read

Ndoa Ya Mitala (Mke Zaidi Ya Mmoja)

Ndoa ya mke mmoja ndio muundo wa asili zaidi wa ndoa. Hali ya kumiliki kitu peke yako, au uhusiano ambao wewe tu ndio unashikilia nafasi hiyo na umiliki binafsi umejikita katika aina hii ya ndoa, japo umiliki huu ni tofauti na umiliki wa mali au utajiri. Katika mfumo huu mume na mke, kila mmoja huhisi hisia za moyoni na faida za ngono za mwenzake kuwa ni zake peke yake.

Kinyume na ndoa ya mke mmoja ni ndoa ya mke zaidi ya mmoja (mitala) kwa wakati mmoja na Ukomonisti wa ngono. Jimai ya ngono, kimaana pia inaweza kuitwa mitala.

Ukomonisti Wa Ngono.

Ujimai wa ngono maana yake hakuna kuwa peke yako. Kwa mujibu wa nadharia hii, hakuna mwanaume ambaye anapasa kuwa mali ya mwanamke mmoja tu wala mwanamke kuwa mali ya mume mmoja tu. Maana yake ni kupinga (kuikana) kuwepo maisha ya familia.

Historia na nadharia zinazohusiana na zama za kale kabla ya kuanza kuandikwa kwa historia haionyeshi kipindi chochote ambapo mwanadamu hakuwa na familia na ambapo Ukomonisti wa ngono ulikuwa umestawi. Kinachodaiwa kuwepo katika baadhi ya makabila ya kishenzi (yasiyo na ustaarabu na utamaduni) ilikuwa ni hali ya kati na kati, kati ya maisha ya familia (yaani kila mtu na mke wake au mume wake) na Ukomonisti wa ngono. Inasemekana kwamba katika baadhi ya makabila ilikuwa ni jambo la kawaida kwamba wavulana kadhaa kwa pamoja waliwaoa wasichana kadhaa, au wanaume kadhaa wa ukoo mmoja waliwaoa kwa ushirikiano wanawake kadhaa wa ukoo mwingine.

Will Durant katika kitabu chake, ‘History of Culture’ Jalada la 1, anaandika kwamba katika baadhi ya maeneo ndoa za ushirikiano zilikuwa mashuhuri kwa maana kuwa wanaume kadhaa wa ukoo mmoja walishirikiana kuwaoa wanawake kadhaa wa ukoo mwingine, kwa mfano imekuwa ni mila huko Tibet kwamba ndugu kadhaa wa kiume wana idadi sawa ya madada (ambao ni ndugu) kama wake zao. Kila kijana huingiliana na yeyote katika wale akina dada anayempenda. Hapa kuna aina fulani ya Ukomonisti wa ngono.

Mila kama hii ilipata kuwepo huko Uingereza enzi za kale. Mila ambayo ilikuwa maarufu miongoni mwa Wayahudi na makabila mengine ya zamani na ambapo kwa mujibu wa mila hiyo, baada ya kufa ndugu mmoja wa kiume, ndugu yake mwingine wa marehemu alimuoa mjane wake, ilikuwa ni masazo ya mila ya kale.

Maoni Ya Plato

Inaelekea kwamba wakati akiitangaza nadharia yake ya ‘wanafalsafa watawala’ Plato amependekeza katika kitabu cha ‘The Republic,’ aina fulani ya ujamaa wa kifamilia kwa tabaka hili. Viongozi kadhaa wa kikomunisti wa karne ya 19 pia walitoa pendekezo kama hilo, lakini kama ilivyoripotiwa na mwandishi wa kitabu, ‘Freud and the Prohibition of Consanguineuous Marriage,’ baada ya machungu mengi, dola nyingi za kikomunisti zenye nguvu, zilitangaza rasmi kuitambua sheria ya mke mmoja mume mmoja mwaka 1938.

Kuwa Na Mume Zaidi Ya Mmoja (Polyandry).

Muundo mwingine wa mitala ni hali ya mke kuwa na mume zaidi ya mmoja (polyandry) kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Will Durant mila hii inapatikana miongoni mwa makabila fulani ya Tibet na kwingineko.

AlBukhari katika mkusanyiko wake maarufu wa hadithi, asSahihi, anamripoti Aisha kuwa alisema kuwa miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu kulikuwa aina nne za mahusiano ya ngono. Mojawapo ni ndoa sahihi ambayo bado ipo hadi sasa. Katika muundo huu mwanaume hutoa pendekezo kwa msichana kupitia kwa baba yake na baada ya kupanga mahari, humbeba mke wake. Hapawezi kuwa na utata juu ya watoto waliozaliwa katika ndoa hii.

Kulikuwa na aina nyingine ya ndoa, ambayo ilikuwa ikiitwa Istibza. Ili kuzaa (kupata) kizazi kizuri, mume alimchagua mwanaume na kumuomba mke wake aingiliwe na huyo mwanaume kwa muda fulani. Yeye mwenywe alijitenga na mke wake hadi mwanamke alipopata mimba. Ilikuwa ni ndoa ndani ya ndoa iliyofanywa ili kuboresha kizazi.

Kwa mujibu wa mila nyingine, kundi la wanaume kumi au pungufu ya hapo, walishirikiana kufanya mapenzi na mwanamke mmoja. Baada ya kuwa mjamzito, mke aliwaita wote, na kwa mujibu wa mila ya enzi hizo, wote walipaswa kwenda. Hapo alimteua mwanaume mmoja kuwa baba wa mtoto wake na kuwaacha wale wengine ambao nao pia walikuwa tayari kukubali jukumu hilo. Mwanaume huyo baada ya kuchaguliwa, hakuwa na hiari ya kukubali au kukataa kuwa baba wa mtoto.

Aina ya nne ya mahusiano ya unyumba ni umalaya. Malaya walikuwa na bendera juu ya nyumba zao. Hii ilitumika kama alama ya kuwatambulisha. Mwanaume yeyote alikuwa anaweza kuwaingilia wanawake hawa. Mwanamke yule alipozaa, aliwaita wanaume wote waliomwingilia, na kwa msaada wa mtaalamu wa kutambua tabia kwa kuangalia uso, alimteua baba wa mtoto. Mwanaume mhusika alipaswa kukubali uamuzi wa mtaalamu huyu na kummiliki mtoto.

Hizi ni aina za mahusiano ya kinyumba zilizokuwepo Arabuni kabla ya Uislamu. Mtume alizipiga marufuku zote na kubakiza moja iliyopo sasa. Hii inaonyesha kuwa mila ya mke kuwa na mume zaidi ya mmoja ilikuwepo miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu pia.

Montesquieu anaripoti kuwa Mwarabu mtembeaji wa dunia nzima, Abu Zahir alHassan, aliikuta mila hii China na India alipozitembelea nchi hizi katika karne ya 19 na aliichukulia kama aina ya ufisadi. Pia anaandika: “Katika Pwani ya Malabar kuna kabila liitwalo Nair. Waume wa kabila hili hawawezi kuwa na mke zaidi ya mmoja lakini wanawake wanaruhusiwa kuchagua waume wengi. Labda sababu ni kuwa Wanair ni jamii ya wapiganaji na wawindaji. Kama tunavyowazuia kuoa askari wetu wa Ulaya ili ndoa isiingiliane na kazi zao za kupigana, makabila ya Malabar pia yameamua kuwa, wanaume wa Nair wajitahidi kadri wawezavyo kuepukana na majukumu ya familia. Kutokuwa na hali na tabia ya kitropiki ya eneo hili, haiwezekani kuzuia ndoa kabisa, imeamuliwa kuwa wanaume wengi wawe na mke mmoja ili wasielemewe na majukumu ya kifamilia na hivyo kuathiri ufanisi wao.”

Kasoro Za Mke Mmoja Kuwa Na Waume Zaidi Ya Mmoja.

Kasoro kubwa na ya msingi ya mfumo huu wa mke kuwa na mume zaidi ya mmoja ni kuwa ukoo wa baba wa mtoto hubakia haujulikani kwa uhakika (yaani baba halisi wa mtoto huwa hajulikani). Katika mfumo huu uhusiano kati ya baba na mtoto haueleweki na hii ndio sababu mfumo huu hau jafanikiwa kama ilivyo Ukomonisti wa ngono haujaweza kujikita sehemu yeyote, mfumo huu pia haujakubalika katika jamii yoyote ya maana. Kama tulivyosema awali, maisha ya familia, ujenzi wa nyumba (makazi) ya kizazi kijacho na muunganiko maalumu kati ya vizazi vya zamani na vijavyo ni moja ya mahitaji ya silika za binadamu.

Kuwepo kwa mifano michache ya mke kuwa na waume wengi katika baadhi ya jamii hakuthibitishi kuwa uundaji wa familia sio silika ya mwanadamu. Halikadhalika utawa na useja kabisa (kuepuka kufanya tendo la ndoa), kama inavyofanywa na wanaume na wanawake kadhaa, pia ni aina ya upotofu. Mfumo huu si tu kwamba hauafikiani na asili ya mwanaume ya kuhodhi na upendo wake wa mfumo dume, bali pia unapingana na maumbile ya mwanamke pia. Uchunguzi wa kisaikolojia umebaini kuwa mwanamke anapenda zaidi kuwa na mume mmoja kuliko mwanaume anavyopenda kuwa na mke zaidi ya mmoja.