila shaka katika jamii ambayo staha na usafi wa kimaadili upo na ambapo tendo la ngono haliwezekani isipokuwa ndani ya mipaka ya ndoa, zikiwemo zote mbili, ya muda na ya kudumu, uundaji wa nyumba za wake hauwezekani, hasa inapokuwa matabaka ya kijamii na kiuchumi yameondolewa na haki ya ndoa inapowekwa wazi kwa kila mtu mzima.

Tukiitazama historia kwa haraka haraka tutaona kuwa sheria ya ndoa ya muda haikuwa na ushawishi wowote katika uundwaji wa ‘nyumba za wake’ hata kidogo.

Hakuna khalifa yeyote wa ukoo wa Abbas na masultani wa himaya ya Ottoman ambao hawa ndio walikuwa mashuhuri kwa kuwa na ‘nyumba za wake’ kubwa, aliyekuwa mfuasi wa Theolojia ya Shia na hivyo haitarajiwi kuwa yeyote kati yao angeweza kuwa alitumia fursa ya sheria ya ndoa ya muda.

Masultani wa Kishia, japo wangeweza kuwa waliitumia sheria hii kama kisingizio kamwe hawakupata kufanya hivi kama makhalifa wa Ibn Abbasi na masultani wa himaya ya Ottomani. Hii inaonyesha wazi kuwa nyumba hizi zilisababishwa na sababu nyingine maalum za kijamii.

Je Ndoa Ya Muda Imehalalishwa Ili Kukidhi Tamaa Ya Mwili?

Hapana shaka kwamba dini zote za kimungu zinazuia kabisa uasherati na ukosefu wa maadili, kiasi cha kufikia baadhi ya wafuasi wake kuamua kuishi maisha ya utawa.

Moja ya kanuni za wazi za Uislamu na zinazokubalika ni kupiga vita uzinifu, ambao umelinganishwa na shirki (kwa maneno ya Qur’ani). Uislamu umemuelezea ‘muonjaji’ yaani anayetaka kufaidi kila aina ya wanawake, kuwa anashutumiwa na kuchukiwa na Allah. Tulipokuwa tukijadili suala la talaka, tulilizungumzia hili.

Moja ya sifa (tabia) za Uislamu ni kuwa unapinga utawa na useja (kutooa) lakini hauruhusu uzinifu, kwa mujibu wa Uislamu, matamanio ya haja zote za asili, ikiwa ni pamoja na haja ya ngono yanatakiwa kukidhiwa ndani ya mipaka ya kisheria tu kwa kiasi cha mahitaji ya asili. Uislamu hauruhusu kuwasha moto wa matamanio na kuubadili kuwa kiu isiyokatika. Uislamu unapinga mambo yote yenye sura ya uasherati na dhulma.

Ni ukweli usio na shaka kuwa kamwe haikuwa nia ya Mtungaji wa sheria hii ya ndoa ya muda kutoa njia kwa washerati ya kukidhi matamanio yao yasiyokatika ya ngono na kuleta maafa na maangamizi kwa mwanamke na watoto wake wasio na hatia. Utiaji moyo mkubwa uliowekwa kwenye wazo la ndoa ya muda maalumu na Maimamu (wa Ahlul Bait) una falsafa maalumu, ambayo tutaieleza kwa kifupi.

‘Nyumba Za Wake’ Na Ulimwengu Wa Kisasa.

Sasa hebu tuangalie jinsi ulimwengu wa kisasa ulivyolishughulikia suala la nyumba hizi. Ulimwengu wa kisasa unazitazana nyumba hizi kwa chuki na mila hii imeshaachwa. Moja ya vipengele viwili vilivyosababisha kuwepo kwa nyumba hizo kimeshaondolewa. Lakini ni sababu ipi hiyo? Sio ile ya matabaka ya kijamii bali ile ya staha na uchamungu wa wanawake ndiyo imeondolewa.

Mwanaume mzinifu wa zama hizi hahitaji tena kutaabika kuunda ‘nyumba ya wake’ na kubeba gharama kubwa za kuihudumia. Shukrani kwa utamaduni wa Kimagharibi kwamba kwa mwanaume wa karne hii ‘nyumba ya wake’ ipo katika kila sehemu. Ili kuwafaidi wanawake wa rangi na mataifa mbali mbali, mwanaume wa sasa hahitaji kuwa na madaraka makubwa na fedha nyingi kama Harun alRashid au Fazl Ibn Yahya Barmaki. Anachohitaji ni gari tu na kipato cha elfu kiasi kila mwezi ili kuweza kufaidi ngono kwa kiasi ambacho hata Harun alRashid hakupata kuota. Hoteli za kisasa, migahawa, na mikahawa mara zote zipo tayari kuhudumia (kutumiwa) kama nyumba za wanawake kwa wanaume.

Wakati fulani uliopita kijana wa Kiiran, Adil Kutwali, wazi wazi alikiri kuwa na mabibi (mahawara) 22 wa maumbo na sura mbali mbali kwa wakati mmoja. Shukrani kwa utamaduni wa Kimagharibi kwamba mwanaume wa sasa anafurahia raha zote za nyumba hizi (harem) bila kuwa na hofu ya gharama kubwa ya kuihudumia.

Kama shujaa wa ‘Alfu Lela Ulela’ (masiku elfu moja na moja) angenyanyua kichwa chake kutoka mavumbini na kuona fursa tele za kufaidi ngono na urahisi wa bei pamoja na uwingi wa wanawake, asingefikiri tena haja ya kuwa na nyumba ya wake, na kubeba gharama zote za kuihudumia. Angewashukuru watu wa magharibi kwa kumuokoa na gharama zote za kuunda nyumba ya wanawake na hapo hapo angetangaza kufutwa kwa ndoa za mitala na ndoa za muda, kwa sababu zinawapa wanaume mzigo wa majukumu juu ya wanawake. Ukiuliza ni nani aliyepoteza katika mchezo huu, kwa kuwa mshindi anajulikana toka zamani, tutasema kuwa kwa bahati mbaya mwanamke ndiye mara zote amekuwa mpotezaji. Kwa sababu ya kuamini kirahisi na kuwa rahisi, alipoteza jana na amepoteza leo.

Khalifa Apiga Marufuku Ndoa Ya Muda Maalum.

Ndoa ya muda inaruhusiwa na sheria ya Shia (Jafaria) peke yake. Madhehebu mengine ya Kiislamu hayaruhusu. Sikusudii kuingia katika ubishani wa Shia na Sunni. Napenda tu hapa kutaja kwa kifupi usuli wa kihistoria wa suala hili.

Waislamu wote wanakubaliana kuwa katika kipindi cha awali cha Uislamu Mtukufu Mtume wakati akiwa safarini na ikawa Waislamu walikuwa mbali na wake zao na hivyo wakawa wanapata ugumu, aliwaruhusu kufunga ndoa za muda. Inakubaliwa pia na Waislamu wote kuwa Khalifa wa pili, katika kipindi cha ukhalifa wake, aliipiga marufuku ndoa ya Mut’a kwa mujibu wa taarifa mashuhuri, alisema kuwa: “Leo ninapiga marufuku vitu viwili ambavyo vilikuwa halali wakati wa Mtume. Ni ndoa ya muda na kuhiji ‘Hajj’ na Umra kwa ihram mbili tofauti.”

Baadhi ya Sunni wanaamini kuwa Mtume mwenyewe aliipiga marufuku ndoa ya muda katika kipindi cha mwisho cha uhai wake na Khalifa wa pili alirudia kupiga marufuku ambayo tayari imeshawekwa na Mtume. Lakini maneno ya Khalifa ambayo yamekuja kwetu yanaonyesha kitu tofauti na hiki.

Maelezo sahihi juu ya hili ni yale yaliyotolewa na Allamah Kashif alGhita. Khalifa alipiga marufuku ndoa ya muda kwa sababu alifikiri kuwa jambo hili lilikuwa ndani ya mamlaka yake kikatiba kama Mkuu wa Dola, ambaye angeweza kutumia mamlaka yake maalum kutokana na mahitaji ya wakati. Kwa maneno mengine zuio la Khalifa lilikuwa ni la kisiasa sio la kisheria. Khalifa kamwe alikuwa hafichi wasi wasi wake juu ya kusambaa kwa masahaba wa Mtume katika nchi mpya zilizotekwa na kuchanganyika kwao na Waislamu wapya waliosilimu. Katika muda wote wa uhai wake, alipinga vikali suala la Waislamu (masahaba) kuhama kutoka Madina.

Pia hakutaka damu zao zichanganyike na Waislamu wapya waliosilimu, ambao imani yao ilikuwa bado haijawa kubwa. Ni wazi kuwa hii ilikuwa ni rai ya muda. Waislamu wa wakati ule waliikubali amri yake bila kuonyesha chuki, kwa sababu tu walijua kuwa ilikuwa ni ulazima wa kisiasa na sio sheria ya kudumu. Vinginevyo hailekei kwamba watu wangeridhika, kama wangeona Mtume aliamrisha hivi na Khalifa anaamrisha vinginevyo. Lakini baadaye ambapo kama matokeo ya maendeleo fulani, maisha ya makhalifa wa mwanzo, hususan makhalifa wawili wa mwanzo, yalichukuliwa kama kiigizo, amri zao zilichukua sura ya sheria ya kudumu.

Hivyo ndugu zetu wa kisunni wanapaswa kulaumiwa zaidi kuliko khalifa ambaye aliweka zuio la muda dhidi ya ndoa ya muda kwa sababu za kisiasa (kama ilivyokuwa kwa zuio la tumbaku nchini Iran katika mwanzo wa karne hii) Wengine wasingepaswa kulipa zuio hili sura ya sheria ya kudumu.

Ni dhahiri kuwa Allamah Kashif alGhita hakutoa maoni yoyote juu ya kitendo cha khalifa kama kilikuwa kinakubalika au la. Alieleza tu asili ya zuio hili na kwa nini halikupingwa na Waislamu.

Hata hivyo ni kutokana na ushawishi huu na haiba (shaksia) ya Khalifa, kwamba watu waliacha kuifuata sheria hii na kwa sababu mila ya Uislamu ya ndoa ya kudumu ilidhaniwa ingeachwa basi ikawa ndoa ya muda imeachwa.

Ni katika hali hii kwamba kwa nia ya kuhakikisha kuwa desturi ya Kiislamu haisahauliki kabisa, Maimamu watukufu wa Ahlul Bait, ambao ni watetezi na walinzi wa imani walihimiza na kuitetea sana. Imam Jafar Sadiq (a.s) alikuwa akisema kuwa ndoa ya muda ni nukta ambayo hawezi kuificha kamwe.

Mbali na faida nyingi za ndoa ya muda, jitihada ya kufufua desturi zilizokufa ilikuwa ni sababu nyingine ya Maimamu kuihubiri. Kwa maoni yetu, Maimamu walipowakataza watu kuoa kwa ndoa ya muda, walitaka iwe wazi kuwa ndoa hii haikuwa kwa wale wasioihitaji.

Imam Kadhim (as) alimwambia Ali ibn Yaqtin, ‘Unataka ndoa ya muda ya nini? Allah amekuepusha na tatizo la kuihitaji.”

Alimwambia mtu mwingine kuwa ‘ndoa ya muda, ni kwa yule asiye na mke au mwenye mke lakini mke wake yuko mbali.”

Muongozo na uhimizaji wa umma katika kuoa ndoa za muda ni hatua moja mbele katika “ufufuaji wa mila zilizoachwa” au desturi lakini uhimizaji peke yake kwa wale waliokuwa wakiihitaji haukuwa unatosha kuihuisha tena mila hii tuliyoruhusiwa na Mtume, kama inavyoonyeshwa wazi katika maandiko ya Kishia na vitabu vya hadithi.

Hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa maana na lengo la Mtunzi wa sheria hii katika kuikuza (kuitetea) na maelezo ya sheria hii na lengo la Maimamu Maasumin la kuihimiza halikuwa na nia ya kuruhusu majaribio ya ngono, matamanio maovu na ujenzi wa nyumba za wake kwa ajili ya watu wenye tabia za wanyama wala kuwakandamiza na kuwatesa wanawake wasio na uwezo na waliokandamizwa pamoja na watoto yatima kwa wakati wowote.

Mwandishi wa kimisri, Sheikh Muhammad Abu Zuhra, katika kitabu chake, ‘AlAhwal alShakhsiya, amemnukuu Amirul Muuminina Ali (a.s) kuwa amesema, “Kama nikipata habari kwamba mtu mmoja mwenye mke amefunga ndoa ya muda, nitampiga mawe mpaka afe.”

Hadith hii haina sanad (nyororo) ya wasimuliaji inayoeleweka. Hata hivyo usahihi wake unakubalika, inaunga mkono wazo kuwa ndoa ya muda inaruhusiwa tu kwa yule asiye na mke au ambaye mke wake yuko mbali.

Kwa kifupi kwa nini tushikilie hadith hii moja ya mwanazuoni wa Kisunni (ambayo chanzo chake hakieleweki) na kuziacha hadithi nyingine nyingi za Amirul Muuminina Ali (a.s) zilizoripotiwa katika vitabu vyote vya kisunni na Kishia katika sura ya Mut’ah.

Katika kauli zake nyingi za thamani Imam Ali (a.s), Amiri wa walioamini anasema, “Kama Umar asingeifuta ndoa ya muda, hakuna mtu ambaye angezini, isipokuwa wachache wenye maradhi ya ngono.” Hii ni kuwa kama ndoa ya muda isingekuwa imepigwa marufuku, hakuna mtu ambaye angejenga tabia ya kuzini, ni wale tu ambao mara zote wanapenda kufanya mambo yaliyoharamishwa ndio wangefanya hivyo.