read

Mitala (Mke Zaidi Ya Mmoja).

Muundo mwingine wa mitala ni mtu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mfumo huu umezoeleka na kuwa na mafanikio zaidi kuliko ule wa mke kuwa na waume wengi na ujima wa ngono. Sio tu kwamba umekuwepo miongoni mwa makabila ya kishenzi, bali pia umetumiwa na watu wengi wastaarabu. Mbali na Waarabu, umetumiwa pia na Wayahudi, Wairani wa zama za Sasania na jamii nyinginezo. Montesquieu anasema kuwa huko Malaya ilikuwa inaruhusiwa kuwa na wake watatu. Pia anasema kuwa mfalme wa Urumi, Valentinian II aliwaruhusu watu wake kuoa wake wengi, lakini kwa sababu sheria hii ilikuwa haiafikiani na hali ya hewa (tabia) ya Ulaya, ilifutwa na wafalme wengine kama Theodore n.k.

Uislamu Na Mitala.

Tofauti na ilivyokuwa kwa mfumo wa mke kuwa na mume zaidi ya mmoja, Uislamu haukukataza moja kwa moja ndoa ya mke zaidi ya mmoja (mitala). Badala yake uliweka idadi maalumu, pia umeweka masharti mengine pia na haukumruhusu kila mtu kujiingiza katika kuoa wake wengi. Tutaeleza baadaye masharti yaliyowekwa na Uislamu na tutaeleza kwa nini Uislamu haukupiga marufuku ndoa za mitala moja kwa moja.

Inashangaza kwamba katika zama za kati, ambapo propaganda za kuupinga Uislamu zilikuwa katika kilele chake, wapinzani wa Uislamu walikuwa wakisema kuwa ni Mtume wa Uislamu ambaye kwa mara ya kwanza alianzisha ndoa ya mitala. Walidai kuwa mila hii ilikuwa msingi wa Uislamu na kwamba kuenea kwa Uislamu kwa haraka haraka sehemu mbalimbali duniani kulitokana na mila hii. Wakati huo huo walidai kuwa mitala hii ilikuwa ndio sababu ya kuporomoka kwa watu wa Mashariki.

Will Durant katika kitabu chake “History of Culture” juz. 1, anasema kuwa mapadri na makasisi wa zama za kati waliamini kuwa ndoa za mitala zilianzishwa na Mtume wa Uislamu, ambapo sio kweli. Kama tunavyojua maisha ya ndoa katika jamii nyingi za kijima yalifuata utaratibu huu wa mitala. Kuna sababu nyingi za kuzuka kwa mfumo huu. Katika jamii za kijima, sehemu kubwa ya wanaume walikuwa zaidi wakijishughulisha na uwindaji na upiganaji, hivyo kiwango chao cha vifo kilikuwa juu miongoni mwao. Kwa vile idadi ya wanawake ilizidi ya wanaume, hivyo ilikuwa ni lazima kutumia mfumo huu. Haikuwa inawezekana kuwaacha baadhi ya wanawake bila kuolewa, hasa ikizingatiwa kuwa, kwa vile idadi ya vifo katika jamii za kijima ilikuwa juu, kila mwanamke alitarajiwa kuzaa watoto.

Hapana shaka kwamba mfumo huu ulizifaa jamii hizo, sio tu kwa sababu ya uwingi wa wanawake kuliko wanaume, bali pia mfumo huu uliongeza idadi yao na kuwafanya kuwa na nguvu. Katika zama hizi wanaume wengi wenye nguvu na afya huchelewa kuoa na huzaa watoto kidogo tu. Lakini zamani wanaume wenye nguvu walikuwa na nafasi ya kuoa wake bora kabisa na walikuwa wakizaa idadi kubwa ya watoto. Hii ndio sababu desturi hii iliendelea kwa muda mrefu sana si tu miongoni mwa jamii za kijima bali hata katika jami zilizoendelea. Ni hivi karibuni tu kuwa pole pole desturi hii imeanza kutoweka katika nchi za Mashariki. Kilimo kimeimarisha maisha ya wanaume na kimepunguza ugumu wa taabu za kale, ambapo matokeo yake ni kuwa na idadi ya wanaume na wanawake imeanza kulingana. Hivi sasa mitala imekuwa ni fahari ya kundi dogo la matajiri, hata katika jamii za kijima, na walio wengi wanalazimika kuridhika na mke mmoja, na kwa burudani ya ziada, wanaweza kujiingiza katika zinaa, kila inapowezekana.

Gustav Leabeon katika kitabu chake, ‘History of Culture’ anasema kuwa hakuna mila isiyopendwa Ulaya kama ndoa za mitala, wala Ulaya haijaihukumu kimakosa mila nyingine yoyote kama ilivyofanya kwa ndoa hii. Waandishi wa kizungu wameamini kuwa ndoa za mitala ni msingi wa Uislamu na ndio sababu kubwa ya kuenea kwake. Pia wanashikilia kuwa mila hii ndio sababu ya kuanguka kwa watu wa mashariki. Pingamizi nyingine mbali na hizi, zinazoonyesha huruma kwa wanawake wa Mashariki, zinadai kuwa wanawake hawa walionenepeana wanafungiwa ndani ya kuta nne za nyumba zao chini ya matowashi (wanaume waliohasiwa) wenye mioyo migumu.

Pia wanadai kuwa kosa dogo ambalo wanaweza kumuudhi mkuu wa familia linaweza kuwafanya waadhibiwe adhabu ya kifo. Fikra kama hizi hazina msingi wowote. Wazungu wasio na upendeleo wanapaswa kujua kuwa ni mila ya ndoa ya mitala ambayo imeyapa nguvu mahusiano ya kifamilia na kuinua maadili ya watu hawa. Ni kutokana na mila hii kwamba mwanamke wa Mashariki anaheshimika zaidi kuliko wa ulaya. Kabla ya kuthibitisha nukta hii, lazima tuweke wazi kuwa mila hii haihusiani na Uislamu.

Hata kabla ya Uislamu, mila hii ilikuwa inafuatwa na watu wa Mashariki wakiwamo Wayahudi, Wairani, Waarabu n.k. Watu waliosilimu huko Mashariki hawakunufaika na lolote katika mila hii. Juu ya hayo, hakuna dini yoyote yenye nguvu kama hii iliyobuni au kuzuia mila hii ya mitala. Mila hii haikuanzishwa na dini yoyote. Ilitokana na hali ya hewa na sababu nyingine zilizohusiana na mfumo wa maisha ya Mashariki.

Hata Magharibi, ambako hali ya hewa haiendani na kuweko kwa desturi kama hiyo, lakini ndoa ya mke mmoja inapatikana katika vitabu vya sheria tu. Katika maisha halisi hakuna dalili ya ndoa ya mke mmoja. Haifahamiki ni kwa namna gani mitala ya halali ya Mashariki ni ya hadhi ya chini kuliko ndoa za mitala ya siri za watu wa Magharibi. Watu wa mashariki, wanapotembelea nchi za Ulaya na kukumbana na shutuma kali za Wazungu dhidi ya mila zao hushangazwa na kuona wameonewa.

Ni ukweli kwamba Uislamu haukuanzisha ndoa za mitala. Ulichokifanya ni kuidhibiti tu. Umepanga idadi ya mwisho. Umeweka masharti magumu juu yake. Mila tayari ilikuwepo katika jamii nyingi ambazo zilikuja baadaye kusilimu. Walilazimika tu kufuata masharti yale yaliyowekwa na Uislamu.

Katika kitabu chake ‘Iran During the Sassanian Period,’ Christenson ameandika: “Ndoa za mitala zilichukuliwa kuwa ni msingi wa familia. Kimsingi, idadi ya wake ambao mtu angependa kuwa nao ilitegemea na uwezo wake. Watu maskini hawakuwa wanamudu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mkuu wa familia alikuwa na haki maalum. Mmoja wa wake alichukuliwa kuwa ni mke kipenzi na alipata haki zote.

Wake wengine waliwatendea kama wafanyakazi tu. Haki za kisheria kati ya makundi haya mawili zilitofautiana sana. Watumwa wa kike (masuria) walijumuishwa katika kundi la wake wafanyakazi. Haifahamiki ni wake vipenzi wangapi mume angeweza kuwa nao. Lakini limetajwa suala la wake wawili vipenzi katika maandishi ya kisheria. Kila mmoja wao aliitwa malkia wa nyumba (mama mwenye nyumba). Waliishi katika nyumba tofauti. Mume alipaswa kumhudumia mke wake kipenzi katika maisha yake yote. Kila mtoto wa kiume hadi anapobalehe na kila mtoto wa kike hadi alipoolewa walikuwa na haki sawa. Lakini ni watoto wa kiume tu (wa wake wafanyakazi) walioingizwa katika ukoo wa baba.”

Katika kitabu, “Social History of Iran from tha fall of the Sassanians to the fall of Umayads”, marehemu Sa’id Nafisi anaandika kuwa, “Idadi ya wanawake ambao mwanaume angeoa haikuwa na mpaka na wakati fulani inavyoonekana katika kumbukumbu za Kigiriki mwanaume alikuwa anaweza kuwa na mamia ya wanawake katika nyumba yake.”

Montesquieu, akimnukuu mwanahistoria wa Kirumi, anasema kuwa wanafalsafa wengi wa Kirumi ambao walikuwa wanateswa na Wakristo kwa sababu walikataa kuwa wakristo walikimbia Roma na kwenda kwa Mfalme wa Iran, Khusro Parviz. Walishangazwa kuona kwamba huko si tu kwamba ndoa za mitala zilikuwa zinaruhusiwa bali pia wanaume wa Kifarsi walikuwa wakiingiliana na wake za watu wengine pia.

Lazima ieleweke hapa kwamba wanafalsafa wa Kirumi walikimbilia kwenye kasri la Mfalme wa Iran, Anushirwan na sio kwenye kasiri la Khusro Parviz. Montesquieu amechanganya majina kutokana na kutoelewa vizuri.

Kabla ya Uislamu, Waarabu walikuwa na uwezo wa kuwa na idadi isiyo na mipaka ya wake. Ni Uislamu ulioweka mipaka. Hii bila shaka iliwasababishia usumbufu wale waliokuwa na wake zaidi ya wanne. Kuna baadhi walikuwa na wake kumi. Walilazimika kuwaacha sita.

Kutokana na haya ni wazi kuwa si Uislamu ulioanzisha ndoa za mitala. Uislamu uliziwekea udhibiti tu. Hata hivyo haukuzipiga marufuku kabisa, katika sura zinazofuatia tutataja sababu zilizosababisha mila hii, na tutaelezea sababu ambazo zimewafanya wanaume na wanawake wa zama hizi walazimike kuipiga vita mila hii.

Sababu Za Kihistoria Za Mitala.

Ni sababu zipi za kihistoria na kijamii zilizosababisha mitala? Kwa nini mataifa mengi ya ulimwengu, hasa mataifa ya mashariki yamekubali mila hii na kwa nini mataifa ya Magharibi, kamwe hayakupata kuitumia mila hii? Imekuwaje kwamba katika miundo mitatu ya mitala ni huu muundo mmoja tu wa mume kuwa na wake wengi ndio uliopata umaarufu? Mke kuwa na waume wengi na Ukomonisti wa ngono ama hazikupata kutumiwa kabisa, au zimetumika kidogo sana na katika maeneo machache sana.

Mpaka tuyajadili maswali haya ndio tutaweza kulijadili suala la ndoa za mitala katika Uislamu na kwa mujibu wa mahitaji ya sasa ya mwanadamu.

Tusipoyatumia na kuyazingatia matokeo ya uchunguzi wa kijamii na kisaikolojia yaliyopatikana juu ya mada hii, sisi pia, kama walivyokuwa waandishi wengine wa juu juu, tunaweza kuangukia na kuanza kuimba nyimbo za zamani za kudai kuwa sababu za mitala ziko wazi. Yaani, mila hii imetokana na ukatili wa mwanaume na utawala wake kwa mwanamke. Ni matokeo ya mfumo dume. Kwa kuwa mwanaume amemtawala mwanamke, ametunga sheria na mila ambazo zitamnufaisha yeye. Hivi ndivyo alivyoipa nguvu mila hii yenye manufaa kwake na madhara kwa mwanamke, na amekuwa akiitumia kwa karne nyingi. Mwanamke alikandamizwa, hakuweza kuutekeleza mfumo wa yeye kuwa na waume wengi. Na sasa muda wa uonevu wa mwanaume umekwisha, mila ya ndoa za mitala lazima iondoke kama ilivyokuwa kwa fursa nyingine za uongo ili kuleta haki sawa kwa wanaume na wanawake.

Kufikiri kwa namna hii ni kwa kitoto na kwa juu juu sana. Sababu ya mitala sio ukandamizaji wa mwanaume kwa mwanamke wala kushindwa kwa mfumo wa mke kuwa na waume wengi sio ukandamizaji wa mwanamke. Kama kivitendo mfumo huu umekufa, hii sio kwa sababu muda wa uonevu wa mwanaume umefikia kikomo. Mwanaume hajapoteza fursa yoyote, kimsingi amepata fursa juu ya mwanamke.

Hatukatai kuwa ukandamizaji ni moja ya mambo yaliyobadilisha historia. Pia hatukatai kuwa katika kipindi chote cha historia mwanaume ameyatumia vibaya madaraka yake dhidi ya mwanamke. Lakini tunaamini kuwa ni mawazo finyu kuyaelezea mawazo ya kifamilia kwa kigezo cha dhulma peke yake.

Tukikubali mtazamo huu, lazima pia tukubali kuwa katika kipindi ambacho ndoa za mke kuwa na wanaume wengi zilikuwa maarufu miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu, au kama alivyoripoti Montesquieu, miongoni mwa Wanair katika pwani ya Malabar mwanamke alipata fursa ya kumtawala mwanaume na akawa anakaa na wanaume wengi. Lazima ikubaliwe pia kuwa kipindi hicho kilikuwa ni cha dhahabu kwa mwanamke. Awali tulimnukuu Montesquieu akisema kuwa mila ya mke kuwa na waume wengi miongoni mwa Wanair haikutokana na utawala wa mwanamke au heshima aliyokuwa akipewa, bali ilikuwa ni uamuzi wa jamii wa kuwaepusha askari dhidi ya mzigo wa majukumu ya familia.

Aidha, kama Mfumo dume ndio ulisababisha mitala, kwa nini mfumo huu haukupata umaarufu Ulaya (Magharibi)? Hata hivyo, mfumo dume haukuwepo Mashariki peke yake. Je, watu wa Magharibi tokea awali wamekuwa Wakristo wachamungu wanaoamini juu ya usawa kati ya mwanaume na mwanamke? Je, kigezo cha kumiliki kimemnufaisha mwanaume wa mashariki na kukuza uadilifu huko Magharibi?

Mpaka kufikia nusu karne iliyopita mwanamke wa Magharibi alikuwa miongoni mwa wenye bahati mbaya kabisa duniani. Hata mali yake ilidhibitiwa na mume wake. Wazungu wenyewe wanakiri kuwa katika zama za kati, nafasi ya mwanamke wa mashariki ilikuwa bora sana ikilinganishwa na mwanamke wa Magharibi. Gustav Leabeon anasema kuwa Uislamu, katika kipindi cha mwanzo kabisa, ulimpa mwanamke nafasi (hadhi) ambayo mwanamke wa kizungu alipata baada ya muda mrefu sana, yaani baada ya uungwana na ustaarabu wa Waarabu wa Andolusia kuingia Ulaya.

Tabia njema kwa mwanamke ni sehemu kubwa ya uungwana ambao Wazungu walijifunza kutoka kwa Waislamu. Ilikuwa ni Uislamu (na sio dini ya Kikristo kama inavyoaminiwa na watu wengi wa kawaida), ulioinyanyua hadhi ya mwanamke. Katika zama za kati machifu wa makabila, licha ya kuwa Wakristo kamwe hawakumpa mwanamke heshima anayostahili. Uchambuzi wa historia ya kale unaonyesha kuwa tabia ya wafalme na viongozi wengine wa Ulaya ilikuwa ni ya kishenzi sana.

Waandishi wengine wa Kizungu, pia wametoa maelezo kama haya kuhusiana na nafasi ya mwanamke katika zama za kati. Japo mfumo dume ulikuwa umeenea sana Ulaya katika kipindi hiki, bado ndoa za mitala hazikuweza kuwa ni desturi.

Ukweli ni kuwa ni mfumo wa mke kuwa na waume wengi (popote ulikotumika) hautokani na utawala au nguvu ya mwanamke juu ya mwanaume wala kushindwa kwa mfumo huu hakukutokana na udhaifu wa mwanamke wala ukandamizaji wa mwanaume dhidi yake. Halikadhalika mitala katika nchi za Mashariki haikusababishwa na udikteta na uonevu wa mwanaume wala si kwamba haujaenea huko magharibi kwa sababu ya kuwepo usawa kati ya mwanaume na mwanamke.

Sababu Za Kushindwa Kwa Mfumo Wa Mke Kuwa Na Waume Wengi

Sababu kubwa ya kushindwa kwa mfumo huu ni kuwa ulikuwa haufai kwa maumbile ya mwanaume wala ya mwanamke. Haufai kwa maumbile ya mwanaume, kwa sababu, kwanza hauafikiani na asili yake ya kupenda umiliki pekee (yaani awe wake peke yake) na pili kwa sababu haukubaliani na kanuni ya kwamba baba aweze kujiamini juu ya ubaba wake. Ni maumbile ya mwanadamu kuwa na mafungamano maalumu na wanawe.

Kila mwanadamu kwa asili anatamani kuzaa watoto na anataka uhusiano na kizazi chake kilichopita na kijacho uwe unaeleweka na wa uhakika. Anataka kujua yeye ni mtoto wa nani na ni baba wa nani. Mfumo wa mke kuwa na waume wengi haukubaliani na silika hii ya mwanadamu. Kwa upande mwingine mfumo wa mume kuwa na wake wengi (mitala) hausababishi matatizo haya, si kwa mwanaume, wala mwanamke. Imeelezwa kuwa wakati fulani wanawake wapatao arobaini walimwendea Imam Ali (a.s.) na kumuuliza kwa nini Uislamu umewaruhusu wanaume kuoa wake wengi lakini haujaruhusu wanawake kuwa na waume wengi. Wakamuuliza kama huu sio ubaguzi wa wazi.

Imam Ali (a.s.) aliagiza viletwe vikombe vya maji na akampa kila mwanamke kikombe kimoja cha maji. Kisha akawaamuru wamwagie maji yote yale katika chombo kimoja kikubwa kilichokuwa katikati yao. Baada ya kutekeleza agizo hilo, Imam Ali (a.s.) aliwaamuru kila mmoja wao achukue maji yale tu yaliyokuwa kwenye kikombe chake. Wanawake wote walisema kuwa hilo lilikuwa haliwezekani kutokana na ukweli kwamba maji yote yalikuwa yamechanganyika. Imam Ali (a.s.) alisema kuwa kama mwanamke mmoja angeolewa na wanaume wengi, ni wazi kuwa angeingiliana nao. Akipata mimba na kuzaa, haitafahamika mtoto yule ni wa baba yupi.

Kwa upande wa mwanamke, mfumo huu pia hauafikiani na maumbile yake. Mwanamke hamhitaji mume kwa ajili ya kukidhi silika yake ya ngono tu. Ingekuwa hivyo tungesema kuwa ‘Wanaume wengi zaidi, raha zaidi’. Mwanamke anataka mwanamume ambaye yeye mwanamke ataudhibiti moyo wake, atakayekuwa mlinzi na mwangalizi wake, atakayejitoa mhanga kwa ajili ya mkewe na atakayefanya kazi kwa bidii na kumletea fedha. Fedha anazojitafutia mwanamke huwa hazitoshi kukidhi mahitaji yake wala huwa hazina thamani sawa na zile alizopewa na mwanaume anayempenda. Mume hukidhi mahitaji ya kifedha ya mke wake kwa moyo wa kujitolea. Mke na watoto ni hamasa kubwa na bora kabisa kumhamasisha mwanaume kufanya kazi.

Katika mfumo wa mke kuwa na waume wengi mwanamke hawezi akadai na kupata mapenzi ya kweli na kujitolea kutoka kwa yeyote kati ya wanaume hawa. Hii ndiyo sababu, kama ilivyo tu kwa umalaya, huu umekuwa ni mfumo unaochukiza kwa mwanamke. Hivyo mfumo huu wa mke kuwa na waume wengi haukidhi wala kukubaliana na asili na mahitaji ya mwanaume wala mwanamke.

Kushindwa Kwa Ukomonisti Wa Ngono

Katika mfumo huu si mwanaume wala mwanamke anayeweza kudai au kujinasibisha na mke au mume maalumu kuwa ni wake na hii ndiyo sababu mfumo huu kamwe haukupata kuwa maarufu sehemu yoyote ile. Ilipendekezwa na Plato ambaye aliliruhusu jambo hili kwa tabaka la watawala au ‘wanafalsafa watawala.’ Lakini pendekezo lake halikuwa kama la wengine na yeye mwenyewe baadaye ilibidi abadilishe maoni yake.

Katika karne iliyopita, Frederick Engels, baba wa pili wa ukomunisti alitoa wazo hili na akalitetea kwa nguvu. Lakini halikukubaliwa hata katika ulimwengu wa kikomunisti. Inasemekana kuwa Urusi ilijaribu kutekeleza nadharia ya familia ya Engels, lakini kufuatia machungu waliyayopata yaliyotokana na mfumo huu walilazimika kuutambua mfumo wa mume mmoja mke mmoja kuwa ndio sera rasmi.

Mitala inaweza kuonekana kuwa ni jambo la fahari kwa mwanaume lakini kamwe suala la mke kuwa na waume wengi halijawahi na halitapata kuwa ni jambo la fahari kwa mwanamke. Sababu ni kuwa mwanaume anataka mwili wa mwanamke na mwanamke anataka moyo wa mwanaume. Mwanaume anachojali ni kuumiliki mwili wa mwanamke, haijalishi hata kama haumiliki moyo wake. Hii ndio sababu mwanaume huwa hajali hata kama mmoja wa wake zake atapunguza upendo kwake, lakini kwa mwanamke, kitu muhimu kabisa ni moyo wa mwanaume na hisia zake za moyoni. Akivipoteza hivyo, huwa amepoteza kila kitu.

Kwa maneno mengine, kuna vitu viwili katika maisha ya unyumba, mwili na hisia za moyoni. Mwili unahusiana na ngono, ambayo hamu yake huwa kileleni katika kipindi cha ujana na baadaye hupungua polepole. Hisia za moyoni huhusiana na hisia za upendo, upole na kujitoa. Hisia hizi hukua na kukomaa kwa kadri muda unavyokwenda. Kwa vile maumbile ya mwanamke ni tofauti na ya mwanaume, mwanamke hujali zaidi hisia za moyoni katika maisha yake ya ndoa. Lakini kwa mwanaume, ama mwili ndio muhimu zaidi au vyote viwili, mwili na hisia za moyoni vina umuhimu sawa.

Huko nyuma, tulimnukuu mwanasaikolojia wa kike ambaye ana maoni kuwa mwanamke ana tabia za kipekee za akili. Mtoto hukua katika tumbo lake na kunyonyeshwa na kulelewa katika mapaja yake. Anahitaji sana kujitolea na upendo wa dhati wa mumewe kama baba wa mtoto. Hata kiasi cha upendo kwa wanawe kinategemeana na kiasi cha upendo anachokipata kutoka kwa baba yao. Ni ndoa ya mume mmoja tu ndiyo inaweza kukidhi mahitaji haya.

Ni kosa kubwa sana kulinganisha ndoa ya mke mmoja kuwa na waume wengi na ndoa ya mume mmoja kuwa na wake wengi na kudai kuwa hakuna tofauti yoyote kati ya aina hizi mbili za ndoa.

Pia ni makosa kusema kuwa ndoa za mitala zilikuwa mashuhuri katika baadhi ya sehemu za dunia kwa sababu mwanaume ana nguvu zaidi, na kwamba ndoa za mke kuwa na waume wengi zilishindwa kutokana na mke kuwa ni jinsia dhaifu.

Mwandishi wa zama hizi, ambaye ni mwanamke anasema: “Tunaweza kusema kuwa kwa vile mwanaume anaweza kuwa na wake wanne, basi mke pia anapaswa kuwa na haki hiyo kwani wote ni binadamu. Hitimisho hili la kimantiki ni la kuudhi, zaidi kwa wanaume. Wanakasirishwa kusikia hoja hii na wanapiga kelele: ‘Inawezekanaje mwanamke akawa na waume zaidi ya mmoja?’ Kujibu hilo sisi kwa sauti ndogo tunasema: Inawezakanaje mwanaume akawa na mke zaidi ya mmoja?”

Pia anasema: “Hatukusudii kupalilia ufisadi au kupuuzia umuhimu wa maisha ya usafi wa kimaadili. Tunataka tu wanaume waelewe kuwa maoni yao juu ya wanawake hayakujengwa juu ya hoja za maana. Mwanaume na mwanamke ni sawa kama wanaadamu. Kama mwanaume ana haki ya kuwa na wake wanne, basi mwanamke pia lazima awe na haki kama hiyo. Hata kama tukichukulia kwamba mwanamke kiakili sio bora kuliko mwanaume, lakini ni hakika kwamba kiroho mwanamke sio dhaifu kuliko mwanaume.”

Kama ambavyo utakuwa umebaini kauli hiyo haioneshi tofauti yeyote kati ya mitala na ndoa za mke kuwa na waume wengi, isipokuwa kwamba kwa kuwa mwanaume ni wa jinsia yenye nguvu zaidi basi amechukuwa mfumo wa mitala kwa manufaa yake, na mwanamke kwa kuwa ni wa jinsia dhaifu hakuweza kuutumia utaratibu huo.

Mwandishi huyo pia anasema kuwa mwanaume anamuona mwanamke kuwa ni mali yake, na ndio maana anataka kuwa na wake wengi. Kwa maneno mengine ni kuwa mwanaume anataka kujikusanyia mali nyingi kwa kadri inavyowezekana. Kwa vile mwanamke yupo katika nafasi ya mtumwa, hawezi kuwa anamilikiwa na bwana zaidi ya mmoja.

Kinyume na maoni ya mwandishi huyu, ukweli kwamba mfumo wa mke kuwa na waume wengi haujawahi kukubaliwa na idadi yoyote kubwa ya watu popote pale duniani unathibitisha kuwa mwanaume hamchukulii mke wake kuwa ni mali yake, kwani katika mali, ni mashuhuri duniani kote kuwa mali humilikiwa kwa ubia na wamiliki wote hunufaika na mali hiyo kwa ubia. Kama mwanaume angekuwa anamchukulia mwanamke kuwa ni mali, ni wazi kuwa asingekuwa na pingamiza katika kuichangia na wengine. Hakuna sheria duniani inayolazimisha kuwa mali imilikiwe na mtu mmoja tu.

Inasemwa kwamba mume ni mtu mmoja na mke ni mtu mmoja. Wanapaswa kuwa na haki sawa. Kwa nini mume awe na haki ya kufurahia mitala na mke anyimwe haki hiyo ya kuwa na waume wengi?
Tunasema kuwa hapa ndio kuna makosa. Unadhania kwamba mitala ni sehemu ya haki za mume, na mke kuwa na waume wengi ni sehemu ya haki za mke. Ukweli ni kwamba mitala ni sehemu ya haki za mwanamke, na ndoa ya mke kuwa na waume wengi sio sehemu ya haki za mwanaume wala mwanamke. Ni mfumo usio na faida kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume. Tutathibitisha baadaye kuwa mfumo wa mitala umewekwa na Uislamu kwa nia ya kulinda maslahi ya mwanamke. Kama nia ingekuwa kumpendelea mwanaume, Uislamu ungemruhusu mwanaume kufanya mapenzi na mwanamke mwingine mbali na mke wake na usingeweka uwajibikaji juu yake kuhusiana na mke wake wa halali na watoto wake wa halali.

Mfumo wa mke kuwa na waume wengi kamwe haujapata kuwa na maslahi yoyote kwa mwanamke. Sio haki aliyonyimwa.

Mwandishi ambaye tumenukuu maoni yake anasema: “Tunataka wanaume waelewe kuwa maoni yao juu ya wanawake hayajajengwa juu ya hoja ya maana.”

Kwa bahati sisi pia hicho ndicho tunachokusudia kukifanya. Katika sura zinazofuata tutaeleza msingi wa mtazamo wa Uislamu juu ya mitala.

Tunawaalika watu wote wanaofikiri kuutazama na kuona kama mtazamo wa Uislamu umejengwa au haukujengwa juu ya hoja zozote za maana. Tunaahidi kuwa tutayabatilisha yale yote, tuliyoyasema ikiwa mtu yeyote atathibitisha kuwa msingi wa mtazamo wa Uislamu ni mbovu.