read

Hitimisho

Hapo juu tumejadili sababu zote ambazo zinaweza kudhaniwa kuwa ndio chanzo cha mitala. Kama ambavyo tumeona, baadhi ya sababu hizi kama vile tabia ya nchi (hali ya hewa) ilivyo sio sababu halisi. Hivyo tunazipuuza. Sababu nyingine zinaweza kuwa zile zenye nguvu ya kumshawishi mwanaume kuoa wake wengi lakini hazitoi uhalali juu ya kitendo chake. Zina sura ya ukandamizaji, ubabe na ukatili. Sababu za kiuchumi zinaingia katika kundi hili.

Ni dhahiri kuwa uuzaji wa watoto ni moja ya vitendo vya kikatili na kishenzi kabisa. Kuamua kuoa wake wengi kwa ajili ya lengo hili ni haramu kama kitendo chenyewe kilivyo haramu.

Kundi la pili linajumuisha sababu ambazo zinaweza kuonekana kuwa ni sababu thabiti kwa upande wa mume au jamii. Ugumba wa mke wa kwanza, kufikia kikomo cha uzazi wakati bado mume anahitaji watoto au kama kabila au taifa linahitaji idadi kubwa ya watu. Kama kanuni ya jumla, sababu zote ambazo zinatokana na kutofautiana kati ya mume na mke kuwiana na mahitaji ya jimai na nguvu ya uzazi, zina uthabiti.

Kundi la tatu linajumuisha sababu ambazo kama ikikubaliwa kuwa zilikuwepo au bado zipo, sio tu kwamba huruhusu mitala bali pia huzifanya kuwa ni wajibu. Katika hali hii, mitala ni haki ya mwanamke ambayo mwanaume na jamii wanapaswa kuitoa. Sababu hii ni uwingi wa wanawake kuwazidi wanaume, ikiwa idadi ya wanawake wanaopaswa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa, mitala huwa ni wajibu wa wanaume na haki ya mwanamke, kwani ikiwa itaamuriwa kuwa mume mmoja akae na mke mmoja tu, idadi fulani ya wanawake itakuwa imenyimwa haki ya kuishi maisha ya kifamilia.

Haki ya ndoa ni haki ya msingi ya binadamu na hakuna anayepaswa kunyimwa haki hii kwa kisingizio chochote. Jamii haiwezi ikachukua hatua yoyote ambayo inaweza ikawanyima baadhi ya watu haki hii.

Haki ya ndoa ni haki ya asili kama ilivyo kwa haki ya uhuru, haki ya kufanya kazi na haki ya kupata chakula, malazi na elimu. Hivyo, sheria ya kuwa na mke mmoja inapingana na haki za binadamu pindi inapokuwa wanawake wanaopaswa kuolewa ni wengi kuliko wanaume wanaofaa kuoa.

Kwa uchache, hii ndiyo imekuwa ni hali ya mambo huko nyuma. Katika sura zifuatayo tutaangalia ikiwa bado kuna mazingira ambayo sio tu kwamba yanahalalisha mitala bali pia yanaijenga haki hii kwa ajili ya mwanamke. Na kama mazingira haya bado yapo, sasa ni nini nafasi ya haki hii dhidi ya haki ya mke wa kwanza.

Haki Ya Mwanamke Katika Ndoa Ya Wake Wengi

Tumeshaelezea sababu za kushindwa kwa ndoa za mke mmoja kuwa na waume wengi na kufanikiwa kwa mitala na tumeelezea sababu mbalimbali zilizosababisha kuibuka kwa mitala. Baadhi ya sababu zilitokana na moyo wa ukandamizaji na ubabe wa mwanaume na nyingine zilitokana na kutofautiana kwa mwanamke na mwanaume kuhusiana na kudumu kwa uwezo wao wa kuzaa na idadi ya watoto ambayo kila mmoja wao anaweza kuzaa. Hizi sababu za pili zinaweza kuchukuliwa kuwa ni sababu thabiti za mitala. Lakini sababu yake kuu katika kipindi chote cha historia imekuwa ni idadi ya wanawake inayozidi ya wanaume wanaofaa kuolewa na kuoa sawia. Sababu hii husababisha kuzaliwa kwa haki ya mwanamke na jukumu la mwanaume.

Ili kuepuka mjadala mrefu, tunaziruka sababu hizi ambazo zinaweza kuchukuliwa kuwa ni uhalalishaji tu wa mitala, na kushughulikia tu sababu yake kubwa, ambayo kama ikiwepo hubadilika kuwa haki ya jinsia dhaifu.

Ili kuthibitisha hili, nukta mbili za utangulizi zinapaswa kuwekwa sawa. Kwanza ni kuthibitisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za kuaminika, idadi ya wanawake wanaopwaswa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa. Nukta ya pili tunayotaka kuithibitisha ni kuwepo kwa mazingira halisi yanayounda wajibu kwa wanaume waliooa na wanawake walioolewa juu ya wanawake walionyimwa haki ya kuwa na ndoa. Kuhusiana na nukta ya kwanza, kwa bahati nzuri takwimu zote thabiti zipo duniani. Sensa huchukuliwa katika kila nchi katika kila baada ya muda fulani. Katika nchi zilizoendelea, sio tu kwamba idadi wa wanaume na wanawake hukusanywa bali pia idadi ya wanaume na wanawake katika umri mbalimbali huonyeshwa. Takwimu hizi huchapishwa na Umoja wa Mataifa katika ripoti zake za kila mwaka juu ya idadi ya watu.1

Inaweza kuonyeshwa kwamba kwa madhumuni yetu, haitoshelezi kujua idadi ya wanaume na wanawake katika kila nchi, tunahitaji pia kujua uwiano wa idadi ya wanaume na wanawake wanaofaa kuoa na kuolewa sawia. Mara nyingi uwiano huu unatofautiana na uwiano wa jumla wa wanaume na wanawake. Kuna sababu mbili za tofauti hii. Moja ni kuwa wanawake hupevuka mapema zaidi. Hii ndio sababu katika nchi zilizo nyingi umri unaoruhusiwa wasichana kuolewa upo chini kuliko umri wa wavulana wanaoruhusiwa kuoa. Kwa wastani, umri wa mume huwa ni miaka mitano zaidi kuliko mkewe.

Sababu nyingine na muhimu zaidi ni kuwa idadi ya vifo vya wavulana ni kubwa kuliko wasichana, na matokeo yake ni kuwa katika umri wao wa ndoa, wasichana huwa ni wengi kuliko wavulana. Wakati fulani tofauti huwa kubwa. Inaweza kutokea kuwa idadi ya wanaume na wanawake katika nchi inalingana au hata wanaume wakawa wengi kuliko wanawake, lakini bado idadi ya wasichana wanaofaa kuolewa ikawa kubwa kuliko idadi ya wavulana wanaoweza kuoa, tena kwa idadi kubwa.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Uwingi wa watu kwa mwaka 1964, inashuhudia ukweli huu.

Kwa mfano, kwa mujibu wa ripoti hii, jumla ya watu katika Jamhuri ya Korea ni 26,277,635. Kati ya hawa wanaume ni 13,145,289 na 13,132,326 ni wanawake. Hivyo idadi ya wanaume ni zaidi ya wanawake kwa 12,943. Uwiano huu unabaki hivi katika umri wa miaka 14, 59, 1214 na 1519.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika makundi yote haya ya umri idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake. Lakini katika kundi la umri la miaka,2024, uwiano unabadilika. Katika kundi hili la umri idadi ya wanaume ni 1,083,364, na idadi ya wanawake ni 1,110,051. Katika makundi yote ya umri wa juu, ambayo ni makundi ya wanayoweza kuoa na kuolewa idadi ya wanawake ni kubwa zaidi.

Hata hivyo, Jamhuri ya Korea ni mfano wa pekee ambapo idadi ya wanaume ni kubwa kuliko idadi ya wanawake. Takribani, katika nchi nyingine zote, sio tu kwamba idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni kubwa kuliko ya wanaume, bali hata katika idadi ya jumla, wanawake ni wengi kuliiko wanaume. Kwa mfano idadi ya watu nchini Urusi ni 216,101,000 na wanawake ni 118,261,000, na tofauti hii inaendelea katika makundi yote ya umri, yale ambayo hayajafikia umri wa kuingia katika ndoa na yale yaliyofikia umri huo, hii ni kuanzia 2024, 2529, 3034 na hata 8084.

Hali iko hivi hivi katika nchi nyingine pia kama vile Uingereza, Ufaransa, Ujerumani ya Magharibi, Ujerumani wa Mashariki, Czechoslavakia, Poland, Romania, Hungary, Marekani, Japan n.k. Katika baadhi ya sehemu kama vile Berlin Magharibi na Berlin Mashariki, tofauti ya idadi kati ya wanaume na wanawake ni kubwa mno.

Nchini India, katika makundi ya umri ambapo watu wanaweza kuingia katika ndoa, idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake. Idadi ya wanawake ni kubwa tu kuanzia katika umri wa miaka 50 na kuendelea. Inavyoonekana uchache wa wanawake unatokana na ukweli kwamba watu wengi nchini India hawapendi kutaja majina ya wake zao vijana au binti zao wadogo, wakati wa sensa.

Kwa mujibu wa takwimu za sensa iliyopita, Iran ni moja ya nchi ya pekee ambapo, idadi ya wanawake inaizidi ile ya wanaume.

Inashangaza kwamba baadhi ya wakosoaji wanasisitiza kuwa sheria inayoruhusu mitala ipigwe marufuku angalau katika nchi ambazo idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake. Katika hatua ya kwanza, sheria hii ni ya wote, sio ya nchi maalumu. Pili, haitoshi kujua uwiano wa wanaume na wanawake peke yake. Tumeona kuwa katika Jamhuri ya Korea, idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake, lakini idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ikawa kubwa kuliko idadi ya wanaume wanofaa kuoa. Aidha, takwimu za sensa, sio za kuaminika sana katika nchi zilizo nyingi. Kwa mfano, tunajua kuwa ingawa mitala ni mila iliyozoeleka nchini Iran, mijini na vijijini, lakini haijawahi kutokea upungufu wa mabibi harusi watarajiwa. Ukweli huu peke yake unaongea vizuri zaidi kuliko takwimu za sensa.

Ashley Montaque, katika kitabu chake, “Woman The Superior Sex”, anakiri kwamba duniani kote, idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni kubwa kuliko ile ya wanaume wanaofaa kuoa.

Takwimu za mwaka 1950, zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake waliofikia umri wa kuolewa nchini Marekani inaizidi ile ya wanume takriban kwa 1,430,000.

Bertrand Russel katika kitabu chake, “Marriage and Morality”, anasema kwamba katika Uingereza ya leo, wanawake wanazidi idadi ya wanaume kwa zaidi ya milioni mbili. Kwa mujibu wa mila yao, wanapaswa wabakie bila kupata watoto, jambo ambalo ni dhulma kubwa kwa upande wao.

Miaka kadhaa iliyopita, ilitangazwa kwenye vyombo vya habari kwamba, kufuatia shinikizo kubwa la wanawake wa Kijerumani ambao hawakuweza kupata waume na maisha ya kifamilia, kufuatia vifo vingi vya wanaume katika vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Ujerumani imekiomba chuo kikuu cha AlAzhar kiipatie mwongozo wa mitala. Baadaye ilifahamika kuwa kufuatia upinzani mkali wa kanisa, pendekezo hilo ilibidi liachwe. Kanisa liliona bora wanawake wakae bila kuolewa wala kuzaa wala kuishi maisha ya kifamilia, na ni bora uzinifu na ufuska kuliko kuukubali mfumo wa wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja. Kwa vile tu mfumo huu ni wa Mashariki na wa Kiislamu.

Kwa Nini Kuna Wanawake Wengi Wa Umri Wa Ndoa Kuliko Wanaume?

Ingawa idadi ya wasichana wanaozaliwa sio kubwa kuliko ile ya wavulana, lakini bado kuna idadi kubwa ya wanawake wengi wa umri wa kuolewa kuliko idadi ya wanaume. Sababu iko wazi. Kiasi cha vifo vya wanaume ni kikubwa. Vifo hutokea katika kipindi ambapo mwanamume alipaswa kwa kawaida kuwa mkuu wa familia. Tukizingatia vifo vinavyotokea katika ajali, vita, kufa majini, kuanguka, kugongana kwa magari n.k. tutakuta kwamba wengi wa waathirika ni wanaume.

Ni mara chache sana kukutwa kwamba mwanamke ni moja wa waathirika. Iwe ni migongano (ajali) kati ya wanaadamu au kati ya mwanadamu na maumbile, wengi wa waathirika huwa ni wanaume watu wazima. Ili kujua kwa nini idadi ya wanawake wanaopaswa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa, inatosha kufahamu kuwa tokea mwanzo wa historia ya mwanadamu hakuna hata siku moja ambayo imewahi kupita bila kupigana vita na wanaume kupoteza uhai.

Vifo vinavyotokea kutokana na vita katika hizi zama za viwanda ni vingi mara mia kuliko vile vilivyokuwa vinatokea katika zama za uwindaji na zama za kilimo. Katika vita vya Pili vya Dunia, idadi ya vifo vilivyotokea inafikia milioni saba. Utakubaliana na sisi ukihesabu vifo vinavyotokea katika vita vya kimkoa huko Mashariki ya Mbali, Mashariki ya Kati na Afrika katika miongo miwili iliyopita.

Will Durant anasema kwamba sababu nyingi zimechangia kudondoka kwa mila hii ya mitala. Maisha thabiti ya kilimo yamepunguza ugumu na hatari za maisha ya wanaume, ambapo matokeo yake ni kuwa idadi za wanawake na wanume zinakaribia kulingana.

Anachosema Will Durant kinashangaza sana. Kama ingekuwa kupotea kwa maisha ya watu kunatokana na mapambano ya wanaume dhidi ya muambile tu, kungekuwa kuna tofauti kati ya zama za uwindaji na zama za kilimo. Lakini kadri muda unavyokwenda, vita vimeendelea kuchukua idadi kubwa zaidi ya uhai wa wanaume na idadi ya vifo vinavyotokana na vita haijapata kupungua katika zama zozote. Pia sababu kubwa kwa nini wanawake hawajakumbwa na ajali nyingi ni kwamba wakati wote wanaume wamekuwa wakiwalinda, na wao wanaume ndio wamekuwa wakifanya kazi za hatari zaidi. Hivyo kama ilivyokuwa katika zama za uwindaji, uwiano usio sawa wa idadi ya wanaume na wanawake umeendelea pia katika zama za kilimo.

Will Durant hajasema lolote juu ya zama za viwanda, ingawa hiki ndio kipindi ambacho kimeshuhudia mauaji makubwa zaidi ya wanaume na kipindi ambacho uwiano kati ya idadi ya wanaume na wanawake umepishana mno.

Mwanamke Ana Uwezo Zaidi Wa Kujikinga Dhidi Ya Maradhi.

Imegunduliwa hivi karibuni kuwa mwanaume ana uwezo mdogo zaidi wa kujikinga dhidi ya maradhi kuliko wanawake. Hii ni sababu nyingine kwa nini idadi ya vifo vya wanaume ni kubwa zaidi.

Miaka kadha iliyopita, Tume ya Takwimu ya Ufaransa iliripoti kuwa nchini Ufaransa, wavulana 105 huzaliwa dhidi ya wasichana 100 lakini cha ajabu idadi ya wanawake ilikuwa ni kubwa kuliko wanaume kwa 1,758,000 (milioni moja na laki saba na elfu hamsini na nane). Inaaminika kwamba tofauti hii inatokana na uwezo mkubwa wa mwanamke wa kujilinda dhidi ya magonjwa.

Si muda mrefu umepita, makala moja ilichapishwa kwenye jaria la UNESCO liitwalo Courier. Kwa mujibu wa makala hii, mwanamke ana uwezo mkubwa zaidi wa akili kuliko mwanamume. Wastani wa kinga yake ni kubwa zaidi. Kwa kawaida, ana afya nzuri zaidi kuliko mwanaume na ana uwezo zaidi wa kustahamili maradhi. Hupona haraka kuliko mwanaume. Katika kila mwanamke mmoja mwenye kigugumizi, kuna wanaume watano wenye kigugumizi.

Katika kila mwanamke mmoja asiyeweza kutofautisha rangi, kuna wanaume kumi na sita wasioweza kutofautisha rangi. Na kwa kawaida ni ugonjwa wa wanaume tu. Wanawake wana mfumo bora zaidi wa kinga ya ajali. Wakati wa vita vya Pili vya Dunia ilithibitika kuwa katika mazingira ya aina moja, mwanamke alikuwa na uwezo zaidi wa kustahamili ugumu wa vizuizi, magereza, na kambi za wafungwa wa vita kuliko wanaume. Takribani katika nchi zote, idadi ya kesi za wanaume kujinyonga ni kubwa mara tatu zaidi kuliko wanawake.

Ashley Montague ameitaja nadharia yake ya uwezo mkubwa zaidi wa mwanamke kustahamili maradhi, katika kitabu chake kiitwacho, “Woman, the Superior Sex.”

Ikiwa siku moja itatokea mwanaume ataamua kumpeleka mwanamke katika kazi za hatari na za kifo au kama atamsukumia katika uwanja wa vita kukabiliana na bunduki na mabomu, bado idadi ya wanawake itaendelea kuwa kubwa kwa sababu yeye ana uwezo zaidi wa kustahamili maradhi.

Haya tuliyoyasema yanahusiana tu na uwingi wa wanawake wanaofaa kuolewa dhidi ya wanaume wanaofaa kuoa. Tunajua kwamba uwingi huu ni ukweli halisi. Pia tunajua sababu zake. Na sababu zake, zile zilizokuwepo tokea mwanzo wa historia ya mwanadamu bado zipo mpaka sasa.

  • 1. Tunayo mbele yetu ripoti ya 1964, iliyochapishwa tena 1965